Ni usiku wa manane. Nimeamka kwa nia ya kuanza safari ya kwenda msibani. Nakwenda Bukoba kuhani msiba wa mama wa rafiki yangu. Huyu si mwingine, bali ni Prudence Constantine, Kaimu Mhariri Mkuu wa Tanzania Broadcasting Corporation (TBC).

Machi 2 alfajiri, Prudence amepata pigo la kufiwa na mama mzazi. Nilimfahamu mama huyu. Amefariki akiwa na umri wa miaka 84.

Prudence, kitinda mimba katika familia ya mzee Mugisha Constantine, alimpenda mno mama yake. Alishibana na mama yake. Mama huyu na Prudence walikuwa wakiitana Miss. Prudence ilikuwa akimwita Miss, mama huyu alijibu mapigo kwa kumwita Puru. Hakika ni majonzi, nimesoma michango ya wahariri, wengi wameguswa.

Nikiwa najiandaa kwenda msibani, najua wakati naandika makala haya mambo mengi yana uwezekano wa kubadilika, maana ni karibu wiki kabla ya makala haya kuchapishwa gazetini.

Maswali yanagusa moyo wangu. Najiuliza hivi kweli tutapata Katiba mpya? Je, Katiba mpya itafananaje? Je, Katiba hii itakuwa ya wananchi?

Nimelazimika kusoma utenzi wa Mwalimu Julius Nyerere aliouandika miaka 24 iliyopita. Wiki iliyopita tuliuchapisha utenzi huu katika gazeti letu. Unaitwa ‘Tanzania, Tanzania’.

Mwalimu Nyerere analia sana na kifo tarajiwa cha Tanzania. Anafikia hatua ya kutumia mifano yenye mguso. Anasema si kila wanachotaka wengi lazima kipatikane. Anahoji iwapo kundi kubwa la watu likitaka mama yako mzazi auawe utaunga mkono matakwa yao.

Sitanii, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda, wiki iliyopita ameandika suala lililogusa moyo wangu. Alihoji inakuwaje Watanzania wanathamini kilichoundwa na mkoloni na kutothamini ubunifu wetu sisi Waafrika.

Kibanda alikuwa akihoji inakuwaje watu wanadai Tanganyika, ambayo kimsingi iliundwa kupitia mkutano wa Berlin, Ujerumani, na kubatizwa rasmi mwaka 1920 na Gavana wa kwanza wa Kiingereza, Horace A. Byatt.

Maneno ya Kibanda yamenifikirisha. Nimekaa nikawaza na kuwazua. Mimi ni mmoja wa waumini wa ujio wa Tanganyika. Sitaki ujio wa Tanganyika kwa nia ya kubagua Wazanzibari, bali kwa nia ya kulipa Taifa letu fursa ya kuchora msitari. Tukatenganisha lipi la Muungano, lipi la Tanganyika na lipi la Zanzibar. Niliamini na naendelea kuamini kuwa ujio wa Tanganyika utapunguza matatizo.

Leo Wazanzibari wengi wanajiona ni Watanzania daraja la pili kwa sababu ya uhalisia wa mfumo wa Muungano. Waziri wa Kilimo na Chakula wa Muungano au Waziri wa Maji, hakuna siku anayokwenda nje ya nchi akatangaza kuwa anaiwakilisha Tanganyika. Mara zote husema wanaiwakilisha Tanzania, wakati Zanzibar kuna waziri wa wizara na cheo sawa na hicho, ila huyu hatambuliki kimataifa.

Kimsingi, binafsi nimesema mara nyingi kuwa nakwazwa na jambo moja tu katika mapendekezo ya rasimu ya Katiba mpya — ardhi. Hatuwezi kuwa na Tanzania isiyo na ardhi. Ukiacha mkataba wa Montevideo unaotamka ardhi kama sifa namba moja kwa taifa kutambuliwa kama nchi, ardhi ni nguzo na chimbuko la uraia wa kuzaliwa. Sirudii, hili nililiandika wiki iliyopita.

