Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHAEMA), kupitia tawi la Bonyokwa, limetangaza rasmi kumvua uanachama wake aliyekuwa mwanachama wake, John Mrema.

Uamuzi huo umetangazwa kupitia barua rasmi yenye Kumbukumbu Namba CDM/MTG/KND/01.2025 katika kikao cha Kamati Tendaji kilichofanyika Aprili 29, 2025.

Hatua hiyo imekuja kufuatia mwenendo wa Mrema ambao umedaiwa kwenda kinyume na taratibu, miongozo, na misingi ya chama.

Kabla ya uamuzi huo, Mrema alipewa fursa ya kujieleza kwa maandishi au kufika mbele ya Kamati Tendaji ya Tawi, kama ilivyoelezwa katika barua ya awali ya tarehe 16 Aprili 2025. Hata hivyo, alishindwa kutekeleza masharti hayo.

Kamati ya Tawi imemweleza Mrema kuwa alionesha dharau kwa mamlaka za chama kwa kusambaza barua ya wito wa kujieleza kwenye mitandao ya kijamii badala ya kuitumia kujitetea, jambo linalodaiwa kuwa ni ukiukaji wa nidhamu ya chama.

Aidha, Kamati hiyo imeeleza kuwa Mrema alizidisha makosa kwa kufanya mkutano na waandishi wa habari tarehe 22 Aprili 2025, ambapo alisikika akipinga na kudhihaki misimamo na programu za CHADEMA hadharani, jambo ambalo halilingani na utamaduni wa chama hicho.

Baada ya mjadala wa kina, Kamati ilifikia uamuzi kuwa John Mrema amepoteza sifa za kuwa mwanachama wa CHADEMA kwa mujibu wa Ibara ya 5.4.3 ya Katiba ya CHADEMA ya mwaka 2006, toleo la 2019, na hivyo uanachama wake umefutwa rasmi kuanzia tarehe ya barua hiyo.

Hata hivyo, Mrema amepewa fursa ya kukata rufaa kwa ngazi ya juu ya chama endapo hataridhika na uamuzi huo.

Barua hiyo imesainiwa na Solomin Kagaruki, Mwenyekiti wa Tawi la Bonyokwa Kata ya Bonyokwa Jimbo la Segerea , na nakala imetumwa kwa makatibu wa kata, jimbo, mkoa, kanda, na hata kwa Katibu Mkuu wa CHADEMA Taifa kwa taarifa na kumbukumbu.