“Mheshimiwa Rais, Kenya imewachukua miaka saba kuandika Katiba yao, baada ya mvutano wa miaka 20. Je, sisi Tanzania unadhani tunaweza kuandika Katiba yetu ndani ya miaka miwili?” Hili ni swali nililomuuliza Rais Jakaya Kikwete tukiwa Ikulu, siku ya Ijumaa, Aprili 6, 2012. Hii ndiyo siku alipotangaza majina ya wajumbe wa Tume ya Marekebisho ya Katiba, ikiongozwa na Jaji Joseph Sinde Warioba.


“Kenya ni Kenya na Tanzania ni Tanzania,” haya ni majibu aliyonipa Rais Jakaya Kikwete, tukiwa hapo Ikulu, tena kwa kujiamini kabisa. Baada ya hapo zikaanza sarakasi na matamko ya kila aina. Mara tukaambiwa Aprili 26, 2014 lazima tuwe na Katiba mpya. Baadae hii ikagoma, tukaambiwa Aprili 30, 2015 lazima tupige kura ya maoni, hii nayo imegoma.


Oktoba, mwaka 2013 Mwenyekiti wa CCM, ambaye ndiye Amiri Jeshi Mkuu, Mhe Prof. Dk. Jakaya Kikwete, alikubaliana na vyama vyenye wabunge chini ya mwavuli wa Kituo cha Demokrasia (TCD) kuwa ni vigumu mchakato wa Katiba kuendelea. Kuwa ni vyema yafanywe marekebisho ya msingi katika Katiba ya mwaka 1977 tunayoitumia sasa kisha Katiba Inayopendekezwa igeukiwe mwaka 2016.


Mwenyekiti wa TCD, Mzee wa Mapesa, John Cheyo akautangazia umma wa Watanzania kwa bashasha kuwa Rais msikivu, anayetokana na chama sikivu, amekubali marekebisho ndiyo yafanyike, Katiba mchakato upumzishwe. Kati ya marekebisho waliokubaliana ni pamoja na Tume Huru ya Uchaguzi, mgombea huru na mengine kadha wa kadha. Sina uhakika kama Rais Kikwete aliyasahau haya alipoingia kwenye vikao vya chama, au alitishwa na chama!


Akayaacha, akiwa China akapata tuzo ya kuitwa Profesa, naye akatuzawadia sisi Watanzania katika ardhi ya ugenini kwa kutueleza tarehe ya kupigia kura Katiba Inayopendekezwa. Utamaduni huu ni wa aina yake. Unaacha kutoa tangazo muhimu kama hili kwenye ardhi ya nyumbani, kisha unalitolea ugenini. Hii pekee inatosha kuonyesha uzito anaotoa kwa suala analozungumza.


Sitanii, nilisema kitambo kuwa Katiba Inayopendekezwa haitapatikana mwaka huu. Kifungu cha 5 (3) cha Sheria ya Kura ya Maoni ya Mwaka, 2013 kinasema: “Kwa madhumuni ya kuelimisha na kuhamasisha wananchi kuhusu kura ya maoni Tume, itatoa elimu ya uraia juu ya Katiba Inayopendekezwa kwa kipindi cha siku sitini kuanzia tarehe ya kuchapishwa katika Gazeti la serikali kwa Katiba Inayopendekezwa.”


Kifungu hiki pekee kina ujumbe mzito. Siku ya Aprili 4, 2015 ndipo nimeona Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imepata msaada wa kusambaza nakala za Katiba Inayopendekezwa kwa njia ya nakala tete na machapisho. Hakika, sitaki kuamini au kuaminishwa kuwa elimu ya Katiba Inayopendekezwa kwa umma ndipo imeanza kwa kishondo sasa.
Hata kama ndivyo, basi elimu hii itakamilika mwezi Juni. Tukumbuke Njombe, imewachukua karibu miezi miwili kukamilisha uandikishaji wa wapigakura kwa mfumo wa Biometric Voters Registration (BVR). Kwa maana nyingine, bado kuna mikoa 29 haijaandikishwa. Kuna mikoa ina jiografia mbaya kuliko Njombe. Nenda Mkoa wa Pwani. Mkoa huu umekaa kama pweza. Shughuli yake ni pevu.


Sitazungumzia uharamu wa mchakato, kwani wabunge walioshiriki kutunga Katiba Inayopenekezwa, wao walitunga sheria yenye manufaa kwao. Bunge la Kutunga Katiba, linapaswa kusimamiwa na wajumbe waliochaguliwa na wananchi na kazi yao inakuwa moja tu, Kutunga Katiba. Wakimaliza hawaruhusiwi hata kugombea ubunge katika uchaguzi unaofuata.


