*Akamilisha majengo ya mamilioni yaliyotelekezwa

*Askari Uhifadhi waonja neema, posho zapanda

*Mamilioni ya Ngorongoro sasa mbioni kulipwa

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Loliondo

Uongozi mpya wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) umeanza kufanya mageuzi makubwa ya utendaji kazi.

Miongoni mwa mabadiliko hayo ni pamoja na nyongeza ya posho na stahiki kwa watumishi, walengwa wakuu wakiwa wale wa kada ya chini na ya kati.

Pamoja na marupurupu yaliyorejesha moyo na ari ya uchapa kazi kwa wahifadhi hao, NCAA imeanza kukamilisha baadhi ya miradi iliyokuwa imekwama na hata mingine kutelekezwa kwa muda mrefu.

Hatua zote hizo zimetokana na uongozi wa Kamishna wa Uhifadhi (CC), Abdul-Razak Badru, ambaye Mei mwaka huu Rais Samia Suluhu Hassan alimteua kushika wadhifa huo baada ya kutenguliwa kwa Dk. Elirehema Doriye.

Katika Pori la Akiba la Pololeti ambalo NCAA imepewa ilisimamie, Badru amerejesha ujenzi wa ofisi na nyumba za askari wa uhifadhi uliokuwa umekwama.

Mwishoni mwa mwaka jana, JAMHURI lilifika eneo hilo la Meremi Iloingok lililoko kilometa chache mpakani mwa Tanzania na Kenya; na kushuhudia majengo yaliyojengwa kwa mawe yakiwa yametelekezwa; huku askari wakilala kwenye mabanda na mahema machakavu.

Baada ya kuandikwa kwa taarifa hiyo iliyoambatana na picha, Dk. Doriye, aliamuru kitengo chake cha habari kikanushe.

Hivi karibuni, maofisa kadhaa wa NCAA wakiwa na  JAMHURI walifika eneo hilo na kukuta ujenzi ukiwa umerejea; hali iliyoonekana kubadili kabisa mandhari na hadhi ya eneo hilo.

Mkuu wa Pori la Akiba Pololeti, Mlungwana Mchomvu, anasema: “Ujenzi unaendelea vizuri kama unavyoona, na tunakusudia baada ya hapa ujenzi uendelee kwenye maeneo mengine ya kimkakati kiulinzi.”

Baadhi ya majengo yanayoendelea kukamilishwa ni nyumba za kulala askari, ofisi, bwalo, na vyumba maalumu kwa ajili ya kuhifadhi zana za kazi.

Kuhusu usalama Pololeti, Mlungwana anasema kwa jumla ndani ya pori hali ni nzuri, isipokuwa matukio machache ya ujangili kwenye eneo la kilometa za mraba 2,500 ambalo limeachwa kwa wananchi.

“Wanyamapori wanapotoka huku ndani (kwenye kilometa za mraba 1,500) na kwenda nje huko kunakuwa na matukio kadhaa ya wanyama kuuawa, lakini mamlaka husika tunashirikiana nazo kuhakikisha wanyama wanakuwa salama.

Mlungwana anapinga kuwapo vitendo vya ujangili Magharibi mwa Pololeti, na Mashariki mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

“Nikuhakikishie kuwa ujangili tumeudhibiti, tunawashukuru sana wadau – Kampuni ya OBC (Ortelo Business Corporation) kwa kuwa washirika wazuri kwenye masuala ya doria, tunawashukuru sana kwa msaada wanaotupatia wa magari matatu ya doria,” anasema.

Anasema pamoja na OBC, taratibu zinaendelea ili askari wanyamapori wa vijiji na halmashauri washiriki kuhakikisha wanyamapori wanaovuka kuingia eneo la wanananchi wanakuwa salama.

Kwa upande wa shughuli za utalii wa uwindaji na upigaji picha, bado kuna changamoto, ingawa Mlungwana, pamoja na Mratibu wa Shughuli za Uwindaji wa Kitalii Pololeti, Mussa Mmbaga, wanasema mambo yanaendelea vizuri.

