Wakazi wa Mtaa wa Kimara Stopover, Dar es Salaam wamelalamikia kero ya kinyesi na damu ambavyo vimekuwa vikisambaa katika makazi yao kutoka machinjio ya Suka.

Wakazi hao wameieleza JAMHURI kwamba kutokana na kukithiri kwa uchafu huo, afya zao zimekuwa hatarini kwani makazi yao yamekumbwa na harufu mbaya usiku na mchana kwa miaka zaidi ya 20 ya uwepo wa machinjio hayo.

Wanasema baadhi ya wananchi nao wanatumia nafasi hiyo ya uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na machinjio hayo kwa kuongeza uchafu mwingine kutoka katika vyoo vyao na kuunganishwa katika mtaro unaopokea uchafu unaolalamikiwa.

Wanasema kutokana na hali hiyo wakati wote wanaishi kwa hofu kwamba magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu yataendelea kuwa mgeni wao wa kudumu.

ameelezwa mwandishi wa JAMHURI aliyetembelea maeneo hayo yaliyokumbwa na uchafuzi wa mazingira.

Pamoja na madai hayo ya wananchi yaliyodumu kwa kipindi kirefu bila kupatiwa ufumbuzi licha ya kutoa taarifa kwa mamlaka husika, makazi yao yamezagaa vinyesi vya mifugo na damu kutoka machinjio hayo ya Kimara Suka na mvua zinaponyesha uchafu huo unaingia kwenye makazi yao hasa wale wanaoishi eneo la bondeni.

Wanasema kuhusu suala hilo, wananchi wa mashina namba 5 na 27, mwaka 2012 walifanya vikao ili kuondokana na kero hiyo na kuomba Manispaa ya Kinondoni kufunga machinjio hayo hadi mmiliki wake atakapochimba shimo la kuhifadhia uchafu huo badala ya kuuelekeza katika makazi ya watu.

Wanasema baada ya madai yao kutopatiwa ufumbuzi, waliamua kufungua shauri katika Baraza la Kata ya Saranga lililopewa Na. 110 la mwaka 2013 lililohusu kero wanayoipata ya harufu mbaya ya kinyesi na damu.

Katika shauri hilo, mdai Chinollo Victor Ndunguru akiwawakilisha wananchi 72 wa mashina namba 5 na 27 wa mtaa wa Stopover dhidi ya Yahaya Saidi Singano, mmiliki wa machinjio hayo ya Suka.

Baraza hilo liliridhika na malalamiko ya wananchi wa mtaa wa Stopover kutokana na kero ya harufu mbaya inayowapata na kwamba machinjio hayo yako katika makazi ya watu na pia karibu mno na Barabara Kuu ya Morogoro.

“Pia Baraza lilibaini kwamba harufu haiepukiki wakati wa shughuli za uchinjaji wa ng’ombe na machinjio yako kwenye mkondo wa maji (bonde), kiasi kwamba hata kama watajitahidi kufanya usafi au kujenga makaro bado maji ya mvua yatazoa taka za machinjio na kuathiri afya za wakazi wanaopakana na bonde hilo,” inaeleza sehemu ya hukumu hiyo iliyotolewa Januari 25, 2014.

Hata hivyo, Baraza hilo liliamuru machinjio hayo yafungwe ili wananchi waondokane na kero hiyo ya harufu mbaya inayotokana na kuzagaa kwa kinyesi na damu katika makazi yao.

Naye, Mjumbe wa Mazingira wa Mtaa wa Stopover, Godfrey Misana, ameieleza JAMHURI kwamba kero hiyo ni ya muda mrefu na hata Baraza lilipotoa amri ya kufungwa kwa machinjio hayo waliona tena yakifunguliwa bila kufahamu nini kilichojitokeza na imefunguliwa tena kwa maelekezo ya nani.

Misana anasema machinjio hayo yameendelea na uchafuzi wa mazingira katika makazi ya watu huku Manispaa ikiendelea kukusanya mapato kwa kila ng’ombe anayechinjwa kutozwa ushuru wa Sh 5,000, lakini mmiliki hataki kuboresha miundombinu na kuwaondolea kero wananchi.

Anasema wakati mwingine idadi ya mifugo inayochinjwa inafikia zaidi ya 200 kwa siku moja, lakini wahusika hawaangalii kero inayowakabili wananchi kwa kuchimba shimo la kuhifadhia uchafu huo, na badala yake wamekuwa wakiangalia mapato tu.

Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Stopover, Agatha Mallaba, ameieleza JAMHURI kwamba kero hiyo imekuwa ni ya muda mrefu, lakini kilichowashangaza ni kufunguliwa tena bila taarifa kwa Baraza la Kata ya Saranga lililotoa amri ya kufungwa baada ya kujiridhisha na uchafuzi wa mazingira na kuhatarisha afya za wananchi hao.

Ofisa Mifugo wa Manispaa ya Kinondoni, Mbonea Mgonja, ambaye pia ni msimamizi wa machinjio yote ya manispaa hiyo, alipohojiwa na JAMHURI anasema kwamba machinjio yote yanamilikiwa na manispaa.

Anasema machinjio mengi yanayoonekana kuzungukwa na makazi ya watu yamefuatwa na wananchi wenyewe kama ilivyo kwa hayo ya Suka kwa kuwa yapo eneo hilo kwa zaidi ya miaka 30.

Mgonja, ambaye alieleza kwamba kwa sasa yuko likizo, anasema suala la machinjio hayo hawezi kulielezea kwa kina na kutaka atafutwe Dk. Patricia Henjewele. Hata hivyo, naye hakuweza kupatikana.

By Jamhuri