Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, wiki iliyopita alitoa tangazo la kumtaka Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, kuripoti katika Kituo Kikuu cha Polisi,  Dar es Salaam kutoa maelezo kuhusu tuhuma za kashfa na matusi dhidi ya Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.


Nimeyasikia maneno aliyotoa Askofu Gwajima. Maneno haya nimeyasikia kupitia mtandao wa kijamii ujulikanao kama Whatsapp. Nimesikiliza maneno yake zaidi ya mara 10. Yanasambazwa kwa njia ya sauti na video. Chimbuko la maneno hayo ni kile kinachodaiwa kuwa Kardinali Pengo amewasaliti maaskofu wenzake waliowataka waumini wasiipigie kura ya ndiyo Katiba Inayopendekezwa.


Kardinali Pengo, Machi 14, mwaka huu katika ibada ya Kwaresma kwa Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA), alitofautiana na Jukwaa la Wakristo linalojumuisha Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC).
Pengo alisema Mungu alimuumba kila mwanadamu akiwa huru, hivyo haikuwa sahihi kwa Maaskofu kutoa tamko la kuzuia waamini wao kwenda kupiga kura ya NDIYO kwa Katiba Inayopendekezwa na badala yake wakawachagulia wapige kura ya HAPANA.


Hoja ya maaskofu wale ni kuwa Serikali imeanza mwelekeo wa kuchanganya dini ya siasa. Wanapinga harakati za Serikali zinazoelekeza kuruhusu utunzi wa sheria inayoruhusu ujio wa Mahakama ya Kadhi, itakayokuwa inaendeleshwa kiserikali kwa njia moja au nyingine. Maaskofu wanasema ikiwa Waislamu wanataka Mahakama ya Kadhi basi waanzishe wao kama wao na si kwa sheria ya Bunge.


Masheikh na wanazuoni nao walikaa na kuiweka njia panda Serikali. Kwanza walisema maaskofu wamepotoka kwa kutoa msimamo huo, lakini pili wakaitaka Serikali iwapuuze maaskofu na kuendelea na mpango wake wa kutunga sheria itakayoruhusu ujio wa Mahakama ya Kadhi. Baada ya kauli hizo joto likapanda juu. Ndipo Askofu Gwajima akatoa kauli nzito dhidi ya Kardinali Pengo. Sitazirudia kauli hizo.
Sitanii, tumefika hapa kutokana na ahadi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kwa Waislamu. Pinda aliwaahidi wakati wa Bunge Maalum la Katiba kuwa suala la Mahakama ya Kadhi lisiingizwe kwenye Katiba Inayopendekezwa bali lingeshughulikiwa kwa utaratibu mwingine, akimaanisha kutungiwa sheria na Bunge.


Mwezi huu tena, Pinda amekaririwa akisema Mahakama ya Kadhi itashughulikia masuala ya ndoa na mirathi pekee hivyo wananchi wasihofu. Kwa kauli hizo mbili tu, Pinda alipaswa kujiuzulu kwani amevunja ibara ya 19 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Mwaka 1977. Katiba inazuia Serikali kujihusisha na masuala yanayohusu dini.
Kwa nchi zilizoendelea, kauli hii ingekuwa mwanzo wa maandamano ya amani yasiyo na ukomo hadi Pinda aondoke madarakani. Kama amepata ujasiri wa kuvunja ibara ya 19, nini kitamzuia siku za usoni asivunje ibara nyingine. Pinda ni mwanasheria kwa taaluma, lakini najiuliza inakuwaje anashiriki kubomoa misingi ya nchi iliyojengwa kwa jasho jingi? Sipati jibu.


