DIRA YA WIZARA:

Kuwa na uhakika wa milki za ardhi, nyumba bora na makazi endelevu kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

 

DHIMA:

Kuweka mazingira yanayofaa kuleta ufanisi katika utoaji wa huduma za ardhi, nyumba na makazi

 

MAJUKUMU:

 

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inayo majukumu yafuatayo:-

  • Kuandaa sera na mikakati ya uendelezaji wa sekta ya ardhi,

  • Kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi,

  • Kusimamia upangaji wa miji na vijiji,

  • Kupima ardhi na kutayarisha ramani,

  • Kutoa hati za kumiliki ardhi na hatimiliki za kimila,

  • Kusajili nyaraka za kisheria,

  • Kuthamini mali,

  • Kuhamasisha na kuwezesha wananchi kuwa na nyumba bora,

  • Kutatua migogoro ya ardhi na nyumba,

  • Kusimamia upatikanaji na utunzaji wa kumbukumbu za ardhi, Kusimamia ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali katika sekta ya ardhi,

  • Kusimamia Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Tume ya Taifa ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC), Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba na Vifaa vya Ujenzi (NHBRA),

  • Kusimamia uendeshaji wa Vyuo vya Ardhi vya Tabora na Morogoro,

  • Kusimamia maslahi na utendaji kazi wa watumishi wa sekta ya ardhi.

    Katika kutekeleza majukumu hayo, Wizara inaongozwa na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA II), Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 – 2015/16), Malengo ya Milenia (MDGs), Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2010, Mpango Mkakati wa Wizara (2012/13-2016/17), Sera ya Ardhi ya mwaka 1995, Sera ya Maendeleo ya Makazi ya mwaka 2000 na miongozo mbalimbali ya Serikali.


UTANGULIZI

1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba kutokana na taarifa iliyowasilishwa leo ndani ya Bunge lako Tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, Bunge lako likubali kupokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa kazi za Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika mwaka 2011/12 na malengo ya Wizara katika bajeti ya mwaka 2012/13. Aidha, naliomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2012/13.

2. Mheshimiwa Spika, awali ya yote ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia Waheshimiwa Wabunge kuwa na afya njema na hivyo kuweza kushiriki mkutano huu wa nane wa Bunge la Kumi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Naomba nitangulize dua zangu kwa Mwenyezi Mungu kuwa azipokee na kuzilaza pema roho za Waheshimwa Wabunge waliotangulia mbele ya haki tokea mkutano wa Bajeti wa mwaka 2011/12 ulipofanyika.

3. Mheshimiwa Spika, pili, naomba nitumie fursa hii kuwapongeza Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Mohammed Gharib Bilal, Makamu wa Rais; na Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda, Waziri Mkuu na Mbunge wa Mpanda Mashariki, kwa uongozi wao mahiri. Nawashukuru kwa ushauri, maelekezo na ushirikiano wanaonipa, ulioniwezesha kutekeleza majukumu niliyokabidhiwa ya kuongoza sekta hii muhimu katika maendeleo ya nyanja zote za maisha katika Taifa letu.

Nawapongeza kwa dhati Mheshimiwa Dkt. Ali Mohammed Shein Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi; pamoja na Makamu wake wawili Mhe. Maalim Seif Shariff Hamad, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar; na Mhe. Balozi Ali Idd Seif, Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar. Kwa namna ya pekee namshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa imani kubwa aliyoionesha kwangu kwa kuamua niendelee kuongoza Wizara hii ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wakati wa mabadiliko ya Baraza la Mawaziri aliyoyafanya mapema mwezi Mei 2012. Napenda kumhakikishia kuwa nitaendelea kujenga timu yenye nguvu ili kwa pamoja tujenge sekta ya ardhi yenye tija kwa kuzingatia sera, sheria, kanuni na taratibu.

4. Mheshimiwa Spika, nakupongeza kwa umahiri na umakini ambao umeonesha katika kuongoza shughuli za Bunge. Hongera sana, na Mwenyezi Mungu aendelee kukuongoza na kukupa hekima zaidi. Aidha, nampongeza Mheshimiwa Job Yustino Ndugai, Mbunge wa Kongwa na Naibu Spika wa Bunge letu kwa kazi nzuri katika kuendesha shughuli za Bunge. Pia, nawapongeza Waheshimiwa Wenyeviti Jenista Joakim Mhagama (Mbunge wa Peramiho), Sylivester Massele Mabumba (Mbunge wa Dole) na Mussa Zungu Azzan (Mbunge wa Ilala), kwa kuongoza vyema shughuli za Bunge tangu wachaguliwe kushika nyadhifa za uenyekiti.

5. Mheshimiwa Spika, naomba nichukue fursa hii kuwapongeza wafuatao kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais katika Baraza la Mawaziri kufuatia mabadiliko aliyoyafanya mwezi Mei 2012: Mhe. Dkt. William Augustao Mgimwa (Mb), kuwa Waziri wa Fedha; Mhe. Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo (Mb), kuwa Waziri wa Nishati na Madini; Mhe. Mhandisi Christopher Kajoro Chiza (Mb), kuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika; Mhe. Dkt. Harrison George Mwakyembe (Mb), kuwa Waziri wa Uchukuzi; Mhe. Dkt. Fenella Ephraim Mukangara (Mb), kuwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo; Mhe. Balozi Khamis Sued Kagasheki (Mb), kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii; Mhe. Dkt. Abdallah Omari Kigoda (Mb), kuwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko. Pia, napenda kuwapongeza wafuatao kwa kuteuliwa kuwa Naibu Mawaziri katika Wizara mbalimbali: Mhe. Janet Zebedayo Mbene (Mb), Wizara ya Fedha; Mhe. Saada Mkuya Salum (Mb), Wizara ya Fedha; Mhe. Dkt. Seif Suleiman Rashid (Mb), Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii; Mhe. George Boniface Simbachawene (Mb), Wizara ya Nishati na Madini; Mhe. January Yusuf Makamba (Mb), Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia;

Mhe. Dkt. Charles John Tizeba (Mb), Wizara ya Uchukuzi; Mhe. Amos Gabriel Makalla (Mb), Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo; Mhe. Angela Jasmine Kairuki (Mb), Wizara ya Katiba na Sheria; Mhe. Stephen Julius Maselle (Mb), Wizara ya Nishati na Madini; na Mhe. Mhandisi Dkt. Binilith Satano Mahenge (Mb), Wizara ya Maji. Vilevile, nawapongeza Waheshimiwa Wabunge wote waliochaguliwa na walioteuliwa katika kipindi cha mwaka uliopita kuwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Waheshimiwa Wabunge waliochaguliwa kuiwakilisha Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki na Bunge la Afrika. Ni matumaini yangu kuwa watatuwakilisha vyema kwa maslahi na manufaa ya Taifa letu.

6. Mheshimiwa Spika, napenda nitumie fursa hii kuwashukuru kwa dhati wananchi wa Jimbo la Muleba Kusini kwa kunipa ushirikiano wa karibu katika kutimiza majukumu yangu nikiwa Mbunge wao. Pamoja na kuwa na kazi nyingi za kitaifa, wananchi wa Jimbo la Muleba Kusini wamekuwa wakinipa ushirikiano mzuri na kujitahidi kukutana nami ninapopata nafasi kufika jimboni kwa kuhudhuria vikao na mikutano katika tarafa zao au kupokea wageni na wataalaam waelekezi ninaowatuma kufika kusukuma maendeleo yetu. Ninawashukuru sana kwa uelewa na ushirikiano, na uongozi madhubuti wa madiwani na wenyeviti wa vijiji kuunda Mifuko ya Maendeleo ya Kata ambayo italeta mapinduzi katika kupunguza umaskini na kutuletea maendeleo endelevu.

Ninawapongeza Madiwani ambao tayari wamesajili taasisi ya mifuko hiyo katika kata za Mubunda, Kyebitembe, Rulanda, Muleba, Bureza, Magata Karutanga, Kimwani, Mazinga, Nyakabango, Nshamba, Kishanda, Buganguzi, Burungura, Buhangaza, Kashasha, Ijumbi, Biirabo na Muleba Mjini. Ninawahimiza wale ambao bado hawajakamilisha zoezi hili wakazane tusonge mbele kwa pamoja. Aidha, natuma salamu kwa vijana wanaoshiriki katika mashindano ya kandanda ya Kombe la Anna Tibaijuka. Ninawapongeza wale ambao wameshinda mashindano ya kata na ninaamini mwisho wa mwaka tutakapocheza fainali washindi wataweza kutoa vijana wa Muleba kujiunga na Taifa Stars. Nimefurahi kusikia kwamba na wasichana hawakubaki nyuma wameitikia wito wangu na kushiriki michezo ya riadha inayotangulia mashindano ya mpira.

Vijana michezo ni maendeleo. Kwa wenye vipaji, Muleba tusikubali vijana wetu kubaki nyuma kwa kuwa tu tuko mbali na majiji makubwa nchini hususan Dar es Salaam. Kwa kupitia ligi yetu, wenye uwezo wataibuka na kung’ara na kusonga mbele. Aidha, ninawashukuru ndugu, jamaa na marafiki walionisaidia na kunipa ushirikiano wa karibu katika kutimiza majukumu ya Uwaziri na Ubunge.

Nawashukuru wananchi na kuwahakikishia popote pale mlipo, iwe Tarafa ya Nshamba, Kimwani au Muleba yenyewe, kwamba tutayalinda mafanikio tuliyoyafikia na kuongeza kasi zaidi ili kufikia malengo ya kulinda amani, utulivu na kufikia maisha bora. Namuomba Mwenyezi Mungu amwezeshe kila mwananchi kulitambua hili na kuchangia katika nafasi yake kwa kadri ya uwezo wake kufikia maisha bora. Mwisho ninatuma salamu kwa mama yangu mzazi Ma Aulelia Kajumulo hapo Muleba. Sala zake za kila siku anapokuwa na nguvu zinasikika maana huku mie ni mzima wa afya.

7. Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru kwa dhati viongozi wote wa Chama cha Mapinduzi (CCM), viongozi na watendaji wa Serikali kwa kuniwezesha kutekeleza majukumu ya Wizara yangu. Kwa namna ya kipekee natoa shukurani zangu za dhati kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mheshimiwa James Daudi Lembeli (Mbunge wa Kahama), kwa ushirikiano mkubwa na ushauri wao ambao umeiwezesha Wizara kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi. Natoa shukurani za pekee kwa Naibu Waziri, Mheshimiwa Goodluck Joseph Ole-Medeye (Mbunge wa Arumeru Magharibi) kwa ushirikiano na umoja tuliojenga kutekeleza majukumu yetu na pia nampongeza kwa Mhe. Rais kuamua aendelee na wadhifa wake huo.

Nawashukuru pia Katibu Mkuu Bw. Patrick Rutabanzibwa; Naibu Katibu Mkuu, Bibi Maria Bilia; watendaji katika Idara, Vitengo, Shirika na Taasisi zilizo chini ya Wizara kwa ushauri na mshikamano wao katika kupanga na kutekeleza mipango ili kufikia malengo tuliyojiwekea. Watanzania wengi wanatambua changamoto kubwa zinazoikabili sekta yetu lakini hakuna kinachoshinda umoja, maana ni nguvu ya pekee.

CHANGAMOTO ZINAZOIKABILI SEKTA YA ARDHI

8. Mheshimiwa Spika, ongezeko la mahitaji ya ardhi kwa matumizi mbalimbali haliepukiki kutokana umuhimu wake kijamii na kiuchumi. Ili kuwezesha wananchi na wawekezaji kupata ardhi wanayohitaji, Wizara imeweka vipaumbele katika kupanga matumizi ya ardhi kwa kuzingatia mazingira na mahitaji halisi, kujenga mfumo utakaorahisisha upimaji na kupunguza gharama za kupima ardhi, kumilikisha ardhi kwa haki, pamoja na kulinda haki za wamiliki halali wa ardhi. Katika kufikia malengo hayo Wizara inakabiliwa na changamoto zifuatazo:-

i) Kubadilisha utunzaji wa kumbukumbu za sekta ya ardhi kutoka mfumo usio unganishi kwenda kwenye mfumo unganishi wa ki-elektroniki;

ii) Kukosekana kwa ardhi iliyopangwa na kupimwa kwa ajili ya matumizi mbalimbali mijini na vijijini ikilinganishwa na mahitaji;

  1. iii)  Kuwepo kwa kasi ndogo ya kutoa elimu kwa umma kuhusu sera, sheria na kanuni za uendelezaji ardhi, nyumba na makazi;

  2. iv)  Kukosekana kwa rasilimali za kutosha kwa ajili ya utayarishaji wa mipango ya matumizi ya ardhi, upangaji wa miji na upimaji wa ardhi nchini;

  3. v)  Kukosekana kwa mipango jumuishi ya kuwezesha kupungua kwa gharama za ujenzi wa nyumba bora mijini na vijijini;

vi) Kuwepo kwa uwezo mdogo wa utekelezaji na usimamizi wa sera na sheria za ardhi unaosababisha   kuwepo kwa ongezeko la ujenzi holela na uvamizi wa maeneo yaliyotengwa kwa matumizi mbalimbali ya jamii mijini na vijijini;

  1. vii)  Kuongezeka kwa migogoro ya ardhi na nyumba mijini na vijijini;

  2. viii)  Kuwepo kwa upungufu mkubwa wa watumishi, vitendea kazi na miongozo ya sekta ya ardhi katika ngazi ya Halmashauri;

    ix)  Nakishi ya bajeti inayotengwa kwa sekta ya ardhi na makazi; na

  1. x)  Kuwepo kwa utamaduni ambao bado hauzingatii mfumo wa ubananaji wa makazi ya mijini na kasi yake vinavyolazimisha kuheshimu sheria na taratibu za mipango miji.

