Miongoni mwa maneno muhimu na ninayoyakubali kwa asilimia mia yaliyowahi kusemwa na Mwalimu Julius K. Nyerere, ni haya: “Inawezekana kufanyika, timiza wajibu wako.”

Tumezoea kusikia watu wengi wakilalamika; na ngao kubwa ya kutofanya mambo makubwa huwa wanajikinga na ngao ya umaskini. Utasikia wakisema: “Kwetu tulikuwa maskini wa kutupwa, wazazi wangu hawakuweza kumudu kununua hiki na kile.”

Muda mwingine utasikia wakilalamikia watu wengine kwa kuwasababisha wao kuwa katika hali waliyomo. Mara utasikia: “Ooh asingekuwa mwalimu yule mimi nisingeshindwa shule au kufeli.”

Kumbuka rafiki yangu unapomnyooshea mwingine kidole kwamba yeye ni sababu ya kushindwa kwako, vidole vitatu vinakugeukia wewe na kuonyesha kwamba tatizo ni wewe wala si yule unayemnyooshea kidole. Kidole kingine kinaelekea juu kuweka ushuhuda kwa Mungu kwamba wewe ndiye tatizo.

Jiulize kabla haujaanza kusema wazazi wangu walikuwa maskini ndiyo maana leo hii bado nipo maskini, umefanya jitihada gani za kutoka katika lindi la umaskini ulilokuwa nalo? “Kuzaliwa maskini si kosa lako, kosa lako ni kufa maskini,” anatukumbusha Bill Gates, ambaye ni tajiri namba mbili duniani na mwanzilishi wa Kampuni ya Microsoft.

Ukikubali kufanya sehemu yako na kujitoa kwa ukamilifu, hakuna siku ambayo utakuja kumnyooshea mtu kidole kwa kusababisha wewe usifanikiwe. Kila kitu kinawezekana kama ukifanya sehemu yako. Timu ya mpira hupata ushindi pale ambapo kila mchezaji hucheza kwenye namba yake kwenye viwango vya juu.

Haijalishi leo uko katika mazingira gani, ukikubali kucheza namba yako kwa viwango vya juu siku moja tutaongea lugha nyingine.

Usiseme jambo fulani haliwezekani, maana: “Ukisema siwezi, akili yako huacha kufanya kazi na ukisema, ‘nitawezaje?’ akili yako huanza kufanya kazi,” anasema Robert Kiyosaki, mwandishi wa vitabu vya mambo ya biashara na uchumi. Kwa msingi huo naunga mkono hoja ya Henry Ford, mwanzilishi wa Kampuni ya Ford Motors aliyewahi kusema: “Ukifikiri hauwezi, unaweza. Upo sahihi.” Jinsi unavyoiweka akili yako ndivyo unavyoweza kufanikisha jambo fulani.

Bado unasema mambo hayawezekani na unaendelea kuwalalamikia watu wengine? Haya sasa sikia hii. Luka Modric – mchezaji bora wa UEFA mwaka huu wa 2018 na mwenyeji wa nchi ya Croatia, ni mmoja wa watu waliokulia katika mazingira magumu.

Akiwa na miaka mitano vita ya kupigania uhuru wa Croatia ilianza. Aliishi katika mazingira ambayo vita ilikuwa ikipiganwa na katika wakati huo babu yake aliuawa.

Ilimlazimu yeye na familia yake kuishi katika kambi za wakimbizi huku akiwa anacheza mpira wa kufuma na kamba na makaratasi.

Anasema kwake kelele za makombora, mizinga na risasi zilikuwa kelele za kawaida mno, kama wewe unavyosikia kelele za miziki mtaani kwenu.

Vita ilipokwisha akaanza kucheza mpira wa miguu. Timu aliyoipenda, Klabu ya Hajduk ilimkataa na kusema alikuwa mdogo sana, na ana uzito mdogo pia, na kwamba hawezi kufika popote.

Lakini baba yake akamwambia: “Songambele mwanangu, jiamini.” Baba yake hakuwa na pesa za kumpeleka katika shule za mpira wala hata pesa za kumnunulia viatu vya kuchezea mpira.

Hakukata tamaa. Aliendelea kucheza na hatimaye aliweza kuichezea timu yake ya taifa. Ilifika muda akasaini mkataba na timu ya Tottenham, lakini wakasema eti hawezi kuchezea Uingereza. Hakukata tamaa, akaendelea kusakata kandanda na kuwashangaza wengi. Leo hii anachezea timu maarufu duniani – Real Madrid. Hapo ndipo ninapokuja kuamini msemo wa Muhammad Ali anaposema: “Kutowezekana si azimio, ni kutothubutu. Kutowezekana ni uwezo. Kutowezekana si kitu.”

Kila kitu kinawezekana kama ukiamua kufanya sehemu yako. Soma wakati wengine wamelala. Amua wakati wengine wanazubaa.

Andaa wakati wengine wanaota ndoto za mchana. Anza wakati wengine wanaghairi. Fanya kazi wakati wengine wanatamani. Weka akiba wakati wengine wanatanua.

Sikiliza wakati wengine wanaongea, maana ukiongea unaongea yale unayoyajua na ukisikiliza unajifunza yale ambayo ulikuwa huyajui.

Tabasamu wakati wengine wananuna. Kuwa sugu na komaa wakati wengine wanakata tamaa na kuacha. 

Please follow and like us:
Pin Share