*Ni bingwa wa kutengeneza test tube aliyetelekezwa

*Miaka 27 sasa anapigwa danadana na wakubwa serikalini

*Mitambo, malighafi alivyozawadiwa vinaozea bandarini

*Mwalimu Nyerere, Rais Kikwete, Lowassa walimkubali

*Umoja wa Mataifa, AU, Sudan Kusini, Rwanda wanamlilia

Mwaka 2009 nilikutana na Mtanzania aliyenivutia kwa ubunifu, uwezo wake wa kiakili, na zaidi ya yote ni uzalendo wake kwa nchi yake. Nikamwomba na yeye akakubali kufanya mahojiano. Lengo lilikuwa kuwawezesha Watanzania, hasa watu wenye mamlaka ya uongozi waweze kumtambua, kumsaidia na kumtumia ili ndoto yake itimie.

Wiki hii nilisoma habari iliyoandikwa kwenye Uk. 3 wa Gazeti la HABARILEO, yenye kichwa cha habari, “Ashauri uwekezaji katika masomo ya sayansi uongezwe.”

Haya yalikuwa maneno ya Mwalimu Ibrahim Julius anayefundisha masomo ya sayansi katika Shule ya Sekondari Kaloleni. Aliyazungumza kwenye mafunzo ya siku moja ya kuwajengea uwezo walimu wa masomo ya sayansi. Mwalimu Julius alisema mengi, lakini kubwa ni la kuitaka Serikali na wadau wahakikishe masomo ya sayansi yanapewa kipaumbele kuanzia kwenye vifaa, majengo, kuwaandaa walimu na kuwafanya wanafunzi wapende kusoma masomo hayo.

 

Maneno ya Mwalimu Julius yakanirejesha kwa Mtanzania ninayemzungumzia leo ambaye si mwingine bali ni Eustace Kabantega, Mtanzania wa kwanza kutengeneza kisafisha maji, na mtu anayetambuliwa na kuheshimiwa mno na Shirika la Umoja la Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO) kwa uwezo wake wa kutengeneza vifaa vya maabara. Wakati nikiandika makala ya kwanza mwaka 2009 kulikuwa na Watanzania wawili tu waliokuwa na sifa za usomi na utaalamu kwa kazi hiyo.

 

Nikafanya juhudi za kumtafuta Kabantega ili anieleze amefikia wapi kwenye ndoto yake ya kuwa na kiwanda cha kutengeneza vifaa vya sayansi, zikiwamo test tube ambazo zinaagizwa kutoka nje kwa bei ghali mno.

 

Hatimaye nimefanikiwa kumpata. Safari hii si yule Kabantega niliyemjua. Licha ya kuonekana akiwa mwenye siha njema, usoni amejaa mawazo. Hali hii inatokana na ukweli kuwa safari yake ya kuwa na kiwanda cha aina hiyo aliyoianza mwaka 1986 hadi leo haijatimia. Ana miaka 27 akipambana na urasimu wa watawala katika nchi hii inayoota kuwa na wanasayansi!

 

Baada ya kumwona, nikarejea kwa Mtanzania mwingine, Dk. Ferdinand Masau wa Heat Institute of Tanzania (HIT). Wengi wanaamini kwamba bingwa huyo wa maradhi ya moyo amefariki dunia kwa kiroho, kutokana na kukwazwa na urasimu uliopindukia wa watumishi wa Serikali. Kwa mwenendo wa urasimu wa watawala wetu, Kabantega sijui atakwepa vipi kufikwa na yaliyomfika Dk. Masau.

 

Katika mazungumzo yetu, Kabantega anasema hatua aliyoweza kuipiga tangu tulipoachana mwaka 2009 ni ya kufanikiwa kupata mitambo miwili kutoka kwa ‘marafiki wa Watanzania’ – Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Delft kilichopo nchini Uholanzi.