9. Mheshimiwa Spika, hizo ni baadhi ya changamoto zinazokwamisha uendelezaji wa dhana halisi za upangaji, upimaji na utawala wa ardhi. Ili kukabiliana na changamoto hizo Wizara imepanga kuchukua hatua zifuatazo:

i) Kuendelea kujenga mfumo unganishi wa ki-elektroniki wa kuhifadhi kumbukumbu za ardhi (Integrated Land Management Information System) utakaowezesha upatikanaji na utumiaji wa kumbukumbu za sekta ya ardhi kwa ufanisi;

ii) Kuanza utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Matumizi ya Ardhi (National Land Use Framework Plan) kwa kuongeza kasi ya kupanga na kuandaa mipango ya jumla na ya kina na upimaji wa ardhi;

  1. iii)  Kuendelea kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi nchini hususan katika vijiji vilivyopo mipakani;

  2. iv)  Kuendelea na mchakato wa kuanzisha Wakala wa Hazina ya Ardhi (National Land Bank Agency) na Mfuko wa Fidia ya Ardhi (Land Compensation Fund);

  3. v)  Kuandaa na kutekeleza mpango wa mahitaji ya mafunzo kwa kamati mbalimbali za usimamizi wa ardhi nchini na programu ya elimu kwa umma kuhusu sera, sheria na kanuni za ardhi, nyumba na makazi;

  4. vi)  Kuendelea na mchakato wa kujenga kituo cha kupokea picha za satellite ili kurahisisha utayarishaji wa mipango ya matumizi ya ardhi, upangaji wa miji na upimaji wa ardhi nchini;

  5. vii)  Kubuni mfumo shirikishi wa uendelezaji wa ardhi nchini ambapo watoa huduma wote watashirikishwa katika dhana ya sites and services.

  6. viii)  Kuongeza kasi ya kueneza matokeo ya utafiti unaofanywa na Wakala wa Utafiti wa Nyumba na Vifaa vya Ujenzi (NHBRA) na kuanzisha vikundi vya ujenzi katika ngazi ya Halmashauri na kutoa mafunzo kwa ajili ya ujenzi wa nyumba bora na vifaa vya ujenzi;

ix) Kuhakikisha Shirika la Nyumba la Taifa linaendelea kujenga nyumba za kutosha kwa ajili ya kuuza na kupangisha kwa watu wa vipato mbalimbali na kuhimiza Halmashauri kuanzisha vitengo vya nyumba katika Halmashauri zao, yaani Council Housing pamoja na kuhamasisha sekta binafsi na vyama vya ushirika wa nyumba (Housing Cooperatives) kujenga nyumba za kuuza na kupangisha kwa gharama nafuu;

  1. x)  Kuendelea kutekeleza Programu ya Taifa ya Kurasimisha na Kuzuia Makazi Holela Mijini kwa kushirikiana na Halmashauri;

  2. xi)  Kuandaa utaratibu utakaowezesha mamlaka za upangaji kuweka mfumo wa udhibiti na uendelezaji wa ardhi katika ngazi ya Kata;

  3. xii)  Kuendelea kuimarisha vyombo vya kusimamia maadili na weledi wa wataalam wa sekta ya ardhi katika ngazi zote;

  1. xiii)  Kuendelea kuunda na kuimarisha Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa;

  2. xiv)  Kubuni mbinu mpya za kisasa kupata fedha za kuendelea shughuli za Wizara nje ya bajeti kuu ya Serikali (extra- budgetary financing mechanisms) na Serikali za Mitaa, hususan kupitia mikopo ya benki au hisa za makazi (municipal bonds);

  3. xv)  Kutoa elimu kwa umma kuhusu mabadiliko ya mfumo wa makazi kutoka vijijini kwenda mjini na umuhimu wa mabadiliko ya utamaduni, mila na desturi na tabia zinazoendana na hali hiyo.

MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2011/12 NA MALENGO YA MWAKA 2012/13

Ukusanyaji wa Mapato

10. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12 Wizara ilikuwa na lengo la kukusanya jumla ya Shilingi bilioni 23.6 kutokana na vyanzo mbalimbali vya mapato katika sekta ya ardhi. Hadi Juni, 2012 jumla ya Shilingi bilioni 17.1 ambazo ni sawa na asilimia 72.5 ya lengo zilikusanywa. Upungufu wa makusanyo ya maduhuli ulitokana na baadhi ya changamoto nilizozieleza hapo awali.

11. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2012/13 Wizara imeweka lengo la kukusanya Shilingi bilioni 99.8. Maduhuli haya yatakusanywa kwa kutumia mikakati ifuatayo: kuongeza kodi ya ardhi na tozo; kuimarisha utunzaji wa kumbukumbu za ardhi; kupanga, kupima na kumilikisha maeneo mapya; kukamilisha upimaji na umilikishaji wa viwanja kwenye maeneo ambayo upimaji wake haujakamilika; kuhamasisha wananchi kulipa kodi ya ardhi; na kuwachukulia hatua za kisheria wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi. Naomba nitumie fursa hii kuhimiza wananchi kulipa kodi ya pango la ardhi na tozo nyingine kwa mujibu wa sheria ili kuepuka usumbufu wa kushitakiwa mahakamani, kunyang’anywa ardhi na kulipa faini. Nasisitiza kwamba muda wa kuvumiliana na wa visingizio umekwisha.

Matumizi

12. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12 Wizara iliidhinishiwa jumla ya Shilingi bilioni 50.89. Kati ya fedha hizo Shilingi bilioni 9.3 sawa na asilimia 18 ya fedha zilizoidhinishwa zilitengwa kwa ajili ya mishahara, Shilingi 19.6 sawa na asilimia 39 zilitengwa kwa ajili ya matumizi mengineyo na Shilingi bilioni 21.9 sawa na asilimia 43 zilitengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Hadi Juni, 2012 jumla ya fedha zilizopatikana ni Shilingi bilioni 34.65 sawa na asilimia 68.1 ya fedha zilizoidhinishwa, na jumla ya Shilingi bilioni 34.45 zilitumika. Kiasi kilichotumika ni sawa na asilimia 99.4 ya fedha zilizopatikana. Kati ya fedha zilizotumika Shilingi bilioni 8.96 zilitumika kwa ajili ya mishahara, Shilingi bilioni 19.49 kwa ajili ya matumizi mengineyo, na Shilingi bilioni 6.0 kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Fedha za maendeleo zilizopatikana zilikuwa sawa na asilimia 28 tu ya bajeti ya miradi ya maendeleo (Jedwali Na. 1).

UTAWALA WA ARDHI

13. Mheshimiwa Spika, Watanzania wote wanatambua mchango mkubwa ambao rasilimali ardhi inatoa katika kukuza uchumi wa nchi yetu. Kutokana na umuhimu huo, Wizara yangu imeendelea na jukumu la kuhakikisha usalama wa milki kwa kutoa hati, kukagua na kuhakiki milki. Majukumu mengine ni pamoja na kutwaa ardhi kwa manufaa ya umma na kubatilisha milki kwa wanaokiuka masharti ya milki zao. Vilevile, Wizara inatoa elimu na miongozo kuhusu sera, sheria na kanuni za ardhi. Pia, inatoa vibali vya uhamisho wa milki na kuratibu utoaji wa Vyeti vya Ardhi ya Kijiji na Hati za Hakimiliki ya Kimila kwa kushirikiana na mamlaka ya serikali za mitaa nchini.

14. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria za Ardhi, mamlaka za ugawaji wa ardhi ziko katika ngazi tatu za vijiji; Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji; na Taifa. Majukumu ya mamlaka hizi yameainishwa katika Sheria ya Ardhi Na. 4 ya mwaka 1999, Sheria ya Ardhi ya Vijiji Na. 5 ya mwaka 1999 na Kanuni za sheria hizo. Kwa mujibu wa Kanuni ya 76 ya Kanuni za Sheria ya Ardhi ya Vijiji, Halmashauri ya Kijiji ina uwezo wa kugawa ardhi kwa mwanakijiji au mtu yeyote ilimradi awe ni raia wa Tanzania na ardhi iwe na ukubwa usiozidi hekta 21. Halmashauri ya Wilaya, kupitia kamati yake ya kugawa ardhi, ina mamlaka ya kugawa ardhi ya Kijiji yenye ukubwa wa kati ya hekta 21 na 50.

Ardhi ya Kijiji yenye ukubwa wa zaidi ya hekta 50 inagawiwa kwa ridhaa ya Kamishna wa Ardhi. Kwa upande wa ardhi ya kawaida Halmashauri ya Kijiji inaruhusiwa kugawa ardhi yenye ukubwa usiozidi hekta 21. Halmashauri ya Wilaya inaruhusiwa kugawa ardhi yenye ukubwa wa kati ya hekta 21 na hekta 202. Mapendekezo ya kugawa ardhi katika fukwe, visiwa vidogo na kwa ajili ya uwekezaji kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) yanatakiwa yawasilishwe kwenye Kamati ya Taifa ya Kugawa Ardhi ambayo mwenyekiti wake ni Kamishna wa Ardhi.

Wajumbe wa Kamati hiyo wanatoka Wizara za Ulinzi, Kilimo, Mifugo na Viwanda, na Tume ya Mipango. Kamati hiyo huteuliwa na Waziri wa Ardhi. Hata hivyo, pamoja na sheria kuonesha bayana majukumu ya mamlaka husika, kumekuwepo tabia ya baadhi ya mamlaka kugawa ardhi inayozidi mamlaka yake. Aidha, baadhi ya mamlaka zikiwemo za vijiji zimekuwa zikitoa ardhi kwa waombaji ambao si raia wa Tanzania, kinyume cha sheria. Tabia hii husababisha migogoro na hasara kwa waliopewa ardhi bila kufuata utaratibu. Kupitia Bunge lako Tukufu naziagiza mamlaka za vijiji na Halmashauri kufuata sheria, kanuni na taratibu za kugawa ardhi ili kuepusha malalamiko na migogoro isiyo ya lazima.

Nasisitiza kuwa ardhi kwa ajili ya wawekezaji hutolewa na Kamishna wa Ardhi kwa mamlaka ambayo yako chini ya Rais. Hakuna tena njia nyingine ya kugawa ardhi nje ya utaratibu huu. Ukiwa na ardhi yako ukaamua kumpa mtu mwingine huna budi kuirudisha kwa Kamishna (surrender) ili igawiwe upya kwa mtu mwingine. Tofauti ni kuhamisha miliki yote ya ardhi yako kwa mtu mwingine kwa kumuuzia. Makubaliano yanayofanyika kati ya Halmashauri na Wawekezaji au Wamiliki wengine na wawekezaji nje ya utaratibu huu ni batili, sharti yapate baraka za Kamati ya Kugawa Ardhi ya Taifa kabla hatimiliki mpya hazijatolewa.

Utoaji Milki

15. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12 Wizara ilikuwa na lengo la kutoa hatimiliki 21,000. Hadi kufikia Juni, 2012 Wizara ilitoa hatimiliki 23,610 sawa na asilimia 112.4 ya lengo (Jedwali Na.2). Kwa mwaka 2012/13 Wizara yangu inatarajia kutayarisha na kutoa hatimiliki 40,000. Natoa wito kwa Halmashauri zote nchini kuhakikisha kuwa zinamilikisha viwanja vyote vilivyopimwa na kuandaa hati ili wananchi waweze kuwa na milki salama.

16. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12 Wizara yangu iliahidi kufungua Ofisi ya Ardhi ya Kanda ya Magharibi mjini Tabora itakayohudumia Mikoa ya Tabora, Katavi, Shinyanga na Kigoma. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa, Jengo la Ofisi limepatikana mjini Tabora na ofisi hiyo itaanza kutoa huduma mwaka huu wa fedha. Huduma hizo ni za mipangomiji na vijiji, upimaji, umilikishaji, usajili, uthamini na ushauri kuhusu utatuzi wa migogoro ya ardhi na nyumba.

Utwaaji, Ubatilishaji na Uhamisho wa Milki

17. Mheshimiwa Spika, Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 inatambua kuwa ardhi yote ni mali ya umma hivyo mfumo wa kumiliki ardhi ni ule wa haki ya kutumia na siyo kuhodhi. Kwa maana hiyo, kila anayemilikishwa ardhi ana wajibu wa kuiendeleza kwa matumizi yaliyopangwa na asipofanya hivyo hatua za kufuta milki hizo zitachukuliwa na kurudisha ardhi husika mikononi mwa Mheshimiwa Rais. Aidha, kwa mujibu wa Sheria ya Utwaaji Ardhi, Na. 47 ya mwaka 1967 (Sura ya 118) pale ambapo ardhi itahitajika kwa manufaa ya umma itatwaliwa kwa mujibu wa sheria hii. Utaratibu wa utwaaji na ubatilishaji unaanzia ngazi ya Halmashauri hadi ngazi ya Taifa.

Katika kutekeleza majukumu haya kwa mwaka 2011/12, ilani za ubatilisho zilizotumwa ni 792 na jumla ya milki 72 zilibatilishwa na kutwaliwa na milki 1,512 zilihamishwa. Kwa mwaka 2012/13 Wizara yangu itaendelea kutwaa ardhi na kubatilisha milki kwa mujibu wa sheria na inatarajia kushughulikia maombi 1,700 ya uhamisho wa milki. Ili kuhakikisha kuwa ardhi inatumika kwa ufanisi natoa agizo kwa Halmashauri zote nchini kuwasilisha Wizarani taarifa za viwanja na mashamba yaliyotelekezwa au kutumika kinyume na masharti ya milki ili taratibu za kubatilisha milki ziweze kuchukuliwa.

Utekelezaji wa Sheria ya Ardhi ya Vijiji

18. Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji wa Sheria ya Ardhi ya Vijiji Na. 5 ya 1999, Wizara yangu inaendelea kutoa elimu kwa wananchi, kupima na kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji, kuhakiki mashamba na kuratibu utoaji wa Vyeti vya Ardhi ya Kijiji na Hati za Hakimiliki ya Kimila. Utoaji wa Vyeti vya Ardhi ya Vijiji unaviwezesha vijiji kutambua maeneo yao kiutawala na kuwezesha upangaji wa matumizi ya ardhi. Vilevile, utoaji wa hati za hakimilki za kimila unawezesha wananchi kuwa na milki salama, na kuwawezesha kutumia ardhi kama mtaji, hivyo kuwawezesha kujiletea maendeleo.

19. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12 Wizara yangu iliweka lengo la kutoa Vyeti 3,732 vya Ardhi ya Kijiji. Hadi Juni 2012 ilitoa Vyeti vya Ardhi ya Kijiji 1,950. Idadi hii inafanya jumla ya Vyeti vya Ardhi ya Kijiji vilivyotolewa kufikia 9,460 kati ya vijiji 11,817 vilivyosajiliwa nchini. Pia, Wizara iliandaa, kusajili na kutoa Hati za Hakimilki ya Kimila 21,169 kati ya lengo la hati 45,000 (Jedwali Na.3).

