Wiki iliyopita makala haya yaliishia Mbunge Hafidh Ali Tahir, alipoiomba Serikali kuweka utaratibu wa kuchinja. Je, unajua majibu aliyotoa waziri? Endelea…

Waziri wa Mifugo wa kipindi hicho, Anthony Diallo, akijibu ombi hilo alitoa msimamo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu uchinjaji.  Ninamnukuu kama alivyonukuliwa katika uk. 88 wa Hansard ya Bunge.


Anasema, “Kwa hiyo, muuzaji nyama yeyote ni lazima atazingatia kitu ambacho ni desturi na mila na matakwa ya wanunuzi wa nyama hiyo. Kwa  hiyo, hatuhitaji kuweka kwenye sheria kwa sababu tunafahamu Serikali yetu haina dini na hatuwezi kuanza kuingiza vifungu vya kutamka mahitajio ya dini moja au dhehebu  moja ndani ya sheria tunakiuka Katiba ambayo inatukataza Serikali isijihusishe na uhuru wa dini ni wa kila mtu sio wa Serikali.”


Huu ndiyo msimamo wa Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu suala la uchinjaji wa wanyama ambao haujawahi kutenguliwa na sharia nyingine yoyote. Hii ni kusema hakuna sheria yoyote inayosema mtu wa dini fulani ndiye anayeruhusiwa kuchinja. Mtu yeyote anaruhusiwa kuchinja kwa sharti la kuhakikisha kuwa kile kilichochinjwa, kimekaguliwa na Ofisa Mifugo wa Serikali kama kinafaa kwa matumizi ya binadamu, au la.


Kwa hiyo, kutokana na migogoro inayojitokeza katika jamii yetu kuhusiana na uchinjaji wa wanyama, na kwa kuzingatia majibu haya ya Serikali yetu, ni jukumu la Serikali kuelimisha watumishi wake, hususan maofisa mifugo waelewe msimamo wa Serikali kuhusu suala la uchinjaji kwa sababu wao ndiyo walioko huko kwenye machinjio ya wanyama.


Kwa kufanya hivyo watakuwa wameondoa kabisa migogoro kuhusiana na suala hili. Vinginevyo, Serikali haiwezi kukwepa lawama kuwa inawabagua watu wengine wasio Waislamu kwa kuwapa Waislamu haki zaidi ya wengine.


Lakini pia kwa Serikali isiyo na dini kama Tanzania watu wote wanayo ruhusa ya kuchinja hata kama ni kwa ajili ya jamii maadamu chakula hicho kitakaguliwa na maofisa wa mifugo kama kinafaa kuliwa na binadamu.


Migogoro hii ikiendelea itakuwa inaendelezwa na Serikali ambayo inawatoza kodi raia wake wote bila kujali dini zao ili kujenga machinjio ya Serikali lakini matumizi ya machinjio hayo yahodhiwe na watu wa dini moja. Serikali isipofanya hivyo na yenyewe itakuwa inaongezea nguvu ubaguzi huu wa dhahiri.


Tunaposoma Qur’an, kitabu kinachoiongoza dini ya Kiislamu, kinaeleza kuwa wanaotakiwa kuchinja wanyama kwa ajili ya chakula na chakula hicho kuwa halali kwa Waislamu na Wakristo wametajwa kwamba ni Waislamu, Wayahudi na Manasara (Wakristo).


Tunasoma hayo katika Suratul Al-Maidah, 5:5 “Leo mmehalalishiwa kila vilivyo vizuri na chakula cha wale waliopewa kitabu ni halali kwenu na chakula chenu ni halali kwao……..”

Kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu waliopewa kitabu ni Wayahudi na Wakristo (Manasara).


Unaposoma ufafanuzi wa aya hiyo ndani ya Qur’an unasema, “Chakula cha kuchinja hakiwi halali kwa Mwislamu ila kichinjwe na (a) Mwislamu (b) Myahudi (c) Mnasara (Mkristo) kwa sharti la kuchinja siyo kuwanyonga.”


Hivyo mbali na Mwislamu, Myahudi na Mkristo pia wanayo ruhusa ya kuchinja na Mwislamu akala bila hofu yoyote.

Daniel anapatikana kwa simu: 0687931313


Please follow and like us:
Pin Share