Jiweke karibu na vitu vinavyoongeza uwezo wa kufikiri. Ukitaka kuongeza fikra zako lazima utumie vitu vinavyokuingizia fikra kichwani kwako. Lazima uongeze maarifa. Na njia pekee ya kuongeza maarifa na ufahamu ni kujifunza kila siku.

Soma vitabu, soma makala mbalimbali, soma magazeti yenye mafunzo na taarifa sahihi (siyo ya udaku), tazama video za youtube zinazofundisha na kuhamasisha, jikutanishe na watu wenye maarifa. Tembelea maeneo mapya, Waswahili hawakukosea waliposema, tembea uone. Unapotembelea maeneo mbalimbali unaweza kukutana na fursa tofauti, lakini kujua yale mambo mengi ambayo kabla hukuyajua.

Hakikisha unakuwa mtu wa kujifunza kila siku iitwayo leo. Usiache kujifunza maana maisha siku zote hayaachi kufundisha. Sina shaka na wewe kwa sababu umeamua kusoma maandiko haya, hivyo utakuwa unatafuta maarifa yatakayokuongezea uwezo wa kufikiri.

Njia nyingine ya kuwa mtu mwenye fikra kubwa ni kujenga ukaribu na watu wenye fikra kubwa. Ukikaa karibu na waridi utanukia waridi. Ukikaa karibu na watu wanaofikiri mambo mazuri utakuwa unajiweka katika nafasi nzuri ya kuwa kama wao.

“Kama unataka kuwa mpishi mkuu aliyebobea katika upishi, lazima ufanye kazi na wapishi wakuu waliobobea. Hicho ndicho kitu nilichofanya,” alisema Gordon Ramsay.

Kitu cha kujua hapa ni kwamba watu wa namna hii hutengeneza urafiki na watu wanaofikiri kama wao. Ndege wenye mbawa zinazofanana huruka pamoja. Kumbe watu wenye fikra kubwa daima hujenga ukaribu. Kama huwezi kujijenga na kuwa mtu mwenye fikra kubwa watu hao hawawezi kamwe kutengeneza urafiki na wewe maana wanajua wewe ni sumu.

Jenga urafiki na watu unaotaka kuwa kama wao, tembelea maeneo wanayotembelea, soma vitabu wanavyosoma, wafuatilie wanapenda mambo gani. Kama wanatumia mitandao ya kijamii kuwa mfuasi wao maana sasa hivi dunia imebadilika. Unaweza kujenga urafiki na mtu aliye mbali na mahali unakoishi, usijifunge kwa kukaa na marafiki wa sehemu unayoishi. Tafuta watu walio bora zaidi yako.

“Kama chumba ulichomo wewe ndiye bora zaidi ya wote, chumba hicho hakikufai,” anasema Grant Cardone, mwandishi wa vitabu, mshauri wa mambo ya biashara na mwekezaji katika majengo.

Tatu, jenga tabia ya kuviongezea vitu thamani. Unapoona vitu usivione kwa umbo lake la nje, bali jitahidi kuvipa uthamani. Usiangalie vitu kama vilivyo, bali vinavyoweza kuwa. Baada ya Steve Jobs kuona kompyuta inachukua nafasi ya chumba kizima aliona inaweza kupunguzwa ukubwa huo. Leo hii kuna kompyuta mpakato (laptop). Moja kati ya maswali ambayo huwa ninapenda kuwauliza watu ili wajenge tabia ya kuongezea thamani kwenye vitu ni hili: Fundi seremala, akiona mti anaona mbao nzuri ya kutengenezea samani za kuuzwa pale Keko Modern Furniture.

Ndege, wao huona sehemu ya kutengenezea viota vya makazi na kutua. Precious, anaona sehemu ya kupigia picha.

Mimi naona kivuli cha kupumzika kubadilishana mawazo na wenzangu.

Majuhudi, mganga wa mitishamba anaona dawa ya kutibu presha, sukari na magonjwa yasiyopungua saba.

Savai, mwalimu wa hisabati anaona fimbo nzuri, imara na zilizonyooka za kuwachapia wanafunzi waliofanya vibaya kwenye somo lake.

Rafiki yangu Godius Rweyongeza yeye anaona kurasa zisizopungua mbili za kitabu chake cha Kutoka Sifuri Hadi Kileleni, akisema: “Ukitaka kufanikiwa jifanye kama mti. Refuka uwezavyo usiangalie miti mingine.”

Raymond Nusura Mgeni naye anaona utenzi mzuri wa kuusifia mti.

Je, wewe unaona nini? Inawezekana wewe pia una majibu yako, lakini nia yangu hasa ilikuwa ni kukufikirisha na kuona ni kwa namna gani unaweza kuongeza thamani kwenye vitu vilivyokuzunguka. Mungu aliumba kila kitu kwa mahitaji ya mwanadamu, lakini alimwachia mwanadamu aweze kuona vitu alivyoviumba na kuviongezea thamani.

Aliumba miti, akijua kwamba samani zote kama vile viti, meza na vitanda tutavipata humo. Akaumba wanyama akijua kwamba ngozi za kutengeneza viatu na mikanda tutazipata huko. Akaumba na pamba akijua nguo zetu tutazipata huko, kutaja machache. Jenga tabia ya kuongeza thamani kwenye yale unayoyaona ya kawaida, u-kawaida ni udumavu.

By Jamhuri