 

Anasema mitambo hiyo yenye thamani kubwa, ikiwa pamoja na malighafi ambayo ingeweza kumaliza tatizo la vifaa vya maabara za sayansi hapa nchini, imekwama bandarini baada ya kukosa fedha.

 

“Hii mitambo niliipata kutoka kwa marafiki walioko Delft University of Technology. Wao wenyewe waliniandikia barua Novemba 3, 2011 wakisema walikuwa wakiondoa mitambo hiyo na wakanitaka nikaichukue bure. Gharama za kusafirisha walitoa wao.

 

“Nikaona hili ni jambo jema sana. Nilikwenda chuoni hapo, nikaiona, ikawekwa kwenye makontena hadi Bandari ya Dar es Salaam. Ilipofika hapa nikatakiwa nilipe kodi. Nikaomba nisamehewe kwa sababu sina fedha, lakini pia ni mitambo inayohusiana na mambo ya elimu. Tangu wakati huo nahangaika, hadi leo inaozea kwenye makontena bandarini,” anasema Kabantega ambaye kampuni yake inaitwa Dar es Salaam Scintific (T) Ltd.

 

Kabantega amejitaidi kwenda Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Wizara ya Fedha ili asaidiwe, lakini kote huko anasema bado hajafanikiwa. Kampuni yake imekuwa mara zote ikiwa mshindi wa juu kwenye maonesho ya vifaa vya sayansi na teknolojia. Mwaka 2007 ilikuwa ya tatu, lakini kabla ya hapo ilishashika nafasi ya pili kwenye maonyesho mbalimbali.

 

Kabantega anasema amewafundisha vijana kadhaa kutengeneza vifaa vya maabara, lakini kutokana na kukwama kuanzisha kiwanda, vijana hao hawana ajira.

Ni nani hasa mtu huyu Kabantega?

 

Kwa muda sasa kumekuwa na uhimizaji wa kujenga mazingira mazuri kwa wawekezaji wa nje hapa nchini, na kwa kiasi fulani wale wa ndani wamekuwa wakisahauliwa.

 

Njia moja muhimu kwa Taifa kujitegemea ni kuwa na wawekezaji wengi wa ndani (wazalendo), kuwawezesha na kuhakikisha bidhaa zao zinapata soko kubwa ndani na nje ya nchi, ikiwa ndiyo njia ya kufanya uwekezaji wao huo uwe endelevu.

 

Kabantega anatambuliwa na Umoja wa Mataifa (UN) kama mmoja wa wanasayansi mahiri kabisa wa vifaa vya maabara. Aidha, kazi zake zilipata kuonwa na kukubaliwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Rais Jakaya Kikwete na aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa.

 

Huyu ni mtaalamu wa kutengeneza kifaa cha kusafisha maji (Water Distiller) ambacho hutumika kusafisha au kuchuja maji kwa njia ya mvuke kwa ajili ya matumizi ya utafiti katika maabara za sayansi. Wakati fulani amepelekwa na UN huko Malakal, Sudan kwa ajili ya kuendesha mafunzo ya kutengeneza vifaa hivyo.

 

“Tukizungumzia maendeleo ya Taifa letu ili lijitegemee ni vizuri kuangalia uwekezaji kama huu, kuwapatia ajira ya kudumu Watanzania wengi zaidi, kuwezesha wajasiriamali wazalendo wasio na mitaji ya miradi, wabunifu katika nyanja za sayansi na teknolojia kwa njia mbalimbali, kuwawezesha kwa mikopo yenye riba nafuu na kuepusha matumizi makubwa yasiyo ya lazima ya fedha nyingi za kigeni kununua vifaa nje ya nchi,” anasema Kabantega.

 

Alitokea wapi? Alipata kufanya kazi ya ufundi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa miaka 20.

