Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia,Dodoma
Katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limehusika katika zaidi ya shughuli sita kubwa za uokoaji ndani na nje ya nchi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kushirikiana na mamlaka za kiraia kukabiliana na majanga na maafa mbalimbali.
Hayo yameelezwa leo Mei 22,2025 jijini Dodoma na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Stergomena Tax, wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Idara ya Habari-Maelezo kuhusu mafanikio ya wizara hiyo.

“Tumeimarisha uwezo wa JWTZ katika shughuli za kukabiliana na majanga. Kwa kipindi cha miaka minne, tumeshiriki kikamilifu kwenye matukio makubwa ya maafa kwa kutoa misaada ya uokoaji na kibinadamu,” alisema Dk. Tax.
Ameyataja miongoni mwa matukio hayo ni uokoaji katika mafuriko ya Mtwara,kuzima moto katika Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro,usafirisha misaada na kuokoa wahanga wa mafuriko nchini Malawi,uokoaji katika maporomoko ya matope Hanang’ – Manyara,kuokoa waliopata ajali ya jengo Kariakoo – Dar es Salaam na ujenzi wa nyumba kwa waathirika wa Hanang’ na wakazi waliopisha uhifadhi Ngorongoro waliohamishiwa Tanga.
Aidha, kupitia JWTZ, Serikali imekabidhiwa jukumu la kujenga nyumba 5,000 kwa wananchi waliokubali kuhama kwa hiari kutoka Ngorongoro ambapo hadi sasa, nyumba 2,500 zimekamilika katika eneo la Msomera – Handeni, huku nyingine 1,000 zikijengwa Sauni – Kilindi na 1,500 zikitarajiwa kujengwa Kitwai B – Simanjiro, Manyara.
Kwa upande wa Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMAJKT)katika kuendeleza uchumi na kupunguza mzigo wa gharama kwa serikali, Dk. Tax amesema limechangia jumla ya Shilingi bilioni 2.67 kwa ajili ya malezi ya vijana wa JKT na kutoa gawio la zaidi ya Shilingi bilioni 4.27 kwa Serikali kupitia Hazina.

Miongoni mwa miradi ya kiuchumi iliyoanzishwa ni pamoja na vituo vya madini mikoa saba ikiwemo Tanga, Ruvuma, na Mara,ujenzi wa majengo ya halmashauri na taasisi za serikali,Viwanda mbalimbali ikiwemo vya maji, mavazi, bidhaa za ngozi, na taa za LED,Usambazaji na ufungaji wa umeme vijijini kupitia mradi wa REA,usambazaji wa matrekta na zana za kilimo katika mikoa zaidi ya 10 na huduma ya ulinzi kwa taasisi nyeti kupitia kampuni ya SUMAJKT Guard.
Asema mafanikio haya ni matokeo ya usimamizi madhubuti na dhamira ya serikali katika kujenga nchi inayojitegemea kiusalama na kiuchumi kupitia taasisi zake za kijeshi.


