Kampeni ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, za kusaka watu ambao wanajihusisha na mapenzi ya jinsia moja imeibua mjadala mkali wa sheria, tabia, na tafsiri ya vyote viwili.

Sheria iko wazi: Ni kosa la jinai kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja. Lakini si kosa nchini Tanzania pekee. Taarifa ya mwaka 2016 ilibainisha zipo nchi 74 zenye sheria ya aina hii.

Uwepo wa sheria na kukubalika kwa sheria ni masuala mawili tofauti. Na hii ni sababu mojawapo ya ubishi juu ya sheria hii. Nauita ubishi wa kisomi unaosukumwa na misimamo ya wanaharakati na wanasheria. Ni ubishi wa dhana, kwamba zipo sheria ambazo hazipaswi kuwapo kwa sababu zinakiuka haki za binadamu.

Ingekuwa rahisi kufanya rejea kwenye Tamko la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa la 1948 ili kumaliza ubishi huu. Haki ya usawa na kutobaguliwa ni haki ya msingi kabisa ya haki za binadamu iliyopo ndani ya mkataba wa Umoja wa Mataifa, Tamko lenyewe, na mikataba ya kimataifa ya haki za binadamu.

Utangulizi wa Tamko unasema: “Binadamu wote wanazaliwa huru na sawa katika utu na haki.” Kwa maana hii ni binadamu wote, pamoja na wale ambao wanajihusisha na uhusiano wa mapenzi ya jinsia moja.

Bila shaka ndiyo sababu tukasikia, muda mfupi baada ya kuzinduliwa kwa kampeni ya Makonda, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ikatoa taarifa kusema kuwa msimamo wa Makonda si wa Serikali na kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kuheshimu mikataba yote ya kimataifa inayohusu haki za binadamu ambayo imeridhia na imesaini.

Kwa tamko hili timu yote ya Serikali ilitoka uwanjani na kumuacha Mheshimiwa Paul Makonda peke yake. Ilikuwa ni kama vile tangu awali walichezea timu tofauti na Waziri Dk. Augustine Mahiga alifanikiwa kumpiga Makonda chenga ya mwili.

Lakini si kila mtu anaamini kuwa haki inaheshimika ili mradi tu imetajwa na Umoja wa Mataifa. Mwaka 2016 Mahakama ya Haki za Binadamu ya Nchi za Ulaya iliamua katika kesi iliyowasilishwa na raia wawili wa Ufaransa (Kesi Na. 40183/07) kuwa Mkataba wa Ulaya wa Haki za Binadamu hautowi haki ya kufunga ndoa baina ya wanaume wawili. Mahakama iliendelea kutamka kuwa masuala ya ndoa ya jinsia moja yanapaswa kuamuliwa na sheria za nchi husika.

Tunaweza kutaja hitilafu kadhaa juu ya kampeni za Mheshimiwa Makonda, ikiwa ni pamoja na kuanzisha kampeni ambayo haiungwi mkono na Serikali. Aidha, si sawa kusaka kundi moja la raia kwa kuwashuku kuwa wamekiuka kosa wakati inawezekana wapo raia wengine wengi ambao pia tunaweza kuwashuku kufanya makosa, ikiwa ni pamoja na majambazi, mafisadi, wezi wa mifugo, majangili, wavuta bangi, na wabakaji wa watoto wachanga.

Ingekuwa haki kwa wote tuorodheshe watuhumiwa wa aina zote halafu kila mwaka ukianza tufanye mzunguko wa kampeni ya kutaja majina ya watu wa makosa mbalimbali na tukifikia Desemba turudie tena mzunguko.

Ninachopendekeza kingekidhi kwa kiasi kidogo kuleta mazingira sawa kwa wote, ingawa siamini kwa dhati kuwa huu ni utaratibu ambao unapaswa kufuatwa. Kwa kawaida, kazi kubwa ya polisi ni kuchunguza matukio ya uhalifu na nadhani utaratibu ungebaki hivyo kuliko huu utaratibu wa kutafutwa watu ambao wanashukiwa kufanya uhalifu.

Mimi ni muumini mkubwa wa kuheshimu sheria zilizopo hata kabla ya kuanza mijadala ya kifalsafa juu ya uzuri au ubovu wa sheria. Na hii ni pamoja na Sheria ya Makosa ya Jinai inayokataza mapenzi ya jinsia moja na makosa mengine ya aina hiyo.

Naamini pia kuwa sheria hubadilishwa kwa kufuata taratibu. Labda kuna siku itawadia ambapo makosa haya yataondolewa kwenye Sheria ya Makosa ya Jinai. Jambo la msingi ni kuwa kwa sasa ni makosa.

Katika haya malumbano yanayoendelea kuuliza yupi ni sahihi na yupi hayuko sahihi ni kuuliza swali ambalo halipaswi kuulizwa. Sahihi kwa misingi gani? Ya Tamko la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu? La dini? Dini ipi? La sheria za Tanzania?

Utafikiaje uamuzi iwapo mtu hajavaa inavyostahili iwapo hujaainisha yeye ni nani, na yuko wapi. Yuko ndani ya nyumba ya ibada? Yuko bungeni? Au yuko mtaani kama mjasiriamali wa biashara ya ngono?

Kujaribu kuuliza swali moja tu na kulijibu na kuridhika na jibu moja tu ni jitihada ya kujiweka kwenye kundi la watu wanaotiliwa shaka ya kujifanya viziwi na vipofu wasiyoona wala kusikia kuwa lipo zaidi ya swali moja, na kwamba kila swali linaweza kuwa na jibu tofauti.

Naweza nisikubaliane na misimamo ya Umoja wa Mataifa, ya dini, au ya sheria za nchi, lakini nadhani naelewa vizuri sana misimamo hiyo. Tunajipa fursa nzuri ya kujiongezea shinikizo la damu tunapoanza kutumia kigezo cha msimamo mmoja tunaouamini kujaribu kupima msimamo mwingine.

Kwa sasa huu mjadala haujaisha, lakini unaweza kumalizika kwa kufikia maafikiano ya suala moja tu: kukubaliana kutokubaliana.

Please follow and like us:
Pin Share