 

“Mwaka 1983 nilichaguliwa kuwa mfanyakazi bora katika Idara ya Kemia. Mwaka 1987 kwa mara nyingine tena nilichaguliwa kuwa mfanyakazi bora katika Kitivo cha Sayansi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Wakati huo huo nilipandishwa cheo na baadaye kupelekwa Uingereza kwa ajili ya masomo yangu ya Masters Certificate in Scientific Glassblowing,” anasema na kuongeza:

 

“Chombo cha kuchuja maji (Water Distiller) kwa njia ya mvuke ni muhimu sana katika masuala ya utafiti kwenye maabara ya sayansi. Wakati natafiti kifaa hicho miaka ya 1980 kulikuwa na uhaba mkubwa wa kifaa hicho hapa nchini. Pili, kifaa hicho ni bei ghali sana na kipindi hicho kulikuwa na uhaba mkubwa wa fedha za kigeni na mashirika mbalimbali ya umma hayakupatiwa fungu la kutosha kuagiza kifaa muhimu kama hicho.

 

“Nilionelea nijishugulishe na kifaa hicho kwa sababu ilikuwa katika uwezo wa fani yangu. Ilinichukua miezi 14 kutimiza lengo langu na nilipokamilisha kifaa hicho na kujaribiwa, kilifanya kazi kwa asilimia 69. Haya yalikuwa mafanikio makubwa kwangu kwani ilikuwa mwanzo. Sikutaka kuigiza ndiyo maana ilichukua muda mrefu kukamilika. Pia asilimia kubwa ya malighafi iliyotumika ilipatikana hapa nchini”.

 

Anasema kuwa 1989 Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilifanya kongamano la wabunifu nchini Tanzania ambako wagunduzi na wabunifu wengi walialikwa, akiwamo yeye. Mtambo wake ulikuwa umeoneshwa katika Maonesho ya Kimataifa ya Saba Saba mwaka 1986 katika Banda la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Anasema kuwa kati ya waliovutiwa na mtambo huo ni Mwalimu Nyerere, Mzee Rashidi Kawawa na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Salmin Amour Juma.

 

“Baba wa Taifa aliuliza wakuu wangu wa kazi baada ya kufanikiwa kutengeneza kifaa hicho nilipewa nini. Kwa vile sikupewa kitu, Baba wa Taifa aliagiza aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Geoffrey Mmari, ashughulikie suala hilo. Wiki moja baadaye nilijulishwa na mmoja na makatibu kwamba nilikuwa nimepandishwa cheo, lakini wahusika walikuwa hawajasaini barua hiyo.

 

“Baada ya kusubiri kwa wiki tatu na kuona hakuna kitu, nilijua kuna jambo kwa wakuu wangu wa kazi. Wakati huo huo jamaa mmoja kutoka nchi jirani ya Kenya alifika chuoni kunitafuta baada ya kusikia habari zangu katika masuala ya utengenezaji wa vifaa vya maabara.

 

“Hakika sikuomba kazi nchini Kenya. Oktoba 1989 niliacha kazi na kwenda Nairobi, Kenya, kufanya kazi huko kama Chief Glassblower (expert) kwa muda wa miaka miwili na nusu. Baada ya miaka hiyo nilirudi hapa nchini na kuajiriwa tena kwa mkataba wa idara ya Kemia, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kama mtaalamu chini ya Mfuko wa NORAD kwa miaka saba.

 

Kabantega anasema kwamba Novemba 2004, katika moja ya hotuba za kila mwisho wa mwezi, Rais Benjamin Mkapa alimgusa, na baada ya kutafakari alimwandikia barua kumweleza juu ya mradi huo. Katika wiki tatu alijibiwa kupitia SIDO kwamba Rais Mkapa aliagiza wasaidizi wake wamwezeshe kuwasiliana nao (SIDO), kwa ajili ya mradi huo. Baada ya mawasiliano na SIDO, walimpatia nafasi katika mojawapo ya vyumba katika kitamizi (Incubator) na baadaye akaanza kazi ya maandalizi ya mradi huo.