Narudia, Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, kama kweli mnayo nia ya dhati ya kuhakikisha nchi yetu inabaki kuwa moja, pambaneni ardhi liwe suala la Muungano.

Zanzibar wanaweza kukumbatia ardhi yao, lakini nawahakikishieni kuwa wakiendelea na msimamo huo, watakuwa wa kwanza kupata hasara. Tanganyika nayo itatunga sheria yake ya ardhi, hawatakuwa na sifa za kuishi Bara.

Sitanii, hoja inayotumika kuwa hakuna ardhi Zanzibar kwa maelezo kuwa hakuna ardhi sikubaliani nayo. Dar es Salaam katika maeneo kama Kariakoo, Posta Mpya na ya Zamani, Buguruni, Tandika na kwingineko hakuna ardhi tena. Hata hivyo, haki ya kumiliki ardhi haijafungwa. Ndiyo maana kiwanja kidogo cha mita 20 kwa 20 Posta Dar es Salaam kinauzwa kwa Sh bilioni 8.

Hapa nazungumza nini? Ninachosema hata kama ni eneo la Mji Mkongwe, Micheweni au Chake Chake, kila Mtanzania apate haki ya kununua na kumiliki ardhi, isipokuwa tu awe na uwezo wa kulipia gharama husika ya ununuzi wa ardhi. Mbona Dar es Salaam wanalipa kiasi hicho na hakuna anayezuiliwa asitafute ardhi Posta?

Sitanii, kichwa cha makala haya kinazungumzia mkutano wa Berlin. Mkutano huu uliofanyika Oktoba 1984 hadi Februari 1885, ndiyo uliotumika kuligawa Bara la Afrika katika makoloni.

Taaria za awali nilizosoma zinaonesha kuwa wakoloni walipanga wakutane Berlin, Ujerumani, kwa nia ya kuzungumza na kuamua nani aongoze kipande kipi cha Afrika, hivyo kuepusha migongano.

Makadirio ya awali waliamini mkutano huu ungechukua wiki nne. Wakubwa hawa — Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Ubelgiji, Italia na mataifa mengine — walitarajia kuwa Novemba 1884 ramani ya dunia (hasa Bara la Afrika) ingekuwa imepatikana na kuwapa fursa ya kuendelea kuvuna rasilimali bila migongano.

Wakubwa hawa hawakufanikiwa. Mkutano uliotarajiwa kwisha Novemba 1884, walijikuta ukiendelea hadi Februari 1985. Hata Sikukuu ya Krismasi inayoheshimika kwa kiwango kikubwa walilazimika kuisherehekea wakiwa kwenye mkutano huu wa mabishano. Ubishi ilikuwa ni jinsi ya kuligawa Bara la Afrika na kuweka makoloni ya kudumu.

Sitanii, nimepata wakati mgumu baada ya kushuhudia kinachoendelea Dodoma. Rafiki yangu aliniambia kuwa awali walipanga kanuni zijadiliwe kati ya siku mbili hadi nne. Nilichoshuhudia zimejadiliwa kwa wiki tatu. Bunge linapaswa kujadili rasimu kwa siku 70.

Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kimsingi ukiangalia mwenendo, hawakufikia mwafaka juu ya aina ya kura iwapo ziwe za siri au za wazi.

Ubishi na mzaha unaoendelea katika ukumbi wa Bunge mjini Dodoma unanitia wasiwasi. Najiuliza, hivi hawa wanamaanisha nini? Ikiwa kanuni zimechukua wiki tatu, vipi rasimu yenye ibara zaidi ya 270? Tena si ibara tu, vipi wakifika kwenye sura ya sita na kuanza kuzungumzia muundo wa Muungano?

Rafiki yangu ameniambia (na naona hili litatokea) kuwa kama hawatapigana, basi Serikali mbili zitaendelea kuwapo.

Ubishi ninaouona katika Bunge la Katiba na matukio ya chini kwa chini kama Wazanzibari kulipwa 120,000 ya ziada na Serikali yao, wakidai wako nje ya nchi kwa kupanda boti na kuja Dodoma ambayo ni Tanganyika sehemu ya Tanzania, unanipa wasiwasi mkubwa. Naona Muungano ni kama umekwishaondoka siku nyingi.