Changamoto iliyopo inatokana na ukweli kwamba kitalu cha Pololeti kisheria kimekodishwa kwa mwekezaji OBC anayelipa ada ya kila mwaka ya dola 500,000 (Sh zaidi ya bilioni 1), lakini ndani kuna kampuni mbili – AndBeyond na TAASA – ambazo hazilipi hata senti moja kwa miaka kadhaa sasa.

Awali, kampuni hizo zilikuwa zinalipa Kijiji cha Ololosokwan wakati huo hadhi ya pori ikiwa ni Pori Tengefu. Baada ya Pololeti kupandishwa hadhi na kuwa Pori la Akiba, tangu wakati huo kampuni hizo hazilipi senti yoyote, si kijijini wala wizarani.

Kadhalika, mgongano mwingine ni kati ya OBC yenye leseni zote za uwindaji na upigaji picha, huku kampuni hizo mbili zenyewe zikiwa ni kwa utalii wa picha pekee.

Hali hiyo imeibua mvutano baina yao kwani matumizi ya risasi yanaweza kuwa hatari kwa watalii wa picha wanaoingizwa kwenye kitalu hicho.

Lakini Mlungwana anasema umekuwapo mpango wa kukigawa kitalu hicho ili kutenganisha utalii wa uwindaji na ule wa picha.

Hata hivyo, OBC mara zote wamepinga hatua hiyo wakisema wao waliokodishwa ndio wenye mamlaka kisheria ya kuruhusu watalii wa picha baada ya kuwa wameombwa kwa mujibu wa taratibu.

Serikali imekuwa na kigugumizi cha kumaliza mvutano huo, huku wanufaika wakuu wakiwa ni hizo kampuni zinazoendesha shughuli zake bila kuilipa serikali.

Kwa upande wa uhusiano kati ya NCAA na wananchi kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, hali bado si nzuri sana kutokana na malalamiko ya halmashauri ya kutopata mgawo wa asilimia 25 ya mapato yanayotokana na uwekezaji kwenye kitalu cha Pololeti.

Aliyekuwa Mweyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Marekani Bayo, Desemba mwaka jana alisema ni kwa miaka minne hawakupata fedha hizo, ilhali kila mwaka Mamlaka inapokea Sh zaidi ya bilioni 1 kutoka OBC.

“Uhusiano kati ya wasimamizi wa pori na sisi si mzuri. Awali, pori likiwa chini ya TAWA tulikuwa tunapokea asilimia 25, lakini tangu NCAA wamepewa huu ni mwaka wa nne hatupewi chochote.

“Kwa maoni ya Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, na Kamati ya Fedha tunapendekeza hili pori ni bora likarudi katika usimamizi wa TAWA kwa sababu NCAA hawatupi chochote. Madiwani wanatamani hili pori lirudi katika usimamizi wa TAWA.

“Sisi tunatamani sana tuwe na uhusiano unaoleta manufaa kwa msimamizi wa pori na wananchi wa Ngorongoro kwa sababu pori lipo Ngongoro, na wananchi wanastahili kunufaika nalo. Kwa ufupi niseme Mamlaka hawana uhusiano mzuri na Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro,” anasema Bayo.

Mmbaga anajibu madai hayo sasa kwa kusema taratibu za malipo ya fedha hizo kwa halmashauri ziko ukingoni.

“Bahati nzuri suala hili ninalifuatilia, ninalifahamu vizuri sana, niwahakikishie viongozi na wananchi wa Ngorongoro kuwa fedha hizo zitaletwa muda si mrefu.

“Fedha zinazoletwa ni nyingi, kwa hiyo tunaomba wananchi wa vijiji jirani na Pololeti nao wasaidie kulinda rasilimali hii kwa kutoingiza mifugo eneo la hifadhi, lakini pia kwa kusaidia kuwabaini wote wanaojihusisha na vitendo haramu -ukiwamo ujangili,” anasema Mmbaga.

Anasema kumekuwapo shinikizo kubwa kutoka kwa watu walio nje ya Loliondo na Ngorongoro la kutaka kuingiza mifugo Pololeti.

“Tunaomba wananchi na viongozi watupe support kulinda eneo hili, tuwe na uhifadhi shirikishi kwa faida ya wananchi na taifa, wanapotaka asilimia 25 wajue inapatikana tu endapo uhifadhi eneo hili utaendelea kuwa mzuri,” anasema.