 

Alianza wapi? Kabantega anasema alianza kwa kufundisha wafanyakazi (wanafunzi) na katika kipindi cha miezi sita vijana wanne wakawa wamehitimu.

 

“Kulikuwapo pia wafanyakazi wengine wawili kwa ajili ya shughuli nyinginezo, jumla yao sita. Katika kipindi hicho niliomba mkopo wa Sh 5,000,000 kwa ajili ya kununulia malighafi (glass tubings). Muda si mrefu mzigo wa malighafi nilioagiza kutoka India ulikuwa umefika bandarini na baadaye kufikishwa ofisini.

 

“Kazi ilianza mara moja na katika muda wa miezi mitatu tulishafikisha test tube nyingi za kutosha kupeleka katika soko. Kabla ya mradi huu kuanza na kabla sijawasiliana na Rais (mstaafu) Mkapa nilitembelea shule nyingi Dar es Salaam, Kilimanjaro na Iringa kubaini soko likoje. Shule nyingi nilizotembelea hazikuwa na   vifaa vingi vya maabara wala test tubes imara kuhimili joto kali (heat resistant) na za viwango. Nyingi zilikuwa thin wall na hivyo kupasuka kirahisi wakati wa majaribio na kuosha. Pamoja na hayo, bei yake ilikuwa kubwa,” anasema.

 

Anaongeza kwamba hesabu zake (na kampuni yake) wakati wanatafiti gharama za uendeshaji walipanga bei iwe Sh 500 kwa kila test tube moja, maana zile zisizo na viwango kutoka Ulaya Magharibi aina ya pyrex zilikuwa zinauzwa kati ya Sh 700 hadi Sh 1,000 kila moja.

 

“Bei ya Sh 500 ilikuwa inarudisha mkopo mara nne. Garama ya kutengeneza test tube moja ilikuwa Sh 231. Baada ya muda kupita na kuona bidhaa zetu hazipati soko licha ya matangazo na kuwapelekea sampuli walengwa tuliwasiliana na Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko ili watuwezeshe kupata utambulisho katika taasisi mbalimbali hapa nchini maana juhudi zetu kupata soko kupitia wizara yenye dhamana ya elimu zilikuwa zimeshindikana. Kwa juhudi zote, Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko ilitupatia barua za utambulisho katika taasisi mbalimbali, lakini hatukufaulu kupata soko la bidhaa zetu.

 

Kwa nini mambo yamewawia magumu? Jibu analo Kabantega mwenyewe:

“Kwa mshangao mkubwa tumebaini kuwa bila kutoa ‘kitu kidogo’ hupati soko. Hii ndiyo hali halisi nchini Tanzania. Wengi wa walengwa waliuliza kwa nini tulikuwa tunauza bidhaa zetu kwa bei ya chini sana kama ni bora. Zaidi ya yote, mara nyingi tuliambiwa wanao suppliers tayari, na kuwa iwapo wangetuhitaji wangetuita. Hata mara moja hakuna aliyetuita mbali ya kubembeleza na kutoa samples nyingi.

 

“Baadaye tulipunguza bei hadi Sh 400 kwa kila test tube, maana hiyo ilikuwa azma ya kutaka kuwatumikia Watanzania ili vifaa hivyo bora vipatikane kwa wingi na kwa bei nafuu. Baada ya kukosa soko kwa muda mrefu tuliwasimamisha kazi wafanyakazi ambao tuliwagharimia pesa nyingi wakati wa mafunzo kwa sababu ya kushindwa kuwalipa mishahara. Wakati wa mafunzo malighafi tulikuwa tunazinunua kutoka Nairobi, Kenya kwa gharama kubwa. Wafanyakazi hao hawana kazi sasa (mwaka 2009), lakini ajira zingeweza kuwapo kwenye kampuni yetu ikiwa tungezingatia uzalendo, ubora na kutaka kujiendeleza.