Sitanii, nikirejea kwenye ajenda ya msingi ambayo ni matusi ya Askofu Gwajima kwa Kardinali Pengo, hapo ndipo ninapopata shida. Inawezekana kabisa kuwa Pengo amekwenda kinyume na msimamo wa Kanisa Katoliki hapa nchini. Ni kwa bahati mbaya tu, baadhi ya watu wakisikia Pengo ni Kardinali wanadhani ndiye kiongozi wa Kanisa Katoliki nchini, si kweli.
Pengo ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam sawa na walivyo maaskofu wakuu wengine katika majimbo makuu kama Tabora, Mwanza, Dodoma, Arusha na Songea. Mamlaka yake ya kiutawala yanaishia katika jimbo lake.


Wadhifa wa Ukardinali unamaanisha kuwa yeye ni mshauri wa Papa kule Vatican. Kazi nyingine anayokuwa nayo Kardinali yeyote katika nchi yoyote ni kupiga kura ya kumchagua Papa inapotokea Papa akafariki dunia au akajiuzulu. Na ili apige kura lazima awe na umri usiozidi miaka 78.
Kwa maana nyingine, ni kwamba Mkuu wa Kanisa Katoliki hapa nchini ni Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) na si vinginevyo. Kuna nchi hazina makardinali, na kuna makardinali ambao si maaskofu, alimradi wameteuliwa na Papa kumsaidia katika kazi moja au nyingine. Kuteuliwa kuwa askofu ni uamuzi binafsi wa Papa. Kuna nchi zina makardinali zaidi ya mmoja.


Baada ya ufafanuzi huo, niongeze jingine. Inawezekana Pengo amewaudhi baadhi ya Wakristo kwa kutoa kauli yenye kutofautiana na msimamo uliotolewa na maaskofu kupitia Jukwaa la Wakristo Tanzania.


Wapo watu wanaosema Kardinali Pengo alitoa kauli ya kutetea Katiba Inayopendekezwa kwa sababu ya ukabila tu, kwa kuwa Pinda ambaye anaipigia Mahakama ya Kadhi debe wanatoka pamoja Sumbawanga. Ni mtoto wa nyumbani.
Wengine wanasema Pengo ametumia haki yake ya asili na kikatiba ya uhuru wa kutoa mawazo, hivyo hastahili kusulubiwa. Wengine wanasema Pengo kwa kauli yake ameathiri kuaminiwa kwa Kanisa Katoliki na maaskofu wa madhehebu mengine kwani amesema maaskofu hawana mamlaka ya kuelekeza wananchi wafanye nini, ilhali hili ndilo jukumu kuu la mchungaji yeyote.


Sitanii, inawezekana limetokea moja au jingine katika haya yanayotajwa na kulalamikiwa. Kwa vyovyote iwavyo viongozi wa dini wanapaswa kujua wajibu walioubeba. Viongozi wetu wamebeba dhamana kubwa ya kiimani.
Kuna kauli tunazozitarajia kutoka vinywani mwao, kwa ajili ya kulinda imani ya dini au madhehebu. Hatua ya Askofu Gwajima kumtaja Pengo kama mjinga, mpumbavu, akamlinganisha na mtoto aliyevaa pampasi, naamini ilivuka mipaka.


Kardinali Pengo naye niliamini anaamini katika demokrasia. Kitendo cha kuwakosoa maaskofu wenzake hadharani waliokaa, wakachambua na kuona Katiba ya nchi inavunjwa na Taifa linaelekea kwenye vurugu za kidini, nadhani pia ilivuka mipaka. Naamini Mwadhama Kardinali Pengo alikuwa na fursa ya kukaa na maaskofu wenzake akawaeleza kutoridhishwa kwake na tamko lao ikiwa hakuliasisi.


Yote hayo inaweza kutokea, lakini yananikumbusha maneno ya kinabii katika Injili ya Mathayo 18:21-22 “Kisha Petro akamwendea akamwambia Bwana ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Hata mara saba? Yesu akamwambia sikwambii mara saba bali hata saba mara sabini.” Imani ya Wakristo imejengeka katika kusameheana.


