Kikwete anastahili pongezi

Wiki iliyopita ilikuwa na matukio makuu mawili. Tukio la kwanza ni Alhamisi, ambapo Rais Jakaya Kikwete alihutubia Bunge. Alisema bayana kuwa alikwenda bungeni kuzungumza suala moja tu la msingi, ingawa alichomekea mengine. Suala hili ni mustakabali wa Tanzania ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Rais Kikwete alitumia hotuba hiyo kuthibitisha kuwa kweli ameridhia kwa dhati dhana ya Serikali ya Uwazi. Baada ya kubaini kuwa yapo maneno ya chinichini juu ya nchi za Kenya, Uganda na Rwanda kuzitenga Tanzania na Burundi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, ameamua kuwa wazi. Maneno haya yalikuwa wazi kuwa nchi hizi zimeanzisha miradi mkubwa na kuwatenga washirika hawa wawili.

Miaka ya nyuma tukio kama hili lingetokea ingechukuliwa kuwa ni siri ya taifa. Usiri ugelifikisha taifa kuangukia katika makundi. Baadhi ya watu wangefika mahala wakadhani waliomo ndani kuna jambo wanaficha wasilotaka lifahamike nje. Rais Kikwete kwa kueleza ukiukwaji uliofanywa na wakubwa hawa, ameondoa kiwingu ambacho kingeifanya Serikali yake kugeuziwa kibao.

Leo Watanzania sote tunafahamu kuwa chuki inayooneshwa dhidi ya Taifa letu, imetokana na uamuzi wa kizalendo na thabiti wa Serikali yetu kutetea maslahi ya Tanzania katika eneo la ardhi, kukataa matumizi ya vitambulisho vya Taifa kugeuzwa hati ya kusafiria na kuruhusu uharakishaji wa shirikisho la Afrika Mashariki.

Sisi tunasema ni lazima tufuate utaratibu uliokubaliwa kwa mujibu wa Mkataba wa Afrika Mashariki wa mwaka 1999 pamoja na itifaki zake. Tunataka tukamilishe vizuri hatua ya kwanza ya ushuru wa forodha, soko la pamoja, sarafu moja katika Afrika Mashariki — sote tutumie shilingi na hatimaye Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki baada ya kuridhiwa na wananchi.

La pili, tunapenda kumpongeza Rais Kikwete kwa uamuzi wa busara alioutumia katika kurejesha bungeni Muswada wa Marekebisho ya Katiba, unaoondoa mkanganyiko uliokuwa umejitokeza juu ya aina ya utetezi wa wajumbe wa Bunge la Kutunga Sheria, idadi ya wabunge na utaratibu wa kupiga kura kwa theluthi mbili Tanzania Bara na Zanzibar.

Awali, Chadema walipinga sheria iliyorekebishwa kwa kuwa ilipitishwa kwa mbwembwe na wabunge wa CCM wakiongozwa na Naibu Spika, Job Ndugai, aliyekuwa akitamba kuwa ‘zege halilali’. Busara za Rais Kikwete zimeepusha maafa ambayo yalikuwa yanalinyemelea Taifa hili. Nchi nyingi ziliingia kwenye machafuko kutokana na vyama tawala kupuuza wapinzani.

Tunasema kuna mabadiliko makubwa katika dunia ya sasa. Siasa za wakati huu zinaendeshwa kwa maridhiano badala ya ubabe, fujo, kiburi na kuburuzana. Nguvu ya dola inapaswa kutumika kukuza uchumi, badala ya kutumika kupambana na wananchi. Sheria nyingi zinazotungwa sasa zinajielekeza katika kutoa mwongozo, badala ya kujikita kwenye makatazo.

Tunahitimisha maoni haya kwa kusema hongera sana Rais Kikwete kuwezesha marekebisho ya sheria hiyo na umeonesha mfano. Chama tawala kikiiga mfano huu sasa na siku za usoni, nchi yetu itaendelea kuwa kisiwa cha amani. Hongera Rais Kikwete, Mungu ibariki Tanzania.