Vita dhidi ya ujangili ni kama mapambano mengine ya binadamu katika kujihakikishia usalama. Tofauti tu ni kwamba katika vita dhidi ya ujangili wanaolindwa ni wanyama na makazi yao, badala ya binadamu na mali zake.

 Vivyo hivyo, kama ambavyo mtu hawezi kujihakikishia usalama na mali zake kwa kumwajiri mlinzi kwa wiki moja, ndivyo ambavyo nchi haiwezi kujihakikishia usalama wa wanyamapori kwa operesheni ya muda mfupi kama ilivyokuwa kwa Operesheni Uhai na Tokomeza.

Hii haina maana kwamba operesheni hizo hazina manufaa. La! Hasha! Bali kinachozungumziwa hapa ni kwamba operesheni za namna hiyo siyo suluhu ya kudumu dhidi ya ujangili. Na hii ikiwa ni kwa sababu operesheni ikisitishwa leo, majangili wanaweza kuua wanyama kesho yake eneo hilo hilo, kama hakuna ulinzi. 

Hivyo katika vita dhidi ujangili, operesheni ni mapigano ya wakati na mahali husika; na ufanisi au mafanikio yake ni ya wakati huo huo, na mahali pale pale; na siyo mafanikio ya wakati wote na mahali pote. Kwa maneno mengine ni mafanikio ya mapigano na si ushindi wa vita nzima.

Ili Tanzania ijihakikishie ushindi dhidi ya ujangili, inabidi kujihakikishia kuwa wakati wowote ule jangili anakuwa amedhibitiwa. Na hili haliwezekani kufanyika kwa operesheni kutokana na gharama kuwa kubwa sana na hivyo kutowezekana kuenea nchi nzima na kwa wakati wote.

Takwimu za idadi ya tembo nchini, na hasa za Pori la Akiba la Selous ambalo ni maarufu kwa idadi kubwa ya tembo, zinaonesha idadi ya mnyama huyo kuongezeka kwa wakati na sehemu kulipokuwa na ulinzi wa kuridhisha, na idadi kupungua kwa kasi mara tu ulinzi unapokosekana au kulegalega. 

Kuna sababu mbalimbali zilizosababisha ulinzi wa wanyamapori kushuka na ujangili kuongezeka kwa kasi na kiwango cha kutisha, hasa baada ya mwaka 2010.

Kwa ujumla sababu hizo zinajulikana kwa wanajamii wanaofuatilia taarifa mbalimbali zilizotolewa siku za karibuni kuhusu ujangili. Hivyo si nia ya makala hii kuzungumzia sababu hizo kwa kina.

Makala hii inajikita zaidi katika kuangaza kinachofanyika Idara ya Wanyamapori katika kukabiliana na hali hiyo, upungufu wa jitihada hizo, na kupendekeza cha kufanyika. 

Mbali ya Operesheni Tokomeza ambayo imezungumziwa sana siku za karibuni, Idara ya Wanyamapori, (kama ilivyo kwa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Hifadhi za Taifa (TANAPA)) inaendesha shughuli zake za ulinzi wa wanyamapori kwa askari kufanya doria kwa mguu na kwa kutumia magari wakiwa wamejihami kwa bunduki. Na kwa hakika huu ndio mhimili mkuu wa ulinzi wa wanyamapori. 

Hivyo udhaifu au upungufu wowote kuhusu kazi ya doria unaathiri moja kwa moja ulinzi wa wanyamapori. Ni wazi kwa yeyote aliyebahatika kutembelea mapori makubwa ya kuhifadhi wanyama au kusoma taarifa ambazo zimekuwa zikipatikana kutoka vyanzo mbalimbali kuwa kuna upungufu mkubwa wa idadi ya askari, vitendeakazi na motisha. 

Siyo jambo la ajabu kukuta vituo vya askari wanaotakiwa kulinda maeneo makubwa ya mapori ya wanyamapori kama Selous, Wami-Mbiki, n.k, kuwa na gari moja, au hata kutokuwa na gari la doria kabisa; hali inayosababisha sehemu kubwa ya mapori hayo kutofikiwa na askari, na hivyo kuwa rahisi kufikiwa na majangili.

Hata inapotokea askari hao wakakamata majangilli, inakuwa vigumu kusimamia kesi wanapokuwa hawana usafiri wa kwenda mjini mahakama ziliko.

Mbali na tatizo la usafiri, askari wengi hawana vifaa vya mawasiliano vya kuweza kuwasiliana kwa wakati kuhusu majangili au matatizo wanayokumbana nayo wakiwa kwenye doria, kama kuharibikiwa na gari, au kuzidiwa nguvu na majangili. 

Mara nyingi askari wanazidiwa nguvu na majangili kutokana na idadi yao kuwa ndogo na zana zao kuwa duni. Japokuwa kuna Kikosi Dhidi Ujangili cha Idara, wakati mwingine inakuwa vigumu kuunganisha nguvu ya kikosi hicho na askari walio porini kutokana na changamoto za mawasiliano.

Hali hii siyo tu inasababisha wanyama wengi kuuawa na majangilli, bali pia na askari kupoteza maisha kwa kuuawa na majangili. Kwa mujibu wa Hotuba ya Wizara ya Maliasili na Utalii ya bajeti ya 2013-2014, askari 17 waliuawa na majangili katika kipindi cha 1997-2012.

