Jifunze kushukuru katika maisha (2)

Katika sehemu ya kwanza ya makala hii wiki iliyopita tuliona umuhimu wa mtu kutimiza wajibu wake kwa kutoa shukrani. 

Tuliona msemo wa mwandishi Fred De Witt Van Amburgh anayetukumbusha: “Shukrani ni fedha ambayo tunaweza kujitengenezea sisi wenyewe na kuitumia bila kuogopa kufilisika.”

Duniani hakuna majonzi ambayo mbingu haiwezi kuyaponya. Tujiponye majeraha tuliyonayo kwa kushukuru.

Nitakuwa sahihi kabisa nikisema kwamba, kutoa shukrani si tu ni tendo la ‘unyenyekevu’ lakini pia ni jambo ambalo linahochea fadhila. Kukosa shukrani ni alama ya kiburi. Tafakari jambo hili: Unashindwaje kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyekuumba kwa sura na mfano wake? Unashindwaje kumshukuru mke/mume wako kwa ushirikiano wake mzuri anaokuonyesha? Unashindwaje kuwashukuru wazazi wako kwa zawadi ya malezi bora waliyokupatia? Unashindwaje kumshukuru jirani yako kwa uwepo wake? Wahenga walisema: “Asiye na shukrani ni mtumwa.” Jifunze kutumia maneno ya shukrani katika maisha yako. Shukrani ni wajibu.

Shukrani ni mlango wa mafanikio ya kiroho, kimwili, kiuchumi, kiuongozi na kifamilia. Shukrani ni mlango utakaokufungulia mambo mengi katika maisha yako. Shukrani itakuunganisha na mambo mengi ambayo awali hukudhania kuwa yanaweza kuja upande wako.

Kumbuka kumwambia Mungu asante kwa kuniumba. Kumbuka kumwambia mke/mume wako asante kwa kuwa mke/mume wangu. Shukrani isitolewe tu kwa mtu aliyekuzidi kitu fulani. Hata wale uliowazidi nao wanapaswa kupewa shukrani wanapokutendea jambo jema au wakati mwingine hata jambo baya, kwa sababu haujui makusudi ya Mungu kwa jambo hilo.

Shukuru kwa kila kitu, kibaya au kizuri, ambacho kinatokea katika maisha yako. Usisubiri kushukuru kwa mazuri tu, kwa sababu hata mabaya nayo yanatumika kujenga maisha yako.

Kwa hiyo kumbuka kumwambia mtoto wako asante kwa kuwa mtoto wangu. Kumbuka kumwambia jirani yako asante kwa kuwa jirani yangu mwema. Kumbuka kumwambia rafiki yako asante kwa kuwa rafiki yangu. Kumbuka kumwambia mfanyakazi wako asante. Kumbuka kumwambia mfanyakazi mwenzako asante kwa kuwa rafiki katika kazi hii. Kumbuka kuiambia furaha yako asante. Kumbuka kuyaambia mafanikio yako asante. Kumbuka kuyaambia magumu unayokumbana nayo asante. 

Neno asante ni neno la kimiujiza. Yule mwandishi wa kale aitwaye Tecumseh (1768-1813) anasema: “Unapoamka asubuhi toa shukrani kwa ajili ya uhai wako na nguvu.  Toa shukrani kwa ajili ya chakula chako na furaha yako ya kuishi. Kama huoni sababu ya kushukuru, kosa liko kwako.”

Kushukuru ni kubariki na kubarikiwa.  Kushukuru ni kuridhika. Kushukuru ni kufanya maisha yawe na ladha na maana. Mwandishi wa Marekanni Melody Beattie anasema: “Shukrani hufungua utimilifu wa maisha. Inageuza tuliyonayo kuwa ya kutosha zaidi. Shukrani inageuza mlo kuwa sherehe, nyumba kuwa maskani, mgeni kuwa rafiki. Shukrani huleta maana kwa mambo yetu yaliyopita na zaidi hutengeneza ndoto ya kesho. Shime mwanadamu mwenzangu jifunze na palilia tunu ya shukrani.”

Ndugu msomaji na rafiki yangu mwema, naomba utulie kidogo. Tafakari mapito ya maisha uliyopitia. Sema asante Mungu. Rudia tena kusema, asante Mungu.  Leo kabla hujafikiri kusema neno baya, mfikirie mtu yule asiyeweza kuzungumza. Kabla hujalaumu kuhusu ladha na aina ya chakula, mfikirie mtu yule ambaye hana chochote cha kula. Kabla hujalaumu kuhusu mke/mme wako, mfikirie mtu yule anayemlilia Mungu ampe mwenzi. Leo kabla haujalaumu kuhusu maisha, mfikirie mtu yule aliyefariki dunia mapema akiwa na mipango lukuki katika kichwa chake. Kabla haujalaumu kuhusu watoto wako, mfikirie mtu yule aliye na shauku ya kupata watoto na wakati yeye ni tasa. Wahenga walisema: “Moyo usio na shukrani hukausha mema yote.”

Moja ya deni ambalo hakuna binadamu yeyote anaweza kulilipa ni deni la shukrani. Kama ningekuwa na uwezo wa kulipa madeni yote niliyokopa au kukopeshwa na Mungu au watu ningelipa mengi lakini nisingeweza kuyamaliza yote.  Moja ya deni ambalo nisingeweza kumlipa Mungu na watu wema ni deni la shukrani. 

Katika maisha yetu sisi binadamu tunatendewa mema mengi na Mwenyezi Mungu, lakini ni mara chache sana tunakumbuka kumshukuru. 

Kuna namna mbili za kuishi maisha yako. Namna ya kwanza ni kuishi kwa kushukuru.  Shukuru kwa sababu Mungu amekuumba kwa sura na mfano wake.  Mwanadamu ni kiumbe pekee aliyeumbwa na Mungu kwa mfano wake.