Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha
Baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Pwani wameishukuru Serikali kufanikisha uchaguzi uliomalizika huku wakisema sasa wanaendelea na shughuli zao za kila siku kwa utulivu na usalama.
Wakizungumza Novemba 6,2025 kuhusu muelekeo wa maisha baada ya uchaguzi, wananchi hao wamesema amani ni tunu ya taifa, hivyo kila Mtanzania ana wajibu wa kuilinda na kuitunza.
Mzee Ramadhan Mnyandu na Rehema Bakari wa Kibaha pamoja na Zawadi Abdul wa Kiluvya, Kisarawe, walisema tamko la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linalohimiza wananchi kudumisha amani na kurejea katika shughuli zao mara baada ya uchaguzi limeleta faraja kubwa.
“Bila amani uchumi unayumba, elimu kwa watoto inashuka, hali ya kimaisha inapanda kwa kuwa na mlipuko wa gharama za bidhaa, kwahiyo tumefurahi kusikia Rais akituasa tuendelee na kazi zetu, ni busara kubwa, maana uchaguzi umekwisha, maisha lazima yaendelee,” alibainisha Mzee Mnyandu.

Kwa upande wake, Mama Rehema Mwinuka, mfanyabiashara katika soko la Kwa Mathias, alisema sasa ni muda wa kujenga nchi, maneno ya Rais yamewapa utulivu wa moyo, kazi iendelee.
Mama Rehema alivishukuru vyombo vya ulinzi na usalama kwa kushirikiana kuhakikisha hali ya utulivu inatawala kabla, wakati na baada ya uchaguzi, na kueleza kuwa kwa sasa hali ni shwari.
“Tunamuomba Mbunge aliyyechaguliwa jimbo letu la Kibaha Mjini akasimamie changamoto zote alizopewa na Wananchi na kutimiza ahadi alizozitoa kupitia Chama Cha Mapinduzi”
Alifafanua anaimani na Sera na utekelezaji wa ilani , kikubwa usimamizi ili kutatua changamoto ikiwemo maji, miundombinu ya barabara kwenye mitaa na kuangalia changamoto zinazokabili sekta ya afya.

Naye Zawadi Abdul alisema amani ndiyo msingi wa maendeleo, hivyo kila mwananchi anapaswa kuithamini na kuiepuka tabia ya kufuata mkumbo na vishawishi vinavyoweza kuhatarisha utulivu.
“Kauli ya Rais imekuwa ishara ya umoja, ikiwakumbusha Watanzania kwamba baada ya uchaguzi kinachofuata ni kazi, mshikamano, na kujenga taifa kwa pamoja, ni wakati wa kuweka kando itikadi zetu kwa maslahi ya nchi,” alisema Zawadi.
Hivi karibuni Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani Mkoa wa Pwani, Sheikh Khamis Mtupa, alihimiza Watanzania kuendelea kudumisha amani, akisisitiza kuwa jukumu la kulinda utulivu wa nchi ni la kila raia, kwa kuwa “hakuna Tanzania nyingine ya kwenda kuishi.”

