Epuka kuishi maisha ya kujitenga. Kujitenga na wenzako kunakuletea upweke. Mtaalamu wa magonjwa ya akili na Profesa wa Chuo Kikuu cha Harvard, Robert J. Waldinger, katika programu yake inayojulikana kama TED, inayopatikana katika mtandao wa kijamii wa YouTube anasema: “Tatizo la upweke hugeuka kuwa sumu. Watu ambao wamejitenga zaidi kuliko wanavyotaka kuwa, hujikuta wanadhoofika kiafya katika umri wao wa kati, utendaji wa ubongo wao hufifia haraka na huishi maisha mafupi kuliko watu wasio wapweke.”  

Mama mmoja alinisimulia kisa cha  kusisimua sana:

“Mr. Bhoke, pole kwa majukumu. Ninakushukuru sana kwa makala yako nzuri. Ninaomba kukusimulia kisa kilichonipata katika maisha yangu. Mimi ni mama wa familia niliyebahatika kuzaa mtoto mmoja, jina lake anaitwa [..]. Sikufanikiwa kuishi na mume wangu kwa muda mrefu.

“Nikiwa na ujauzito, mume wangu alifariki dunia kwa ajali ya gari. Baada ya miezi mitatu ya kifo cha mume wangu nilijifungua salama mtoto wa kiume. Nimehangaika na mwanangu mpaka amekua na sasa anajitambua. 

“Ninakumbuka ilikuwa Juni 16, 2014 mwanangu akiwa na umri wa miaka 26 aliamua kuniumiza. Ninapata wakati mgumu kukueleza kisa hiki, lakini ninaomba nikueleze. Huwa si kawaida ya mwanangu kuingia chumbani kwangu. 

“Hiyo tarehe 16 nikiwa chumbani kwangu, ghafla mwanangu aliingia na kunishika kwa nguvu akinitaka nishiriki naye tendo la ndoa. Haaaa! “Nilishangaa kwa mshangao wa kuumiza. Nilimuuliza; unataka nini mwanangu? Akakaa kimya. Ilinilazimu kupiga kelele ili kupata msaada.  

“Baada ya mwanangu kuona nimelia kwa uchungu sana aliniacha na kutokomea kusikojulikana. Mr William, kuanzia siku hiyo nilimlaani mwanangu.” 

Baada ya kuupata ujumbe huu sikuweza kuvumilia. Nilimtafuta mama huyu. Ashukuriwe Mungu nilimpata mama huyu na nikapata fursa ya kukaa naye. Majeraha aliyokuwa nayo yalikuwa yanamuumiza sana. Aliniuliza: “William, kwa nini mume wangu alikufa mapema?” Swali hili nilishindwa kulijibu. Majeraha aliyokuwa nayo mama huyu ni kama kidonda kibichi ambacho kinavuja damu.

Mama huyu aliona suluhisho pekee la kumkomoa mwanaye ni kumlaani. Naomba kukufundisha somo fupi juu ya laana. 

Laana inafunga milango ya baraka. Laana inatabiri mwisho mbaya. Inawezekana maisha yako yana misukosuko kwa sababu umewahi kulaani ama kujilaani wewe mwenyewe. 

 Je, umejilaani mara ngapi kwamba hautafanikiwa katika maisha yako? Umewalaani mara ngapi watoto wako? Umewalaani mara ngapi wazazi wako? Umewalaani mara ngapi ndugu zako? Umewalaani mara ngapi majirani zako? Umemlaani mara ngapi mke/mume wako? Umeilaani mara ngapi ardhi yako unayoishi? Umeilaani mara ngapi kazi yako?

Unapojitabiria maneno mabaya ni kama unajilaani. Unaposema: “Sitafanikiwa katika jambo hili,” ni kama unajilaani. Futa laana uliyowahi kujinenea. Futa maneno mabaya uliyowahi kujitamkia au kutamkiwa na wengine.  Kana kila aina ya maagano uliyowahi kufungamana nayo. Jiweke huru kuanzia sasa.

Ninaomba kukuuliza swali: “Je, moyoni mwako umebeba nini?” Ni amani? Ni upendo? Umebeba nini? Kama umembeba mtu, mtue. Mtue mume wako aliyekuumiza. Mtue mke wako aliyekuumiza. Mtue mtoto wako aliyekuumiza. Mtue jirani yako aliyekuumiza. Mtue mzazi wako aliyekuumiza kwa kukubaka, kukunyanyasa, kukutukana, kukukataa n.k. Mtue rafiki yako aliyekuumiza. Mtue mfanyakazi mwenzako aliyekuumiza. Mtue mteja wako aliyekudhulumu fedha na rasirimali nyinginezo.

Kama una kinyongo, kidondoshe. Kama umeitunza hasira, iondoe. Itafute amani. Utafute upendo. Kristo anasubiri kukuponya. Anasubiri kuyaponya majeraha yako. Anasubiri uwe tayari kuyaachilia yote uliyoyatunza moyoni mwako. Amua kuwa huru kuanzia leo. Toka huko gerezani ulipofungwa. Balidilisha historia ya maisha yako kuanzia leo.

Watu wengi tumejeruhiwa katika maisha yetu. Tunayo majeraha mengi yanayotutesa. Tunazo kumbukumbu mbaya ambazo zinatutesa. Tumeshindwa kuzisahau kumbukumbu hizi mbaya. Wengine historia ya miaka ya nyuma inatutesa. Historia za koo zetu zinatutesa. Tumruhusu Yesu Kristo atuponye majeraha tuliyo nayo. Yeye ndiye tiba pekee ya majeraha yetu. Yeye anajua chanzo cha majeraha yetu na tiba yake.  Mruhusu Yesu Kristo aseme neno juu ya maisha yako.

Hitimisho: Ni nani umeshindwa kumsamehe katika maisha yako? Kwa nini umeshindwa kumsamehe? Je, umepata faida gani kwa muda ambao umeshindwa kumsamehe huyo uliyeshindwa kumsamehe? Unafikiri utaendelea kumweka moyoni mwako mpaka lini? Nisikilize: Acha kuteseka. Acha kuutesa moyo wako. Acha kubeba mzigo wa maumivu ndani ya nafsi yako. Naomba utoe msamaha. Msamehe aliyekuumiza. Haijalishi kama yupo hai au la. Tamka msamaha wako leo.  Nakutakia mafanikio mema. Mungu akubariki sana.

500 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!