Natoa pongezi kwa Halmashauri zote zinazoendelea na utekelezaji wa Sheria ya Ardhi ya Vijiji ya mwaka 1999 kwa kutenga fedha kwa ajili ya uhakiki na upimaji wa mashamba pamoja na utoaji wa hatimilki za kimila kwa wananchi. Halmashauri hizo ni: Moshi Vijijini, Mwanga, Hai, Babati, Nachingwea, Ruangwa, Lindi Vijijini, Mtwara Vijijini, Masasi, Newala na Nanyumbu. Halmashauri nyingine ni Kasulu, Kigoma Vijijini, Kibondo, Bunda, Kilolo, Iringa Vijijini, Ludewa, Njombe, Mpanda na Singida Vijijini.

Natoa wito kwa Halmashauri za Wilaya zote nchini kuiga mfano huu kwa kutenga fedha kwa ajili ya kupima na kuhakiki mashamba ya wananchi na kuwamilikisha. Nawaomba Waheshimiwa Wabunge kwa nafasi zao kama wajumbe wa Baraza la Madiwani kuhamasisha wananchi kudai kumilikishwa ardhi yao na kuhimiza Halmashauri za Wilaya zao kutoa huduma za upangaji, upimaji na umilikishaji wa ardhi kwa wananchi. Napenda kuwahakikishia ushirikiano kutoka Wizara yangu mtakapohitaji.

20. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2012/13, Wizara yangu itakamilisha utayarishaji na utoaji wa Vyeti vya Ardhi ya Vijiji kwa vijiji 2,007 vilivyopimwa. Pia, Wizara yangu kwa kushirikiana na MKURABITA, Halmashauri za Wilaya, na wadau wengine itaendelea kuratibu utayarishaji na utoaji wa Hati za Hakimiliki za Kimila 50,000 nchini.

Usajili wa Hati na Nyaraka za Kisheria

21. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu ilipanga kusajili nyaraka za kisheria 60,000 katika mwaka 2011/12. Hadi kufikia mwezi Juni 2012, nyaraka za kisheria 64,632 zilisajiliwa. Kati ya nyaraka zilizosajiliwa, 27,452 ni hatimiliki na 28,990 ni nyaraka nyingine zilizosajiliwa chini ya Sheria ya Usajili wa Ardhi (Sura ya 334) (Jedwali Na. 4a). Vilevile, nyaraka 7,280 zilisajiliwa chini ya Sheria ya Usajili wa Nyaraka (Sura ya 117) (Jedwali Na. 4b) na nyaraka 910 zilisajiliwa chini ya Sheria ya Usajili wa Rehani ya Mali Zinazohamishika (Sura ya 210). Kwa mwaka 2012/13, Wizara inakusudia kusajili hatimiliki na nyaraka za kisheria 75,000. Kati ya hatimiliki na nyaraka hizo, 35,000 zinatarajiwa kuwa hatimiliki na 40,000 ni nyaraka nyingine za kisheria.

22. Mheshimiwa Spika, wananchi wanahamasishwa kupima maeneo yao na kupata hatimiliki, kwani hati hizi zina umuhimu mkubwa ni pamoja na kuwawezesha kutumia kama dhamana za mikopo kwenye taasisi za kifedha na kuepusha migogoro ya ardhi. Natoa rai kwa wananchi kufanya uhakiki kwenye ofisi za usajili wa hati wanapokusudia kufanya miamala inayohusu ardhi. Hii itasaidia kuwaepusha na wimbi la utapeli ambao umepelekea kuwepo kwa hatimiliki za kughushi.

Uthamini wa Mali

23. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inahusika kufanya na kuidhinisha taarifa za uthamini wa mali zinazohamishika na zisizohamishika na kusimamia utendaji wa taaluma nchini. Uthamini wa mali unafanyika ili kuwezesha maamuzi ya miamala mbalimbali ya mali kufanyika. Zipo aina kuu mbili za uthamini ambazo ni Uthamini wa Ujumla na Uthamini wa Kisheria. Uthamini wa Ujumla ni ule unaofanyika kwa kuzingatia misingi ya kitaaluma na hazina maelekezo maalum ya kisheria. Mifano ni uthamini kwa ajili ya kuwezesha maamuzi ya mauzo au manunuzi ya mali, kuweka mali rehani, kuomba mikopo benki, dhamana ya mahakama, mizania, na bima. Uthamini wa Kisheria ni ule ambao pamoja na misingi ya kitaaluma unazingatia maelekezo maalum ya sheria mahsusi ya Bunge kwa mfano ni uthamini kwa ajili ya fidia,

kukadiria kodi za mapato, ushuru wa serikali, kodi za majengo na kodi za viwanja.

24. Mheshimiwa Spika, uthamini wa mali unategemea maombi yanayowasilishwa kutoka kwa wadau mbalimbali ambao ni taasisi za umma, makampuni na watu binafsi. Hata hivyo, katika mwaka 2011/12 Wizara yangu ililenga kufanya na kuidhinisha taarifa za uthamini wa Jumla wa mali zipatazo 13,000. Hadi Juni 2012 wizara iliidhinisha taarifa za uthamini 11,445 ambazo kati yake taarifa 1,507 ziliandaliwa na Wizara na 9,938 zilipokelewa kutoka kampuni binafsi za uthamini na Halmashauri za Miji na Wilaya (Jedwali Na.5). Kwa mwaka 2012/13 Wizara yangu imelenga kuthamini na kuidhinisha taarifa za uthamini wa mali zipatazo 14,000 kwa madhumuni mbalimbali.

25. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu pia inaandaa na kuidhinisha taarifa za uthamini, hususan uthamini kwa ajili ya ulipaji fidia kwa wananchi wanaoguswa na utekelezaji wa miradi yenye manufaa kwa umma. Katika mwaka wa fedha 2011/12, Wizara imeidhinisha taarifa za uthamini wa mali 11,256 ikilinganishwa na lengo la 9,000 la walioguswa na miradi ya kitaifa iliyojumuisha uwekezaji kwenye maeneo ya migodi katika vijiji vya Katoma na Nyamalembo Wilayani Geita, Nyamongo North Mara na Nyalanguru Wilayani Tarime; uwekezaji kwenye eneo la mtambo wa gesi asilia huko Mnazi Bay na njia ya bomba la gesi eneo la Somanga-Kilwa. Pia, uthamini ulifanyika kwenye eneo linalotarajiwa kumilikishwa kwa Kampuni ya Ecoenergy kwa ajili ya uwekezaji wa kilimo cha miwa na kiwanda cha sukari lililoko kijiji cha Makurunge Wilayani Bagamoyo. Vilevile, maeneo ya barabara chini ya TANROADS zinazojumuisha barabara za Babati- Singida, Dumila-Rudewa na Mangaka- Nanyumbu-Mtambaswala; na maeneo ya miradi ya upimaji viwanja Wilaya za Masasi na Mtwara.

Kwa mwaka 2012/13 Wizara imelenga kufanya uthamini wa fidia kwa mali zipatazo 15,000 kutokana na miradi mbalimbali itakayokuwa inatekelezwa nchini ikiwepo mradi wa kuendeleza eneo la Kigamboni na mradi wa ujenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Biashara Kurasini, Jijini Dar es Salaam.

26. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu ni msimamizi wa taaluma ya uthamini. Imeendelea na jukumu la kujenga Hazina ya Takwimu za Uthamini (Valuation Database) kwa lengo la kuwa na takwimu madhubuti za ukokotoaji wa thamani ya ardhi, majengo, mazao na mimea kwa kiwango cha soko. Katika mwaka 2011/12, Wizara yangu kwa kushirikiana na Halmashauri iliandaa viwango elekezi vya thamani ya ardhi katika Miji 10 ambayo ni Jiji la Dar es Salaam, Mbeya, Tanga na Arusha; Manispaa ya Morogoro, Iringa, Sumbawanga, Lindi na Bukoba na Halmashauri ya Mji wa Kibaha. Ili kuwajengea uwezo na kuimarisha ushiriki wa wathamini katika zoezi la kujenga Hazina ya Takwimu za viwango vya thamani vya soko, Wizara iliendesha mafunzo kwa wathamini katika Kanda za Mashariki (Dar es Salaam), Kaskazini, (Moshi), Ziwa (Mwanza) na Kusini Magharibi (Mbeya).

27. Mheshimiwa Spika, zoezi la kuhuisha viwango vya thamani ni la kudumu na litaendelea kila mwaka kwa vile thamani ya ardhi na majengo katika soko hubadilika kutokana na sababu mbalimbali za kiuchumi na kijamii kwa kadri miaka inavyopita. Kwa mwaka 2012/13, Wizara yangu itaendelea kuandaa viwango elekezi kwa miji ya mikoa 11 sambamba na uchambuzi wa kina wa takwimu kwenye miji yenye viwango elekezi. Aidha, Wizara itaanda mfumo wa uthamini wenye uwezo wa kutunza, kuchambua na kutoa taarifa ya takwimu hizo kwa wadau mbalimbali wa huduma za uthamini na kuhuisha viwango hivyo kwa kuzingatia mwenendo wa soko la mali.

Ni matumaini yangu kuwa, Wataalam wa uthamini nchini watatumia ujuzi walioupata kutokana na mafunzo hayo kushiriki kikamilifu katika zoezi la kujenga mifumo ya kukusanya, kutunza na kutumia takwimu za viwango vya thamani katika maeneo yao. Vilevile, nazishauri Halmashauri za Miji na Wilaya zote nchini kutenga fedha kwa ajili ya kuwawezesha wataalam wa uthamini kutekeleza majukumu yao hususan hili la kusimika viwango vya thamani ya ardhi na mazao katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri zao.

Kuanzishwa kwa Hazina ya Ardhi (Land Bank)

28. Mheshimiwa Spika, ili ardhi iweze kuingizwa kwenye hazina ya ardhi, ni lazima ardhi hiyo iwe imepangwa, imepimwa na imesajiliwa na haina mgogoro kuhusu umiliki wala matumizi yake; na iwe na ukubwa wa kutosha kulingana na matumizi yaliyokusudiwa. Kwa mwaka 2011/12 Wizara iliahidi kuanzisha chombo kwa ajili ya kusimamia Hazina ya Ardhi na kuanzisha Mfuko wa Fidia ya Ardhi. Kazi hiyo imeanza, na kwa mwaka 2012/13 Wizara inatarajia kukamilisha uanzishaji wa chombo hicho na Mfuko wa Fidia ya Ardhi.

Chombo hicho kitasimamia utoaji wa ardhi kwa wawekezaji wa ndani na nje kwa misingi ya kuingia ubia wa kumiliki pamoja hisa kati ya wananchi na wawekezaji hao (land for equity), ambapo hisa zitatolewa kwa uwiano na thamani ya mtaji wa mwekezaji (Invested value method of land valuation). Lengo ni kuhakikisha kuwa wananchi wananufaika zaidi na ardhi katika maeneo yao, na kuongeza usalama wa miradi ya wawekezaji (Sustainability of extensive land- based investments).

Kiwango cha chini cha hisa za Serikali katika ubia huo kitakuwa asilimia 25, na kati ya hizo mapendekezo ni kwamba angalau asilimia 5 zitagawiwa kwa Halmashauri yenye eneo hilo, asilimia 5 zitauzwa kwa bei ya soko kwa wananchi watakaotaka kushiriki katika miradi husika. Natoa wito kwa Bunge lako Tukufu kuunga mkono utaratibu mpya wa kutoa ardhi kwa wawekezaji kwa msingi wa kugawana hisa utakaofuta taratibu zinazotumiwa na Halmashauri na Vijiji kwa sasa za kupewa gawio lisilozingatia msingi ya kichumi, kwa mfano wawekezaji kutoa zawadi ndogondogo kama visima vya maji, madarasa na kadhalika. Taratibu zitakapokamilika tutawasilisha muswada wa sheria ya kuanzisha rasmi chombo hicho.

KUMBUKUMBU ZA ARDHI NA TEKNOLOJIA YA HABARI NA MAWASILIANO

29. Mheshimiwa Spika, katika Hotuba yangu ya mwaka 2011/12 niliahidi kuendelea na zoezi la kuweka mfumo wa kompyuta kwa ajili ya kukusanya kutunza na kukadiria kodi ya pango la ardhi kwenye Halmashauri kumi, pamoja na kuunganisha Ofisi za Ardhi za Kanda za Kaskazini na Ziwa kwenye mtandao wa kompyuta wa Wizara na kuweka mfumo mmoja wa ki-elektroniki.

Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba hadi kufikia Juni 2012, Wizara yangu ilikuwa imekamilisha kuweka mfumo ya kompyuta wa Land Rent Management System – LRMS katika Ofisi za Ardhi za Halmashauri kumi na moja (11) za Hanang, Njombe, Makambaku, Same, Hai, Mbeya (W), Muheza, Kilosa, Masasi, Mpanda na Manispaa ya Dodoma na kutoa mafunzo kwa watumiaji wa mfumo huo. Sambamba na hilo mfumo wa kompyuta wa LRMS wa vituo 17 kati ya 29 iliboreshwa. Vituo hivyo ni pamoja na Jiji la Mbeya, Mwanza, Tanga, Arusha Manispaa za Bukoba, Sumbawanga, Kigoma, Singida, Songea, Moshi, Shinyanga, Mji wa Babati, Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Kilombero, Kahama, Bagamoyo na Kibaha. Aidha, Wizara imesaini mkataba na mtaalam mshauri atakayesanifu na kusimika mfumo unganishi wa kuhifadhi kumbukumbu za ardhi Integrated Land Management Information System – ILMIS. Mtaalam huyo anatarajiwa kukamilisha kazi hiyo katika kipindi cha miezi 24.

30. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Wizara itaendelea na kazi ya kujenga mfumo wa ILMIS. Vilevile, itaendelea kuweka na kuhuisha mfumo wa kutunza kumbukumbu wa LRMS katika Ofisi za Ardhi za Halmashauri 30 (Jedwali Na.6). Mpango huu utafanikiwa tu ikiwa Halmashauri zote nchini zitaandaa na kutekeleza mpango endelevu wa kuweka na kutunza kumbukumbu sahihi za mashamba na viwanja vilivyopimwa na kumilikishwa.

MABARAZA YA ARDHI NA NYUMBA YA WILAYA

31. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu ndiyo yenye dhamana ya kuunda na kusimamia Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya. Katika mwaka 2011/2012, Wizara ilikamilisha taratibu za kuunda Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya katika Wilaya tatu (3) za Nzega, Kilosa na Manyoni kama nilivyoahidi na yataanza kutoa huduma katika mwaka huu 2012/13. Vilevile, tutaimarisha Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya za Kinondoni na Ilala kwa kuyapatia majengo yenye kukidhi mahitaji. Kutokana na kuanzishwa kwa Mabaraza mapya matatu (3), kwa sasa nchi nzima inayo Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya 42. Pia, Wizara yangu inakusudia kukamilisha uundaji wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya 6 za Ngorongoro, Tunduru, Mpanda, Muleba, Karagwe na Kyela.

32. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kupitia Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya iliendelea kushughulikia migogoro 15,754 ya ardhi na nyumba iliyokuwepo mwezi Juni, 2011 na mingine 10,428 iliyopokelewa hadi Juni, 2012. Mwaka 2011/12 mashauri 8,528 yaliamuliwa, na mashauri 17,654 yanaendelea kusikilizwa (Jedwali Na. 7). Kwa mwaka 2012/13, Wizara itaendelea kuimarisha Mabaraza yaliyopo kiutendaji ili kupunguza mlundikano wa mashauri katika Mabaraza hayo.

Pia, itasikiliza na kutolea maamuzi mashauri 17,654 yaliyopo. Ili kupunguza kiwango cha mashauri yanayokatiwa rufaa kwenye mabaraza ya ardhi na nyumba ya wilaya na hivyo kuongeza ufanisi wao nahimiza Halmashauri zote nchini kuwa ziandae mpango utakowezesha kuyaimarisha Mabaraza ya Vijiji na Mabaraza ya Kata ili yaweze kushughulikia migogoro ya ardhi kwa ufanisi katika ngazi hizo.

Pia, nichukue nafasi hii kuhimiza Wenyeviti wa Mabaraza haya kutambua kwamba wananchi wamekuwa wakiilalamikia Wizara kuhusu uadilifu na utendaji usioridhisha wa baadhi yao. Bila kupenda kuingilia uhuru wa Mabaraza, nimelazimika kuunda Tume ya kuchunguza baadhi ya malalamiko. Wale watakaobaininika wana makosa watachukuliwa hatua stahiki. Mantiki ya Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ni kusogeza huduma ya utoaji haki karibu na wananchi.

Kwa kuwa hadi sasa hatuna uwezo kuanzisha Mabaraza kila Wilaya, Mabaraza mengi yanafanya kazi kimkoa na hii imekuwa ni usumbufu kwa wananchi. Tunawasiliana na Wizara ya Katiba na Sheria kuangalia utaratibu wa kutumia Mahakimu Wakazi wa Wilaya kwa wakati huu ambapo mtandao wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya bado haujafikia Wilaya nyingi. Migogoro ya ardhi ni mingi sana, na wanaopendekeza kwamba Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya yafutwe wasisahau kwa nini yaliundwa. Ilikuwa ni kwa lengo la kupunguza msongamano wa kesi za ardhi katika mahakama zetu ambazo zina mambo mengine mengi na nyeti ambayo nayo yamerundikana huko.

HUDUMA ZA UPIMAJI NA RAMANI

33. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inaendelea na utekelezaji wa majukumu yake ya upimaji ardhi na utayarishaji wa ramani za msingi kwa nchi nzima ambazo huonesha hali halisi ya sura ya nchi na maendelezo yaliyo juu yake. Ramani hizo ni chanzo muhimu cha taarifa zinazohitajika katika kubuni na kutayarisha mipango ya matumizi mbalimbali.

Utayarishaji Ramani

34. Mheshimiwa Spika, mahitaji ya huduma ya upimaji ardhi nchini yanaongezeka kwa kasi kutokana na mwamko mkubwa kati ya wananchi wa kutaka kumilikishwa ardhi ili waweze kuitumia katika kupambana na umaskini. Vilevile, mahitaji ya ramani na taarifa za kijiografia yanaongezeka kwa kasi kutokana na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi na kijamii. Ramani za nchi zinahitajika kwa matumizi mbalimbali katika sekta zote. Baadhi ya sekta hizo ni ardhi na makazi, madini, nishati, ujenzi, maliasili, kilimo, maji, elimu na ulinzi.

35. Mheshimiwa Spika, utayarishaji, wa ramani unastahili kupewa umuhimu ili kuratibu vema mipango endelevu ya matumizi ya raslimali za nchi. Katika mwaka 2011/12, Wizara yangu iliahidi kufunga mtambo mpya wa kisasa wa kuchapisha ramani kwa mahitaji mbalimbali nchini, na kujenga kituo cha kupokelea picha za satellite (Satellite Image Receiving Station) ili kupata takwimu mbalimbali za ardhi kwa ajili ya kuhuisha na kutengeneza ramani mpya za nchi. Mchakato wa kutafuta fedha za utekelezaji wa mpango wa kujenga kituo cha kupokelea picha za satellite unaendelea.

36. Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu Serikali imekuwa ikiainisha mipaka ya mikoa, wilaya, vijiji na hifadhi za Taifa. Uwekaji wa mipaka hiyo umekuwa ukifanyika kwa kufuata Matangazo ya Serikali ambayo hutoa maelezo yanayozingatia alama mbalimbali za asili kama vile mito, maziwa, mabonde, milima na kadhalika. Kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, baadhi ya alama hizo wakati mwingine hubadilika au kutoweka na kusababisha migogoro ya kiutawala katika maeneo husika.

Ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa sahihi za mipaka ndani ya nchi, matumizi ya teknolojia ya kisasa ni muhimu. Kwa hali hiyo, katika mwaka 2012/13 Wizara yangu itajenga na kuimarisha taarifa za kijiografia (geo-database). Taarifa hizo zitatumika kutafsiri Matangazo ya Serikali yanayoainisha mipaka ya kiutawala ndani ya nchi ili mipaka hiyo iweze kueleweka kwa wahusika wote. Kazi hii itaanza kwa mikoa na wilaya mpya zilizoanzishwa hivi karibuni.

Mipaka ya Kimataifa

37. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu ina jukumu la kuweka na kutunza alama za mipaka ya Tanzania na nchi jirani. Katika mwaka 2011/12 Wizara iliahidi kufanya mazungumzo na nchi jirani katika juhudi za kukamilisha makubaliano juu ya mipaka yetu. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa majadiliano na nchi za Comoro na Msumbiji yalikamilika. Mkataba wa kwanza kati ya Tanzania, Msumbiji na Comoro kwenye alama ya utatu baharini inayotenganisha nchi hizi tatu ulikamilika na kutiwa saini tarehe 5 Desemba 2011. Mkataba wa pili kati ya Tanzania, Shelisheli na Comoro ulitiwa saini tarehe 17 Februari 2012. Kwa mantiki hiyo Tanzania imekamilisha upimaji wa mipaka katika Bahari ya Hindi na itatangaza eneo lake lote la ukanda wa kiuchumi baharini (Economic Exclusive Zone) bila ya pingamizi kutoka kwa nchi jirani.

38. Mheshimiwa Spika, Serikali ilifanya mazungumzo na nchi za Burundi na Kenya juu ya uimarishaji wa alama za mipaka. Tanzania na Kenya zimekubaliana kuanza kazi ya uimarishaji wa alama kuanzia Jasini katika mkoa wa Tanga hadi Mkomazi katika mkoa wa Kilimanjaro. Sehemu hiyo ina urefu wa kilometa 100 na alama nyingi zimeharibiwa na ujenzi wa nyumba kwa pande zote za mpaka. Kazi hii itafanyika mwaka 2012/13. Ukaguzi na uimarishaji wa mpaka kati ya Tanzania na Burundi vilevile utafanyika mwaka wa fedha 2012/13.

Upimaji Ardhi chini ya Maji

39. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu ina jukumu la kupima ardhi chini ya maji na kutayarisha ramani. Ramani hizo huonesha kina cha maji, miamba iliyopo na hutumika katika kuongoza vyombo ndani ya maji, kubaini maeneo yanayofaa kwa bandari na utafiti wa aina mbalimbali. Katika mwaka 2011/12 watumishi watatu walihudhuria mafunzo ya muda mfupi nje ya nchi yaliyohusu upimaji ardhi katika maji yenye kina kifupi baharini. Katika mwaka 2012/13 Wizara yangu inatarajia kununua kifaa cha kupimia vina vya maji (echo sounder). Aidha, Wizara itaendelea kuwapatia mafunzo wataalam katika fani hii ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi.

Kuongeza eneo Nje ya Ukanda wa Kiuchumi Baharini

40. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa 2011/12 Wizara yangu iliahidi kukamilisha na kuwasilisha Umoja wa Mataifa Andiko la kudai eneo la nyongeza nje ya maili 200 za ukanda wa kiuchumi baharini. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa niliongoza ujumbe wa Tanzania kuwasilisha Andiko hilo tarehe 18 Januari 2012. Hivi sasa Tume ya Mipaka ya Baharini ya Umoja wa Mataifa inapitia andiko hilo. Serikali ya Tanzania inatakiwa kwenda tena Umoja wa Mataifa kutetea hoja ya kudai eneo hilo tarehe 7 Agosti, 2012. Ninatarajia kuongoza tena ujumbe wa Tanzania kwenye utetezi wa hoja hiyo.

Napenda kuchukua fursa hii kuwatambua na kuwashukuru kwa dhati wajumbe wa Kamati ya Uongozi, Kamati ya Ufundi na Kikosi kazi cha Mradi huu. Kwanza ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge walioshiriki katika ziara yangu kuwasilisha andiko letu Umoja wa Mataifa, Mhe. Abdulkarim Esmail Hassan Shah, Mbunge wa Mafia na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira na Mhe. Zakia Hamdani Meghji, Mbunge wa Kuteuliwa. Pili nimtambue mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi iliyoongozwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi Ndugu Haji Adam Haji aliyekuwa Mkurugenzi wa Upimaji na Mipangomiji Zanzibar na Dkt. Sellasie David Mayunga, Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Tanzania Bara.

41. Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kumpongeza kwa dhati Mwenyekiti wa Kikosi Kazi kilichoandaa Andiko, Profesa Evelyne I. Mbede wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Sayansi na Teknolojia katika Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia; Katibu wake Bw. Justo Lyamuya kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, na Wajumbe ambao ni Bw. John A.Msemwa wa Wizara ya Ardhi, Bw. Abdon D. Makishe, Bw. Omary J. Mtunguja na Bw. Kelvin R. Komba wote kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli. Wengine ni Prof. Desiderius C.P. Masalu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mhadhiri Bw. Issa A. Hemedi wa Chuo Kikuu cha Ardhi, Bw. Adam I. Zuberi wa Wizara ya Nishati na Madini, Bw. Donald L. Chidowu wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw. Richard A. Maridadi Mwanasheria wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Bw. Pandu S. Makame Mwanasheria aliyekuwa Ofisi ya Makamu wa Rais, Zanzibar.

42. Mheshimiwa Spika, Kamati hizi zimefanya kazi nzuri ambayo imewezesha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kukamilisha Andiko la kudai kuongeza eneo ndani ya bahari lenye ukubwa wa kilomita za mraba 61,000. Eneo hili litakapopatikana litaiwezesha Tanzania kuvuna rasilimali mbalimbali chini ya bahari kwa manufaa ya sasa na ya vizazi vijavyo.

Ni sifa kubwa kwa nchi yetu kufanikisha kazi hii kwa kutumia wataalamu wetu wazawa. Nichukue fursa hii kuwashukuru kwa dhati waajiri wa wajumbe wa Kikosi Kazi kwa kuwaruhusu watumishi hawa kufanya kazi hii, na nawaomba wasichoke kuendelea kutoa ushirikiano hadi kazi hii itakapokamilika na eneo kupatikana. Na inshallah eneo hilo litapatikana kwa manufaa ya Watanzania wote.

Nitatumia uzoefu wangu katika Umoja wa Mataifa katika kutekeleza kazi hii nyeti na muhimu. Niwaombe Watanzania wote, wa bara na visiwani kutambua kwamba tunachoshughulikia sasa ni maombi ya eneo ambalo tusipofanikiwa kulipata litabaki chini ya himaya ya Umoja wa Mataifa ambapo mataifamakubwa yatalifaidi. Ninashukuru Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kufafanua kwamba kazi hii imeshirikisha pande zote za taifa letu ipasavyo na kufuta hisia potofu zilizokuwa zimeibuka zikidai vinginevyo.

Upimaji wa Mipaka ya Vijiji.

43. Mheshimiwa Spika, Upimaji wa mipaka ya vijiji nchini huwezesha kutolewa kwa Vyeti vya Ardhi ya Vijiji, kupanga matumizi bora ya ardhi na hatimaye kuweza kutolewa kwa Hati za Hakimilki ya Kimila. Katika mwaka 2011/12 Wizara yangu iliahidi kupima mipaka ya Vijiji 350 ambapo hadi kufikia Juni, 2012 jumla ya vijiji 206 vimepimwa katika wilaya za Same (12), Arumeru (28), Longido (10), Mbulu (64), Uyui (66) Manyoni (22) na Kiteto (4). Kutokana na upimaji huo, mpaka sasa jumla ya vijiji vilivyopimwa mipaka nchini ni 11,467. Kwa mwaka 2012/13, Wizara yangu itaendelea na upimaji wa mipaka ya vijiji 200. Aidha, upimaji wa mipaka ya vijiji utaendelea kwa kadri vitakavyokuwa vikiongezeka.

Upimaji Milki

44. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, Wizara yangu imeratibu na kuidhinisha upimaji wa viwanja 34,049 na mashamba 2,169 kati ya lengo la viwanja 35,000 na mashamba 800 (Jedwali Na.8a). Katika utunzaji wa kumbukumbu jumla ya plani za viwanja 15,116 zimeingizwa hivyo kufanya jumla ya viwanja vilivyoingizwa katika mfumo wa kielektroniki kuwa 30,304. Vilevile, plani za hati (deed plans) 1,685 kwa viwanja vilivyopimwa nchini zilitayarishwa. Kwa sasa utoaji wa plani za hati unafanyika haraka zaidi kutokana na matumizi ya teknolojia ya digitali.

45. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2012/13 Wizara yangu inatarajia kuidhinisha upimaji wa viwanja 40,000 na mashamba 1,000 kutoka katika miji na vijiji mbalimbali nchini. Pia, Wizara itajenga alama 300 za vianzio vya upimaji (Control points densification) katika miji 50 ili kurahisisha upimaji ardhi nchini (Jedwali Na.8b). Vilevile, Wizara yangu itaendesha mafunzo ya utumiaji wa mtandao mpya wa upimaji ardhi nchini kwa wapima ardhi. Ili kuharakisha upangaji na upimaji wa ardhi Halmashauri zote nchini zinashauriwa kununua vifaa vya kisasa vya upimaji ardhi. Ni jambo la kusikitisha kwamba katika Halmashauri kadhaa wapima hawana hata darubini ya kawaida, achilia mbali vifaa vya kisasa kama GPS (Global Positioning System) na Total Station. Hii si kwa sababu ya umaskini bali kutoelewa kwamba fani hii haiwezi kuwa na manufaa bila kuwa na vifaa vya msingi.

