Na Mwandishi Maalumu – Dar es Salaam

Jumla ya Waumini 93 wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Mbezi Beach wamefanyiwa uchunguzi wa magonjwa mbalimbali yakiwemo ya moyo katika jitihada za kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi na kupunguza vifo vya ghafla vinavyosababishwa na kutofanya uchunguzi wa afya mara kwa mara.

Uchunguzi huo ulifanyika kupitia kambi maalumu ya siku moja iliyoendeshwa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Usharika wa Mbezi Beach jijini Dar es Salaam.

Kambi hiyo iliyofanyika mwishoni mwa wiki ni sehemu ya mkakati wa JKCI wa kuimarisha kinga na kutoa elimu dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza hususan magonjwa ya moyo, shinikizo la juu la damu na kisukari.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha zoezi hilo Afisa Masoko wa JKCI, Agness Mndasha alisema mwitikio wa waumini hao ulikuwa wa kuridhisha na unaonesha namna jamii inavyoendelea kutambua umuhimu wa kuchunguza afya zao mapema.

Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Morisi Budotela akizungumza na muumini wa Kanisa la Kiinjili ya Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Mbezi Beach Magrateh Misericordias mara baada ya kufanya vipimo vya moyo wakati wa kambi maalumu ya siku moja iliyofanyika mwishoni mwa wiki katika Kanisa hilo lililopo jijini Dar es Salaam.

Alieleza kuwa jitihada hizo zinaungwa mkono na maboresho makubwa ya sekta ya afya yanayofanywa na Serikali chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan jambo linaloiwezesha JKCI kupanua wigo wa huduma za kibingwa na kuokoa maisha ya Watanzania wengi zaidi.

“Ni muhimu wananchi wakajenga utamaduni wa kujitokeza kupima afya zao pindi fursa za uchunguzi zinapotolewa. Kinga ni bora kuliko tiba na magonjwa ya moyo pamoja na shinikizo la damu yameendelea kuathiri jamii kwa kiwango kikubwa”, alisema Agness.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Huduma za Jamii na Mzee wa Kanisa wa Usharika huo Winytyapa Malawa, aliishukuru JKCI kwa kusogeza huduma hizo kanisani hapo huku akisema zimewapa fursa ya kupata uchunguzi bila gharama na elimu ya kujiepusha na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo itakayowasaidia kubadili mtindo wa maisha.

“Kutokana na majukumu mengi ya kazi niliyokuwa nayo, mara nyingi nakosa muda wa kwenda hospitali kupima afya yangu. Leo nimepata nafasi ya kujua hali yangu ya afya bila ya kulipia gharama zozote zipo jambo lililonipa faraja kubwa”, alisema Malawa.

Naye Katibu wa KKKT Usharika wa Mbezi Beach, Mhandisi Lilian Marry alisema elimu ya lishe bora na uchunguzi wa mapema uliotolewa umeongeza uelewa miongoni mwa waumini ambao wameahidi kuwa mabalozi wa kuhamasisha jamii kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.

Mtalaamu wa vipimo vya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Yatimuni Mushi akimpima kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi mwananchi aliyefika katika kambi maalumu ya siku moja ya uchunguzi na matibabu ya moyo iliyokuwa ikifanywa na Taasisi hiyo katika Kanisa la Kiinjili ya Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Mbezi Beach jijini Dar es Salaam.

“Hatua hii ni muhimu kwetu kwani mbali na kuombea afya ya miili yetu leo tumejifunza kulinda miili yetu kwa kuzingatia lishe bora na kuepuka kutumia vitu ambavyo vinasababisha magonjwa ya moyo na shinikizo la juu la damu”, alisema Lilian.

Bendriba Lyanga muumini wa Kanisa hilo aliipongeza JKCI kwa kuwafikia wananchi moja kwa moja huku akisema amekutana na madaktari bingwa wa moyo na kufanyiwa vipimo na kupata ushauri kitu kilichomfungua macho na kumpa matumaini mapya.

Kambi hiyo imeendelea kudhihirisha dhamira ya JKCI ya kuhakikisha huduma za kibingwa za moyo zinawafikia wananchi popote walipo huku ikisisitiza umuhimu wa kinga, elimu na uchunguzi wa mapema katika kulinda afya ya jamii.

Mtalaamu wa vipimo vya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Yatimuni Mushi akimpima kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi mwananchi aliyefika katika kambi maalumu ya siku moja ya uchunguzi na matibabu ya moyo iliyokuwa ikifanywa na Taasisi hiyo katika Kanisa la Kiinjili ya Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Mbezi Beach jijini Dar es Salaam.
Afisa Masoko wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Agness Mndasha akimpatia zawadi Mzee wa Kanisa na Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii wa Kanisa la Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Mbezi Beach Wintyapa Lionel wakati wa kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo iliyofanyika mwishoni mwa wiki katika Kanisa hilo lililopo jijini Dar es Salaam. (Picha na Khamis Mussa)