Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Serikali imezitaka jamii zenye watoto walio chini ya umri wa miaka 18 na makundi mengine maalum yanayokabiliwa na changamoto za usimamizi wa mirathi kutoa taarifa kwa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) ili kupata mwongozo wa kisheria na kulindwa kwa haki zao za msingi.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Bi. Zainabu Katimba, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria wakati wa hafla ya kumpongeza Bi. Anna Zambi, ambaye alipatiwa msaada wa kisheria na RITA kupitia huduma ya Udhamini wa Umma.
Bi. Katimba amesema kuwa bado kuna wananchi wengi wenye uhitaji wa huduma za msaada wa kisheria kuhusu mirathi, lakini wanashindwa kufikiwa au hawajui mahali sahihi pa kupata msaada huo, hali inayosababisha kupoteza haki zao za msingi.

“Jamii, hususan watoto walio chini ya umri wa miaka 18, wamekuwa wakikumbwa na changamoto nyingi zinazowasababishia kupoteza haki zao za kisheria katika kumiliki na kurithi mali za wazazi wao wanapofariki,” amesema.
Ameeleza kuwa changamoto hizo mara nyingi husababishwa na watu wenye tamaa ndani ya familia wanaotumia nguvu au ujanja kupora mali za warithi, hususan watoto, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Akitoa mfano, Bi. Katimba amesema tukio la Bi. Anna Zambi, aliyepewa msaada na RITA wa kusimamiwa mirathi yake upitia amri ya mahakama ni mfano wa vijana wengi wanaopitia changamoto kama hizo katika jamii.
“Msaada wa kisheria alioupata Bi. Anna ni ushahidi wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha wanufaika wa huduma ya udhamini wa umma wanalindwa na kupata haki zao stahiki kupitia RITA,” amesema.

Ameongeza kuwa makundi mbalimbali yakiwemo watoto, watu wenye ulemavu, watu wenye matatizo ya afya ya akili na makundi mengine maalum, yamekuwa yakipoteza haki zao kwa kukosa uelewa wa mahali sahihi pa kupata msaada wa kisheria wa kusimamia mirathi zao.
Kutokana na hali hiyo, Naibu Waziri ametoa wito kwa wananchi kupewa elimu zaidi kuhusu huduma za udhamini wa umma ili kuzuia migogoro ya mirathi katika jamii.
“Ni wakati sasa jamii iamke na kupambana na uporaji wa mali za warithi kwa kutumia fursa ya huduma za RITA, kama ilivyokuwa kwa Bi. Anna,” amesema.
Katika hatua nyingine, Bi. Katimba amewaagiza wadhamini wa umma kutekeleza mpango madhubuti wa kutoa elimu kwa umma kwa kushirikiana na wadau, ili kuimarisha utoaji wa huduma za udhamini wa umma nchini.
“Mdhamini wa Umma ahakikishe anaendelea kuimarisha mahusiano na ushirikiano na wadau mbalimbali ili wananchi wapate haki kwa wakati,” ameagiza.

Amesema pia utaratibu maalum unapaswa kuwekwa ili kuwezesha wananchi na wadau kutoa taarifa kuhusu mali zinazopaswa kusimamiwa chini ya Sheria ya Mdhamini wa Umma (Mamlaka na Majukumu) Sura ya 31.
Kwa upande wake, Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Bw. Frank Kanyusi, amesema kuwa taasisi hiyo inatekeleza jukumu la udhamini wa umma kwa mujibu wa Sheria ya Mdhamini wa Umma (Mamlaka na Majukumu) Sura ya 31, ambapo Kabidhi Wasii Mkuu ndiye Mdhamini wa Umma.
Amesema sheria hiyo inamtambua Mdhamini wa Umma kama mtu mwenye utu wa kisheria unaomruhusu kushitaki au kushitakiwa kwa niaba ya wanufaika, pamoja na kusimamia mirathi kwa maslahi yao.
Bw. Kanyusi amesema RITA imekuwa ikikumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo uelewa mdogo wa jamii kuhusu huduma za udhamini wa umma, wananchi kushindwa kutoa taarifa za mali zinazopaswa kusimamiwa chini ya udhamini wa umma, pamoja na baadhi ya taasisi kuendelea kusimamia mali ambazo kisheria zinapaswa kusimamiwa na Mdhamini wa Umma.

Amesema ili kukabiliana na changamoto hizo, RITA inaendelea kutoa elimu kwa umma na kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali ili kuboresha utoaji wa huduma za udhamini wa umma.
Kwa upande wake, Bi. Anna Zambi, ambaye ni mnufaika wa huduma ya udhamini wa umma na mhitimu wa Shahada ya Sheria, amemshukuru RITA kwa msaada wa kisheria alioupata baada ya kupitia changamoto mbalimbali za mirathi.
Amesema elimu ya kisheria aliyoipata itamwezesha kuwa balozi mzuri kwa watu wengine wanaokabiliwa na changamoto kama hizo kwa kuwapa mwongozo wa upatikanaji wa huduma za udhamini wa umma ili kulinda haki zao za msingi.




