Kenya kuandaa riadha ya vijana wasiozidi miaka 20 mwaka 2020

Bodi ya shirikisho la riadha duniani , IAAF imeuchagua mji mkuu wa Kenya, Nairobi kuwa mwenyeji wa mashindano ya riadha ya ulimwengu ya vijana wenye chini ya umri wa miaka 20 yatakayoandaliwa mwaka 2020.

Uamuzi huo wa kuchagua mji huo kama uwanja wa kuandaliwa kwa shindano hilo la kimataifa ni baada ya bodi hiyo kuyataja mashindano ya riadha ya vijana wenye chini ya umri wa miaka 18 yalioandaliwa nchini humo mwaka 2017 kuwa ya ‘kipekee’

Pia bodi hiyo imeitambua Kenya kama taifa lenye wanariadha halisi.

”Mashindano ya vijana wenye chini ya umri wa miaka 20 yanadhihirisha siku zijazo za michezo , kwa kuwa Kenya ina idadi kubwa ya vijana na historia ya riadha , ni mahali bora kwetu sisi,” Rais wa shirikisho la riadha Sebastian Coe amesema.

Shindano hilo la wanariadha walio chini ya umri wa miaka 18 liliwavutia zaidi ya watu elfu 60 kulingana na IAAF.

Kenya ina matumaini kwamba siku moja itakuwa mwenyeji wa mashindano yote ya kimataifa ya riadha ambayo hayajawahi kufanyika barani Afrika.

Kufaulu kwa Kenya kwa kuyavutia mashindano ya riadha kunakuja baada ya kushindwa kuandaa michuano ya mataifa 16 barani Afrika – CHAN mwaka jana.

Baada ya kuchelewa kwa muda na matatizo na viwanja, bodi ya shirikisho la soka Afrika (Caf) iliinyima Kenya haki ya kuandaa mashindano ya CHAN na kuyapeleka nchini Morocco.