Jakaya_Kikwete_-_Partnerships_for_Development_-_World_Economic_Forum_on_Africa_2011_-_2Tulikuwa na Rais ambaye hakuona mbali kuna wakati tuliambiwa kuwa tusiwazungumzie marais wastaafu hata kama hawakufanya vizuri wakati wa utawala wao. Tuwaache wapumzike.

Kwa Tanzania si kweli kwamba kuna Rais mstaafu ambaye anapumzika baada ya kumaliza muda wake. Wote wanajihusisha na siasa na wote wanapambana na upinzani. Kwa kifupi hakuna Rais mstaafu anayeamua kupumzika kama wanavyofanya marais wastaafu wa nchi zingine. Hawa wetu wanaendelea kutawala kwa mbali.

Sheria za Tanzania zinazuia pia kushtakiwa Rais kwa jambo lolote alilolitenda akiwa madarakani. Lakini sheria inawakataza wananchi kuzungumzia utendaji mbovu wa Rais aliyeondoka madarakani na ulivyoathiri utendaji wa Rais aliyeingia madarakani.

Tukitaka kusema kweli (na hapa lazima tuseme kweli) Rais aliyeondoka madarakani alifanya mambo kana kwamba angeendelea kuwa madarakani milele. Hakuona mbali. Haijulikani kilichomharibu Rais huyo mstaafu hata akashindwa kuona mbali.

Labda yalikuwa matokeo ya baadhi ya viongozi wa dini waliomwaminisha kuwa yeye alikuwa chaguo la Mungu. Lakini pia inawezekana yalikuwa matokeo ya mataifa makubwa ambayo huko nyuma yalimsifu kuwa alikuwa anaongoza barani Afrika kwa utawala bora wakati hakuwa na utawala bora nchini.

Kwa kweli tabia ya Rais huyo mstaafu ya kukosa kuona mbali imesababisha yeye kujikuta anaumbuka na kusemwa vibaya hivi sasa kila kona ya nchi kwa kushindwa kutimiza wajibu wake kwa taifa lake na watu wake. Kwa jumla kilichomponza Rais aliyeondoka madarakani ni kupuuza kila kitu hata mambo muhimu ambayo leo anaweza kujutia kwa nini aliyapuuza.

Rais aliyeondoka madarakani aliyapuuza sana magazeti. Akayaamini magazeti machache yaliyoendelea kumbeba.

Wakati wa utawala wa Rais aliyeondoka madarakani magazeti yalifanya kazi kubwa na nzuri kufichua uozo wa aina mbalimbali mojawapo likiwa gazeti la Jamhuri. Magazeti yaliandika vya kutosha kuhusu uozo bandarini, uozo kwenye Hifadhi za Taifa na uozo kwenye maeneo mengine mengi.

Kuna baadhi ya magazeti hapa nchini yana safu maalumu zinazotoa nafasi kwa wananchi kuandika kero zao. Wananchi waliendelea kuandika kero za michango mingi mno mashuleni, kero za wagonjwa kulala sakafuni mahospitalini, na kero zingine. Lakini serikali ya Rais aliyeondoka madarakani iliendelea kupuuza magazeti.

Leo Rais aliyeingia madarakani anashughulikia kero hizo hizo ambazo Rais aliyemtangulia alizipuuza. Kwa hiyo Rais anayeshughulikia kero za wananchi ambazo ni za wazi kabisa anapewa heshima kubwa huku Rais aliyeondoka madarakani akipuuzwa.

Katika jambo hili haihitaji kumhimiza Rais Magufuli kuona umuhimu wa kujali yanayoandikwa magazetini. Si sahihi kuamini kwamba magazeti yote yanafanya kazi ya uchochezi. Magazeti mengi ni msaada mkubwa kwa serikali katika kurekebisha mambo nchini.

Si vibaya serikali ikimwajiri mtu wa kuorodhesha kila siku kero muhimu zinazoandikwa magazetini kutoka maeneo mbalimbali ya nchi na kuzifanyia kazi au kuwataka viongozi wa serikali wa maeneo husika wazifanyie kazi.