Mfuko wa kupima Viwanja

46. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeendelea kusimamia mfuko wa mzunguko wa kupima viwanja (Plot Development Revolving Fund – PDRF) unaozipatia mikopo Halmashauri kwa ajili ya kutayarisha michoro ya mipango miji, kulipa fidia, kupima viwanja na kumilikisha. Hadi Juni 2012 mfuko wa PDRF ulikuwa na jumla ya Shilingi milioni 606. Aidha, Halmashauri 29 hazijarejesha jumla ya Shilingi milioni 466.6 (Jedwali namba 9a).

Wizara imepokea maombi kutoka Halmashauri 8 ya jumla ya Shilingi milioni 5,050 (Jedwali 9b). Kwa sasa Wizara inachambua maombi hayo na kutayarisha utaratibu mpya utakaowezesha kukopesha na kurejesha kwa wakati. Napenda kurudia maelekezo yangu kwa Halmashauri zilizokopeshwa kurejesha mikopo hiyo kwa wakati ili kuziwezesha Halmashauri nyingine kukopa kwa ajili ya kutwaa maeneo na kupima na kumilikisha ardhi.

47. Mheshimiwa Spika, kupitia mradi wa viwanja 20,000 Wizara yangu ilizikopesha Halmashauri nne jumla ya Shilingi bilioni 1.87. Fedha hizo zilitolewa kwa ajili ya kuandaa ramani za mipango miji, kulipa fidia, kupima na kumilikisha viwanja. Hadi Juni 2012 jumla ya Shilingi milioni 650 zimerejeshwa na Shilingi bilioni 1.22 hazijarejeshwa. Halmashauri ambazo bado hazijarejesha ni za Manispaa ya Morogoro (Shilingi milioni 50); Mji wa Kibaha (Shilingi milioni 270.4); Manispaa ya Kinondoni (Shilingi milioni 500) na Manispaa ya Ilala (Shilingi milioni 400) (Jedwali 9c).

Kwa mwaka 2012/13 Wizara yangu kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) zitaweka utaratibu utakaozilazimisha Halmashauri zilizokopeshwa kurejesha mikopo hiyo kwa wakati. Napenda kuzikumbusha Halmashauri kutumia fursa hii kutambua kwamba kushindwa kurejesha mikopo hiyo kunaathiri utendaji kazi wa Wizara yangu na kuzinyima haki Halmashauri nyingine ambazo zingekopeshwa kama mikopo ingerejeshwa kwa wakati. Ninachukua pia fursa hii kutangaza kuwa nimeagiza kwamba Wizara yangu ikate madeni ya wadaiwa hawa sugu kwenye mgao wao wa asilimia 30 ya makusanyo ya kodi za ardhi kabla ya kuwalipa. Sina budi kuzipongeza Halmashauri za Bagamoyo na Manispaa ya Temeke, kwa kumaliza kulipa madeni yao. Jambo hili nalo si umaskini bali ukosefu wa nidhamu ya kifedha (financial indiscipline).

MIPANGO MIJI NA VIJIJI

48. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu ina jukumu la kusimamia upangaji na uendelezaji wa miji na vijiji ili wananchi wawe na makazi nadhifu na yaliyopangwa. Majukumu hayo yanaratibiwa na kutekelezwa kwa mujibu wa sera, sheria, kanuni, na taratibu za uendelezaji wa miji na vijiji zilizopo zikiwemo Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Makazi ya mwaka 2000, Sheria ya Mipangomiji ya mwaka 2007, Sheria ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya mwaka 2007 na Sheria ya Usajili wa Wataalam wa Mipangomiji ya mwaka 2007.

49. Mheshimiwa Spika, idadi ya watu nchini imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka. Kulingana na takwimu ya sensa ya watu ya mwaka 1957 Tanzania Bara ilikuwa na watu 8,788,466 kati yao watu 276,362 sawa na asilimia 3.1 walikuwa wakazi wa mijini. Idadi ya wakazi hao iliongezeka hadi kufikia 679,291 sawa na asilimia 5.7 mwaka 1967 na kufikia watu 7,970,000, sawa na asilimia 23.1 mwaka 2002. Ongezeko hilo la watu limesababisha miji yetu kukua kwa kasi.

Kama miji yetu itaendelea kukua kwa kasi ya sasa ya asilimia 4.5 kila mwaka, ifikapo mwaka wa 2025 zaidi ya nusu ya wananchi wote hapa nchini watakuwa wanaishi mijini. Kasi kubwa ya ongezeko la watu mijini imefanya mamlaka za upangaji ambazo ni mamlaka za Serikali za Mitaa kushindwa kumudu kupanga, kupima na kuweka miundombinu na huduma za msingi. Hali hii inaonyesha kuwa makazi mijini yatakabiliwa na changamoto nyingi, hivyo kuna umuhimu wa kubuni mbinu za kisasa za kupanga na kuendeleza miji.

Uandaaji na Utekelezaji wa Mipango ya Uendelezaji Miji

50. Mheshimiwa Spika, katika upangaji wa miji, Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri huandaa mipango ya jumla (General Planning Schemes) ya aina mbili ya kuongoza uendelezaji wake. Mipango hiyo ni ya muda mrefu (Master Plans) ambayo hutoa mwongozo wa uendelezaji kwa miaka ishirini, na ya muda mfupi (Interim Land Use Plans) ambayo ni ya miaka kumi.

Katika mwaka 2011/12, Wizara yangu kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Misenyi ilikamilisha uandaaji wa Mpango wa muda mfupi wa mji mdogo wa Kyaka – Bunazi. Aidha, Wizara yangu kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Tanga ilikamilisha uandaaji wa Mpango kabambe wa Jiji la Tanga na kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo iliendelea na maandalizi ya Mpango Kabambe wa Mji wa Bagamoyo. Pia, Mtaalam mshauri anayeandaa Mpango Kabambe wa Jiji la Dar es Salaam aliwasilisha rasimu ya awali ya mpango huo ambao ataukamilisha mwaka 2012/13.

51. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2012/13 Wizara yangu kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo itakamilisha Mpango Kabambe wa mji mdogo wa Bagamoyo na kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Mbeya itaandaa Mpango Kabambe wa Jiji hilo. Vilevile, Wizara yangu itaendelea kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Njombe katika kuandaa mpango wa mji mdogo wa Makambako, na Halmashauri ya Wilaya Mafia katika ukamilishaji wa Mipango ya miji hiyo.

52. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12 Wizara yangu kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni iliendelea kuandaa mpango wa uendelezaji upya eneo la Manzese na ilikamilisha maandalizi ya mpango wa Makongo Juu na kuanza maandalizi ya kutafuta fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mpango. Pia, Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri ya Mji wa Njombe, ilianza uandaaji wa mpango wa uendelezaji upya wa eneo la kati la mji huo. Kwa mwaka 2012/13 Wizara itaendelea kushirikiana na Halmashauri hizo kukamilisha na kutekeleza mipango hiyo. Natoa wito kwa Mamlaka zote za Miji na Wilaya nchini kutenga fedha za kuandaa na kutekeleza mipango hiyo ambayo ni msingi wa usimamizi wa uendelezaji wa miji.

53. Mheshimiwa Spika, Wizara inaendelea na utekelezaji wa mradi wa uendelezaji upya eneo la Kurasini ulioanza mwaka 2006, kwa lengo la kuwezesha eneo hilo kutumika kikamilifu kwa upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam na kuifanya iwe lango kuu la biashara kitaifa na kimataifa. Katika mwaka 2011/12 Wizara ililipa fidia ya jumla ya Shilingi milioni 550 kwa wakazi wa Mtaa wa Kurasini waliopo jirani na mabwawa ya majitaka.

Pia, kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi imetayarisha michoro inayoonesha ukanda wa barabara inayounganisha barabara ya Mandela na daraja la Kigamboni kwa upande wa Kurasini na kutambua ardhi na mali zilizopo katika ukanda huo wa barabara. Kwa mwaka 2012/13 Wizara yangu itaendelea kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara kufanya maandalizi ya eneo la ujenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Biashara kwenye eneo lililotengwa kwa ajili ya upanuzi wa Bandari Kurasini Jijini Dar es Salaam. Aidha napenda kulijulisha Bunge lako tukufu kuwa Serikali imetenga fedha kwenye bajeti ya mwaka 2012/13 chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara kulipa fidia kwa wananchi watakaopisha mradi huo katika eneo la Kurasini na Shimo la Udongo.

Urasimishaji Makazi Holela

54. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, Wizara yangu ilikamilisha uandaaji wa Programu ya Taifa ya kuzuia na kurasimisha Makazi Holela na iko katika hatua ya utekelezaji. Pia, kwa kushirikiana na Jiji la Mwanza ilirasimisha makazi 2,810. Aidha, Wizara kwa kushirikiana na Manispaa ya Kinondoni ilihakiki mipango ya urasimishaji 16 katika Mitaa ya Makabe na Mshikamano kata ya Mbezi Luis na Mitaa ya

Malamba Mawili na Msigani. Mipango hiyo iko katika hatua ya kuidhinishwa ili wananchi waweze kupimiwa maeneo yao na kuandaliwa hatimiliki. Kwa mwaka 2012/13, Wizara itachapisha, kusambaza na kuanza utekelezaji wa Programu ya Taifa ya Kuzuia na Kurasimisha Makazi Holela mijini kwa kushirikiana na MKURABITA, Halmashauri za Miji na Wilaya na wadau wote.

Pia itarasimisha makazi 4,000 katika Jiji la Mwanza. Halmashauri zote nchini zinaagizwa zihakikishe kuwa zinapima viwanja na kuvigawa kwa wananchi ili kuepushai ujenzi holela. Wananchi wanaokaidi mipangomiji na kujenga kiholela, kuvamia maeneo ya wazi na kujenga katika maeneo yanayolindwa kisheria hususan fukwe na maeneo hatarishi, wasitegemee kupewa fidia wakati wa kuhamishwa. Tuko tayari kupokea maombi yenu kupewa viwanja au nyumba kuliko kupoteza akiba yenu kujenga visivyo.

Uendelezaji Miji Mipya na Vituo vya Huduma

55. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2011/12, Wizara yangu iliendelea kushirikiana na Halmashauri za Jiji la Dar es Salaam katika kutekeleza mkakati wa kuanzisha vituo vya Huduma kwenye maeneo ya pembezoni mwa miji kwa kushirikisha sekta binafsi. Kwa upande wa Kituo cha Huduma cha Luguruni, Wizara imekamilisha mchakato wa kupata mwendelezaji mwenza (Co – Master Developer) ambaye ni kampuni binafsi itakayoshirikiana na Serikali katika uendelezaji wa kituo hicho.

Aidha, Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke imeainisha eneo jipya la Mikwambe kwa ajili ya kujenga kituo cha huduma katika Manispaa hiyo badala ya Kongowe. Kwa mwaka 2012/13 Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni itaanza utekelezaji wa ujenzi wa Kituo cha Huduma cha Luguruni kwa ushirika kati ya Sekta binafsi na Serikali.

56. Mheshimiwa Spika, Mpango Kabambe wa Mji Mpya wa Kigamboni uliandaliwa kwa kuzingatia Sheria ya Mipangomiji sura Na. 8 ya 2007 kama historia yake inavyoonesha. Yafuatayo yalifanyika: kuitisha mkutano wa wakazi wa Temeke, kutangaza mipaka ya eneo kwenye Gazeti la Serikali, kuandaa andiko na kufanya uhamasishaji katika ngazi zote. Uhamasishaji ngazi ya mkoa ulifanyika tarehe 2 Desemba, 2008 katika Ukumbi wa Mkuu wa Mkoa.

Washiriki katika mkutano huo ni Mkuu wa mkoa, Katibu Tawala wa Mkoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri zote za Dar es Salaam na Katibu Tawala wa Wilaya ya Temeke; Mkutano katika ngazi ya Wilaya ulifanyika katika Ukumbi wa JKT Mgulani tarehe 11 Januari, 2009 na walihudhuria Wabunge, Madiwani na watendaji wa Wilaya ya Temeke; Mkutano wa kujenga uelewa wa pamoja ulifanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Temeke tarehe 14 Januari, 2009 na wadau walitoka Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI na viongozi wa Manispaa ya Temeke, Mkoa wa Dar es Salaam na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Mkutano wa ngazi ya kata ulifanyika tarehe 16 Januari, 2009 Kigamboni na viongozi wa ngazi ya Kata walishirikishwa; Mikutano katika ngazi ya mitaa ilifanyika kati ya tarehe 18-24 Machi, 2009.

57. Mheshimiwa Spika, tarehe 20 Januari, 2009 katika kikao chake cha kawaida, Halmashauri ya Manispaa ya Temeke ilijadili na kuridhia mpango wa uendelezaji wa mji wa Kigamboni. Tarehe 9 Mei, 2009 kilifanyika kikao cha kutoa taarifa ya kuanza kutambua mali na milki kwenye eneo lote la mpango. Kutokana na maazimio ya kikao hicho kazi ya kutambua mali na milki kwenye eneo la mpango ilianza tarehe 12 Mei, 2009. Jumla ya milki 32,000 zilitambuliwa katika kata zote sita za Kigamboni, Mji Mwema, Vijibweni, Kibada, Somangila na Gezaulole. Mtaalamu Mwelekezi aliwasilisha mpango katika ngazi zote kama ilivyokuwa awali kati ya 2 Desemba 2009 hadi 28 Juni, 2010. Tarehe 4 Julai 2010 Waheshimiwa Wabunge walifanyiwa semina kwenye ukumbi wa Pius Msekwa Dodoma kuhusu mpango wa uendelezaji wa mji mpya wa Kigamboni.

58. Mheshimiwa Spika katika mwaka 2011/12 Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, ilikamilisha maandalizi ya msingi ya kuwezesha kutekeleza Mpango Kabambe wa Mji Mpya wa Kigamboni. Kwa mwaka 2012/13 Wizara itasimamia uundwaji wa Wakala; Kuidhinisha mpango na kuanza utekelezaji; Kufanya uthamini wa mali zilizomo katika maeneo ya miundombinu, huduma za jamii na eneo la makazi mbadala (resettlement area); Kulipa fidia kwa mali zilizomo katika maeneo yaliyofanyiwa uthamini; Kuandaa michoro ya kina; kupima na kuandaa ramani za ujenzi zilizomo katika eneo la makazi mbadala; Kupima maeneo nje ya maeneo ya miundombinu kwa awamu na kuendelea na utekelezaji kwa awamu watatu.