 

Viongozi wengi walishaona bidhaa za Kabantega, mmoja wao ni aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa. Baada ya kuvutiwa na bidhaa hizo, kwa mujibu wa Kabantega, aliagiza Shirika la Viwango Tanzania (TBS) lifanye uchunguzi ili kubaini ubora wake. Kazi hiyo ilifanyika na baada ya muda mfupi walipewa cheti cha ubora wa bidhaa zao. Wizara ya Elimu na Utamaduni (enzi hizo) nayo iliunda tume kuhakikisha ubora wa vifaa hivyo kuvithibitisha mwaka 2007.

 

“Pamoja na juhudi zote hizi, soko lilikuwa gumu kwa sababu ya bei kuwa mbaya kwa wateja, maana haina maslahi ndani yake. Hawapati kitu. Baada ya kuona hivyo hata mimi niliyebaki na usukani ilinibidi kusimamisha uzalishaji, maana gharama za kuzalisha zilikuwa kubwa na hapakuwa na mapato. Wakati huo wote tunatafuta soko, muda wa grace period wa kuanza kulipia mkopo ulikuwa tayari umepita, tena na kuanza kulipia penalty.

 

“Mpaka sasa (mwaka 2009) deni ambalo lilikuwa halijalipwa pamoja na riba limefikia Sh 6,800,000, hii ni pamoja na kiasi kidogo lililorudishwa cha Sh 2,000,000.

 

Septemba 22, 2009 nililetewa barua na dalali wa kudai mikopo sugu isiyolipwa, ikinitaka kulipa deni hilo la Sh 6,800,000 katika muda wa siku saba, vinginevyo dhamana zingepigwa mnada kulipia deni hilo. Hii ndiyo hali halisi ya mjasiriamali wa Tanzania,” alilalamika Kabantega na kuongeza:

 

“Kazi kubwa na nzuri, kwa sababu za wazi bidhaa bora za kisayansi na bei nafuu zimekosa soko, na dhamana (nyumba mbili) zinapigwa mnada. Katika nchi nyingi, wabunifu na watafiti huhitimu kwa kutafutiwa soko kama mradi ni kwa manufaa ya Taifa. Hapa kwetu, pamoja na kuwa mradi huu ni kama wa kitaifa ambao ungetusaidia kupunguza gharama za uendeshaji katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi umehujumiwa na kufa kwa maslahi ya wachache na kuendelea kudumaza maendeleo ya sayansi na teknojia hapa nchini.

 

“Tukumbuke kuwa tunaponunua bidhaa hizi nchi za nje tunatumia pesa nyingi za kigeni na kutoa ajira katika nchi hizo bidhaa zinakotoka, pamoja na kuwa hapa kwetu ajira ni haba. Hivi kweli miaka 50 ya Uhuru tunaendelea kuagiza kifaa kama test tube kwa pesa nyingi za kigeni kutoka nchi za nje? Ningelikuwa nimetengeneza kifaa hicho kwa garama kubwa na kiwango duni na kukosa soko, hili lingekuwa jambo jingine, lakini hili ni kinyume chake; bei nzuri, teknolojia mpya, bidhaa bora na bado hakuna soko!

 

“Mimi niliamua nitaifanyia nini nchi yangu. Niliamua utengenezaji wa vifaa vya maabara vilivyo bora na kwa bei nafuu. Huu ndiyo mchango wangu ambao kwa makusudi umehujumiwa na Watanzania wenzangu….”

 

Kabantega anabainisha kuwa bidhaa zao mwaka 2007 zilioneshwa katika mkutano wa Umoja wa Afrika (AU) mjini Addis Ababa, Ethiopia, na kuwa washiriki wengi walifurika kuona vifaa hivyo vinazalishwa na mojawapo ya nchi wanachama wa AU, yaani Tanzania.