Hapa kwetu tumeiona kachumbari. Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wote, Wabunge wote na wajumbe wa kuteuliwa 201, akiwamo hadi Mwenyekiti wa Chama cha Waganga wa Kienyeji, wakateuliwa si kwa mapenzi ya wananchi, bali kwa utashi wa Rais, pengine na chama chake. Hii pekee ilitosha kuharamisha mchakato wa Katiba Inayopendekezwa.


Sitanii, kama hiyo haitoshi kura zikatafutwa kwa udi na uvumba. Wagonjwa hospitalini wakapiga kura, watu waliokwenda hija wakaacha swala wakaenda kupita kura! Nasikia hata binadamu wenye hadi nyingine, tusio nao tena hapa duniani, siku ya kupiga kura walirejea, wakapiga kura, kisha wakarejea kwenye pumuziko la milele!
Jaji Damina Lubuva amenisikitisha, alipohojiwa na waandishi wa habari juu ya utata wa Rais Kikwete kutangaza tarehe ya kupiga kura kwa Katiba Inayopendekezwa, akasema: “Kifungu cha tano cha Sheria ya Maoni, kinampa nguvu (Rais) ya kutangaza muda wa kufanyika kwa Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa, japo kutangaza tarehe rasmi ya shughuli hiyo ni kazi yetu. Hivyo Rais alikuwa within the spirit of the law (ndani ya dhamira ya sheria).”


Hapa nimepata tabu kidogo. Kwanza Sheria aliyoitaka Jaji Lubuva haipo. Kama anaitumia hiyo aliyoitaja ama siyo iliyotungwa na Bunge au kuna sheria mbili katika suala moja. Yeye amesema “Kifungu cha tano cha Sheria ya Maoni.” Nilipoirejea sheria iliyopitishwa na Bunge, Kifungu cha Kwanza kinasema:
“Sheria hii itaitwa Sheria ya Kura ya Maoni ya mwaka, 2013, na itaanza kutumika katika tarehe ambayo itatangazwa na Waziri kwa Amri itakayochapishwa katika Gazeti la Serikali.” Nimepata wasiwasi kuwa huenda hiyo ‘Sheria ya Maoni’ aliyoitaja Jaji Lubuva ni nyingine kutokana na yanayotamkwa na Kifungu cha Tano juu ya mamlaka ya kutangaza siku ya kura ya maoni. Sheria iliyopitishwa na Bunge Kifungu cha Tano kinasema hivi:


“5.-(1) Tume ndani ya siku kumi na nne baada ya kuchapishwa kwa swali la kura ya maoni katika Gazeti la Serikali itaainisha: (a) muda wa kuelimisha na kuhamasisha wananchi kupiga kura ya maoni kuhusu Katiba Inayopendekezwa; (b) siku ambayo kura ya maoni itafanyika; na (c) muda wa upigaji kura ya maoni.” Ikiwa kuna pahala kifungu hiki kinampa mamlaka Rais kutangaza siku ya kura ya maoni, basi nasema kichwa changu na iwe halali yake Jaji Lubuva.


Hii ni Kwaresima. Nyakati ambazo Bwana Wetu Yesu Kristu alifia ukweli. Nitatenda dhambi isiyosameheka, nikiona aibu kuusema ukweli halisi. Kwa sisi tunaoamini katika Kristu, kuuonea aibu ukweli ni sawa na kuona aibu kutamka jina Yesu. Sijajiandaa kuonewa aibu na Yesu machoni pa Baba yetu aliyepo mbinguni.
Katika Injili ya Luka Sura ya 9:26, Yesu anasema: “Mtu akinionea aibu mimi na mafundisho yangu, Mwana wa Mtu atamwonea aibu mtu huyo wakati atakapokuja katika utukufu wake na wa Baba na wa malaika watakatifu.” Narudia ukweli mchungu ni tiba. Inawezekana Jaji Lubuva anayo sheria nyingine, anayoitumia kuendesha Tume, hivyo Rais naye ni sehemu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi na sheria aliyonayo Jaji Lubuva inampa Rais mamlaka ya kutangaza siku ya kura ya maoni!


Sitanii, nimepata kulisema hili na hapa nalirudia. Mimi nimeisoma Katiba Inayopendekezwa. Katiba hii inayo mambo mengi mazuri, mfano wa msingi ni Uhuru wa Vyombo vya Habari na Haki ya Kupata Habari. Haki hii ambayo ni haki wezeshi, iliyopo kuwezesha haki nyingi kupatikana haijawahi kutolewa na Katiba yoyote ya nchi hii tangu tupate uhuru.


Zipo haki nyingine zilizokuwa zikitajwa kwa chini chini au ndani ya sheria kama Haki ya Kupata Elimu, Haki ya Ardhi, Haki za Watoto, Haki za Wanawake, hizi nazo zimewekwa vizuri mno. Hata hivyo, kuna sehemu kadhaa ambazo hazijatulia. Moja na ya msingi, ikiwa ni aina ya Muungano. Muundo uliopendekezwa ndio mwisho wa uwapo wa Tanzania.


