Nimepata kuifananisha hali ya sasa ya mapambano ya kuijenga nchi yetu na ile ya nchi iliyo vitani.

Taifa linapokuwa vitani, hasa vita hiyo inapokuwa halali, wananchi wazalendo huungana kuitetea nchi yao isitwaliwe na adui.

Kwa wazalendo, ushindi ndiyo dhima yao kuu.

Serikali ya Awamu ya Tano haiwezi kuwa ya miujiza ya kuishinda vita hii ya kimaendeleo bila ushiriki wa wananchi wote bila kujali itikadi, jinsi, hali, dini, kabila au kanda zetu.

Tunaweza kutofautiana kutofautiana mbinu za kuleta ushindi, lakini lililo muhimu ni kwamba tunazo sababu za msingi za kuishinda vita hii.

Serikali ya Awamu ya Tano imeanza kutekeleza ahadi zake. Miongoni mwazo ni utoaji elimu bure-kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha nne. Huu ni mpango mzuri ingawa wakosoaji wa mambo huwa hawakosekani. Wapo wanaobeza, lakini ukweli unabaki kuwa dhamira ya Serikali ni njema.

Hofu yangu kwenye mpango huu ni kwa Serikali kutojisahau na kuanza kuwafanya wananchi wabweteke kwa sababu Serikali imeamua kuchukua dhima ya kuwasomesha watoto!

Tusijidanganye. Bado kunahitajika msaragambo wa hali ya juu sana kutoka kwa wananchi; si tu katika kuboresha elimu yetu, bali kujiletea maendeleo katika sekta na huduma mbalimbali za kijamii.

Msaragambo bado ni muhimu kwenye ujenzi wa vyumba vya madarasa, ujenzi wa vyoo, ujenzi wa nyumba za walimu; ujenzi au ukarabati wa barabara zetu mijini na vijijini, uchimbaji visima, huduma za usafi; na kadhalika.

Kwa ufupi ni kwamba tunayo mambo mengi mno katika Taifa letu yanayohitaji ushirikishwaji wananchi kupitia nguvu kazi zao. Kuamini kuwa Serikali sasa ndiyo yenye wajibu pekee wa kuboresha huduma hizi ni kujidanganya. Tuifanye Serikali kama nyongeza tu kwenye chachu ya maendeleo yetu.

Miongoni mwa mambo ya msingi yanayofanywa sasa na Serikali yetu ni hili la kupambana na wahamiaji haramu, kudhibiti ajira kwa wageni na kukomesha wimbi la raia wa kigeni wanaoishi nchini bila kufuata sheria za nchi yetu.

Tumesikia kiwanda kimoja tu mkoani Mtwara kina wageni zaidi ya 300 wasiokuwa na vibali vya kuishi na kufanya kazi nchini! Hicho ni kiwanda kimoja tu! Hali ni mbaya kuliko wengi wetu wanavyodhani.

Wakati huu tunapoiunga mkono Serikali kwa kupeleka huduma za kijamii kwa wananchi, tunapaswa kwanza kuwatambua Watanzania ni nani. Hili tulitamke na kulisimamia bila woga kwa sababu ni jambo la msingi.

Hatutarajii kuyasikia mashirika yanayoishi kwa fadhila za wafadhili Wazungu, yakisimama kupinga uamuzi huu sahihi unaotuwezesha kutambuana ndani ya nchi yetu. Wageni hawajafukuzwa, lakini wametakiwa wafuate sheria, na kwa wale wanaofanya kazi zinazoweza kufanywa na Watanzania, waziache. Duniani kote ndivyo mambo yalivyo.

Kwa miaka mingi Tanzania imekuwa na historia ya ‘kutowabughudhi’ wageni na kwa maana hiyo wapo walioingia nchini wakasomeshwa bure (wakati ule wa elimu bure), wakapata huduma zote kama raia halali, lakini mwishowe walirejea kujenga mataifa yao.

Miaka ya karibuni imebainika kuwa hata katika vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kulikuwa na watu wenye vyeo vikubwa kabisa ambao si raia wa Tanzania, lakini wakawa wamefaidi huduma zote walizostahili Watanzania. Ukarimu huo una gharama zake.

