Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani

VIONGOZI wa dini kupitia Kamati ya Amani Mkoa wa Pwani wameviasa vyama vyote vya siasa na wagombea kufuata kanuni na taratibu za uchaguzi, na kuepuka kuwa chanzo cha vurugu wakati wa mchakato wa kupiga kura.

Aidha, kamati hiyo imewaomba wasimamizi wa uchaguzi kuhakikisha wanatenda haki na usawa kwa vyama vyote na wagombea, ili kudumisha imani ya wananchi katika uchaguzi huo.

Akizungumza na waandishi wa habari mkoani humo oktoba 28, 2025, Mwenyekiti Mwenza wa Kamati hiyo, Sheikh Khamis Mtupa, alitoa wito kwa Watanzania kudumisha amani na kujitokeza kupiga kura kwa utulivu, akisisitiza kuwa yeyote mwenye nia ovu ya kusababisha vurugu au machafuko aache mara moja.

“Tupuuze uchochezi wa aina yoyote unaolenga kuvuruga uchaguzi na amani ya nchi yetu. Tanzania ibaki salama kabla na baada ya uchaguzi,” alisema Sheikh Mtupa.

Aliongeza kuwa ni jukumu la kila Mtanzania kulinda amani, akisisitiza:“Hatuna nchi nyingine ya kwenda kuishi.

“Uchaguzi ni haki ya kila mtu, hivyo asitokee yeyote kumzuia mwingine kutumia haki yake hiyo kwa sababu zozote binafsi.”alieleza Mtupa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti Mwenza wa Kamati hiyo, Mchungaji Julius Shemkai wa Kanisa la KKKT, alisisitiza umuhimu wa utulivu siku ya kupiga kura, na kuwataka wananchi kujiepusha na vitendo vyote vinavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani.

“Tujiepushe na maandamano yasiyoruhusiwa, uharibifu wa vituo vya kupigia kura au mikusanyiko isiyo halali”

” Yesu Kristo alipofufuka aliwaambia wanafunzi wake ‘Amani iwe kwenu’, na kama Biblia inavyosema katika Waefeso 4:3 — ‘Tujitahidi kuuhifadhi umoja katika kifungo cha amani’,” alifafanua Shemkai.

Pamoja na hayo, aliwapongeza wagombea na vyama vya siasa vilivyoshiriki kampeni kwa kipindi cha miezi miwili kwa kuendesha kampeni kwa ustaarabu na amani, bila kashfa, matusi, au migogoro na vyombo vya ulinzi.

Mchungaji Shemkai pia aliwahimiza wapiga kura kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi kumchagua Rais, Mbunge na Diwani, na baada ya kupiga kura kurejea majumbani au kuendelea na shughuli zao wakisubiri matokeo kwa utulivu.

Kamati hiyo inayoundwa na viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini mkoani Pwani, imetoa tamko hilo baada ya kufanya tafakuri ya kina na kufuatilia mwenendo wa kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa upande wake, Mratibu wa Uchaguzi wa mkoa huo, Gerald Mbosoli alisema, maandalizi yote yamekamilika kuelekea uchaguzi oktoba 29,2025.

Mbosoli alielezea jumla ya vituo 3,941 vya kupigia kura vimeandaliwa mkoani humo na wananchi zaidi ya milioni 1.413 wenye sifa wanatarajiwa kushiriki katika zoezi hilo.