 

Mwaka 2008 mojawapo ya vitengo vya kukuza sayansi na teknolojia katika AU kilimwita Kabantega na kumtaka azalishe au awe wakala wa kusambaza bidhaa hizo kwa shule katika nchi za AU. Kwa bahati mbaya, anasema hakuwa na bidhaa nyingi wala nguvu kazi ya kufanya hivyo. Mwaka huohuo alialikwa Zimbwabwe kushiriki kongamano la sayansi na teknolojia na baadaye alialikwa Afrika Kusini katika maonesho ya bidhaa za sayansi na teknolojia zinazozalishwa Afrika.

 

Awali, Kabantega alipata kutengeneza glasi za kunywea mvinyo Ikulu ya Dar es Salaam enzi za utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi. Anasema kwamba alitengeneza glasi 93 na baada ya kufikishwa Ikulu na kuona zinafaa, alitakiwa kutengeneza nyingine kwa ajili ya ofisi ya Waziri Mkuu, ambako alitengeneza 33 na mambo yakaishia hapo!

 

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, naye alipata kuelezwa juu ya matatizo ya soko la vifaa hivyo vya maabara, naye akasema TAMISEMI wangeagiza shule kununua vifaa hivyo ikiwa kuna ubora, lakini hawakufanya hivyo.

 

Kwa mwaka 2009, gharama zote za uzalishaji wa test tubes milioni mbili kwa ujumla wake zilikuwa Sh milioni 300. Hiyo ilikuwa pamoja na ununuzi wa malighafi na ajira kwa wafanyakazi 50.

 

“Ukiuza test tubes milioni mbili kwa Sh 400 utapata Sh 800,000,000. Ukiagiza test tubes milioni mbili kutoka nje na kufika maduka ya watu binafsi kwa bei ya Sh 800 hadi 1,200 utalipa kati ya Sh bilioni 1.6 hadi Sh bilioni 2.4. Je, hii ni sahihi? Wakati mwingine tunanunua bidhaa hizi Kenya.

 

“Tunapeleka mabilioni yote hayo ya shilingi nje wakati bidhaa hizo zingezalishwa hapa Tanzania ambako kodi mbalimbali zingelipwa na kutoa ajira kwa raia wetu. Pia hili lingekuwa jukwaa la kukuza na kuinua vipaji katika sayansi na teknolojia kwa vijana wetu wa Tanzania. Inasikitisha sana.

 

“Katika kipindi hicho chote cha kukosa soko UNIDO, kwa kutambua kuwapo kwangu walinitaka kwenda Sudan Kusini, Upper Nile State, Malakal katika Chuo cha Ufundi kwenda kufundisha utengenezaji wa vifaa vya maabara. Tangu mwaka 2007 kwa nyakati tofauti nilikuwa huko,” anasema Kabantega.

 

Serikali ya Sudan Kusini inatarajia kupata soko kubwa katika nchi jirani za Kenya na Uganda baada ya kugundua vifaa hivyo havizalishwi katika sehemu hizo kwa wingi. UNIDO waliwapatia vifaa vingi ambavyo baada ya kumalizika mafunzo walianza uzalishaji wa uhakika.

 

Vifaa vya maabara Tanzania kwa sasa hununuliwa kutoka Kenya, hatimaye Tanzania inaweza kununua bidhaa hizo kutoka Sudan ambako Kabantega ndiye kawafundisha.

“Hapa ndipo nashindwa kujua nilifanyie nini Taifa langu Tanzania?” Anahoji.

 

“Mimi kama mjasiriamali mdogo sina mtaji wowote, naomba suala hili liangaliwe kwa mapana na marefu ili Tanzania iwe Taifa la kwanza kuzalisha vifaa hivi vya sayansi kwa wingi hapa Afrika.

 

Toleo lijalo nitaeleza mikasa na ‘njoo kesho’ zilizomkwaza kwa miaka 27 sasa, na namna Rwanda wanavyommezea mate.

By Jamhuri