Uamuzi wa Serikali wa kuanza kutekeleza mpango wa utoaji elimu bure ni moja ya vivutio na vishawishi vyenye kuongeza idadi ya ‘Watanzania’. Serikali yetu inaweza kujikuta ikishindwa kuhimili wingi wa wanafunzi ikidhani kuwa wote wanaoandikishwa ni raia halali.

Hali kama hiyo inaweza pia kuongezeka endapo huduma katika zahanati, vituo vya afya na hospitali zitaboreshwa. Watu wengi wanaweza kujipatia uraia pacha (ambao haupo kisheria) kwa lengo tu la kufaidi huduma za kijamii katika Taifa letu.

Amani na utulivu katika nchi yetu, vikijumlishwa na ukarimu uliopitiliza wa Watanzania, ni sababu nyingine inayowavutia wageni wengi kuja kuishi hapa nchini.

Lakini wingi wa mali, hasa madini, ardhi nzuri ya kilimo na ya kufugia mifugo ya aina zote, ni chanzo kingine cha kuwafanya watu wengi zaidi kuja nchini mwetu.

Pamoja na hayo, vimelea vya rushwa na kupungua kwa uzalendo miongoni mwa wananchi ni sababu nyingine zinazochochea ongezeko la wahamiaji haramu na watu wanaoishi nchini mwetu kinyemela.

Zipo mbinu nyingi za kupambana na matatizo haya na mengine ambayo sikuyaainisha hapa. Lakini silaha kubwa kuliko zote inayopaswa kushikwa na kila Mtanzania katika moyo wake ni uzalendo. Uzalendo miongoni mwetu ndiyo silaha pekee yenye uwezo wa kuwatambua na kuwashughulikia wote wanaoishi nchini mwetu kinyume cha sheria.

Kwa miaka kadhaa Watanzania walipoteza moyo wa uzalendo. Hilo halikutokea kwa bahati mbaya. Lilitokea kwa sababu ya aina ya uongozi tuliokuwa nao, hasa miaka 10 hii iliyopita.

Daraja la watawala lilipoamua kuwa mbali na daraja la watawaliwa, makabwela hawakuona sababu nyingine, isipokuwa kuyaacha mambo yajiendeshe kadri ya kudra za Mwenyezi Mungu.

Kushuka kwa kiwango cha elimu, ada za kutisha katika shule na vyuo binafsi, tofauti za kipato, ukosefu wa huduma muhimu za kijamii-elimu, afya, maji, umeme na kadhalika; ni mambo yaliyowafanya wananchi wajione hawana lolote la kufaidi katika nchi yao.

Utapanyaji mali za umma uliofanywa na watawala, wizi, ufisadi na uhujumu wa rasilimali za nchi; ulisababisha wananchi wa kawaida nao waone hawana namna, isipokuwa kufaidi kila kilicho mbele yao hata kama ni kwa kuiba alama za barabarani au mifuniko ya mitaro ya maji machafu! Tukawa tumejenga nchi ya kila mtu kujitwalia kilicho karibu kadri awezavyo. Dereva anajilipa masurufu. Dereva anaiba mafuta-alimradi kila ‘mbuzi’ alihakikisha anakula kulingana na urefu wa kamba aliyofungwa.

Wananchi wanyonge wengi hawakuwa na haki mbele ya vyombo vya utoaji haki. Kabwela aliweza kuijua hukumu kabla haijatolewa mahakamani!

Tunajadili mauaji yanayofanywa na wananchi eti waliopewa jina la ‘watu wenye hasira kali! Mauaji mengi ya aina hii ni matokeo ya maskini waliokata tamaa au kuondosha imani yao kwenye vyombo vya utoaji haki.

Kama mtaani wanamkamata mtuhumiwa wa ujambazi, wanampeleka polisi, lakini ndani ya muda mfupi mtuhumiwa anarejea mtaani akitamba na hata kuwashughulikia waliomshitaki; nini kitawazuia safari nyingine wasimtoe uhai pindi akikamatwa kwa tuhuma zile zile au zinazofanana na hizo?

Zahanati, vituo vya afya na hospitali vikageuzwa kuwa vituo vya mkusanyiko wa wagonjwa waliopoteza matumaini au wale walioana ijulikane tu ‘wamefia hospitali’ kama ushahidi!

Hao maskini wakawaona watawala na watu wenye ukwasi wakienda kutibiwa ughaibuni kwa maradhi hata ya kawaida kabisa.

