Wakati fulani wabunge waligombana na aliyekuwa Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Omar Mahita. Hoja ilikuwa kwamba Jeshi la Polisi lilistahili kuvunjwa ili liundwe upya. Wakatoa mfano wa Jeshi la kikoloni la King African Rifles (KAR), lilivyovunjwa baada ya maasi ya mwaka 1964 na kuundwa kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Hoja ya wabunge hao ilitokana na ongezeko la ujangili na mauaji. Mtazamo wao ukawa kwamba Polisi wameshindwa kazi. IGP Mahita alijibu mapigo kwa kusema kama wabunge wanataka kuona utendaji kazi wa Polisi, basi wawe tayari kuwalipa vizuri kama wao wanavyolipwa.

 

Ujio wa IGP Said Mwema ukawa wa ahueni kwa wananchi. Polisi walipata vitendea kazi vya kutosha. Wakapambana na ujambazi na majambazi. Uporaji fedha ulioshamiri kwenye benki, ukapungua na pengine kukoma. Kwa upande huo Jeshi la Polisi limefanikiwa.

 

Polisi wameanza kulalamikiwa tena. Ukiacha ubabe na mauaji wanayoyafanya kwa wananchi wasio na hatia, walinzi hao wa raia na mali zao ndiyo walioamua kuwa wahalifu wakuu.

 

Gazeti hili limeripoti habari zinazomhusu Mohamed Malele kujitokeza kwenye vyombo vya ulinzi na usalama kuweka wazi mtandao wa mauaji na uhalifu ndani ya Polisi katika Kanda ya Ziwa. Habari kwamba Polisi ndiyo waliohusika kumuua Kamanda Barlow, zinatisha na kushangaza.

Juzi, polisi kadhaa kutoka Arusha walikamatwa mkoani Kilimanjaro wakiwa wamepakia shehena ya magunia 18 ya bangi ndani ya gari la Kamanda wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) Mkoa wa Arusha. Fikiria, gari la Kamanda wa Polisi ndilo linalotumika kupakia bangi! Kana kwamba haitoshi, mmoja wa watuhumiwa muhimu kwenye tukio hilo tunaambiwa eti alitoroka akiwa chini ya ulinzi wa polisi! Huu ni uhuni.

 

Lakini kabla ya tukio hilo, tunakumbuka polisi wengine watatu waliokutwa wakiwa na fuvu la kichwa cha mtu, wakipanga utaratibu wa kumbambikia kesi mfanyabiashara mmoja mkoani Morogoro. Polisi wetu wamefikia hatua ya kuwa na mafuvu ya binadamu kwa ajili ya kujipatia fedha!

 

Lakini ni polisi hawa hawa ambao tayari walishamwachia mtuhumiwa wa ujangili, maarufu kwa jina la Ojungu mkoani Arusha. Baada ya vyombo vya habari kuandika, mtuhumiwa huyo karejeshwa rumande. Inawezekana hiyo ni danganya toto. Pengine mtuhumiwa huyo kwa vile ana fedha, si ajabu akawa analala katika hoteli ya nyota nne au tano mjini Arusha! Tanzania kila kitu kinawezekana.

 

Wakati naandika makala haya, polisi walikuwa wamelewa katika vurugu zilizojitokeza mjini Mtwara. Kwa sababu hiyo, ukaombwa msaada kutoka kwa askari wa JWTZ na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT). Askari wanne walikufa ajalini wakielekea kwenye dhima yao halali ya kurejesha amani mjini Mtwara.

 

Tunaambiwa kwamba baada ya JWTZ na JKT kuingia Mtwara, hali imerejea kuwa ya kawaida. Wamepokewa kwa shangwe. Wananchi wamefurahi. Kwanini JWTZ wapokewe kwa shangwe tofauti na Polisi? Jibu ni moja, polisi wanatuhumiwa kujihusisha kwenye uporaji. Zipo tuhuma kwamba polisi waliopelekwa Mtwara, miongoni mwao ni wahuni. Badala ya kutuliza ghasia kwa busara, waliamua kuumaliza umaskini wao kwa kuendesha vitendo vya uporaji na ubakaji!

 

Mara zote nimewapenda JWTZ. Nimepata bahati ya kushiriki kwenye shughuli zao nyingi, zikiwamo za kivita. Nidhamu ya JWTZ ni kubwa na ya kutukuka. Ndiyo maana kila linapotokea suala la ulinzi katika ukanda huu na hata kimataifa, JWTZ imepewa dhima hiyo. Hakuna mahali ambako askari wa JWTZ wamelalamikiwa kujihusisha na uporaji, ubakaji au wizi, hasa wanapokuwa kwenye operesheni au mapambano ya kimataifa.

 

Sikushangaa kuwasikia wana-Mtwara wakiwapokea kwa shangwe na kuwafurahia JWTZ. Wakati umefika wa kujiuliza maswali na kutafuta mwarobaini kwa Jeshi la Polisi. Je, vijana wanaojiunga Polisi wanachujwa? Je, si kweli kwamba wanaokotwa tu wale vijana walioshindikana mitaani?

 

Je, kuna uhalali wa kuendelea na mfumo wa kiutendaji na kimfumo wa Jeshi la Polisi ambao tumeurithi kutoka kwa wakoloni? Ukifuatilia mtiririko wa matukio ya aibu ndani ya Polisi, utaona kuna kila aina ya sababu za kulifumua Jeshi hili.

 

Please follow and like us:
Pin Share