Karibu 2020, tumejiandaaje?

Toleo la leo ni la kwanza kwa mwaka 2020. Mwaka 2000 tukiwa Buruguni eneo la Sewa, nilikuwa na marafiki zangu kadhaa. Baadhi Mungu amewapenda zaidi, ila wengi bado tupo. Zilivuma taarifa kuwa mwaka 2000 ulikuwa mwisho wa dunia. 

Wakati huo nilikuwa na mtoto mmoja. Kichwani nilijawa masikitiko. Wakati huo baba alikuwa amefariki dunia miaka mitano iliyopita. Moyo wangu ulikwenda mbio. 

Hata hivyo, nilikumbuka maneno ya bibi yangu, Rozalia Kilungo. Yeye alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 102. Akiwa na umri wa miaka 80, alipanda miche ya michikichi 10. Baadhi ya watu pale kijijini kwetu walimshangaa. Wakamwambia kwa umri huo yeye anapanda miwese afaidi nini? Yeye alikuwa na jibu rahisi: “Miwese niliyoikuta sikuipanda mimi, hivyo hata mimi nitakayoipanda wataikuta wengine.”

Jibu lake halikuishia hapo, aliniambia: “Katika maisha, weka mipango kama vile utaishi milele bila kufa. Mwaka usianze bila wewe kuwa na mpango wa maendeleo.” Maneno haya yalinigusa tangu wakati huo hadi leo.  Kila mwaka ukianza ninafikiria ninataka kufanya nini. Nimeona ni vema niwashirikishe Watanzania wenzangu juu ya jambo hili. 

Sitanii, ninafahamu Watanzania wengi ni kama wamekata tamaa ya maisha. Maisha yamekuwa magumu kwa familia nyingi kiasi kwamba chakula wanapiga pasi ndefu. Chai inanywewa saa 7 mchana na chakula cha jioni kinaliwa saa 1 usiku. 

Siku inakuwa imekwisha hivyo. Wazazi wengi waliokuwa wanapeleka watoto wao kwenye shule za binafsi, sasa wanawahamishia katika shule walizokuwa wanaziita “St. Kayumba.”

Kwa hakika hiki ni kipindi kigumu kwa mtu asiyefikiri. Napata fursa ya kuwasiliana na watu wa kada mbalimbali. Kwa watu walioamua kuwekeza katika viwanda, hakika kwa sasa wanamshukuru Mungu. 

Serikali imedhibiti bidhaa feki kutoka nje ya nchi, na matokeo yake kila wanachokizalisha kinauzwa. Ni kutokana na hili, tunashuhudia serikali ikiongeza makusanyo ya kodi. Kwa mwezi Desemba, 2019 imekusanya Sh trilioni 1.9. 

Makusanyo haya ni historia. Makusanyo haya yanapaswa kutufahamisha kuwa kumbe dhana ya kuondoa umaskini kwa Watanzania inawezekana. Kwa nchi yetu kulingana na ukubwa wake, idadi ya wananchi, maliasili inayopatikana Tanzania na jiografia yetu, basi soko kwa bidhaa zote zinazouzwa, Tanzania soko liko wazi. 

Sitanii, ninafahamu mawazo ya Watanzania wengi yameanza kujielekeza kwenye uchaguzi. Kupanga ni kuchagua. Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, tunapaswa kuuwaza kwa machale. 

Nashauri kwa uzoefu tulioupata katika uchaguzi wa serikali za mitaa, bora Watanzania tuwaze kujenga uchumi kuliko vyama vya siasa. Atakayewekeza nguvu kubwa kwenye uchaguzi huu akasahau uchumi wa familia yake, atayakumbuka maneno yangu.

 Mara kadhaa nimesoma maandishi ya Padri Faustine Kamugisha, ambaye mara zote anasema: “Kushindwa kupanga ni kupanga kushindwa.” 

Hakika ingawa baadhi ya watu wanasema huenda wamekwisha kuchelewa, walipaswa kupanga mipango mwaka jana, lakini mimi ninasema heri nusu shari kuliko shari kamili. Hii ni Januari. Ni vema kila Mtanzania akapanga analenga kufanya nini kwa ajili yake, familia yake na taifa kwa ujumla.

Wala huu si muda wa kukaa chini kulia. Si muda wa kutafuta mchawi, kwamba ni nani aliyekwamisha biashara zako au aliyekufanyia fitina ukafukuzwa kazi. Nafahamu wapo watu waliodhani mwaka wa uchaguzi serikali ingelegeza kamba. 

Kwamba fedha zingerejea mtaani kama zamani. Binafsi naona dalili za mvua ni mawingu. Hakuna uwezekano wa fedha kufurika tena mtaani kwa sasa. 

Ikiwa tunajiandaa kwenda katika ‘Uchumi wa Kati ifikapo mwaka 2025’, basi kila familia, kila mtu anapaswa kuwaza kwa mkondo huo. Serikali inajenga miundombinu, ambayo tukiitumia vema tutapata faida kubwa katika biashara tufanyazo. Sera ya Viwanda ni wazi, inalenga kuliondoa taifa letu katika jembe la mkono na kuliingiza katika ulimwengu wa teknoloja.

Sitanii, naomba usisubiri mambo yatokee kwa neema za Mungu. Huu ni wakati wa kuweka mipango inayotekelezeka. Mtu binafsi na familia zinapaswa kujipanga kujenga uchumi wa familia, ambao hatimaye utajenga uchumi wa taifa. Heri ya Mwaka Mpya 2020, tuweke mipango itusaidie kujikwamua kiuchumi.