Na Mary Margwe, JamhuriMedia, Simanjiro

Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini Mkoa wa Manyara, (Marema) Justin Nyari amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Manyara Queen Sendiga kwa kuadhimisha siku ya mtoto wa Afrika kwa kutembelea kituo cha watoto wenye mahitaji maalumu cha Light In Africa.


Nyari ameyasema hayo Jana kwenye Maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika ambapo ametembelea kituo cha watoto wenye mahitaji maalumu cha Light In Africa kilichopo Mji Mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro Mkoani humo.

Amesema Mkuu wa Mkoa amefanya jambo kubwa na sahihi, kitendo cha kutembelea Kituo hicho na kujumuika na watoto nao pamoja kama sehemu ya Kiongozi lakini pia kama sehemu ya Mzazi.

” Tunamshukuru Mkuu wetu wa mkoa wa Manyara, Kwa kutembelea Kituo cha watoto wenye mahitaji Maalum hakika amefanya jambo sahihi kujumuika nao kwani hawa watoto wa kituo hiki cha Light in Africa ukiwaona hakika watakutoa machozi hivyo wanapaswa kutembelewa na kusaidiwa amesema Nyari.

Awali akizungumza mbele ya viongozi hao MKUU wa mkoa wa Manyara, Queen Cuthbert Sendiga amesema lengo la kutembelea na kuadhimisha siku ya mtoto wa Afrika kwa kutembelea kituo cha Light In Africa ili watoto wajione nao wanao Wazazi wanaowathamini.

Aidha Mkuu huyo wa Mkoa ametumia siku hiyo kwa kuwataka wazazi na walezi kuhakikisha wanawapa urithi wa elimu watoto wao ili iweze kuwasaidia kwa miaka ijayo kwani ni jambo lisilo hamishika wala kufilisika.

” Urithi wa Elimu ni bora zaidi kuliko urithi wa mali kwani mtoto akipatiwa elimu hawezi kufilisika tofauti na mali au rasilimali nyingine inayohamishika na isiyohamishika ila inauzika,hivyo jamii inapaswa kuishi kupitia kauli mbiu ya siku ya watoto inayosema Elimu Jumuishi kwa watoto, izingatiwe maarifa, maadili na stadi za kazi.

Aidha Sendiga amefafanua kuwa kitendo cha kumpa mtoto urithi wa Elimu unakuwa umewekeza jambo kubwa kwenye maisha yake na hata akiwa mkubwa ataitumia Elimu hiyo kwa manufaa yake na jamii inayomzunguka,.

Mkuu huyo wa mkoa wa Manyara, katika kukitembelea kituo hicho amekabidhi kiasi cha fedha kwa ajili ya kununulia mahitaji muhimu ambayo yatawasaidia .

“Tumetoa sadaka yetu kwa watoto hawa ili waweze kununuliwa mahitaji muhimu na tunawapongeza wasimamizi na walezi wa watoto hawa kwa namna mnavyokuwa nao karibu ,” amesema Mkuu huyo wa Mkoa .


Hata hivyo Mkazi wa Mji Mdogo wa Mirerani, Shujaa Baruti amesema amekuwa akijumuika na watu mbali mbali wanaokwenda kutoa sadaka kwa watoto hao ambao ni walengwa husika katika jamii inayowazunguka.


“Unapaswa kumshukuru Mungu kwa zawadi ya uzima kwani ukiwaona watoto wa kituo hicho utatoa machozi kwa namna walivyo ila nawapongeza wanaowaea na kuwapa uangalizi mkubwa wenye furaha ndani yao, kwani wanawahudumia kwa moyo mkunjufu,” amesema Baruti.