Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC), Mahmoud Ali Youssouf, amemteua Rais Mstaafu wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, kuwa Mwakilishi wa Ngazi ya Juu wa Mwenyekiti wa AUC katika eneo la Pembe ya Afrika na Bahari ya Shamu.

Uteuzi huo uliotangazwa rasmi leo, Machi 25, 2026, unalenga kuimarisha juhudi za Umoja wa Afrika katika kushughulikia changamoto za kisiasa, amani, na masuala ya kiusalama yanayoikabili kanda hiyo.

Kufuatia uteuzi huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amempongeza Dkt. Kikwete na kueleza kuwa ni heshima kubwa kwake na kwa Tanzania. Aidha, amemtakia majukumu mema katika kuimarisha Umoja wa Afrika na kupata suluhu ya amani ya kudumu kwa manufaa ya Afrika na ulimwengu wote.

Katika nafasi hiyo, Dkt. Kikwete atakuwa na jukumu la kuunga mkono jitihada za AU kupitia: kuendeleza diplomasia ya kuzuia migogoro na kuratibu mazungumzo jumuishi ya kisiasa. Aidha, kujenga uaminifu miongoni mwa wadau mbalimbali wa kikanda na kuimarisha ushirikiano wa kikanda unaolenga kukuza amani na utulivu wa kudumu.

Mhe. Dkt. Kikwete, kama Mwakilishi wa Ngazi ya Juu, atafanya kazi kwa uratibu wa karibu na AU na washirika muhimu wa kikanda na kimataifa, ikiwa ni pamoja na Mamlaka ya Kiserikali ya Maendeleo (IGAD), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Umoja wa Nchi za Kiarabu, na Umoja wa Mataifa (UN) ili kujenga amani na utulivu wa kudumu.

Ushirikiano huo ni muhimu kutokana na nafasi ya kimkakati ya Pembe ya Afrika na Bahari ya Shamu kwa biashara ya kimataifa na utulivu wa Bara la Afrika kwa ujumla.

Mhe. Youssouf ameeleza kuwa na imani kubwa na uzoefu, uongozi, na hekima za Dkt. Kikwete, na kwamba atatoa mchango mkubwa katika kuzisaidia nchi za kanda hiyo kukabiliana na changamoto zilizopo, kukuza ustawi pamoja na amani ya kudumu.

Uteuzi huu unakuja wakati ambapo eneo la Pembe ya Afrika na Bahari ya Shamu linaendelea kuhitaji ushirikiano wa karibu wa kidiplomasia ili kuhakikisha usalama wa kanda na ulinzi wa njia kuu za biashara duniani.