Na Cresensia Kapinga, JakhuriMedia,Madaba
KATIBU Tawala wa Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma Mtela Mwampamba amewaagiza viongozi wa vijiji na kata kusimamia sheria ndogo ndogo zilizowekwa ili waweze kuepusha majanga ya uharibifu wa mazingira ikiwemo uchomaji moto misitu kinyume na taratibu zilizowekwa.
Agizo hilo amelitoa jana kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Mtepa Halmashauri ya Madaba baada ya wakala wa huduma za Misitu Tanzania (TFS)kugawa vifaa vya viwandani vyenye thamani ya sh. Milioni 39.9 kutoka shamba la miti la Wino kwaajiri ya umaliziaji wa majengo ya serikali shule,Zahanati pamoja na Taasisi za kidini.
Katibu Tawala huyo amesema kuwa kumekuwepo na tabia ya uharibifu mkubwa wa mazingira ikiwemo ukataji wa miti na uchomaji moto ovyo wa misitu huku viongozi wa vijiji na kata wakiangalia bila kuwachukulia hatua wahusika vitendo hivyo havipaswi kufumbia macho kila mtu awajibike katika eneo lake.
“Ndugu zangu kumekuwa na changamoto mbalimbali ambazo kwa namna moja ama nyingine zinakuwa zitatupata sisi ambao tunamiliki hifadhi yetu na shamba letu pale Wino, moto umekuwa ukitokea lakini tumekuwa tukipambana nao kuhakikisha tunauzima lakini uharibifu mkubwa sana unaofanyika na ninyi ndugu zangu watu wa Madaba, Mtepa mnajuwa kuhusiana na Elimu ya utunzaji wa miti ninyi mnafahamu na Elimu hii mmeanza kupata toka mkiwa wadogo kwamba uchomaji moto holela hautakiwi.” Alisema Mwampamba.
Aidha amewaagiza TFS kuendelea kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa utunzaji wa mazingira kwani imeonekana wananchi wengi hawajui umuhimu wake hivyo kufanya vitendo vya ukataji wa miti na uchomaji moto holela kuwa ni vya kawaida na ni sehemu ya maisha yao ya kila siku pasipo kujua athari zake.
Kwa upande wake Muhifadhi Mkuu wa shamba la miti Wino Grory Kasmir amesema kuwa wanalazimika kuunga mkono juhudi za wananchi ili waweze kuhifadhi misitu vizuri na kwamba wananchi wanatakiwa kuhifadhi mazingira yao ikiwemo wanapoandaa mashamba wanatakiwa kuweka barabara ili moto unapotokea inakuwa rahisi kuuzima.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi wameshukuru Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ( TFS), kwa kuwapatia vifaa vya viwandani vyenye thamani ya sh. Milioni 39.9 na wameomba Taasisi zingine za serikali na binafsi kuendelea kuwasaidia ili nguvu za wananchi zisipotee bure.