Awamu ya kwanza ni kati ya 2012-2022, awamu ya pili ni kati ya 2022- 2027 na awamu ya tatu ni 2027-32. Pia wizara yangu itaendelea kutafuta fedha za kuendeleza eneo la mpango kwa kuuza Municipal bonds. Gharama ya mradi inakisiwa kufikia Shiling trillion 11.6. Pamoja na kwamba asilimia 59 ya bajeti ya Wizara, takriban bilioni 60, zimetengwa kwa ajili ya Mradi wa Kigamboni, kiasi hiki ni asilimia 10 tu ya pesa tunazohitajika mwaka huu. Kwa hiyo tutatumia mbinu za kisasa kutafuta pesa nyingine, takribani bilioni 605 nje ya bajeti kutekeleza mradi huu bila kuchelewa zaidi.

Mradi utahitaji kiasi hicho cha fedha kwa miaka 3 ya kwanza. Napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wananchi wa Kigamboni kwa uvumilivu wao na ushirikiano wanaotuonesha na ninawahakikishia kuwa Serikali sasa imetenga bajeti ya kuhakikisha utekelezaji wa mpango huu unaanza na kushamiri. Nitasimamia mradi huu kwa karibu kwa kasi, ari na nguvu mpya. Ninataka kuanza na ziara za mafunzo (study tours) kwa wawakilishi kutoka Kigamboni kutembelea miji mipya ili tuwe na uelewa wa pamoja juu ya kazi iliyombele yetu. Aidha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi watapewa maeneo ya kuanza kujenga makazi ambayo yatatumika kuwahamisha wananchi watakaopenda kubaki Kigamboni.

Tunashauri ikiwezekana wote wachague kubaki maana hivi sasa kuna wananchi takribani 82,000 wakati tunajenga mji mpya wenye uwezo wa wakazi 400,000. Hakuna sababu ya wananchi kuhama eneo hili ila makazi yao yatapangwa upya na kuboreshwa. Serikali imeamua kuunda wakala mpya, Kigamboni Development Agency (KDA) kusimamia mradi huu wa kipekee katika historia ya Taifa letu. Wananchi ambao hawajakiuka maagizo ya mradi kwa kufanya maendelezo haramu, wasiwe na wasiwasi kuhusu fidia kwa sababu mradi utazingatia haki zao na ni endelevu. Fidia itatolewa kwa mujibu wa sheria, kwa tathmini ya kiujumla ambayo itakokotolewa kutokana na viwango vya soko na kuhuishwa ili iwe sahihi (land values under mass valuation).

Usimamizi wa Uendelezaji Miji

59. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, Wizara ilikamilisha uandaaji wa Kanuni za Sheria ya Mipangomiji (Na. 8) ya mwaka 2007. Vilevile, Wizara imetafsiri kwa Kiswahili Sheria ya Mipangomiji na rasimu yake inafanyiwa maboresho. Kwa mwaka 2012/13 Wizara yangu itaendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya Sheria ya Mipangomiji ya mwaka 2007, Sheria ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya mwaka 2007 na kanuni zake, pamoja na miongozo mbalimbali inayohusiana na masuala ya uendelezaji na upangaji wa ardhi mijini na vijijini ili kurahisisha utekelezaji wake. Aidha, Wizara inakusudia kuanzisha Ofisi za Kanda kwa wataalamu wa Mipangomiji kwa lengo la kukasimu mamlaka ya kuidhinisha Mipango ya Uendelezaji Miji kutoka kwa Mkurugenzi wa Mipangomiji.

60. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12 Wizara yangu iliajiri Askari Ardhi (Land Rangers) 15 waliohitimu kutoka Chuo cha Ardhi Tabora na Morogoro kwa mikataba ya muda mfupi. Askari hao walipangwa katika Halmashauri za Manispaa za Jiji la Dar-es- Salaam (Temeke, Kinondoni na Ilala) kwa ajili ya kufanya kazi ya ufuatiliaji wa maendelezo mbalimbali Jijini pamoja na ukaguzi wa matumizi mbalimbali ya ardhi kwenye maeneo yaliyopangwa ili kupunguza kasi ya uvamizi wa maeneo ya wazi na ujenzi holela kwenye maeneo yenye mipango ya miji. Aidha, Wizara imeandaa muundo wa utumishi wa kada hii na utawasilishwa katika Mamlaka husika kwa ajili ya kuidhinishwa na kuanza kutumika. Nashauri Halmashauri zote ziweke utaratibu wa kuajiri na kuwatumia watumishi wa kada hiyo.

61. Mheshimiwa Spika, eneo la mto Msimbazi ni eneo ambalo lilibainishwa kuwa wazi katika mpango kabambe wa Jiji la Dar es Salaam wa mwaka 1979. Hata hivyo eneo hilo limeendelezwa kwa matumizi mbalimbali ambayo yanakinzana na mpango huo. Kutokana na uvamizi huo, madhara makubwa hutokea katika eneo hilo. Mfano mwezi Desemba mwaka 2011 watu walipoteza maisha na mali kutokana na mafuriko katika eneo hilo. Hali hii iliigharimu Serikali fedha nyingi katika kuwaokoa, kuwahifadhi na kuwatafutia makazi wahanga wa mafuriko. Natoa pole kwa waathirika wa mafuriko hayo pamoja na Waheshimiwa Wabunge wao.

62. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, Wizara yangu kwa kushirikiana na Halmashauri za Manispaa za Ilala na Kinondoni ilianza maandalizi ya mpango wa kuhifadhi Bonde la Mto Msimbazi kuwa eneo la kijani. Eneo hilo linaanzia milima ya Pugu hadi Daraja la Salenda lina hekta 1,924. Mchakato wa kuhifadhi bonde hilo utafanyika kwa awamu mbili, awamu ya kwanza itaanzia kwenye Daraja la Salenda Upanga hadi Vingunguti lenye ukubwa wa hekta 1,121. Awamu ya pili itaanzia Vingunguti hadi milima ya Pugu. Hadi sasa Wizara imebainisha mipaka na kuandaa mchoro wa eneo la mpango na kutangaza kwenye Gazeti la Serikali (GN Na. 227) la tarehe 5 Aprili, 2011. Kwa mwaka 2012/13 Wizara yangu kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Ilala na Kinondoni zitaendelea na uandaaji wa mpango huo.

63. Mheshimiwa Spika, napenda kusisitiza tena kuwa eneo la Bonde la Mto Msimbazi ni eneo hatarishi kwa makazi ya binadamu, hivyo mamlaka za upangaji zichukue hatua za haraka kuondoa makazi na maendelezo yote yaliyofanyika humo kwani hayana mustakabali. Ni dhahiri kwamba maafa ya mara kwa mara katika eneo hilo hayaepukiki hasa ukizingatia mabadiliko ya tabianchi. Vilevile, naagiza Halmashauri zote kuainisha maeneo yote hatarishi hususan mabonde na milimani na kuyawasilisha kwangu kwa ajili ya kuyatangaza kwenye Gazeti la Serikali. Natoa wito kwa wadau wote, kutoa ushirikiano unaostahili ili kuhakikisha kuwa zoezi hilo linafanyika kwa manufaa ya wakazi wote wa Jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine.

MIPANGO YA MATUMIZI YA ARDHI

64. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu ina jukumu la kusimamia na kuratibu kazi za uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji. Lengo ni kuziwezesha mamlaka za upangaji zikiwemo Halmashauri za Wilaya na Vijiji kupanga, kutekeleza na kufuatilia uendelezaji wa Mipango ya makazi vijijini katika maeneo yao ya utawala. Mipango hiyo ni nyenzo muhimu katika kuendeleza ardhi na rasilimali zake kwa ufanisi, kuzuia migogoro baina ya watumiaji ardhi, kuimarisha milki za ardhi hususan za kimila, kuwezesha upatikanaji wa maeneo ya ardhi kwa ajili ya uwekezaji, kuhifadhi mazingira na vyanzo vya maji na kuongeza ustawi wa jamii na maendeleo ya kiuchumi kwa watumiaji wa ardhi ambao wengi wao ni wananchi wa kawaida wanaoishi vijijini.

65. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, Wizara yangu kupitia Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, ilitoa mafunzo kuhusu sheria za ardhi, matumizi ya teknolojia ya utunzaji wa kumbukumbu (Geographical Information System) na mbinu shirikishi za utayarishaji wa mipango ya matumizi ya ardhi. Katika kipindi hicho, jumla ya watendaji 51 kutoka Halmashauri za Wilaya 14 za ukanda wa Pwani walipatiwa mafunzo hayo (Jedwali Na. 10a).

Vilevile, Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri ilifanya tathmini ya uwezo wa rasilimali za ardhi ngazi ya kijiji katika vijiji 18 vya Wilaya za Pangani, Muheza, Mkinga, Rufiji na Mafia kwa ufadhili wa Benki ya Dunia. Matokeo ya tathmini hiyo ni kufahamika kwa uwezo wa rasilimali ardhi pamoja na vikwazo vinavyoathiri uwezo wa ardhi kwa matumizi mabalimbali endelevu (kama vile kilimo, upandaji wa miti, makazi, viwanda na ufugaji) na kuwezesha kijiji kufanya maamuzi sahihi juu ya mgawanyo na matumizi ya rasilimali ardhi.

Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Wilaya na Vijiji

66. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, Wizara kupitia Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi iliendelea kushirikiana na Halmashauri za Wilaya na wadau mbalimbali katika kuandaa na kutekeleza mipango ya matumizi ya ardhi katika ngazi za vijiji na wilaya. Katika kipindi hicho mipango ya matumizi ya ardhi iliandaliwa katika vijiji 82 kwenye Wilaya 26 (Jedwali Na. 10b).

Katika vijiji hivyo, maeneo ya makazi, huduma za jamii, hifadhi za vyanzo vya maji, misitu, ufugaji, wanyamapori, mashamba makubwa na maeneo ya kilimo cha umwagiliaji yametengwa kwa kuwashirikisha wananchi. Vilevile, Wizara iliendelea kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa Mipango iliyoandaliwa ya vitovu vya vijiji na vituo vya biashara. Pia, ilitekeleza ombi la mkoa wa Tabora la kuandaliwa Mipango ya kina ya makazi ya vijiji vinavyozunguka hifadhi ya misitu kwenye vijiji vinne katika Wilaya ya Urambo. Kwa mwaka 2012/13, Wizara yangu itaandaa taarifa mbalimbali za vijiji nchini ili kuwa na kumbukumbu sahihi zitakazosaidia katika uandaaji wa mipango ya makazi vijijini.

67. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2012/13, Wizara kupitiaTume itatekeleza Mpango wa Taifa wa Matumizi ya Ardhi kwa kutayarisha mipango ya matumizi ya ardhi kwa ushirikishwaji katika vijiji 150. Mipango hiyo itaandaliwa katika wilaya za Kilombero, Ulanga na Rufiji ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa programu ya Southern Agriculture Growth Corridor of Tanzania (SAGCOT). Aidha, vijiji vingine vya mipakani katika wilaya 16 za Tarime, Rorya, Same, Kibondo, Ngara, Misenyi, Longido, Ngorongoro, Rombo, Mwanga, Hai, Momba, Kyerwa, Karagwe, Karambo na Kakonko vitaandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi. Mipango hiyo itaandaliwa kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya husika. Vilevile, itaandaa mipango ya matumizi ya ardhi ya Wilaya 4 za Mpanda, Chunya, Kilombero na Ulanga na kutoa mafunzo kwa watendaji katika Wilaya hizo kuhusu matakwa ya sheria za ardhi na mbinu shirikishi za utayarishaji wa mipango hiyo. Pia, Wizara itaendelea kutekeleza programu za kilimo, maji na mifugo kwa kushirikiana na Wizara husika.

68. Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii kuzipongeza Halmashauri za Wilaya zilizokuwa zimetenga fedha katika mwaka 2011/12 kwa ajili ya kutayarisha mipango ya matumizi ya ardhi katika ngazi za vijiji ambazo ni Tandahimba, Korogwe, Monduli na Songea Vijijini. Napenda kuendelea kusisisitiza umuhimu wa Halmashauri za Wilaya kutenga bajeti kwa ajili ya kupanga mipango ya matumizi ya ardhi ngazi ya vijiji.

MAENDELEO YA NYUMBA

69. Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa nyumba bora za bei nafuu kwa wananchi walio wengi ni moja ya kiashirio cha kukukua kwa uchumi na maendeleo ya jamii. Ubora wa mazingira, zikiwemo nyumba unachangia kulinda afya ya jamii na kuongeza uwezo wa kufikiri na kutafakari. Sekta ya nyumba inatoa mchango mkubwa katika kukuza uchumi, mapato ya Serikali, kuongeza nafasi za ajira na kupunguza umaskini.

70. Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua mchango wa sekta ya nyumba kwa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla. Serikali inajielekeza katika kuweka mazingira wezeshi ya uendelezaji wa sekta hii. Changamoto kubwa zinazoikabili sekta ya nyumba ni namna ya kukabili ongezeko katika gharama za ujenzi wa nyumba, upatikanaji wa miundombinu na huduma za jamii katika maeneo ya makazi, upungufu wa nyumba bora na za bei nafuu na riba kubwa katika mikopo ya nyumba.

71. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeendelea kuelekeza na kuhamasisha Serikali za Mitaa kuratibu na kusimamia upatikanaji wa ardhi na uendelezaji wa miundombinu ili kuwezesha makampuni ya uendelezaji milki na watu binafsi kujenga nyumba na uendelezaji miji kwa namna bora na endelevu. Katika mwaka wa fedha 2011/12 tayari baadhi ya Halmashauri zimeanza kuomba mikopo kutoka mabenki kwa ajili ya uendelezaji wa ardhi na kuweka miundombinu. Halmashauri hizo ni pamoja na Temeke na Kinondoni.

