Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
BURUDANI na michezo mbalimbali vilitawala Tamasha la Kids Holiday Festival lililowakusanya mamia ya watoto wakati wa likizo, huku likiwa jukwaa muhimu la kuwajengea watoto uelewa wa masuala ya fedha, uchumi na ujasiriamali tangu wakiwa katika umri mdogo.
Tamasha hilo, ambalo Benki ya CRDB ni mdhamini mkuu, lililenga kuwaandaa watoto kama taifa la kesho kwa kuwapa maarifa yatakayowasaidia kujenga maisha bora binafsi na kwa jamii kwa ujumla.

Akizungumza katika tamasha hilo lililofanyika mwishoni mwa wiki, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Insurance Company, Wilson Mnzava, alisema benki hiyo imedhamiria kuanza na watoto katika kuwaandaa kifedha mapema.
“Tunafahamu watoto ndio taifa la kesho. Tukianza nao mapema kuwafundisha masuala ya fedha na uchumi, tunawaandaa kuwa mabalozi wazuri wa maendeleo katika familia, jamii na taifa,” alisema Mnzava.
Alisema CRDB haikuishia kudhamini tamasha hilo pekee, bali pia iliandaa mashindano ya uelewa yaliyowahusisha watoto, ambapo washindi walipatikana baada ya kuonesha umahiri mkubwa katika kujibu maswali mbalimbali.
“Tumewadhamini watoto walioshinda kwa kuwalipia ada za shule. Hili ni jambo la kutia moyo na tunaahidi mwakani kuongeza idadi ya watoto watakaonufaika,” aliongeza.

Mnzava alisema lengo la kukusanya watoto katika kipindi cha likizo lilikuwa ni kuwapatia elimu ya fedha kwa vitendo, huku akibainisha kuwa baadhi ya watoto waliohudhuria tamasha hilo tayari wameanza kujihusisha na biashara ndogondogo.
“Kauli mbiu yetu ni ulipo tupo, leo tupo na watoto, na tupo tayari kuwahudumia,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kids Holiday Festival, Geraldine Mashele, alisema tamasha hilo ni la pili tangu kuanzishwa kwake na linaendelea kukua kwa kuvutia watoto wengi zaidi.
Alisema tamasha hilo linahusisha burudani, michezo na matukio mbalimbali ya kielimu, huku akishukuru Benki ya CRDB kwa udhamini wake na kubainisha kuwa tamasha hilo ni endelevu na linafanyika katika mikoa mbalimbali nchini, likiwa linatoa fursa kwa watoto kupata uelewa mpana wa masuala muhimu ya maisha.





