Kabla ya kufanyika kwa mkutano mkuu wa Wekundu wa Msimbazi Simba Sports Club ya Dar es Salaam siku kadhaa zilizopita, baadhi ya wanachama wa klabu hiyo walitaka kuwapo agenda ya kufanya marekebisho katika baadhi ya vipengele vya katiba ya Wekundu hao wa Mtaa wa Msimbazi.

Huenda kundi lililotaka kuwapo na agenda hiyo lilichukuliwa kama watu wanaotaka kuleta fujo, au wasiotaka mkutano huo ufanyike. Lakini kulikuwa na kila haja ya kuwapa nafasi baadhi ya wanachama hao waseme ni kitu gani wanadhani kinatakiwa kufanyiwa marekebisho kuboresha katiba ya klabu hiyo.

 

Hali hii ndiyo iliyosababisha uongozi wa klabu hiyo kuweka msisitizo kuwa mkutano utafanyika, na kama kutakuwa na mwanachama yeyote atakayeleta vurugu atachukuliwa hatua za kisheria.

 

Ni dhahiri kuwa klabu za Simba na Yanga mikutano yake huwa haikosi tafrani za hapa na pale. Na ndivyo ilivyokuwa katika mkutano wa Simba ambapo ilibidi Mwenyekiti wake, Aden Ismail Rage, ambaye pia ni Mbunge wa Tabora, kuomba msaada wa nguvu ya dola kutuliza ghasia pale baadhi ya wajumbe walipotaka kwenda kinyume na alivyotaka yeye katika mkutano huo.

 

Nakumbuka kauli hii “Askari mtoe nje huyo mama ambaye anataka kuvuruga mkutano halafu nipe jina lake nimfute uanachama, katiba inaniruhusu mimi kama mwenyekiti kumfuta mwanachama yeyote ambaye anakwenda kinyume na katiba, na pia katiba inamtaka mwenyekiti kuhakikisha mkutano unafanyika kwa amani,” ilikuwa kauli ya Rage mara baada ya mama mmoja mwanachama wa klabu hiyo kutaka kuhoji baadhi ya mambo yanayohusu mwenendo wa klabu hiyo.

 

Baada ya majibizano kati ya Rage na mama huyo, niligundua kwamba Katiba ya Simba ina upungufu, tena ambao huenda ukawa ndiyo unawapa viongozi jeuri ya kuwa na kauli nzito dhidi ya wanachama na hata wakati mwingine kuwa na kauli za kejeli.

 

Hali kadhalika, kuwapa viongozi wa klabu hiyo vifua wakati mwingine kutoa ahadi hewa na baadaye kuleta visingizio vya hapa na pale wanaposhindwa kuzitekeleza.

 

Si vyema kumlaumu Rage kuwa anaiongoza Simba kibabe kwa sababu yeye anafuata Katiba ya Klabu hiyo, ambayo kwa asilimia fulani ina vipengele vya kuwakingia kifua viongozi na kuwanyima nafasi wanachama kuhoji mambo ya msingi.

 

Huu ni ubabe ambao kama Klabu ya Simba haitakubali kufanya mabadiliko katika baadhi ya vipengele vya katiba yake ya sasa, hadithi itabaki kuwa ile ile ya migogoro na makundi kila siku.

 

Lakini katika mkutano huo, nilisikia kuwa kuna mpango kazi kwa ajili ya maendeleo ya klabu hiyo ulioandaliwa na wataalamu kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

 

Itakuwa vizuri mpango kazi huu kama utaanza na baadhi ya marekebisho ya katiba, ili mambo mengine yatakayofuata yaweze kwenda vizuri ikiwa ni pamoja na kutoa fursa kwa wanachama kuhoji mambo muhimu pasipo vitisho kwa kusingizia katiba.

 

Uongozi wa Simba unahitaji kuwa msikivu kwa wanachama wake na kuhoji endapo kuna kundi linahitaji mabadiliko ya kikatiba lieleze manufaa yake. Soka la siku hizi linaendeshwa kisomi, kwa hiyo ni vigumu kumwambia Mtanzania wa sasa anayeishi katika ulimwengu wa ukweli na uwazi ndani ya karne hii ya sayansi na teknolojia, kuwa hii ni rangi nyekundu wakati yeye anaona ni nyeupe.

 

Uongozi wa Simba unatakiwa kukubaliana na mabadiliko katika baadhi ya vipengele vya katiba yake. Kwa mfano, unawezaje kuwaita wanachama wote kwenye mkutano mkuu, wakati kuna uwezekano wa kuwa na wawakilishi?

 

Haya mambo ya wengi wape hayawezi kutumika tena katika kuongoza soka la kisasa, ambalo limegeuka kuwa ajira kwa wachezaji wa kisasa.

 

Hii ni mojawapo ya mambo ambayo Simba wanahitaji kuyafanyia marekebisho, la sivyo, Rage ataendelea kuwaburuza na hakuna atakayeweza kumlaumu kwa sababu anafanya mambo kwa mujibu wa katiba.

 

Rage huyo huyo siku hiyo ya mkutano nikasikia anawaambia Wanasimba; “Mimi kwanza ni mheshimiwa nikitoka hapa napigiwa saluti, sina shida hata kidogo.” Maneno kama haya hayapendezi kwa watu ambao wana uchungu na wanahitaji kujua fedha za klabu yao zinatumikaje.

Please follow and like us:
Pin Share