📌Mkurugenzi Mtendaji TANESCO akagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho na kuridhishwa na kasi ya ujenzi wake

📌Ni katika kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Mhe.Dkt Doto Biteko NWM&WN katika kuusimamia mradi kwa karibu

📌Asifu kasi ya Mkandarasi TBEA Katika ujenzi wa kituo hicho

Na Agnes Njaala, JamhuriMedia, Tabora

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mha. Gissima Nyamo-Hanga Mei 22, 2024 ametembelea na kukagua maendeleo ya utekelezaji wa ujenzi wa kituoa cha kupokea, kupoza na kusambaza umeme cha Uhuru – Urambo ( Kilovolti 132) mkoani Tabora ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt Doto Biteko aliyoyatoa Machi 27, 2024  alipotembelea mradi huo na kusisitiza usimamizi wa karibu ili kuhakikisha  mradi unakamilika kwa wakati uliopangwa .

Mhandisi Gissima amesema kuwa, utekelezaji wa mradi huu utaenda kuondoa adha ya upatikanaji wa huduma ya umeme katika wilaya za Urambo, Kaliua na Uyui ambapo itapelekea wananchi kupata huduma bora ya umeme kwasababu mradi huo ni mahsusi kwaajili yao kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii ili waweze kufurahia matunda ya juhudi ambazo serikali inafanya kuhakikisha wanapata umeme .

Akieleza hatua iliyofikiwa mara baada ya kufanya ukaguzi huo Gissima amesema kuwa Mhe.Dkt Doto Biteko alipotembelea kituoni hapo  ujenzi  ulikuwa umefikia asilimia 84 lakini katika kipindi cha miezi miwili kutoka mwezi Machi mwishoni  mpaka sasa ujenzi  umefika asilimia 92 na hivyo kufanya ongezeko la asilimia 8.

” Niwapongeze TBEA kwa kasi ya ongezeko la asilimia za ujenzi wa kituo lakini pia niwaombe msiridhike mkalala bali muendeleze kasi hiyo ili mtimize matarajio ya kukamilisha ujenzi wa kituo kwa wakati “, amesisitiza Gissima.


Kwa upande wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme amesema kuwa Mhe. Dkt. Doto Biteko aliwataka ETDCO waongeze jitihada kuhakikisha kasi yake inaendana na ujenzi wa kituo ambapo kwasasa umefikia asilimia 25 kutoka asilimia 10 za Mwezi Machi ,2024 .

” Natambua ya kuwa kasi hiyo ndogo ya utekelezaji imetokana na hali ya mvua nyingi  tuliyokuwa nayo ambayo ilipelekea ugumu kuendelea na ujenzi wa njia hiyo  lakini kwasasa mvua zimeacha kunyesha na ardhi nayo imeanza kukauka hivyo tutafute namna kuhakikisha ujenzi unaendelea kwa kasi zaidi “, amesema Mha. Gissima.

Utekelezaji wa mradi huu ulianza 18, Septemba, 2021 na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Juni, 2024 ambapo kazi ya ujenzi wa kituo cha kupoza   imegawanyika katika sehemu mbili ya ujenzi wa kituo  ambao unafanywa na kampuni ya TBEA kutoka China   huku kazi ya ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Tabora hadi Urambo (Km 115) ikifanywa na kampuni ya ETDCO .

By Jamhuri