Nimesikiliza kauli ya Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro, kuhusu kupatikana kwa Mo Dewji. IGP Sirro amesema pamoja na mengi mengine kwamba wanaotafuta uadui na Jeshi la Polisi wasije wakalaumu litakapowatokea la kutokea.

Kwake yeye, kukosoa utendaji wa Jeshi la Polisi katika masuala makubwa kama utekaji nyara wa raia ni kukosa uzalendo.

Amehoji uraia wetu wote ambao tumekosoa sana utendaji wa Jeshi la Polisi katika sakata hili la utekaji nyara wa Mo Dewji na Watanzania wengine, baadhi yao wakiwa hawajapatikana kwa karibu miaka miwili. Badala ya kulaumu wakosoaji, IGP Sirro anahitaji kujiangalia katika kioo yeye na Jeshi la Polisi analoliongoza.

1. Kwa ushahidi wa hili la Mo Dewji peke yake, Jeshi la Polisi limeonyesha hadharani udhaifu mkubwa katika utendaji kazi wake na katika mawasiliano yake na umma:

(i) Je, Mo Dewji alitekwa na Wazungu wawili (RPC Mambosasa, Oktoba 11, 2018); au na watu wanaozungumza mojawapo ya lugha za makabila ya Afrika Kusini (RPC Mambosasa, alfajiri Oktoba 20, 2018); au na watu wanaozungumza Kiingereza na Kiswahili cha hovyo hovyo (IGP Sirro, asubuhi ya Oktoba 20, 2018)?

(ii) Je, gari lililotumika kumtekea Mo Dewji (picha zilitolewa na IGP Sirro Oktoba 19, 2018) ni lile lile lililotumika kumrudisha uraiani (picha za Oktoba 20) kweli? Hata kwa muuza mihogo wa barabarani Dar es Salaam, picha za gari hilo zilizotolewa na Jeshi la Polisi zinaonyesha tofauti kubwa sana.

(iii) Je, Mo Dewji aliwasilianaje na ndugu zake baada ya kuachiliwa usiku wa Oktoba 20? Tuliambiwa na RPC Mambosasa (Oktoba 11, 2018) kwamba alidondosha funguo na simu yake wakati anatekwa nyara. Oktoba 20 tumesikia kwa ndugu zake kwamba baada ya kuachiwa usiku ule, aliwapigia simu ndipo wakaenda kumchukua alikotupwa bila kulitaarifu Jeshi la Polisi.

Je, alidondosha simu yake siku ya kutekwa, au alikuwa nayo muda wote wa siku tisa akiwa mateka, au watekaji walimrudishia simu yake wakati wanamwachia? Je, ni kitu kinachoingia akilini kwamba alikuwa na simu yake kwa siku tisa bila kuichaji? Je, inaingia akilini kwamba watekaji wake walimwachia akae na simu yake muda wote huo? Je, inaingia akilini kwamba watekaji wake watakuwa wamempa simu ili awasiliane na ndugu zake baada ya kumwachilia huru?

(iv) Gari lililotumika kumtekea liliingia kutokea Kenya (IGP Sirro, Oktoba 19, 2018), lakini namba za usajili (AGC 404 MC) zinasemekana ni za Msumbiji. Namba za usajili za gari la Oktoba 20 (?304 AXX) ni za wapi? Hii habari mbona haijakaa sawa Afande IGP?

(v) Picha za gari tulizoonyeshwa tangu Oktoba 11 hadi leo ni za CCTV au ni za SisiTV? Kama ni za CCTV kweli mbona zinatofautiana sana na zinazoonyeshwa na BBC, CNN au Al Jazeera katika sakata la mwandishi wa habari Jamal Khashoggi? Kama ni za SisiTV, nani amezitengeneza, na kwa malengo gani?

2. Kutekwa kwa Mo Dewji si tukio la kawaida, lakini si la kwanza tangu Rais Magufuli aingie madarakani. Wanaokosoa utendaji wa Jeshi la Polisi wamehoji na kuunganisha na matukio mengine ya aina hii ambayo hayajapewa uzito wowote ule na Jeshi la Polisi:

(i) Msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Ben Saanane, ametoweka tangu Novemba 2016 hadi sasa na Jeshi la Polisi halijatoa taarifa yoyote rasmi kwa umma; na licha ya madai ya wabunge, serikali haijatoa taarifa yoyote rasmi kwa umma. Kama alivyo Mo Dewji, Ben Saanane ni Mtanzania na ana ndugu na familia vilevile.

