Makamanda wa wapiganaji shupavu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wako mbioni kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kuimarisha amani.

Hii itakuwa ni safari ya pili kwa wanajeshi hao kwenda DRC, baada ya mapema mwaka huu kwenda huko na kuwafyeka na kuwasambaratisha waasi wa kundi la Machi 23 au M23.

Serikali Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeihakikishia Jumuiya ya Kimataifa kwamba itaendelea kushirikiana na wapenda amani katika kuisaidia DRC kuwa na amani na usalama.

Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa (UN), Balozi Ramadhan Mwinyi, amesema hayo alipochangia majadiliano juu ya ajenda inayohusu tathmini ya jumla ya Operesheni za Ulinzi wa Amani chini ya Umoja wa Mataifa.

Anasema Tanzania inafanya hivyo kwa kutambua wajibu wake katika medani ya ujenzi wa amani ya kimataifa.

Anasema kwa kutambua wajibu huo, ndiyo sababu iliyoifanya Serikali ya Tanzania kufikia makubaliano na nchi wanachama wenzake katika SADC na Maziwa Mkuu (ICGLR).

Balozi Mwinyi anasema kwamba Tanzania imeamua kujitolea kupeleka wanajeshi wake huko DRC, ili kuunga mkono juhudi za kuwasaidia wananchi wa huko kuwa na amani, usalama na maisha yenye uhakika.

Anasema Tanzania inajivunia kuwa na wanajeshi wanaohudumu kupitia FIB ambayo ni sehemu ya MONUSCO licha ya mazingira magumu na hatari wanayokabiliana.

“Wameonesha umahiri mkubwa ikiwa ni pamoja na kujitoa muhanga maisha yao kuwalinda raia wasiokuwa na hatia DRC pamoja na kurejesha amani na usalama,” anasisitiza Balozi Mwinyi.

Kwa sababu hiyo, Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania amesema ni vema na haki, kujitoa muhanga huko kwa wanajeshi wanaohudumu FIB kutambuliwa na wapenda amani wote na vile vile FIB iendelee kupata uungwaji mkono stahili.

Kadhalika, Balozi Mwinyi anasema kutokana mabadiliko ya mwenendo mzima wa machafuko na vita katika maeneo mbalimbali barani Afrika, ikiwa ni pamoja na matishio na kutumika kwa mbinu za kigaidi na mabomu ya kutengenezwa kienyeji, kunalazimisha kufanyika mabadiliko katika mfumo mzima wa ulinzi wa amani.

Anasema mabadiliko hayo yanasababisha Umoja wa Mataifa kulazimika kuidhinisha matumizi ya nguvu katika baadhi ya misheni zake kutokana na ukweli kwamba matishio hayo si tu ni hatari kwa raia lakini pia yamekuwa tishio kwa walinzi wa amani.

Kwa sababu hizo, Tanzania inataka kuwapo kwa majadiliano ya kina ndani ya Umoja wa Mataifa kuhusu dhana nzima ya mabadiliko ya mwenendo wa machafuko na vita vinavyoendelea, na hatari inayowakabili walinzi wa amani pamoja na matumizi ya nguvu kuwa sehemu ya mamlaka nguvu ya misheni nyingi.

“Tunahitaji majadiliano ya kina katika eneo hili, kwa sababu, mwenendo wa machafuko na mbinu za maadui zimebadilika kabisa. Kuna matumizi makubwa ya mbinu za kigaidi na mabomu yanayotengenezwa kienyeji, haya yote na mengine mengi yanabadilisha kabisa historia ya asili ya ulinzi wa amani,” anasema Balozi Mwinyi.

Anasema majadiliano ya kina yanahitajika katika eneo la matumizi ya teknolojia za kisasa katika operesheni za kulinda amani, zikiwamo ndege za kiuchunguzi zisizoendeshwa na binadamu ( UAS).

Anasema hapana shaka, kama walivyozungumza wajumbe wengine, matumizi ya teknolojia hizo pamoja na umuhimu wake yanahitaji majadiliano ya kina na makubaliano ya pamoja.

Aidha, Balozi Mwinyi amesema Tanzania inakaribisha nia ya Katibu Mkuu wa UN kufanya mapitio ya Operesheni za Ulinzi wa Amani za Umoja wa Mataifa (UNPKOs) na Misheni Maalum za Kisiasa (SPMs). Na ameahidi kuwa Tanzania itashiriki kikamilifu katika mchakato huo.

Awali akizugumza mwanzoni mwa majadiliano hayo, Mkuu wa Idara ya Operesheni ya Kulinda Amani ya Umoja wa Mataifa (DPKO), Herve Ladsous, amezungumzia mafanikio na changamoto mbalimbali zinazokabili shughuli za ulinzi wa amani.

Anasema nchini DRC, Misheni ya Kulinda Amani (MONUSCO) ambayo ndani yake kuna FIB imeonesha umahiri na ujasiri mkubwa wa kutokubali kurudi nyuma katika mapambano yake dhidi ya makundi ya waasi yenye silaha.

Akasema ushupavu na uhodari huo, licha ya kutoa ulinzi kwa raia, pia umefungua fursa mpya ambapo mamlaka za kiutawala za DRC zimeweza kutawala maeneo ambayo huko nyuma yalikuwa yakishikiliwa na kukaliwa na makundi ya waasi.

Katika majadiliano hayo, wazumgumzaji wengi wameelezea kusikitishwa kwao na ongezeko la vitendo vya kuvamiwa kwa walinzi wa amani na kusababisha wengi wao kupoteza maisha.

Wakasema jambo hilo halikubaliki na halipaswi kuendelea kufumbiwa macho na kwamba ni lazima pafanyike utafiti wa kina wa kwanini kumekuwa na ongezeko la mashambulizi kwa walinzi wa amani.

Wachangiaji wengine wameshauri na kutoa wito kwa UN kupitia DPKO na taasisi nyingine zinazohusika na masuala ya operesheni za ulinzi wa amani, kuangalia upya mazingira ya utendaji kazi ya walinzi hao wa amani, ikiwa ni pamoja na kuwapatia mafunzo zaidi yanayoendana na wakati, vifaa na zana za kisasa na vya uhakika, malipo stahili na pia mamlaka zinazotekelezeka.

By Jamhuri