Sina uhakika kama Kardinali Pengo ndiye aliyekwenda polisi kufungua jalada au la, maana Kamanda Kova amesema ni kutokana na taarifa walizozipata kupitia mitandao ya kijamii. Kwa vyovyote iwavyo, sifurahishwi na wala nisingependa kuona Kardinali Pengo na Askofu Gwajima wanashitakiana mahakamani, hata kama kuna aliyemkashifu mwenzake.


Ajenda iliyoko mezani kwa sasa ni kuhakikisha nchi yetu haiingizwi kwenye misukosuko ya kidini. Sitamani kuona ikitungwa sheria ya kuruhusu ujio wa Mahakama ya Kanisa, wala Mahakama ya Kadhi. Natamani tuendelee kuwa na Tanzania ambayo Serikali haina dini, ila wananchi wake wana dini. Najua wapo wenye kutamani kinyume chake, na wapo kazini.


Sitanii, wala tusishangae. Katibu cha Zakaria 13:7 kinasema: “Amka, ee upanga! Inuka umshambulie mchungaji wangu; naam, mchungaji anayenitumikia. Mpige mchungaji na kondoo watawanyike. Nitaunyosha mkono wangu, kuwashambulia watu wadhaifu.” Leo tunao wachungaji wawili; Gwajima na Pengo wanashambuliana. Wamewaacha kondoo wao ikiwa watakubali mapigo haya yawayumbishe.


Awali nimesema dhana ya kusameheana, Papa John Paul II alipigwa risasi, akamsamehe aliyempiga risasi. Maaskofu hawa wakiruhusu hali ya kushambuliana iendelee, wakati wanamaliza kesi zao mahakamani, watakuta kondoo wametawanyika na Mahakama ya Kadhi imepitishwa. Wasiruhusu hili litokee. Ndiyo maana nadiriki kutumia maneno ya kinabii kuwa Kardinali Pengo na Askofu Gwajima bila kujali nani kamkosea nini nani, futeni kesi hiyo polisi.


Kuendeleza hiyo kesi ni kudhoofisha makanisa mnayoyaongoza na hatimaye imani kwa mujibu wa dini zenu. Wakati umefika wa kukumbuka maneno ya Biblia kuwa “Wasamehe wenye dhambi muweze kuuona ufalme wa mbingu.” Narudia, nawapenda sana ndugu zetu Waislamu. Binafsi napinga ujio wa Mahakama ya Kadhi kwa kuona hatari inayoweza kutufika kama Taifa.


Sitanii, vurugu hizi tunazozishuhudia ni kwa sababu Serikali imeonesha nia ya kupeleka muswada wa kuanzishwa kwa Mahakama hii bungeni. Viongozi wa juu kama Pengo na Gwajima wameanza kuparurana. Tena hii si kati ya Wakristo na Waislamu bali Wakristo wenyewe. Je, tutarajie nini kwa waumini walioko kwenye ngazi ya jumuiya? Je, tutarajie nini mvutano huu ukifikia Waislamu na Wakristo kurushiana maneno makali kama walivyofanya maaskofu, kisha masheikh na wanazuoni wakajibu mapigo?


Narudia na nahitimisha, nchi hii ni yetu sote. Tusifukue makaburi. Misingi tuliyoijenga tuikubali bila kuishi maisha ya kutazamia eti mbona Zimbabwe, Uganda, Saudia au nchi nyingine wanayo Mahakama ya Kadhi na inafanya kazi bila vurugu. Rais Kikwete bado unayo nafasi. Kama ulivyosema kuwa wakati wa Mahakama ya Kadhi haujafika, narudia kauli yangu niliyoitoa hivi karibuni.


Nakuomba usiruhusu Tanzania kutumbukia kwenye vurugu na wewe ukawa wa mwisho kutawala Tanzania yenye amani. Hili la Mahakama ya Kadhi tuliweke kando, Pengo, Gwajima, masheikh na wanazuoni na wengine, hawatakuwa na pa kuanzia kuteteresha amani ya nchi yetu. Mungu ibaridi Tanzania.

By Jamhuri