Wakati Serikali ya Awamu ya Tano ikisisitiza ubanaji matumizi, Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) ya jijini Arusha, imebainika kukodisha nyumba na kulipa mamilioni ya shilingi kila mwaka bila kuitumia. Nyumba hiyo ipo Kitalu ‘C’ eneo la Njiro jijini humo. 

Imekodiwa kwa malipo ya Sh 1,500,000 kwa mwezi kwa maelekezo ya makamu mkuu wa chuo, licha ya kuwapo ukinzani kutoka kwa Baraza la Uongozi la Chuo. Huu ni mwaka wa tatu malipo hayo yakifanywa kila mwezi.

Uchunguzi umebaini kuwa Sh milioni 43 zimeshatumika kumlipa mmiliki wa nyumba na mlinzi kwa upangaji huo ‘hewa’.

JAMHURI inaendelea kufanya utafiti kumjua mmiliki wa nyumba hiyo ingawa kwenye ankara ya maji jina la mmiliki linasomeka la Mina Said Mohamed, lakini kwenye ankara ya Luku jina ni la Saum Ally Said.

“Kwanza hakuna umuhimu wa nyumba hiyo kwani tuna nyumba nyingi sana na za kisasa zilizo tupu ndani ya chuo, tuna Researchers Village nyumba zake ziko tupu ndani ya chuo, na tuna Rest House ndani ya chuo. Pamoja na kupiga sana kelele katika Baraza la Uongozi la Chuo, mkuu wa chuo hajakubali kuiachia nyumba hiyo.

Makamu Mkuu wa NM-AIST, Profesa Burton Mwamila, anajibu tuhuma hizo kwa kukiri kukodiwa kwa nyumba hiyo.

“Siyo kweli kwamba nyumba hiyo imekuwa haitumiki. Awali, ilikuwa inatumiwa na aliyekuwa Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma, Utafiti na Ubunifu, Profesa Dunstan Shemwetta. Baada ya Profesa Shemwetta kuondoka, nyumba hii imekuwa ikitumiwa na wataalamu wanaoletwa na washirika wetu kutoka nje ya nchi ambao wanakuja kufanya kazi mbalimbali hapa chuoni ikiwa ni pamoja na kufundisha, utafiti na ubunifu, kwa mujibu wa makubaliano kati ya chuo chetu na taasisi husika.

“Hivi karibuni nyumba hiyo ilikuwa inatumiwa na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Wageningen nchini Uholanzi na baada ya wataalamu hao kuondoka, ilitegemewa kuwa wataalamu wa mradi wa pamoja na Taasisi ya Kimataifa ya Kilimo katika Nchi za Tropiki (International Institute of Tropical Agriculture – IITA) wangeingia mara moja, lakini taratibu za wao kuanza kazi zilichelewa.

“Kwa sasa tunategemea kuwa wataalamu kutoka India ambao watakuwa wanajenga uwezo wa chuo katika kuendesha Kituo cha Tehama (ICT Resource Centre), ambao watakuwa hapa chuoni kwa miaka mine, wataishi katika nyumba hiyo.

“Nyumba zilizopo chuoni ni chache, na zimetengwa kwa ajili wa wahadhiri kutoka nje ya nchi, ambao wengine ajira zao bado zinashughulikiwa na Ofisi ya Rais (Utumishi), Wizara ya Kazi na Ajira, na Uhamiaji.”

Hata hivyo, JAMHURI imefika katika nyumba hiyo na kujiridhisha kuwa hakuna mpangaji wala mgeni anayeishi humo. Majani yametanda eneo lote kuanzia katika lango hadi ndani ya uzio.

Mtoa habari wetu amesema: “Hapa anaishi mlinzi tu kusaidia mali zisiibwe ndani. Nyumba hii inalipwa kutokana na soko la nyumba kwa sasa Arusha kuwa gumu. Kinachofanywa ni viongozi wa chuo kuingia mkataba huu ili mwenye nyumba apate, na wao wapate fedha. Nakuhakikishia nyumba hiyo haitumiwi na chuo, lakini kila mwezi kuna kodi inalipwa.”

