Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernad Membe, amesema anaamini kuwa msimamo na uamuzi wa kupeleka kikosi cha kulinda amani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) utaleta amani ya kudumu nchini humo.

 

DRC imekuwa katika vita ya wenyewe kwa wenyewe kwa miaka mingi. Ripoti ya Shirika linaloshughulikia Watoto (UNICEF) zilieleza kuwa makundi ya wanamgambo wa DRC yanakusanya vijana wenye umri mdogo kutoka kwenye vijiji na kuwapa elimu na kuwatumia katika silaha.

UNICEF imesema watoto zaidi ya 1,500 wamekuwa waathirika wa makundi hayo kusini-magharibi mwa Congo.

 

Akihutubia Bunge la Bajeti mjini Dodoma hivi karibuni wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake, Waziri Membe amesema uamuzi wa kupeleka jeshi DRC unatokana na azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Namba 2098 la mwaka 2013, linaloruhusu kuundwa na kupelekwa kikosi maalum.

 

“Mheshimiwa Spika, hali ya eneo la mashariki ya DRC imeendelea kuwa tete kwa majeshi ya kundi la waasi la M23 kuendelea kushambulia wananchi, na hivyo kusababisha kuanza kuongezeka kwa wimbi la wakimbizi.

 

“Kundi hili la waasi limeendelea kushambulia wananchi wasio na hatia kwa kuua watoto, kulazimisha watoto kujiunga na kundi hilo, kubaka akina mama, kuiba na kufanya vitendo vingi vya kinyama visivyokubalika.

 

Hali hii imesababisha uvunjifu mkubwa wa haki za binadamu. Nchi za Afrika na dunia kwa ujumla zimeshindwa kuendelea kuvumilia kuona maovu hayo yakitendeka, na hivyo kufanya uamuzi wa kuimarisha Jeshi la Umoja wa Mataifa la kulinda amani.

 

Waziri Membe amesema kutokana na hali hiyo na historia ya Tanzania kwenye harakati za ukombozi duniani, imeshiriki kikamilifu katika kufikia uamuzi wa kutuma Kikosi cha Kulinda Amani cha SADC nchini DRC. Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza kujitolea kutoa kikosi kimoja cha wanajeshi watakaoshiriki katika zoezi la kulinda amani nchini DRC.

 

Machi 28, mwaka huu, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha Azimio Namba 2098 la mwaka 2013 linaloruhusu kuundwa na kupelekwa Kikosi Maalum (Force Intervention Brigade – FIB) Mashariki ya DRC.

 

Amesema  kwa kuanzia, FIB inatarajiwa kutekeleza jukumu lake kwa kipindi cha mwaka mmoja hadi Machi 31, 2014 ambapo Baraza la Usalama litajadili tena uwezekano wa FIB kuendelea na majukumu yake, kulingana na hali ya amani itakavyokuwa imefikia wakati huo.

 

Amesema kikosi hicho chenye wanajeshi 3,069 kinaundwa na nchi za Tanzania, Afrika Kusini na Malawi. Na kitaongozwa na Tanzania, ambayo jumla ya wanajeshi wake katika kikosi hicho watakuwa takriban 1,283.

 

Amesema gharama za kupeleka vikosi hivyo DRC zitalipwa na Umoja wa Mataifa.

Amesema pamoja na masuala mengine, malengo makuu ya FIB yanajumuisha; kudhibiti kujipanua kwa M23 na vikundi vingine vya waasi Mashariki mwa DRC; kuvinyang’anya silaha vikundi hivyo; na hatimaye kutokomeza harakati za uasi katika eneo hilo la DRC.

 

Amesema lengo jingine ni kuwezesha kurejea kwa muunganiko wa kijamii na majadiliano yatakayosababisha kufikiwa amani ya kudumu nchini humo.

 

Tanzania imechukua hatua hizo kwa kuwa inaamini amani na usalama ndiyo msingi wa maendeleo, bila amani na usalama hakuna maendeleo.

 

Amesema kukosekana kwa amani kwenye nchi jirani kama ilivyo DRC, kuna athari kubwa za kiuchumi, kisiasa, kiusalama na kijamii kwa Tanzania.

 

“Majeshi yetu sasa yapo Kongo na kutokana na nidhamu yao ya hali ya juu, yamepokewa kwa shangwe kubwa huko Goma. Ni matumaini yetu kuwa msimamo na uamuzi huo utaleta amani ya kudumu nchini Kongo”.

 

Malawi

Kuhusu mgogoro wa Ziwa Nyasa, Waziri Membe amesema anaamini kuwa Tanzania itashinda katika kesi hiyo.

 

Mheshimiwa Spika, tujikumbushe kuhusu mgogoro wetu na Malawi. Wanadai kuwa Ziwa Nyasa ukiacha sehemu waliyokubali kugawana na Msumbiji, ni mali yao.

 

“Tanzania kwa upande mwingine tunadai ziwa hilo ni mali yetu wote na kwamba mpaka wake upo katikati ya ziwa kama ulivyo mpaka wa Msumbiji na Malawi kwenye ziwa hilo. Huu ndiyo msimamo wa Tanzania.

 

Amesema suala la mgogoro huo lipo mikononi mwa Jukwaa la Marais Wastaafu wa SADC, likiongozwa na Mheshimiwa Joaquim Chissano, Rais mstaafu wa Msumbiji.

 

Amesema hatua hiyo ilifikiwa kutokana na mchakato wa majadiliano ya awali kati ya nchi zetu mbili kutokuzaa matunda. Tanzania imekwishawasilisha andiko lenye hoja zake kuhusu mgogoro huo kwa Mwenyekiti wa Jukwaa hilo.

 

“Mheshimiwa Spika, pande mbili zimekubaliana hatutafanya shughuli yoyote kwenye mpaka huo hadi mgogoro huu utakapopatiwa ufumbuzi. Tanzania tunaamini kuwa tutashinda kesi hii,” amesema Waziri Membe

 

By Jamhuri