Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imeanzisha huduma mpya za tiba mtandao na huduma ya kufuatilia maendeleo ya mgonjwa anayetibiwa akiwa nyumbani kwa kutumia kifaa kijulikanacho kwa jina la DOZEE.

Hayo yameelezwa na Daktari wa Moyo kutoka JKCI, Marsia Tillya kwenye banda la taasisi hiyo lililopo katika maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (DITF) maarufu kama Sabasaba.

Amesema katika maonesho hayo wananchi 883 kutoka maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam na mikoa jirani wamefanyiwa uchunguzi wa awali wa magonjwa ya moyo.

“Kati yao 196 wamefanyiwa kipimo kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (ECHO), 212 kipimo cha umeme wa moyo (ECG) na wengine wamepimwa uzito, kisukari na kupewa ushauri kuhusu lishe,” amesema.

Amefafanua kuwa, baadhi ya watu walioonwa wamebainika kuwa magonjwa ya milango ya moyo ambao wamepewa rufaa kwenda katika taasisi hiyo kwa ajili ya uchunguzi zaidi na matibabu endelevu na wengine wamebainika kuwa na presha lakini hawajui, wenye uzito uliopitiliza na wenye kisukari.

“Tumewafanyia vipimo na kuwapa elimu ya lishe na kuwasaidia jinsi ya kufanya mabadiliko kwenye maisha yao, tumewapa elimu ya jinsi ya kuishi na ugonjwa wa kisukari na kuna ambao tumewaanzishia tiba na wengine tumewaelimisha umuhimu wa kuendelea na kliniki ya moyo au ya sukari.

“Tunahimiza jamii wajitokeze zaidi kufanya uchunguzi, ni vizuri kujua afya yako kabla tatizo halijatokea hivyo, tunawakaribisha waje kwenye banda letu tunatoa elimu na watakutana na madaktari tofauti,” amesema Dk. Tillya.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano JKCI, Anna Nkinda, amesema watu hao wamehudumiwa tangu yalipoanza maonesho hayo na wanatarajia idadi itaongezeka kutokana na kuwapo kwa mwitikio mkubwa.

Amesema wanashiriki katika maonesho hayo kwa kutoa huduma za upimaji na matibabu ya moyo ambapo wanapima vipimo vya damu, kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi, mfumo wa umeme wa moyo, vipimo vya sukari, uzito na ushauri wa lishe.

“Tunaomba wananchi waje Sabasaba katika banda letu kwa sababu huduma tunazotoa tumepunguza gharama, watapata ushauri wa jinsi ya kutumia dawa za moyo, ushauri wa lishe na tunao madaktari wa watu wazima na watoto,” amesema Nkinda.

Aidha amesema katika maonesho hayo wanawaelekeza watu namna ya kupata huduma ya tiba mtandao ambapo mgonjwa anaweza kutibiwa kokote aliko kwa kuchagua daktari anayemtaka.

Nkinda amesema pia wana huduma ya matibabu ya moyo kwa wagonjwa majumbani ambapo mgonjwa hupewa kifaa maalumu kinachowekwa chini ya kitanda chake ili kufuatilia presha, oksijeni na umeme wa moyo ambacho kimeunganishwa na simu ya daktari anayemtibu.

“Kama kukitokea tofauti yoyote kifaa hutuma taarifa kwenye simu ya daktari kisha atawapigia simu wanaomuuguza wampe huduma ya kwanza wakati huo tunatuma gari la wagonjwa liende kumfuata na kumleta hospitali,” amesema Nkinda.

Mmoja wa wananchi waliopatiwa huduma katika banda la JKCI, Juma Mpanda, amemshukuru kwa huduma nzuri alizopatiwa.