Nchi ya aina hiyo ambayo ilikosa usawa, uzalendo usingeweza kujengaka. Hata wale tunaounga mkono kurejeshwa kwa mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa vijana wa Tanzania, hatukuona kama mafunzo hayo yanaweza kweli kujenga uzalendo.

JKT ya miaka ile iliwajenga vijana hata wakawa wamoja na wapenda nchi yao kwa sababu walichohubiriwa ndicho walichokutana nacho kwenye uhalisia wa mambo katika maisha yao.

Walipoambiwa kuwa Tanzania si nchi ya matabaka, waliyaona hayo kwa vitendo. Watoto wa rais, watoto wa mawaziri, watoto wa wakurugenzi na wakubwa wengine walijumuika na watoto wa makabwela katika masuala mbalimbali. Kwa sasa tofauti zetu za maisha zinaanzisha mitaani na katika shule. Watoto hawachangamani. Matajiri wana sehemu zao. Maskini wana sehemu zao. Hawa wawili ni vigumu sana kufika mahali wakaungana kujenga uzalendo kwa lengo moja la kuijenga Tanzania mpya.

Ndiyo maana wapenda maendeleo ya nchi hii kwa sasa wameanza kujawa furaha pale wanapoona juhudi za Rais John Magufuli, za kuthubutu kuwafanya Watanzania kuwa moja kupitia haki na uwajibikaji.

Kuboresha elimu, huduma za afya, huduma za maji, barabara na nyingine ni mambo yanayowavutia mno wananchi, hasa maskini.

Haya yote hayatawezekana endapo vita hii itaachwa iwe ya rais, mawaziri, makatibu wakuu na watendaji wengine wa Serikali.

Vita ya kuijenga Tanzania mpya ni vita ya kila mzalendo katika nafasi yake.

Kama haki ya mwananchi ni kupata tiba sahihi, basi mwananchi huyo awe tayari kutekeleza wajibu wa kumsema hadharani na hata kumshitaki kunakostahiki, mhudumu au mtumishi anayejaribu kuukwaza mpango huo.

Tunaposema trafiki wanaomba na kupokea rushwa, hatuna budi kujiuliza ni mambo gani yanayowafanya trafiki wafanye hivyo? Je, wanadai rushwa kwa ubabe tu au ni kutokana na sisi wenye magari kukiuka sheria za usalama barabarani? Kama dereva hana kosa, kwanini akamatwe? Kama ana kosa, kwanini amlalamikie trafiki?

Wananchi hatuna budi kuwa wawazi na wakweli katika kusaidiana na viongozi wetu kwa ajili ya kuijenga Tanzania mpya. Malalamiko pekee hayatosaidia kuipata Tanzania tunayoitamani.

Juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano za kupambana na maovu zinapaswa ziungwe mkono. Ni jambo la faraja kuwasikia wananchi sasa wakisifu aina ya huduma katika zahanati, vituo vya afya, hospitali, vituo vya polisi na kwingineko.

Mabadiliko wanayoyataka hayawezi kuonekana mara moja kwa sababu nchi hii ilishafikia hatua mbaya. Kila kitu kilishakwenda ovyo. Rais Magufuli, hawezi kuwa na miujiza ya kuyamaliza hayo kwa miezi miwili, lakini kwa umoja wetu tunaweza kuushangaza ulimwengu.

Zipo dalili za wazi kuwa endapo wananchi watamuunga mkono, Tanzania yenye neema haipo mbali. Kwa umoja wetu tunaweza kabisa kuifanya Tanzania kuwa mahali pazuri pa kupigiwa mfano kimaendeleo.

Pamoja na nia yetu njema ya kuthamini haki za binadamu, bado tunao wajibu wa kuwatambua watu wasio raia ili haya yanayofanywa sasa na Serikali yawanufaishe Watanzania wenyewe kwanza. Kufanya hivyo si ubaguzi.

Majirani zetu na wale waliozoea kuifanya Tanzania shamba la bibi (tena aliyekufa) watapiga kelele. Tusibabaike. Kama Tanzania wameiona ni pepo inayowafaa, basi wafuate sheria. Kila mmoja wetu na ashiriki kutekeleza wajibu wake pale alipo.

Please follow and like us:
Pin Share