Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita (kushoto) na Mkurugenzi wa Jiji, Sipora Liana.
Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita (kushoto) na Mkurugenzi wa Jiji, Sipora Liana.

Serikali imemkabidhi Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mkoa wa Dar es Salaam jukumu la kukusanya mapato ya maegesho ya magari kuanzia Februari mwaka huu.

Mratibu wa TARURA Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi George Tarimo, ameliambia Gazeti la JAMHURI kwamba mchakato wa zabuni ya ukusanyaji wa mapato ya maegesho ya magari bado unaendelea. 

Mhandisi Tarimo amesema wanasubiri kumalizika kwa mkataba baina ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na Kampuni ya Excel Parking Services (EPS), mkataba huo unamalizika mwishoni mwa Januari, mwaka huu. 

“Siwezi kueleza zaidi kuhusu suala hili hadi mchakato wote utakapokamilika, lakini tutakachohakikisha ni malengo ya makusanyo kupatikana kila mwezi,” amesema Mhandisi Tarimo.

TARURA inakusudia kutumia huduma za mawakala kukusanya ushuru unaotokana na maegesho ya magari katika maeneo ya hifadhi za barabara zote zilizo chini ya mamlaka yake katika Mkoa wa Dar es Salaam.

TARURA katika kutekeleza majukumu yake hayo iliwakaribisha watu binafsi, taasisi, kampuni na vikundi vya watu vilivyosajiliwa kisheria na kutambuliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kufanya kazi hiyo.

Wakala huyo wa serikali iliwataka wenye nia na uwezo wa kufanya kazi za uwakala wa kukusanya ushuru unaotokana na maegesho ya magari katika maeneo ya hifadhi za barabara watume maombi yao kwa ajili ya zabuni hizo.

Zabuni zilizotangazwa ni uwakala wa ukusanyaji ushuru wa maegesho ya magari katika hifadhi ya barabara zilizo chini ya TARURA katika halmashauri za Manispaa ya Kinondoni, Ubungo, Ilala, Temeke na Kigamboni.

“Wakala atakayepewa tuzo ya zabuni atapatiwa mashine za kielektroniki ‘Point of Sale Machines’ na ‘Roller’ zitakazotumika kukusanyia mapato kulingana na idadi ya ‘Parking Slots’ zilizomo katika zabuni atakayoshinda.

“Mzabuni anaweza kuomba zabuni moja au zote mbili, endapo atashinda zote atapewa mkataba wa zabuni moja tu na kwamba atatakiwa kukusanya ushuru si chini ya viwango vilivyotajwa katika mkataba wake,” inasema sehemu ya taarifa ya TARURA.

Pia taarifa hiyo imeeleza kuwa wakala atawajibika kununua vifurushi vya mtandao kwa ajili ya mashine za ‘Point of Sale (POS)’ na kuhakikisha zipo hewani muda wote wa kazi ili kuiwezesha TARURA kupata taarifa sahihi za makusanyo ya kila siku.

Sharti jingine ni wakala kukusanya mapato ya siku na kuyaweka kwenye akaunti ya TARURA Makao Makuu siku inayofuata kabla ya muda uliotajwa katika mkataba wake.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, muda wa mkataba wa uwakala utakuwa kwa kipindi cha mwaka mmoja tangu siku ya kusaini mkataba na uzoefu wa miaka mitatu wa kukusanya mapato ya maegesho kwenye majiji.

Akizungumza na Gazeti la JAMHURI, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya EPS, Hassan Khan, ameliambia JAMHURI kuwa kampuni yake imeomba zabuni hiyo kupitia TARURA lakini bado hawajapata jibu lolote hadi sasa.

“Tumewafahamisha wafanyakazi wetu kwamba mwishoni mwa mwezi huu mkataba wetu utafikia mwisho na iwapo EPS haitashinda zabuni hiyo waombe kazi katika kampuni itakayoshinda,” amesema Khan.

Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita, amesema makusanyo ya ushuru huo kuanza kukusanywa na TARURA kutaliweka jiji hilo katika msukosuko mkubwa wa mapato.

“Kweli tutapata msukosuko, lakini naamini mipango imewekwa vizuri na Mkurugenzi wa Jiji na yeye ndiye msemaji, hivyo atakuwa na majibu sahihi,” amesema Mwita.

Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Sipora Liana, ameliambia Gazeti la JAMHURI kuwa bado taratibu za suala hilo zinaendelea na zitakapokamilika zitawekwa wazi kwa kila mmoja, ikiwemo vyanzo mbadala vya mapato kwa jiji hilo.

Bajeti na makusanyo

Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam katika mwaka wa fedha wa 2017 na 18 ilipitisha bajeti yake ya Sh bilioni 16.413 kutegemea vyanzo mbalimbali vya mapato ikiwemo ushuru wa maegesho.

Jiji la Dar es Salaam lenye idadi ya watu zaidi ya milioni 5 likiwa na halmashauri sita ambazo ni Kigamboni, Kinondoni, Ubungo, Ilala, Temeke na Halmashauri ya Jiji bado lina nafasi kubwa ya kubuni vyanzo vipya vya mapato.

Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni katika bajeti yake ya mwaka wa fedha wa 2017/2018, mapato ya ndani ni Sh bilioni 9.218 lakini ikakusanya Sh bilioni 5.478 ikiwa ni asilimia 59.

Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni katika mwaka huo wa fedha makadirio ya bajeti yake kwa mapato ya ndani ni Sh bilioni 31.619 na makusanyo halisi yalikuwa ni Sh bilioni 29.754 ikiwa ni asilimia 94.

Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo makadirio yake ya bajeti yalikuwa Sh bilioni 16.505, ikakusanya Sh bilioni 13.496 sawa na asilimia 81.8.

Halmashauri ya Manispaa ya Ilala walipanga kukusanya Sh bilioni 46.621 na makusanyo yalikuwa Sh bilioni 44.505 ikiwa ni asilimia 95.5.

Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam makadirio ya mapato ya ndani kwa mwaka yalikuwa ni Sh bilioni 16.413 na wamekusanya Sh bilioni 16.849 sawa na asilimia 102.

Halmashauri ya Manispaa ya Temeke katika bajeti yake ya mwaka wa fedha 2017/2018 walipanga kukusanya Sh bilioni 30.910, wamepata Sh bilioni 29.034 sawa na asilimia 94.

Jumla ya Sh bilioni 151.290 zilipangwa kukusanywa halmashauri zote za Dar es Salaam, lakini wakafanikiwa kukusanya Sh bilioni 139.118 sawa na asilimia 91.95.

Priscus Emily, mfanyabiashara katika Soko Kuu la Kariakoo jijini Dar es Salaama, amesema ushuru wa maegesho ya magari umekuwa mzigo mkubwa kwa watu wanaofanya shughuli zao katika maeneo ya soko hilo.

Emily amesema licha ya msongamano wa watu na magari katika soko hilo mtu anayeegesha gari lake kwa muda wa saa moja anatozwa Sh 500 na kwa siku nzima analazimika kulipa Sh 4,500.

“Ukiegesha gari katika kipindi cha mwezi mmoja unalazimika kulipa Sh 135,000 na ukiongeza kodi ya pango ya chumba cha duka kwa mwezi Sh milioni 2 ni mzigo mkubwa sana,” amesema Emily.

Amesema pamoja na kuliomba Jiji la Dar es Salaam kupunguza ushuru huo wa maegesho, hakuna hatua zozote zilizochukuliwa hadi sasa na kwamba TARURA itakapoanza kutoza ushuru huo iweke gharama ambazo zitakuwa rafiki kwa wananchi wote.

By Jamhuri