Najiuliza wapi mbali kati ya Tandahimba au Karagwe na Dodoma, ikilinganishwa na Mji Mkongwe au Mjini Magharibi na Dodoma. Wenzetu hawa wanajiona kwa kuja Dodoma wako nje ya nchi? Kweli? Hapa nayakumbuka maneno ya Mwalimu Nyerere. Tupo mbioni kutengeneza dhambi ambayo milele haitasahaulika.

Sitanii, Tanzania ndiyo nchi pekee katika Bara la Afrika, iliyojaribu na kufanikiwa kwa miaka 50 sasa kuunganisha nchi mbili. Nafahamu viongozi wetu wanapenda sifa za kupigiwa nyimbo za taifa. Wanafurahi kupokewa kwa vimulimuli na kuitwa rais, ila sina hakika kama wanakerwa na uduni wa maisha ya wananchi.

Binafsi nasema sisumbuliwi na idadi ya Serikali. Tuweke hata Serikali za majimbo, si Tanganyika tu. Ila nasema mamlaka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano yabaki palepale. Na hapa naomba nieleweke. Sisemi madaraka ya Rais Jakaya Kikwete wa CCM yabaki pale pale, nasema hata kama akishinda Dk. Willibrod Slaa wa Chadema madaraka ya rais yabaki pale pale.

Mapendekezo yaliyomo kwenye rasimu ya Katiba, ikiwa wajumbe wa Bunge la Katiba hawataona hatari yake, na Mzee wa Viwango na Kasi akashinikiza ajenda ya Tanganyika ikapatikana bila kupiga moyo konde, huo ndiyo utakaokuwa mwisho wa Tanzania. Hutakaa uione Tanzania njema. Sifa ya amani na utulivu inawezekana hatuoni umuhimu wake leo.

Ninaye rafiki yangu ambaye huniambia, “Kazi ni nzuri mno siku ya kwanza na siku ya mwisho.” Hii maana yake ni nini? Anasema mtu anapoajiriwa kazini, mshahara anaopewa humpa furaha. Miezi 12 baada ya kuwa kwenye ajira, mshahara huonekana ni mkia wa mbuzi. Ni hatari kubwa kuizoea kazi. Ukifukuzwa kazi ukaenda kijiweni, ndipo utakapobaini kumbe mshahara uliokuwa unalipwa ulikuwa mkubwa.

Sitanii, leo Watanzania hawaoni umuhimu wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Muungano huu unabezwa na kuitwa kila jina. Wazanzibari wanaotaka Muungano wa Mkataba leo, mwaka 1964 walipokuwa wakiliona tishio la Mwarabu kuiangusha tena Serikali ya Rais Sheikh Abeid Amani Karume, walikuwa tayari hata kutokuwa na Serikali kabisa.

Mwalimu Nyerere alisema mara kadhaa kuwa yeye ndiye aliyekataa Serikali ya Zanzibar kuingizwa katika Muungano kwa hofu ya kuimeza Zanzibar. Wao walikuwa tayari. Hofu ilikuwa imetawala kwao. Leo ni sawa na kwamba wamekuwa kazini kwa muda mrefu. Muungano wanauona sawa na mshahara. Wameishaona Muungano hautoshi tena.

Ukiacha yote hayo nihitimishe makala haya kwa kusema kuwa utaratibu wanaotumia wajumbe wetu huko Dodoma unanitia shaka iwapo Katiba mpya itapatikana. Kwa kasi waliyoionesha kwenye kutunga kanuni, ikiendelezwa kasi hiyo hiyo, watakaa Dodoma hadi 2015, mwisho wa siku tutaambulia ngumi, lakini Katiba mpya haitapatikana.

Nachelea kusema kuwa kinachoendelea Dodoma leo hakitakuwa na tofauti na kilichotokea Berlin mwaka 1884/85. Yetu macho.

1717 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!