Furaha ni mtihani. Si kila tabasamu ni ishara ya furaha na si kila chozi ni ishara ya huzuni. Si kila kicheko ni ishara ya furaha na si kila kilio ni ishara ya masikitiko. Kwa msingi huo, furaha ni mtihani. Si kila maneno, “karibu sana” ni ishara ya furaha na si kila maneno “kwaheri nitakukosa” ni ishara ya huzuni.

Kwa msingi huo, furaha ni mtihani. Watu wanaposalimiwa kwa maneno, “habari ya asubuhi” na wanajibu “njema”, wanasema njema hata kama si njema. Watu wengi wanapata wanachokitaka maishani lakini si watu wengi wanafurahia walichokipata. Furaha ni mtihani.

Furaha haipo katika kutokuwa na imani. François-Marie Arouet, mwandishi na mwanafalsafa kutoka Ufaransa alikuwa mmojawapo wa watu ambao hawakuwa na imani, aliandika: “Natamani nisingezaliwa.” Hakuwa na furaha. Furaha haipo katika anasa. Lord Byron aliishi maisha ya anasa, lakini aliandika: “Huzuni ni yangu peke yangu.” Hakuwa na furaha. Furaha kamili haipo katika pesa. Jay Gould, milionea wa Marekani alikuwa na pesa kama njugu. Alipokuwa katika hali ya kufa alisema: “Nafikiri, mimi ni mtu mwenye taabu sana duniani.” Hakuwa na furaha. Ndugu msomaji unajisikiaje ikitokea ukakaa siku mbili bila elfu tano mfukoni? Utajibu mwenyewe. Furaha haipo katika cheo na umaarufu. Lord Beaconsfield alikuwa na vyote, lakini aliandika: “Ujana ni kosa, utu uzima ni hangaiko, uzee ni majuto.” Hakuwa na furaha. Furaha haipo katika utukufu wa kijeshi. Alexander the Great aliishinda dunia ya wakati wake. Baada ya kufanya hivyo alilia katika hema lake, alisema: “Hakuna himaya zaidi za kushinda.” Hakuwa na furaha.

Watu wanatafuta furaha katika mambo mbalimbali. “Anthony alitafuta furaha katika mapenzi; Brutus katika utukufu; Ceasar katika utawala; wa kwanza alipata aibu, wa pili alipata maudhi, wa tatu alipata kutoshukuriwa,” aliandika C.C. Colton katika kitabu chake kilichoitwa Lacon (1820).

Hao waliotajwa hapo hawakupata furaha kamili na furaha ya ukweli. Je, furaha ipo katika vitu? Tony de Mello anasema katika kitabu chake cha Awareness: “Tuna kila kitu tunachokihitaji, hivyo tunapaswa kufurahi. Tatizo tulilonalo ni kwamba tunataka kuitambua furaha yetu kwa vitu ambavyo hatuna na uwezekano wa kuvipata ni mdogo sana.” Badala ya kutafuta furaha katika vile ambavyo hatuna, kwanini tusitafute furaha katika vile tulivyonavyo? Lakini hata hivyo vitu havitupi furaha kamili.

Kuna maeneo ambapo furaha inajificha. Kwanza, furaha ipo katika kuungana na Mungu. Pili, furaha ipo katika eneo la kuwafanya wengine wawe na furaha. Kila siku mfanye mtu mmoja awe na furaha, katika kipindi cha miaka arobaini utawafanya watu 14,600 wawe na furaha. Furaha ni kama marashi, huwezi kumpulizia mtu bila kupata matone. Tatu, furaha inajificha katika eneo la shukrani.

“Shukrani inaweza kubadili siku za kawaida kuwa siku za shukrani, kubadili kazi za kila siku kuwa  furaha, na kubadili fursa za kawaida kuwa baraka,” alisema William Arthur Ward.

Nne, furaha ipo katika eneo la mambo madogo madogo. Carol Holmes alithibitisha hilo: “Maisha yenye furaha yanafanywa na mambo madogo madogo, zawadi inapotumwa, barua inapoandikwa, mtu anapoitwa, barua ya kumpendekeza mtu inapotolewa, usafiri unapotolewa, keki inapotengenezwa, unapoazima, cheki inapotumwa.”

Tano, huduma kwa wengine ni eneo ambapo furaha inajificha. Sita, furaha inapatikana katika eneo la kupenda na kupendwa. Saba, furaha inakaa katika eneo la kutoa na kupokea. Nane, furaha inajificha katika eneo la kuwa na jambo la kutumainia, jambo la kupigania au jambo la kufia. Tisa, eneo la shughuli ni eneo la furaha. Chapa kazi, shughulika. Mtu mwenye shughuli nyingi hana muda wa kutokuwa na furaha. Kumi, eneo la mtazamo chanya ni eneo la furaha. Usifikirie uliyoyapoteza, fikiria uliyoyapata, fikiria upande mzuri wa maisha.

Please follow and like us:
Pin Share