72. Mheshimiwa Spika, kuhusu upatikanaji wa mtaji wa kukopesha kwa muda mrefu, Serikali ilianzisha Tanzania Mortgage Refinancing Company (TMRC) mwaka 2010, ambayo imeendelea kuvutia uwekezaji wa mabenki zaidi. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa baadhi ya mabenki na vyombo vya fedha vimekubali kutoa mikopo kwa wananchi ili kuwawezesha kununua nyumba kwa kutumia mikopo ya muda mrefu hadi kufikia miaka 25. Nachukua fursa hii kuyapongeza mabenki yaliyojitokeza kutoa mikopo kwa ajili ya kuendeleza nyumba. Kwa upande wetu Wizara itaendelea kuboresha mazingira kwa mabenki kutoa mikopo ya kujenga na pia kununua nyumba kwa kuhimiza Wizara ya Fedha na Benki kuu kuunda chombo cha kutoa bima ya mikopo ya nyumba (housing loans insurance mechanism).

73. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu, kwa kutambua faida za ushirika, inahimiza uanzishwaji na uendelezaji wa vyama vya ushirika wa nyumba ili kuwawezesha wananchi hasa wenye kipato cha chini kupata nyumba bora kwa gharama nafuu. Katika mwaka 2011/12 Wizara yangu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ilikamilisha kuandaa mwongozo wa kuunda na kuendesha vyama vya ushirika wa nyumba. Mwongozo huo utatumika wakati wa uhamasishaji wa wananchi kuunda vyama vya ushirika wa nyumba. Kwa wananchi wanaofanya kazi za kujiajiri wanashauriwa waanzishe vikundi vya ushirika wa nyumba katika maeneo yao. Chama cha ushirika wa nyumba kinaweza kusajiliwa ikiwa idadi ya wanachama waanzilishi inatimia watu kumi (10) au zaidi. Natoa wito kwa waajiri kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuhamasisha uanzishwaji wa vyama vya ushirika wa nyumba kwenye sehemu za kazi.

74. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, Wizara yangu ilikusanya takwimu za hali ya nyumba katika miji ya Shinyanga, Musoma, Bukoba, Tabora, Singida, Mtwara, Songea, Lindi, Njombe, Kigoma, Manyara, Rukwa, Bagamoyo na Kibaha. Taarifa zilizopatikana zitaiwezesha Serikali na wadau wengine wakiwemo waendelezaji milki na benki kufanya maamuzi yanayohusu nyumba kwa kuzingatia takwimu za uhakika. Pia, taarifa hizo zitawezesha nchi yetu kupima mafanikio yake Kikanda na Kimataifa katika sekta ya nyumba.

75. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/13 Wizara yangu itaendelea kuboresha mazingira ya uendelezaji wa nyumba kwa kutoa elimu kwa umma kuhusu mfumo wa mikopo ya nyumba (mortgage finance) na utaratibu wa kumiliki sehemu ya jengo (condominium housing); kuandaa taarifa ya hali ya nyumba nchini; kuhamasisha uundaji wa vyama vya ushirika wa nyumba na waendelezaji milki (Real Estate Developers) hasa wanaojenga nyumba za gharama nafuu.

76. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imekamilisha maandalizi ya rasimu ya Sera ya Taifa ya Nyumba. Sera hiyo inaweka msingi wa kuongoza na kusimamia uendelezaji wa nyumba. Kwa mwaka 2012/13, Wizara yangu itaratibu ukamilishaji wa Sera ya Nyumba na kutayarisha mpango mkakati na programu ya utekelezaji wake. Pia, itaanza mchakato wa kutunga Sheria ya Nyumba. Sheria itakayotungwa, itaweka utaratibu au kuanzisha chombo kitakacho simamia masuala ya mahusiano kati ya mpangaji na mmiliki wa nyumba na viwango vya ubora wa nyumba za kuuza na kupangisha bila kuathiri motisha wa kujenga nyumba za kupangisha au kuuza.

Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba na Vifaa vya Ujenzi

77. Mheshimiwa Spika, Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba na Vifaa vya Ujenzi (NHBRA) una jukumu la kutafiti, kukuza, kushauri, kuhamasisha na kusambaza matokeo ya utafiti na utaalamu wa ujenzi wa nyumba bora na za gharama nafuu nchini. Kazi hizo zikifanyika kikamilifu zitainua na kuboresha viwango vya nyumba zinazojengwa kwa kutumia vifaa vinavyopatikana hapa nchini na kuinua maisha ya wananchi wanaoishi vijijini na mijini.

78. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12 Wizara yangu kupitia Wakala iliendelea kufanya utafiti na kubuni mbinu za kujenga nyumba kwa gharama nafuu kwa kutumia malighafi zinazopatikana hapa nchini. Utafiti ulifanyika ndani na nje ya maabara. Vilevile, kazi za ushauri zilifanyika kwa wateja mbalimbali zikiwemo Ofisi za Serikali na watu binafsi. (Jedwali Na.11a).

79. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12 mafunzo ya vitendo yalifanyika kwa vijana 380 kutoka katika Halmashauri za Wilaya za Mkoa wa Pwani. Mafunzo hayo yaliwezesha kuanzishwa kwa vikundi 38 vya ujenzi wa nyumba na uzalishaji wa vifaa vya ujenzi na vilipatiwa mashine 114 za kufyatulia matofali yanayofungamana na mashine 28 za kutengenezea vigae vya kuezekea pamoja na kalibu za vigae 1,400. Pia, mashine za uzalishaji wa vifaa vya ujenzi zilisambazwa katika maeneo mbalimbali nchini (Jedwali Na. 11b). Lengo ni kuhakikisha kuwa teknolojia ya ujenzi wa nyumba bora na za gharama nafuu inawafikia wananchi walio wengi. Wakala ulijitangaza kwa kutumia vyombo vya habari na maonesho mbalimbali ya Kitaifa na Kimataifa kueneza matokeo hayo.

80. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2012/13 semina za uhamasishaji na kueneza teknolojia za ujenzi wa nyumba bora na za gharama nafuu zitafanyika katika Wilaya za Arusha Vijijini, Nkasi, Kishapu, Chunya, Tandahimba na Muleba. Pia, Wizara itafanya uhamasishaji wa kuanzisha vikundi vya ushirika vya ujenzi na uzalishaji wa vifaa vya ujenzi na kuvitumia katika ujenzi wa nyumba. Vilevile, Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri za Miji na Wilaya itaimarisha vikundi vya ujenzi wa nyumba vilivyoanzishwa na itaendelea kutangaza huduma zinazotolewa kupitia vyombo ya habari kama televisheni, vipeperushi na magazeti na kwa kushiriki katika maonesho ya Kitaifa na Kimataifa.

81. Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Wakala itaendelea kutoa huduma ya upimaji wa ubora wa vifaa mbalimbali vya ujenzi kutoka kwa wateja kwa kutumia maabara katika maeneo ya ujenzi. Pia, ushauri wa kitaalam wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu utaendelea kutolewa kwa wateja. Napenda kutoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge kuzishauri na kuzihamasisha Halmashauri za Majiji, Miji na Wilaya zitumie huduma za Wakala kwa kazi za ujenzi wa majengo yao na ya Serikali ili wanufaike na huduma za Wakala ambazo ni za gharama nafuu ikilinganishwa na bei za soko. Ninazishauri Idara za Serikali na Taasisi za Umma zitoe kipaumbele kwa matumizi ya teknolojia iliyobuniwa na Wakala ili kupunguza gharama za usanifu na ujenzi wa nyumba na majengo nchini.

SHIRIKA LA NYUMBA LA TAIFA Kuimarisha Utendaji kazi wa Shirika

82. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12 Shirika la Nyumba la Taifa liliendelea na utekelezaji wa mpango mkakati wa kipindi cha miaka mitano (2010/11-2014/15). Kulingana na malengo ya mpango huu, Wizara kupitia Shirika la Nyumba la Taifa, iliimarisha ufanisi wa utendaji kazi kwa kuweka mfumo wa tathmini na ufuatiliaji na kuboresha utendaji wao; kuwapatia mafunzo wafanyakazi 535 kati ya 546 kuhusu mbinu za utendaji wa kisasa na kuingia mikataba ya kiutendaji; kufuta mikataba ya ubia 59 isiyokuwa na tija kwa Shirika na kurekebisha mikataba 311 kati ya Shirika na wadau wake.

Vilevile, Wizara iliendelea na zoezi la kuhuisha mikataba ya pango katika nyumba zake; kuanzisha kitengo cha huduma kwa wateja; kurekebisha miongozo ya Shirika; kuimarisha uthibiti wa matumizi ya fedha na mali za Shirika; kuanzisha mfumo mpya wa mawasiliano ya kompyuta hasa utambuzi wa kijiografia wa nyumba za Shirika; na kupunguza kesi zilizoko mahakamani kutoka 288 na kufikia 167. Juhudi hizi zimeliwezesha Shirika kuongeza ufanisi katika utendaji na kuboresha taswira yake kwa jamii.

Ardhi kwa Ajili ya Ujenzi wa Nyumba

83. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, Shirika limeanza utekelezaji wa jukumu la kuwa Mwendelezaji Mkuu (Master Developer). Katika kutekeleza jukumu hili, Shirika lilinunua ardhi yenye ukubwa wa ekari 1,372.1 katika maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya ujenzi wa nyumba. Lengo la ununuzi huu, ni kuongeza hazina ya ardhi.

Vilevile, ununuzi wa maeneo mengine yenye ukubwa wa ekari 26,887.9 katika Wilaya mbalimbali nchini uko katika hatua mbalimbali za utekelezaji (Jedwali Na.12). Juhudi za upatikanaji wa ardhi zinafanyika sambamba na upangaji wa maeneo; upimaji; utayarishaji wa michoro ya kiusanifu na kiufundi; na upatikanaji wa vibali mbalimbali kama vile vya mazingira, ujenzi na motisha za uwekezaji kutoka Kituo cha Uwekezaji cha Taifa (TIC). Kwa mwaka 2012/13, Wizara kupitia Shirika la Nyumba la Taifa itaendelea na ununuzi wa vipande vya ardhi vilivyotambuliwa katika maeneo mbalimbali nchini. Natoa wito kwa Halmashauri za Miji na Wilaya kutenga ardhi kwa ajili ya ujenzi wa nyumba kwa pamoja (Real estate) utakaofanywa na Shirika la Nyumba.

Ujenzi wa Nyumba za Biashara na Makazi

84. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, Shirika liliendelea na matayarisho ya miradi ya ujenzi wa nyumba za makazi na biashara 9,000 katika maeneo mbalimbali nchini. Kati ya nyumba hizo, ujenzi wa nyumba 1,620 ulikamilika. Miradi iliyokamilika na inayoendelea kutekelezwa iko katika maeneo mbalimbali nchini zikiwemo Wilaya mpya ambazo ni Mvomero, Kongwa, Longido na Ilembo – Mpanda. Kwa mwaka 2012/13, Shirika litaendelea utekelezaji wa ujenzi wa nyumba 7,380 katika Wilaya mbalimbali nchini ikiwemo makao makuu ya mikoa na Wilaya mpya.

85. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12 Shirika liliendelea na utekelezaji wa miradi kumi ya ujenzi yenye jumla ya nyumba za makazi 823 katika maeneo mbalimbali nchini. Kati ya miradi hiyo, mitatu yenye jumla ya nyumba za kuuza 86 ilikamilika. Shirika pia liliweza kukamilisha mradi wa jengo la biashara lenye ghorofa nne lililoko Mtaa wa Lumumba mjini Kigoma. Kwa mwaka 2012/13 Shirika litakamilisha miradi saba yenye nyumba 737 na miradi mipya 38 yenye jumla ya nyumba 4,114 ikiwa ni jumla ya miradi 45 yenye nyumba 4,877. Kwa kuwa Shirika lipo tayari kujenga nyumba katika sehemu mbalimbali nchini, ni vyema Halmashauri zitakazohusishwa, zikalitengea ardhi kulingana na mahitaji. Pia, Shirika litaanza utekelezaji wa miradi mingine 14 ya majengo ya biashara katika maeneo mbalimbali nchini (Jedwali Na. 13).

86. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, Serikali kupitia Wizara ya Fedha ililiruhusu Shirika kukopa kiasi cha Shilingi bilioni 300 kutoka kwenye vyombo vya fedha vya ndani na nje ya nchi. Kutokana na kibali hicho, benki 15 za ndani na nje ya nchi zilikubali kulikopesha Shirika kiasi hicho. Hadi Juni, 2012 Shirika liliingia mikataba na benki tisa (9) zilizokubali kutoa mikopo ya jumla ya Shilingi bilioni 165.4. Fedha hizi zinatumika kwa ajili ya kuongeza hazina ya ardhi na kutekeleza miradi ya ujenzi wa nyumba.

Sambamba na juhudi hizi, Shirika pia liliingia makubaliano na benki tisa (9) kwa ajili ya kuwakopesha wanunuzi wa nyumba zinazojengwa na Shirika. Benki hizo ni Azania Bank, Bank of Africa (BOA), Commercial Bank of Africa (CBA), Benki ya CRDB, Exim Bank, Kenya Commercial Bank (KBC), Benki ya NBC, Benki ya NMB na Stanbic. Benki hizi zimeanza kutoa mikopo kwa wanunuzi wa nyumba zinazojengwa na Shirika. Kwa mwaka 2012/13, Wizara kupitia Shirika la Nyumba la Taifa itaendelea kuzihamasisha benki nyingine kutoa mikopo kwa ajili ya ujenzi wa nyumba na kuwahamasisha wananchi kununua nyumba zinazojengwa na Shirika.

87. Mheshimiwa Spika, gharama kubwa za ununuzi wa ardhi; upatikanaji wa vibali vya ujenzi; na gharama za uwekezaji kwenye miundombinu, ni kati ya changamoto zinazolikabili Shirika la Nyumba la Taifa katika suala zima la ujenzi wa nyumba za gharama nafuu. Wizara yangu itashirikiana na Halmashauri za Miji na Wilaya kutatua changamoto hizi ili kuliwezesha Shirika hili kuharakisha utekelezaji wa miradi yake na kupunguza gharama. Natoa wito kwa taasisi zinazohusika na uendelezaji wa sekta ya nyumba hususani Halmashauri za Miji na Manispaa pamoja na mamlaka za huduma za maji na umeme, kutoa huduma zinazowahusu ili kuliwezesha Shirika kutekeleza miradi yake kwa ufanisi na kwa wakati na kwa gharama nafuu.

88. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, Shirika lilitarajia kukusanya kiasi cha Shilingi bilioni 43.14 kutokana na kodi za pango la nyumba linazozimiliki. Hadi Juni, 2012, Shirika lilikusanya jumla ya Shilingi bilioni 53.17 sawa na asilimia 123 ya lengo. Mchanganuo wa mapato kutoka kila tawi umeoneshwa kwenye jedwali lililoambatishwa (Jedwali Na. 14). Ongezeko hili, linatokana na kuongezwa kwa viwango vya kodi kwa baadhi ya nyumba kutoka wastani wa asilimia 25 ya kodi za soko hadi asilimia 60.