Halafu Rais aliyeondoka madarakani aliendelea kuwapuuza wapinzani kiasi cha kuleta picha kwa wananchi kwamba wapinzani si watu muhimu katika taifa hili. Kwa mfano, wapinzani walikuwa wa kwanza kuhukumu safari zisizo na idadi za Rais nchi za nje na zilivyoendelea kupoteza fedha za umma. Lakini Rais akisaidiwa na wasaidizi wake wa Ikulu waliendelea kuzitetea safari hizo wakidai kuwa zilikuwa na manufaa makubwa kwa taifa hili. Leo Rais huyo aliyeondoka madarakani ameumbuka baada ya Rais aliyeingia madarakani kuliambia taifa kwamba fedha za safari hizo zingeweza kufanya makubwa hapa nchini. Kwa kweli Rais aliona fahari kubwa kusafiri na watu zaidi ya hamsini huku wengi wao wakiwa hawana la kufanya huko nchi za nje.

Matumizi mabaya ya fedha za umma hayakuishia hapo. Sherehe mbalimbali zilikomba fedha ambazo hakuna aliyefuatilia matumizi yake huku hospitali zikiwa hazina dawa wala vitanda vya wagonjwa vya kutosha. Juu ya yote Rais aliyeingia madarakani ameachiwa deni la shilingi laki saba kwa kila mtanzania wakati Rais aliyeondoka madarakani aliachiwa fedha za kutosha na Rais Mkapa.

Japokuwa Rais aliyeondoka madarakani aliwapuuza wapinzani wananchi waliendelea kuwaamini wapinzani. Akaamuru Polisi watumie nguvu kubwa kupambana na wapinzani. Lakini haikusaidia kitu. Tumesikia kwamba wapinzani wana takwimu zinazothibitisha kwamba walishinda uchaguzi huo.

Ni kweli Rais mstaafu amejigamba kwamba wale waliosema kwamba CCM ingemfia mkononi hawakusema kweli. Ukweli ni kwamba CCM ilimfia mkononi kama si matumizi mabaya ya madaraka yaliyoepusha maafa. Wananchi hawakumkataa Dk. Magufuli. Waliikataa CCM na mwenyekiti wake.

Rais aliyeondoka madarakani hakuishia kwenye kupuuza magazeti na wapinzani. Pia aliwapuuza watu waliokuwa na nia njema ya kumsaidia yeye na kulisaidia taifa hili. Kwa mfano, Rais mstaafu aliwahi kupewa orodha ndefu ya majina ya wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya. Akapuuza. Hakuifanyia kazi. Leo Tanzania imekuwa soko kuu la dawa za kulevya barani Afrika kiasi Rais aliyeingia madarakani ana kazi ngumu ya kupambana na dawa hizo.

Halafu kuna huyo David Kafulila aliyeibua kashfa ya fedha za Tegeta Escrow. Badala ya kufanya naye kazi serikali ilipambana naye na inaendelea kumkumbatia fisadi mkubwa anayeendelea kuifilisi Tanzania. Mwishoni Rais, na wala si mahakama, akaamua fedha hizo za Escrow zichotwe Benki Kuu. Mabilioni ya fedha wakachotewa watu wa Ikulu kutoka Benki ya Stanbic. Watakiwa kuzirejesha. Ukweli ni kwamba ufisadi Tanzania umeongozwa na Ikulu wengine wakafuata. Tena serikali imeendelea kutumia vibaya Benki ya Stanbic.

Mwisho, Rais aliyeondoka madarakani alipuuza hata chama chake tawala cha CCM. Kwa mfano, chama kilipowasemea wananchi kuwa kuna mawaziri mizigo Rais alikanusha akisaidiwa na Katibu Mkuu Kiongozi. Kwa kifupi, chama kilishindwa kumdhibiti mwenyekiti wake. Na hapa kuna haja kwa CCM kutenganisha kofia ya Urais na ya Uwenyekiti.

Basi Rais aliyeondoka madarakani alishindwa kuona mbali. Akafanya mambo ambayo leo yanamwondolea heshima.

2719 Total Views 2 Views Today
||||| 3 I Like It! |||||
Sambaza!