Kinachosikitisha zaidi ni kwamba, licha ya hali hii kujulikana, bunduki 500 aina ya AK47 zilikwama zaidi ya miaka miwili bandarini kutokana na Wizara kushindwa kuzilipia ushuru! 

Kwa maoni yangu, kikubwa kinachotakiwa kufanywa ili kushinda vita dhidi ya ujangili ni kujenga uwezo wa ndani ya Idara ya Wanyamapori kutumia askari wake kwa ufanisi. 

Ufanisi katika ulinzi wa wanyamapori utapatikana pale tu kutakapokuwa na askari wa kutosha na wenye ujuzi, ari, na vitandeakazi vinavyokidhi haja ya kudhibiti jangili katika mazingira ya sasa. 

Pamoja na vitendeakazi, kunatakiwa pia kuboresha miundombinu; hii ikiwa ni pamoja na barabara za porini na mabanda ya ulinzi (game posts).  

Katika kuboresha vitendeakazi na miundombinu, suala la mawasiliano ni muhimu sana, na la msingi. Imefika wakati wa kuondokana na “radio call” na simu za kawaida porini. 

Japo vyombo hivyo vilikidhi matakwa ya ulinzi wa wanyamapori katika miaka 70, 80 na 90, na ambavyo sasa vimepitwa na wakati, na hasa kwa vile majangili wanaweza kutumia simu za satellite na mitandao ya simu za kisasa. Hivyo serikali haina budi kuwapatia askari wake vifaa vya mawasiliano vya kisasa.

Jingine linalotakiwa kufanywa katika kujenga uwezo wa kukabiliana na ujangili, na ambalo halijapewa kipaumbele stahili, ni kushirikisha jamii zinazozunguka mapori mbali mbali ya uhifadhi. Juhudi zilizopo kwa sasa zimebebwa sana na mashirika ya kimataifa na wafadhili wengineo. Juhudi hizi hazitoshi. Bado mtazamo alionao mwananchi anayeishi jirani na pori la wanyamapori kuhusu juhudi za kuhifadhi wanyamapori, kwa ujumla, haujawa rafiki kwa juhudi hizo. 

Kwa ujumla, mtazamo alio nao mwananchi wa  kawaida anayeishi jirani na pori la wanyamapori hausaidii juhudi za kupambana na ujangili. Kwa mfano, katika sehemu kadhaa alikofanya kazi na wananchi jirani na mapori ya kuhifadhi wanyamapori mwandishi wa makala hii alishuhudia kuweko mtazamo hasi kuhusu uhifadhi wa wanyamapori, na hata chuki dhidi ya wafanyakazi wa Idara ya Wanyamapori na wafanyakazi wa Halmashauri wanaohusika na uhifadhi wa wanyamapori wakiwaita jina la ujumla, “magemu”.

Ili kufanikisha vita dhidi ya ujangili, mwananchi jirani na pori la kuhifadhi wanyampori si tu anatakiwa atii sheria, bali pia anatakiwa ajione mdau mkuu na rafiki wa mamlaka zenye jukumu la kulinda wanyamapori. Sera ya Uhifadhi wa Wanyamapori ya 1998 inaelekeza hivyo, na kitaalamu inatakiwa hivyo.

Hivyo suala la utendaji kutokidhi haja hizi, ni dosari kubwa inayohitaji kupewa kipaumbele katika vita dhidi ya ujangili.

Japokuwa kuboresha na kuimarisha ulinzi pamoja na kushirikisha jamii jirani na mapori ya uhifadhi wa wanyama ni mambo yanayoeleweka kuwa ya msingi, na ambayo yamekuwa yakifanyika kwa kiwango fulani, iko haja ya kutumia huduma ya kitaalamu katika kuandaa mikakati na mipangokazi ya kuhuisha shughuli hizo ili kuhakikisha inakuwa tayari na madhubuti kwa wakati na kwa mafanikio zaidi.

Yote haya yanahitaji rasilimali fedha ambazo, yamkini, hazikuwa kwenye bajeti ya 2013/2014. Hivyo hakuna budi kutafuta fedha za kushughulikia masuala ya haraka na muhimu wakati bajeti ya 2014-2015 ikingojewa. Kwa maana kama kutekeleza shughuli hizo kutangojea fedha za bajeti hiyo, hazitafanywa mpaka baada ya miezi mine na zaidi. Huu ni muda mrefu sana kusubiri; hasa ukizingatia ukubwa wa tatizo la ujangili tulilo nalo kwa tembo na faru. Kwa makadirio yanayoripotiwa na watafiti ya kupoteza tembo 30 kwa siku, tunazungumzia kupoteza tembo wapatao 120 katika kipindi hicho.

Hivyo serikali haina budi kufanya juhudi za makusudi kuhakikisha kwamba Idara ya Wanyamapori inapata fedha za kutekeleza shughuli muhimu na za haraka mapema iwezekanavyo.  Nina imani kuwa fedha hizi zinaweza kupatikana kutoka kwenye Mfuko wa Kuhifadhi Wanyamapori (Tanzania Wildlife Protection Fund) na vyanzo vingine.

 

tkaiza@gmail.com

1450 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!