Mimi naamini hatujaharibikiwa lolote. Fedha zilizotumika zingeweza kufanya kazi nyingine, lakini zimesaidia tumepata fundisho. Tumepata fundisho kuwa kumbe kama tunataka kutunga sheria mama; Katiba, lazima kufuata misingi yote ya utungaji wa Katiba bila kuruka hata kifungu kimoja. Pia tumejifunza kuwa kumbe jamii yetu imegawanyika na tumepata msingi wa kuanzia.


Sitanii, ubabe uliotumika katika kuandika Katiba hii unaacha maswali mwengi. Wengine tunafika mahala pa kujiuliza kuwa hii Katiba tunajiandikia ni yetu au kuna mtu yuko Ulaya na Amerika anatuendesha kwa rimoti? Mwalimu Nyerere alikwishatuwekea misingi. Tanzania ni taifa la maafikiano. Hili limegoma, tusubiri mwakani tufanye mchakato kwa njia nyoofu.
Kichwa cha makala hii kinasema: “Tukicheza hakuna uchaguzi Oktoba.” Hapa kuna mambo mawili. Tumekwishakubaliana kuwa daftari la zamani lina matundu mengi. Wapo waliokufa, wapo waliohama na vijana wengi waliotimiza umri wa kupiga kura hawamo kwenye daftari hilo. Kasi ya sasa ya uandikishaji wa wapigakura katika BVR, kinyonga mwendo wake afadhali.


Kama Njombe wametumia miezi miwili, sitashangaa mikoa 29 iliyosalia kutumia miaka 2. Tena tunashikilia kuwa lazima uchaguzi wa Oktoba ufanyika kwa daftari jipya. Jaji Lubuva katwambia litakuwa tayari Julai. Julai hiyo, tuunganishe elimu ya Katiba Inayopenekezwa, tuunganishe na siku 60 au 90 za Kampeni za Uchaguzi Mkuu!


Hapo, sijataja harakati za uchaguzi ndani ya vyama. Jaji Lubuva ameahirisha kura ya maoni kwa muda usiojulikana. Hii imenikumbusha kilichotokea Aprili 25, mwaka 1965. Ilikuwa Zanzibar na Tanganyika zipitie makubaliano ya Muungano baada ya mwaka mmoja. Ilipofika tarehe hiyo, Mwalimu Nyerere akatoa Waraka wa Kirais, ulioahirisha upitiaji wa makubaliano ya Muungano hadi baadae. Hiyo baadae hadi leo haijafika.


Hofu kuu niliyonayo ni daftari linaloandaliwa. Hili haliwezi kutumika katika Uchaguzi Mkuu. Daftari hili limetajwa kisheria kuwa ni la Kura ya Maoni. Sheria ya Kura ya Maoni ya Mwaka 2013 katika Kifungu cha 9 (1) inasema: “Daftari la wapiga kura lililoanzishwa chini ya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi na Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar litakuwa ni daftari la wapiga kura kwa madhumuni ya kura ya maoni.”


Kwa tafsiri ya kifungu hiki, litapaswa kuwapo daftari la wapiga kura kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu. Ikumbukwe, Bunge la Jamhuri ya Muungano limekwishafanya mikutano 19. Mkutano wa 20 unaotarajiwa kuanza hivi karibuni ni wa Bajeti. Katika mkutano wa bajeti inaruhusiwa kutungwa sheria moja tu inayohusiana na masuala ya fedha (the Finance Bill) kwa ajili ya mapato na matumizi.


Sitanii, ni kwa misingi hiyo tupo katika kona mbaya. Ama litaitishwa Bunge la Dharura uwepo mkutano wa 21 au Rais aliyepo madarakani itabidi aongezwe muda, kisha aitishe mkutano wa 21 wa Bunge kurekebisha Sheria ya Kura ya Maoni ya Mwaka 2013 iruhusu daftari lake litumike kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Oktoba au tunaweza kuacha uchaguzi au tukatumia daftari la zamani.


Msomaji usishangae wala kuduwaa. Hiyo ndiyo hali halisi. Chini yetu kuna makaa ya moto, kwenye kikaango ambapo tungejipumizisha kuna mafuta yaliyochemka tayari. Tanzania sasa inageuka bakuli la aina hiyo. Kumbuka Katiba Mpya haikuwa sehemu ya Ilani ya CCM, wamedandia treni kwa mbele. Je, tunafanyaje kukabiliana na changamoto hizi? Nipe jibu kupitia simu au barua pepe niliyoweka hapo juu. Mungu ibariki Tanzania.

 

By Jamhuri