Wapo wafanyakazi wengi wanaosumbuliwa na migogoro ya kikazi maofisini kwao, lakini hawajui cha kufanya. Wengine hufanyiwa mambo ya ajabu makazini yumkini wakashindwa kuchukua hatua yoyote kutokana na kutojua pa kuanzia.

Na hizo ni ajira rasmi tusiongelee hizo zisizo rasmi. Tusiongelee vibarua huko viwandani na kwenye maeneo mbalimbali ya ujenzi hasa yale yenye miradi mikubwa kama ya barabara, madaraja nakadhalika. Tusiongelee wafanyakazi wa ndani na kazi nyingine zinazofanana na hizo. Hawa hupata shida sana na mbaya zaidi hukosa msaada hata wa kujua ni hatua gani wachukue. Kimsingi unaposumbuliwa na mgogoro wowote wa kazi zipo hatua za kuchukua zilizoainishwa kisheria. Ni hatua nyepesi tu labda mtu usipende kuzichukua.

 

1. Kujiunga na vyama vya wafanyakazi

Huwa kuna umuhimu mkubwa wa kujiunga na vyama vya wafanyakazi. Hii ni kwa sababu unapokuwa mwanachama pindi unapotokea mgogoro kitu cha kwanza unatakiwa kutoa taarifa kwenye chama chako na uongozi hauna budi kuwasiliana na waajiri wako kwa ajili ya kukutetea.

Pia ikiwa mazungumzo kati ya chama chako na waajiri yatashindikana basi chama hubeba jukumu la kwenda mahakamani moja kwa moja kukutafutia haki yako. Huu ndio umuhimu mkubwa wa kujiunga na vyama  hivi. Unapokuwa unafanya kazi hebu jaribu kuuliza kuhusu vyama hivyo utaelezwa, utajiunga na kuwa mwanachama kwa ajili ya  maslahi  yako kesho.

 

2. Peleka mgogoro Tume ya Usuluhishi

Tume ya usuluhishi wa migogoro ya kazi huitwa MEDIATION. Kisheria tume hii inaainishwa na sehemu ya II ya sheria Na. 7 ya taasisi za masuala ya kazi ya 2004. Unapokuwa na mgogoro kwa mara ya kwanza ni vema ukatafuta tume hii na kupeleka mgogoro wako.

Ukifika hapo utapewa fomu maalum ya kujaza na baada ya hapo mwajiri wako ataitwa kwa ajili ya usuluhishi. Kwa walio Dar  es  Salaam tume hii ipo jengo la msalaba mwekundu eneo la akiba makutano ya bibi titi na morogoro.

Mgogoro wowote unakubalika unaweza kuwa mgogoro wa kimaslahi kwa mfano kutaka kuongezewa mshahara,  kutoridhishwa na mazingira ya kazi, kufanya kazi kinyume na mkataba nakadhalika. Pia unaweza kuwa mgogoro wa malalamiko kwa mfano kufukuzwa kazi bila kufuata taratibu, kupunjwa mafao, kuvunjiwa mkataba kinyume na sheria n.k. 

Hakikisha unapeleka mgogoro wako ndani ya siku 30 tangu kutokea kwa mgogoro huo. Hata hivyo kama zimepita siku 30 na unazo sababu za msingi za kwanini hukupeleka mgogoro ndani ya muda huo basi utajaza fomu ya kuomba kuongezewa muda huku ukitoa sababu za kwanini  ulichelewa.

 

3. Mgogoro kwenda Tume ya Uamuzi

Hapo juu tumeona kuwa mwajiri wako ataitwa kwa ajili usuluhishi ili kupata muafaka wa mgogoro. Hata hivyo suluhishi unaweza kushindikana kwa kutoelewana katika nukta fulani fulani. Ikiwa usuluhishi utashindikana basi mgogoro utaenda tume ya uamuzi.

Katika tume hii kila upande utatoa maelezo yake na ushahidi. Upande wa mwajiri utatoa maelezo na upande wa muajiriwa nao utatoa maelezo. Tume hii itasikiliza na kutoa maamuzi. Uamuzi wa tume hii yana nguvu za kisheria kama maamuzi ya mahakama  na hivyo yakitolewa ni lazima yafuatwe. 

Zingatia kuwa katika hatua zote hizo juu yaani wakati wa suluhishi na wakati wa uamuzi unaweza kumtafuta mtu wa kukuwakilisha ikiwa ni mwanasheria, chama cha wafanyakazi au mtu unayeamini anaweza kukusaidia katika masuala ya kazi. Hili linaruhusiwa.

 

4. Mgogoro kwenda Korti Kuu ya Kazi

Ikiwa hukuridhishwa na maamuzi ya tume ya uamuzi hapo juu basi unaruhusiwa  ndani ya siku 30 tangu siku ya kutolewa uamuzi huo kupeleka shauri hilo katika mahakama kuu ya Tanzania.

Utaiomba mahakama kuu irejee (revise) vipengele kadhaa unavyolalamikia unavyohisi tume ya uamuzi haikutenda haki.  Ikiwa pia haukuridhika na maamuzi ya mahakama kuu basi utapeleka rufaa yako mahakama ya rufaa ikiwa suala lako lina hadhi ya kwenda huko. 

Kubwa na muhimu kuliko yote kwenye makala haya ni kujua kuwa mgogoro unapotokea, haraka ndani ya siku 30 upelekwe baraza la usuluhishi. Kwa walio mikoani au wilayani kujua ilipo tume hii nenda makao makuu ya wilaya au mkoa ulizia hapo watakuonesha ilipo tume. Hapo utapata muongozo wa kila kitu nilichosema humu na ni bure.

 

Kuhusu sheria za ardhi, mirathi, makampuni, ndoa n.k, tembelea  SHERIA  YAKUB  BLOG.

3408 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!