Pia, ongezeko la makusanyo linatokana na ukusanyaji wa kodi na malimbikizo ya madeni kwa kila mwezi. Pia, Shirika lilichangia jumla ya Shilingi bilioni 11.47 kwenye pato la Serikali kutokana na kulipa kodi mbalimbali kutokana na shughuli zake. Kwa mwaka 2012/13, Shirika linatarajia kukusanya jumla ya Shilingi bilioni 52.97 kutokana na kodi ya pango la nyumba zake na kuchangia mapato ya Serikali jumla ya Shilingi bilioni 24.2 kwa kulipa kodi ya pango la ardhi, kodi ya ongezeko la thamani na kodi ya majengo.

89. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12 Shirika lilitenga kiasi cha Shilingi bilioni 6.8 kwa ajili ya ukarabati na matengenezo ya nyumba zake 16,324 zilizoko kwenye majengo yake 2,392. Katika kipindi hicho, jumla ya nyumba 1,400 na majengo 140 yalifanyiwa matengenezo ya kawaida na makubwa. Kwa mwaka 2012/13, Shirika litaendelea kutenga jumla ya Shilingi bilioni 8.9 kwa ajili ya kuzifanyia matengenezo nyumba na majengo ya Shirika.

Nachukua fursa hii kumpongeza Mkurugenzi Mkuu wa Shirikika la Nyumba la Taifa, Nd. Nehemia Kyando Mchechu na timu yake kwa kufanikiwa kubadilisha sura ya Shirika la nyumba kwa mda mfupi. Changamoto nyingi zimejitokeza katika kuleta mabadiliko hayo lakini ubunifu na bidii inayoshuhudiwa unaridhisha na kuashiria mageuzi makubwa zaidi hasa kama mikopo ya benki iliyochukuliwa italipwa kama ilivyopangwa na kukomesha ukata uliotishia uhai wa Shirika kabla ya mageuzi haya. Bila kuingilia menejimenti ya siku hadi siku, Wizara inasimamia kwa karibu masuala ya kisera ikiwemo kuanzisha utaratibu wa kuwapunguzia kodi wale ambao kwa sababu za msingi watashindwa kulipa kodi mpya za pango la nyumba za Shirika.

HUDUMA ZA KISHERIA

90. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu ilianzisha Kitengo cha Sheria (Legal Services Unit) kwa lengo la kutoa huduma mbalimbali za kisheria katika Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Huduma za Kisheria zinajumuisha uhuishaji wa sheria na usimamizi wa mashauri yanayohusu Wizara. Katika mwaka 2011/12 Wizara ilikamilisha marejeo ya Sheria ya Mipangomiji ya mwaka 2007 na kuiwasilisha kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili iandaliwe muswada wa sheria.

Vilevile, rasimu ya Muswada wa marekebisho ya Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Usajili wa Ardhi (Sura ya 334), Sheria ya Usajili wa Nyaraka (Sura ya 117) na Sheria ya Usajili wa Rehani ya Mali Zinazohamishika (Sura ya 210) ziliandaliwa ili ziendane na mabadiliko ya sera na sheria nyingine za sekta ya ardhi. Aidha, Rasimu ya Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini iliandaliwa na inaboreshwa kwa kuzingatia maoni ya wadau; na kamati ya wataalam iliundwa ili ipitie upya na kupendekeza marekebisho ya Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999, Sheria ya Ardhi ya Vijiji ya mwaka 1999 na Sheria ya Mahakama za Ardhi ya mwaka 2002 ambayo yataziwezesha kukidhi changamoto zilizojitokeza katika sekta ya ardhi.

91. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2012/13, Wizara yangu itakamilisha marejeo ya Sheria ya Mipangomiji ya mwaka 2007; Sheria ya Usajili wa Ardhi (Sura ya 334); Sheria ya Usajili wa Nyaraka (Sura ya 117); na Sheria ya Usajili wa Rehani ya Mali Zinazohamishika (Sura ya 210). Pia itakamilisha muswada wa sheria uthamini na usajili wa Wathamini na kuendelea kuzifanyia mapitio Sheria za Ardhi ili ziendane na matakwa ya wadau. Natoa wito kwa wadau wa sekta ya ardhi kutoa maoni yao mara watakaposhirikishwa ili kuboresha sheria hizo.

MAWASILIANO SERIKALINI

92. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya ardhi. Katika mwaka 2011/12 Wizara kupitia vyombo vya habari: redio, televisioni na magazeti, ilitoa elimu kwa umma kuhusu huduma zake, sera, mikakati, sheria na kanuni. Kadhalika ilitoa machapisho mbalimbali na kuyasambaza wakati wa maonesho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara. Kwa mwaka 2012/13 Wizara itaendelea kuimarisha Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kwa kuajiri wataalam wa mawasiliano na kuongeza vitendea kazi. Wizara itahuisha mkakati wa mawasiliano (Communication Strategy) kwa kupanua ushirikishaji wa wadau wa sekta.

HUDUMA ZA UTAWALA NA RASILIMALI WATU

93. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu iliendelea kuboresha na kusimamia rasilimali watu kwa kutoa mafunzo kwa watumishi, kuboresha mazingira ya kazi na kutoa vitendea kazi, kuwapatia watumishi stahili zinazoendana na ajira zao, kusimamia nidhamu ya watumishi, kusisitiza kuhusu utawala bora, kupiga vita rushwa na kuendeleza mapambano dhidi ya UKIMWI.

94. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12 Wizara yangu iliendelea kuwawezesha watumishi kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi. Katika kipindi hicho jumla ya watumishi 190 walipandishwa vyeo na 5 walithibitishwa kazini. Aidha, watumishi 586 walihudhuria mafunzo mbalimbali kama ifuatavyo:- Mafunzo ya muda mrefu na mfupi ndani na nje ya nchi watumishi 60, mafunzo yaliyohusu maadili katika utumishi wa umma watumishi 206, mafunzo elekezi ya awali kwa waajiriwa wapya 106, na mafunzo kuhusu utunzaji wa siri na nyaraka za serikali kwa watumishi 214 (Jedwali Na. 15). Kwa mwaka 2012/13, Wizara inatarajia kuwapatia mafunzo watumishi 400 katika fani mbalimbali.

95. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/2012 Wizara yangu iliendelea na ujenzi wa kituo cha huduma kwa mteja (customer service centre) makao makuu ya Wizara. Kazi hii ipo katika hatua za mwisho kukamilika. Kituo hiki kitawezesha mteja kupata huduma za ardhi sehemu moja.

96. Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa michezo kwa afya za watumishi, katika mwaka 2011/12 Wizara yangu ilishiriki katika mashindano ya SHIMIWI na kufanikiwa kupata ushindi wa pili katika mpira wa pete na ushindi wa tatu katika mpira wa miguu. Wizara ilizawadiwa vikombe na medali. Aidha, Wizara imeendelea kuelimisha watumishi juu ya namna ya kujihadhari na UKIMWI na kuhamasisha watumishi kupima afya zao.

Watumishi waliojitambulisha kuwa wanaishi na virusi vya ukimwi wameendelea kupatiwa huduma na msaada wa fedha kwa ajili ya dawa na lishe. Kwa mwaka 2012/13 Wizara yangu itaendelea kushiriki katika michezo na kutoa huduma kwa watumishi wanaoishi na virusi vya UKIMWI na kuendelea kuhamasisha upimaji wa afya za watumishi.

Vyuo vya Ardhi

97. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inasimamia vyuo vya Ardhi vya Tabora na Morogoro ambavyo vinatoa mafunzo ya Stashahada (Ordinary Diploma) katika fani za urasimu ramani na upimaji ardhi, na Cheti (Certificate) katika fani za umiliki ardhi, uthamini na uchapaji ramani. Fani zinazofundishwa katika vyuo hivi zinakidhi mahitaji ya soko la wataalam wa sekta ya ardhi.

Katika mwaka 2011/12 walihitimu wanafunzi 153. Kati ya hao, 92 walitoka Chuo cha Ardhi Morogoro na 61 walitoka Chuo cha Ardhi Tabora. Kati ya wahitimu hao wanawake ni 31 na wanaume ni 122 (Jedwali Na.16). Naomba nisisitize kuwa Halmashauri ziajiri wataalam hawa ili kuziba pengo la ajira lililopo katika maeneo yao. Wataalam wanaohitimu katika vyuo hivi ndio wanaofanya kazi uwandani (field work). Sioni sababu ya baadhi ya Halmashauri kutokuwa na watumishi wakati vyuo vyetu vinatoa wataalam kila mwaka.

98. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, Wizara imekamilisha ujenzi wa bweni la wavulana katika Chuo cha Ardhi Tabora ikiwa ni hatua muhimu katika kuongeza udahili na kuboresha huduma ya malazi kwa wanafunzi. Kutokana na kukamilika kwa ujenzi wa bweni hili, mwaka 2012/13 Wizara itaongeza idadi ya wanafunzi watakao dahiliwa katika chuo cha Ardhi Tabora. Pia, vyuo hivi vitaandaa na kutekeleza mpango wa mafunzo ya muda mfupi kwa wataalam wa sekta ya ardhi katika Halmashauri zote nchini kwa lengo la kuboresha utaalam wao. Mafunzo hayo yatatolewa kwa wataalam walioko katika taasisi za umma na sekta binafsi kwa kuwasilisha maombi. Natoa wito kwa taasisi za umma hasa Halmashauri kutumia fursa hii kuwapeleka wataalam wao kujifunza ili waende sanjari na mabadiliko ya teknolojia.

SHUKRANI

99. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu ina majukumu mengi na yanayogusa moja kwa moja Watanzania wote. Ni mategemeo yangu kwamba, Bunge litaendelea kuwa na mtizamo chanya na kuipa kipaumbele sekta ya ardhi kwa ujumla ili kuiwezesha kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

100. Mheshimiwa Spika, mafanikio yaliyofikiwa na Wizara yangu ni kutokana na kuwepo kwa ushirikiano kati ya Serikali na Wadau wa Maendeleo zikiwemo taasisi za fedha za kimataifa, nchi wahisani, taasisi zisizokuwa za kiserikali na mashirika ya kidini. Wadau hao ni pamoja na Benki ya Dunia, Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa (UN-HABITAT), Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ); na Serikali za Denmark, Sweden, Uholanzi na Uingereza kupitia Mradi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (Business Environment Strengthening for Tanzania); na Serikali za Finland na Norway.

101. Mheshimiwa Spika, kwa mara nyingine napenda kumshukuru Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa Goodluck Ole-Medeye (Mb), kwa kunisaidia katika kutekeleza majukumu yangu. Pia napenda kumshukuru Katibu Mkuu Bw. Patrick Rutabanzibwa, na Naibu Katibu Mkuu Bibi Maria Bilia kwa ushirikiano mkubwa wanaonipa. Nawashukuru Wakuu wa Idara na Vitengo, Makamishna Wasaidizi na Wasajili Wasaidizi wa kanda, viongozi wa taasisi zilizo chini ya Wizara, watumishi na wataalamu wote wa sekta ya ardhi kwa kunisaidia katika kutimiza majukumu yangu kwa ufanisi. Naomba waendelee kutekeleza majukumu yetu kwa kujielekeza katika kuiwezesha ardhi kuwaondolea wananchi umaskini. Natambua kuwa Wizara yangu haina nyenzo na rasilimali za kutosha kutimiza matarajio ya Watanzania, lakini hata kwa kutumia rasilimali chache zilizopo kwa uangalifu tutatoa mchango mkubwa kwa Taifa. Mwisho, namshukuru Mpigachapa Mkuu wa Serikali kwa uchapisha Hotuba hii kwa wakati.

HITIMISHO

102. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2012/13 Wizara yangu imeazimia kutekeleza mipango ya kuendeleza ardhi, nyumba na makazi ili kufikia malengo yaliyoainishwa kwenye kaulimbiu ya Kilimo Kwanza na Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 – 2015/16). Aidha, mbali na kuunda Wakala wa Kuendeleza Mji Mpya wa Kigamboni (KDA), Serikali itakamilisha uanzishaji wa chombo kitakachosimamia utoaji wa ardhi kwa wawekezaji kwa utaratibu mpya wa wananchi kutumia ardhi kama mtaji (land for equity). Vilevile, itahakikisha kuwa migogoro ya ardhi inayoendelea kujitokeza inatafutiwa ufumbuzi na kuzuia migogoro mingine isitokee.

103. Mheshimiwa Spika, kwa hali hiyo Wizara yangu imejipanga kutayarisha mipango ya kuendeleza miji na vijiji na kuisimamia, kupanga matumizi ya ardhi, kupima ardhi, kuhakiki milki, kusajili na kutoa hati ili kuwezesha kuwepo kwa usalama wa milki. Natoa rai kwa mamlaka na asasi mbalimbali kutoa ushirikiano unaotakiwa kuhakikisha kuwa ardhi inaziwezesha sekta zote ili kufikia malengo ya maisha bora kwa kila Mtanzania.

MAOMBI YA FEDHA KWA MWAKA 2012/13

104. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imejipanga kutekeleza majukumu yake iliyojiwekea ili kufikia malengo ya MKUKUTA II, Dira ya Taifa ya 2025, Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 – 2015/16), Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2010 na Malengo ya Milenia. Hivyo, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu liidhinishe Makadirio ya Mapato na Matumizi kama ifuatavyo:-

  1. (i) Mapato:

    Mapato ya Serikali Sh. 99,816,438,480

    (ii) Matumizi ya Kawaida

    Matumizi ya Mishahara Sh.10,422,891,000

    Matumizi Mengineyo (OC) Sh. 20,308,831,000

    Jumla Shilingi Sh. 30,731,722,000


  2. (iii) Matumizi ya Miradi ya Maendeleo

    Matumizi ya Maendeleo

    o Fedha za Ndani   Sh. 61,000,000,000

    o Fedha za Nje Sh. 10,000,000,000

    Jumla Shilingi Sh. 71,000,000,000

    Jumla ya Matumizi ya Mishahara, Matumizi Mengineyo na Matumizi ya Miradi ya Maendeleo ni Shilingi 101,731,722,000.

105. Mheshimiwa Spika, napenda kukushukuru tena wewe na Waheshimiwa Wabunge wote kwa kunisikiliza. Hotuba hii inapatikana kwenye tovuti ya Wizara www.ardhi.go.tz.

106. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

page84image2720


By Jamhuri