Na Mwandishi Wetu, JamhuriMdia, Dar es Salaam
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imesaini mkataba wa kushirikiana na Shirika la UNA VOCE PER PADRE PIO lililopo nchini Italia kuwasaidia watoto wenye magonjwa ya moyo waliopo barani Africa.
Mkataba huo umesainiwa leo jijini Dar es Saalam baada ya kuona maendeleo makubwa yaliyopo katika Taasisi hiyo kwa ukubwa Afrika na Taasisi ya kipekee inayoweza kuwasaidia watoto wenye matatizo ya moyo barani Afrika.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kusaini mkataba huo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema kupitia mkataba huo Shirika la UNA VOCE PER PADRE PIO watakuwa wanawachukua watoto wenye magonjwa ya moyo kutoka nchi mbalimbali Afrika na kuwafikisha JKCI kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji wa moyo.

Siku ya jana Shirika hili limewaleta watoto watatu kutoka nchini Cameron ambao tayari tumewapokea na watafanyiwa upasuaji wa moyo kesho”, alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge alisema Shirika hilo limeingia mkataba na JKCI ili waweze kuchukua watoto wenye magonjwa ya moyo waliopo barani Afrika na kuwapeleka JKCI kufanyiwa upasuaji wa moyo lakini pia kulipia gharama za matibabu ya watoto hao.
“Kupitia mkataba huu nchi yetu itaendelea kutangaza utalii tiba na hii ni kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali kupitia Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza kwenye vifaa tiba na rasilimali watu”, alisema Dkt. Kisenge.
Kwa upande wake Rais wa Shirika la UNA VOCE RER PADRE PIO la nchini Italia Palumbo Vincenzo alisema Shirika hilo linathamini maisha ya watoto hivyo kuona umuhimu wa kuwasaidia kwa njia mbalimbali ikiwemo kusaini mkataba na JKCI kwani wakiokoa maisha hata ya mtoto mmoja ni muhimu kwao.

Vincenzo alisema wamekuwa wakiifahamu JKCI kuwa ni taasisi kubwa na yenye viwango vya juu katika kutoa huduma za upasuaji wa moyo barani Afrika na kutokana na uhaba wa huduma hizi katika nchi nyingine za Afrika wakaona ni vizuri kuitumia JKCI kuokoa maisha ya watoto.
Vincenzo alisema wanaona fahari na bahati kubwa kushirikiana na kusaini makubaliano na JKCI kwani ni Taasisi kubwa yenye viwango vya juu Afrika hivyo kuifanya Tanzania kuwa kituo kikubwa cha matibabu ya magonjwa ya moyo Afrika
“Tunawashukuru kwa kutupa nafasi hii kushirikiana nanyi, tunaahidi kuwa sehemu ya kuleta maendeleao katika kutoa huduma za upasuaji wa moyo na tutaitangaza Tanzania kama kituo kikubwa cha kutoa huduma za upasuaji wa moyo kwa watoto”, alisema Vincenzo.
Naye Mkurugenzi wa Upasuaji wa Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya alisema Shirika hilo kutoka Italia limekubali kufanya kazi na JKCI ya kuwasaidia watoto wa Afrika wanaohitaji kupata huduma ya matibabu ya moyo.
JKCI imekuwa ikifanya matibabu ya upasuaji wa moyo kwa kiwango kikubwa lakini katika Africa ndio Taasisi pekee inayofanya upasuaji wa aina mbalimbali na ule ambao ni mgumu kwa watoto wenye magonjwa ya moyo.
“Tunashukuru tumepata washirika ambao wataweza kusaidia kuwalipia na kuwawezesha watoto kutoka nchi za Afrika kupata matibabu ya kibingwa ya upasuaji wa moyo ambayo hawawezi kuyapata katika nchi zao”, alisema Dkt. Angela.