Katika hatua nyingine, imebainika kuwa viongozi kadhaa wa NM-AIST wanaishi katika nyumba zinazolipiwa kiasi kikubwa cha fedha kinyume cha maelekezo yaliyo kwenye waraka wa Serikali wenye kumbukumbu Na. TYC/T/200/583/18.

Waraka unaagiza viongozi hao wakuu watumie Sh 800,000 kwa mwezi.

Makamu Mkuu wa NM-AIST, Profesa Mwamila, amepanga nyumba Njiro Block ‘F’ inayolipiwa dola 900 za Marekani (zaidi ya Sh 1,800,000) kwa mwezi.

Makamu Mkuu wa Chuo, Lughano Kusiluka, anaishi katika nyumba iliyopo Njiro ambayo malipo yake kwa mwezi ni dola 800 za Marekani (zaidi ya Sh 1,600,000) kwa mwezi.

Pia kuna mtu mwingine anayetajwa kuwa rafiki wa karibu na Profesa Mwamila, mwajiriwa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambaye amepangishiwa nyumba inayolipiwa na NM-AIST. 

“Kwa miaka mitatu amempa nyumba ya taasisi yenye samani zote bure; halipi umeme wala maji. Wakati profesa huyo si mfanyakazi wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela. Matokeo yake, nyumba hiyo inatumika mara chache mno ikitokea yeye au familia yake wamekuja Arusha,” kimesema chanzo chetu.

Kwenye mlolongo huo, Profesa Mwamila anatajwa kumpa nyumba ya kuishi mmoja wa ndugu zake (jina tunalihifadhi kwa sasa) katika ‘Researchers Village” ilhali akiwa si mwajiriwa wa taasisi.

Profesa Mwamila anajibu tuhuma hizo kwa kusema: “Stahili na maslahi ya viongozi wakuu wa chuo vimeainishwa kwenye nyaraka mbalimbali za Serikali na maamuzi (uamuzi) ya Baraza la Uongozi la Chuo ambalo ni chombo cha juu cha maamuzi (uamuzi) katika ya taasisi kwa mujibu wa Hati Idhini (Charter) ya Chuo.

“Aidha, wakati nyumba hizo zinapangishwa na mikataba kuandikwa, dola moja ya Marekani ilikuwa sawa na shilingi Kitanzania takribani 1,000 na kwa bahati mbaya wenye nyumba wengi Arusha wanapangisha kwa dola. Ongezeko la bei linatokana na kuporomoka kwa shilingi.

“Hata hivyo, nyumba anayoishi makamu mkuu wa chuo na wasaidizi wake ni za hadhi ya kawaida tu na gharama zake zinalingana na hali ya soko la nyumba katika Jiji la Arusha ambazo ziko juu sana.”

NM-AIST ilizinduliwa mwaka 2012 na kuanza kazi zake rasmi mwaka 2013. Tofauti na majibu ya Profesa Mwamila, wakati huo dola moja ya Marekani ilikuwa sawa na wastani wa Sh 1,600.

Anaongeza: Profesa (jina tunalihifadhi) hakuwahi kuajiriwa na NM-AIST pamoja na kwamba aliomba kwani taratibu hazikukamilika. Si kweli kwamba anatumia nyumba ya chuo anapokuwa Arusha, lakini alikuwa anatumia nyumba ya chuo wakati anakuja kufundisha chuoni kwa muda fulani tu (part-time). Chuo kiliamua kuwa akae ndani ya kampasi anapokuwa amekuja kufundisha badala ya kukaa hotelini, ambao ni utaratibu unaotumika kwa wahadhiri wote wanaokuja kufundisha hapa chuoni kwa muda.”

NM-AIST ilianzishwa na Serikali. Ilifunguliwa rasmi na Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete, Novemba 2012. Lengo kuu la chuo ni kuiwezesha Tanzania kupata wataalamu wake katika utafiti wa sayansi na teknolojia. Ujenzi wake uliogharimu dola milioni 60 za Marekani ulitokana na fedha za Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSPF), Mfuko wa Jamii kwa Wafanyakazi wa Mashirika ya Umma (PPF), Mfuko wa Akiba kwa Watumishi wa Serikali za Mitaa (LAPF), na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).

3258 Total Views 2 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!