Michezo ya kamali hapa nchini licha ya kuwa inaendeshwa kwa mujibu wa sheria chini ya usimamizi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), imeendelea kuathiri taifa kwa namna mbalimbali hasa vijana.

Nitakijikita kwa wanafunzi ambao ndio tegemeo la taifa kuwapata wataalamu wa sasa na baadaye!

Kamali ama kubeti, umekuwa mchezo maarufu zaidi kinyume cha sera ya mwelekeo wa nchi yetu kuwa nchi ya viwanda na unaweza kusema ni dawa za kulevya zilizoibuka kwa kasi sana hapa nchini.

Wachezaji wa mchezo huo huamini kuwa watabahatika kushinda pindi wanapochagua namba fulani au kutabiri mchezo husika. Na wengi wao hudiriki hata kumwomba Mungu awasaidie kushinda.

Pamoja na kwamba kila kitu kina faida na hasara, mchezo huo ambao umeanza kuwa maarufu nchini unazo hasara nyingi kuliko faida!

Nijikite kwenye mada yangu ya jinsi gani kamali inaathiri mustakabali wa wanafunzi:

Wanafunzi wengi wanaocheza kamali huamini na hutegemea bahati nasibu kuwa ndiyo njia bora na rahisi ya kufanikiwa kwenye maisha kuliko kusoma.

Vilevile kamali huwachochea wanafunzi kupenda sana fedha kuliko masomo, hata kusababisha kutoroka shuleni na kwenda kubeti, hivyo kukosa masomo na mwisho wake kufeli vibaya na lawama pengine kurudishwa kwa walimu.

Mchezo huo wa kubahatisha umewafanya wanafunzi wengi kuwa ‘walevi’ wa kubahatisha kiasi kwamba wanashindwa kujizuia kuacha, mwisho wake wanapoteza mwelekeo katika masomo yao.

Kukosa raha na morali ya kusoma ni miongoni mwa athari za michezo ya kubahatisha pale ambapo wanafunzi wanaocheza michezo hiyo husononeka na kukata tamaa kwa kujiona si lolote na hawana bahati kabisa pindi wanaposhindwa/kuliwa.

Kutumia fedha za akiba au matumizi (pocket money) wanazopewa na wazazi/walezi wao. Hii husababisha tabia ya utapeli na udanganyifu kwa mwanafunzi dhidi ya mzazi/mlezi wake.

Mwanafunzi kuaminishwa kuwa utajiri au mafanikio yanapatikana kwa njia rahisi, hivyo kuwa na kizazi tegemezi kwa taifa ambavyo ni kinyume cha maono na kaulimbiu ya Mheshimiwa Rais, Dk. John Magufuli ya hapa kazi tu, inayolenga na kuhimiza watu wafanye kazi na kuleta maendeleo binafsi na taifa.

Rai yangu kwa serikali hasa kupitia Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania licha ya kuwa wamesitisha matangazo yote yaliyokuwa yakihamasisha mchezo huu wa kamali, wasitishe usajili wa michezo ya kubeti na ambayo wamekwisha kuisajili waifuatilie kwa karibu.

Serikali idhibiti mifumo ya mtandao na kuanzisha sehemu maalumu ya kuchezea michezo yote ya kamali kama ambavyo kasino wanafanya, na hii itasaidia kuzuia wanafunzi na watoto wanaomiliki simu kutoshiriki michezo hii ambayo imezagaa mitaani na inachezwa holela.

Hii ndiyo sauti ya Mwalimu kwa leo.

Tukutane tena kwa mada inayofuata!

Mwalimu Mujuni.

Simu: 0765757179/0623937857

E-mail:[email protected]

Please follow and like us:
Pin Share