Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mbozi
Mahakama ya Wilaya ya Mbozi imemuhkumu kifungo cha maisha mfanyabiashara Athumani Mohamed Mtimbwa (35) kwa kosa la kumvuta na kumuingiza katika kibanda chake cha biashara na kumbaka mwanafunzi wa darasa la awali mwenye umri wa miaka minne.
Mbali ya adhabu hiyo pia mtuhumiwa ametakiwa kulipa fidia ya sh milioni 1 kwa muhanga.
Mtimbwa alikamatwa Oktoba 21, 2024 maeneo ya kiwandani Mlowo Wilaya ya Mbozi, ilielezwa mahakamani hapo kuwa, Mtimbwa alitekeleza tukio hilo la ubakaji kwa kumvizia muhanga akiwa anatoka shule na kumvuta kwa nguvu kisha kumuingiza katika kibanda chake cha biashara na kumbaka mwanafunzi wa darasa la awali mwenye umri wa miaka 04.
Akitoa hukumu hiyo Julai 29, 2025 kesi namba 32392 ya mwaka 2024 Mheshimiwa Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Mbozi, Nemes Chami amesema Mahakama imejiridhisha pasipo na shaka ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri na kumtia hatiani mtuhumiwa huyo.
Mshtakiwa amehukumiwa kifungo pamoja na fidia hiyo ili iwe fundisho kwa watu wengine wanaojihusisha na vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto.