(ii) Mwandishi wa habari Azori Gwanda wa Gazeti la Mwananchi aliyekuwa anachunguza taarifa za mauaji ya askari na raia Kibiti, Mkuranga na Rufiji amepotea tangu Februari 2017, baada ya kuchukuliwa nyumbani kwake Dar es Salaam na watu waliokuwa kwenye gari lenye vioo vyeusi. Na yeye pia ni raia wa nchi hii mwenye ndugu na familia.

(iii) Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko, Mkoa wa Kigoma, Simon Kanguye, naye amepotea baada ya kuchukuliwa nyumbani kwake na watu wanaodaiwa kuwa wa vyombo vya dola. Hadi leo hii mwaka umepita na hajaonekana na hakuna taarifa yoyote rasmi ya Jeshi la Polisi au ya serikali kuhusiana na kupotea kwa Mwana CCM huyu.

(iv) Kuna raia zaidi ya 300, kwa taarifa zilizotolewa bungeni, ambao wametoweka baada ya kuchukuliwa na askari polisi kutoka majumbani, mashambani na madukani kwao, na wengine hata misikitini katika maeneo mbalimbali ya Kibiti, Kilwa, Mkuranga na Rufiji. Hadi sasa hakuna taarifa yoyote rasmi ya Jeshi la Polisi au ya serikali kuhusu kutoweka kwao. Hawa wote ni Watanzania waliokuwa na haki ya kulindwa na Jeshi la Polisi na wana ndugu na familia vilevile.

(iv) Wasanii Roma Mkatoliki na Ney wa Mitego nao walitekwa nyara, lakini wakaachiliwa katika mazingira yanayofanana na hili la Mo Dewji baada ya kelele kubwa ya umma mitandaoni na kwingineko. Hadi leo hii Jeshi la Polisi liko kimya na matukio hayo.

3. Zaidi ya utekaji nyara, kuna matukio ya mauaji yenye sura ya kisiasa ambayo Jeshi la Polisi limeyanyamazia hadi sasa:

(i) Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo, aliuawa kwa kukatwa mapanga mchana kweupe mwezi Novemba 2015. Hadi sasa hakuna taarifa yoyote rasmi ya Jeshi la Polisi.

(ii) Diwani Luena wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero (Chadema) naye aliuawa kwa kukatwa mapanga usiku. Hadi leo hii Jeshi la Polisi liko kimya.

(iii) Katibu Kata ya Hananasif (Chadema), Daniel John, alitekwa nyara na baadaye maiti yake kuokotwa Coco Beach, Dar es Salaam. Jeshi la Polisi liko kimya hadi leo.

(iv) Mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji Dar es Salaam (DIT), Akwilina Akwilini, aliuawa mchana kweupe na askari polisi maeneo ya Kinondoni. Polisi waliohusika na mauaji hayo wamesafishwa na Jeshi la Polisi, hivyo hakuna taarifa yoyote rasmi juu ya nani hasa ndiye mhusika hadi sasa.

4. Mashambulio ya mabomu (mkutano wa hadhara wa kampeni za uchaguzi wa marudio Soweto, Arusha, Kanisa Katoliki Olasiti, Arusha na ofisi za Kampuni ya mawakili ya IMMA Advocates ya Dar es Salaam, Julai 26, 2017); na mashambulizi ya risasi dhidi yangu Dodoma, Septemba 7, 2017, yamenyamaziwa na Jeshi la Polisi hadi sasa.

Hapa bado hatujagusa tukio la kujihami kwa mfanyabiashara Peter Zakaria kule Tarime, aliyedaiwa kutekwa na watu ‘wasiojulikana’, lakini akajihami kwa kuwajeruhi kwa risasi.

Katika mazingira haya, IGP Sirro anawezaje kuwashangaa watu wanapohoji utendaji na uadilifu wa Jeshi la Polisi?

Tunahitaji majibu ya maswali haya, si vitisho vya wale tunaowalipa mshahara ili wawe na majibu sahihi badala ya propaganda. Tuna wajibu wa kuhoji. Kuyanyamazia haya ni kuungana na watekaji nyara na wauaji. Tunakataa kunyamaza kimya.

Mwandishi wa makala hii, Tundu Lissu, ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), ambaye kwa mwaka mzima sasa yuko nje ya nchi akitibiwa majeraha ya risasi.

Please follow and like us:
Pin Share