Na Kulwa Karedia,Jamhuri lMedia, Kigoma

Mratibu wa Kanda Chama cha ACT Wazalendo, Said Rashid, ametangaza rasmi kuondoka na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Amesema amefikia uamuzi huo baada ya kuvutiwa na utendaji wa serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Ametangaza uamuzi huo wakati wa mkutano wa kampeni za kumnadi mgombea wa CCM, Samia Suluhu Hassan uliofanyik Uwanja Katosho mkoani Kigoma leo Septemba 14,2025.

Amesema ameamua kwa hiari kuachana na ACT Wazalendo na kujiunga na CCM mchana kweupe kwa sababu ameona ni jambo sahihi.

“Kwa ridhaa yangu, nimeamua kuachana na ACT Wazalendo na kujiunga na CCM, nimevutiwa na kazi kubwa inayofanywa na Dk. Samia.

“Mimi ni mchumi, ninaangalia muda, rasilimali na matokeo,ndiyo maana nimechukuwa uamuzi huu,” amesema .

Amesema aliwahi kuwa mgombea ubunge kupitia ACT Wazalendo katika majimbo ya Kigoma Mjini na Uvinza,anasisitiza sababu ya kuhama ni kuondokana na siasa zisizo na uthabiti.

“Naachana na chama ambacho mtu mmoja akiamka na hasira, wote mna hasira. Akifurahi, wote mnafurahi. Nimechoka. Nimeamua kujiunga na chama chenye mfumo wa kitaasisi,” amesema.

Amesema CCM ni chama imara chenye dira, kinachoongozwa na maono ya kitaifa, na kinachotekeleza miradi inayogusa maisha ya watu moja kwa moja.

“Hata kama Afrika Mashariki itakuwa nchi moja, bado Samia atakuwa mgombea bora,”amesema.

Amesema ameridhishwa na miradi ya kimkakati mkoani Kigoma, ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya barabara, upatikanaji wa maji, huduma za afya na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), vitu ambavyo vinampa amani ya moyo.

Asema mkoa huo ulikuwa miongoni mwa mikoa iliyosahaulika kwa muda mrefu, lakini chini Samia, umeanza kupata maendeleo ya haraka na makubwa.