*Ameichezea Stars miaka 15, sasa yu hohe hahe

*Sura yake ilipamba stempu kwenye miaka ya 1980

*Azzan: Ngoja wafe… msome wasifu wao mrefu

Majibu ya Serikali kuhusu kutomsaidia Nahodha wa zamani wa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Jellah Mtagwa, yamewaudhi baadhi ya wabunge.

Hatua hiyo ilimfanya mmoja wao, Mbunge wa Nzega, Dk. Khamis Kigwangalla, aombe mwongozo wa Spika kutokana na majibu yasiyoridhisha yaliyotolewa na Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla. Mtagwa amekuwa Nahodha kwa Taifa Stars kwa miaka 15.

 

Swali la msingi lililoulizwa na Mbunge wa Kinondoni, Iddi Azzan (CCM), ambaye alisema kwa kuwa Serikali imeshindwa kuwaenzi baadhi ya wana michezo walioliletea Taifa sifa kubwa, je, ni kwanini Serikali inashindwa kumpatia matibabu Mtagwa, na je, Serikali ina mkakati gani wa maisha ya baadaye ya wachezaji wa timu za Taifa?

 

Akijibu maswali hayo, Makala alisema, “Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba kulialifu Bunge lako tukufu kwamba Serikali haijaweka utaratibu rasmi wa kuwaenzi baadhi ya wana michezo walioliletea Taifa sifa kubwa.

 

“Utaratibu unaotumika kwa sasa na ambao siyo rasmi, ni ule ambao viongozi wa juu wa Serikali na sekta binafsi huwapa zawadi wachezaji wanaofanya vizuri kwenye mashindano mbalimbali na wengine hupewa tuzo zinazotolewa na asasi zisizo za kiserikali kama vile Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA).

 

“Hata hivyo, tunaangalia uwezekano wa kuanzisha utaratibu wa kuwaenzi wanamichezo mahiri na pindi tutakapopata namna bora inayotekelezeka tutawafahamisha wananchi.”

 

Kuhusu Serikali kutompatia matibabu Nahodha wa zamani wa Timu ya Taifa, Mtagwa, Naibu Waziri alisema, “Ningependa ifahamike kwamba mchezaji huyo amepatwa na matatizo akiwa amekwishastaafu kucheza mpira katika klabu aliyoichezea mwishoni ya Pan African. Baada ya kuichezea Timu ya Taifa, mchezaji huyo wa zamani aliendelea kuichezea Pan African na kuifundisha timu ya Pan African.”

 

Makalla akahitimisha jibu la msingi kwa kusema, “Kimsingi Wizara yangu haina utaratibu wa kugharimia tiba ya wanamichezo wanaoumia wakiwa michezoni au wakiwa wamestaafu. Inapotokea wanamichezo hao wakaumia wakiwa na timu za Taifa hugharimiwa moja kwa moja na vyama vinavyosimamia michezo husika au kupitia bima walizowekewa.

 

“Kwa wachezaji wanaoumia wakiwa na klabu zao, hugharimiwa tiba na klabu zenyewe. Hata hivyo, panapokuwepo na uwezo na kwa maombi maalumu, Wizara yangu imekuwa ikisaidia gharama za wanamichezo wanaoumia wakiwa na timu za Taifa.”

 

Majibu hayo ya Serikali yalimfanya Azzan aulize swali la nyongeza. Akionekana mwenye hasira, alisema, “Majibu hayaridhishi. Ngoja wafe, msome wasifu mrefu…pengo lake halitazibika .”

 

Katika maelezo ya swali lake la nyongeza, Azzan alisema Mtagwa ni kielelezo cha Tanzania kwani amekuwa nahodha wa Timu ya Taifa ya mpira wa miguu kwa miaka 15. Akasema umaarufu wake uliifanya Serikali iweke sura yake kwenye stempu.

 

“Serikali ilikusanya mamilioni ya shilingi, leo anaumwa kwa michezo hiyo. Je, Serikali haioni muhimu kutoa gawio hilo la stempu zimsaidie Mtagwa?”

 

Katika majibu yake, Makalla, alisema Serikali haiwakatishi tamaa wachezaji. Akasema upo utaratibu wa wachezaji katika ajira zao ambako wanapata haki zao zote. Akaongeza kuwa Kanuni ya 11 na 12 (za mpira wa miguu) inataka ngazi zote kuanzia daraja la nne hadi Taifa kuwakatia bima wachezaji wao. “Wana haki ya kupata matibabu kutoka kwa mwajiri.”

 

Makalla akatoa mfano wa wachezaji waliokwishasaidia na Serikali, akiwamo Lawrence Mwalusako na John Akhwari.

 

Alikiri kuwa Mtagwa ana sifa kubwa, lakini akasisitiza kuwa endapo Serikali itaamua “kuwatunza” wachezaji wote maarufu, itakuwa nao wengi. “Tutakuwa nao wengi, Serikali itakuwa ikibeba …itakuwa na msururu.”

 

Baada ya kipindi cha maswali na majibu, ndipo Dk. Kigwangalla alipoomba mwongozo wa Spika akitaka kujua ni hatua gani kinachopaswa kufanywa kutokana na Naibu Waziri kushindwa kujibu swali la namna Mtagwa anavyoweza kunufaika na mapato makubwa yaliyotokana na mauzo ya stempu.

 

Spika Makinda, kwa namna ambayo haikukata kiu ya wabunge, alimtetea Makalla kwa kusema, “Mbona ameshalijibu swali hilo?” Mjadala wa majibu hayo ya Serikali baadaye uliendelea nje ya ukumbi wa Bunge, kwa wabunge wengi kuonyesha kutoridhishwa na majibu ya Serikali.

 

 

Please follow and like us:
Pin Share