Nimesoma makala ya rafiki na kaka yangu Joster Mwangulumbi, iliyokuwa na kichwa cha habari: “Yako mengi tunayopaswa kuyatafakari”.

Makala hiyo fupi, lakini kali, inamhusu mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli.

Aya moja inasema: “Rais Kikwete na makanda wengine wanampamba Dk. Magufuli kwa sifa kwamba ni mzalendo, mwadilifu, mchapakazi na hana makuu, wanaficha ukweli kwamba Dk. Magufuli ni kiongozi mwenye papara, mjeuri na mpenda sifa.”

Mwangulumbi amejitahidi kujenga hoja za kuhalalisha mtazamo na msimamo wake. Ametaja baadhi ya mambo kama ubomoaji wa nyumba katika hifadhi ya barabara, meli iliyokamatwa ikivua katika bahari eneo la Tanzania, na mzozo wake wake na wamiliki wa malori ya mizigo.

Mwangulumbi, amehitimisha makala yake kwa kuhoji: “CCM wamempitisha mtu ambaye wanajua hana sifa anazopewa kwani katika utumishi wake Dk. Magufuli amejipambanua kuwa mtu mwenye papara, asiyejali umasikini wa watu wala utu wao. Kama ilibidi adhibitiwe ili asiwasababishie hasara wananchi, itakuwaje Magufuli akiwa Rais na Mwenyekiti wa CCM?”

Kwanza, kabla ya kuijadili makala ya Komredi Mwangulumbi, niweke wazi (nitangaze maslahi) kuwa mimi ni mfuasi mkuu wa wagombea urais wawili-Dk. John Magufuli, na Edward Lowassa. Wawili hawa ni marafiki zangu.

Dk. Magufuli, kama alivyo Lowassa; nawapenda kwa sababu staili zao za uongozi zinafanana. Nimesafiri nao wilaya na mikoa karibu yote nchini. Nimeona namna wanavyokagua na kusimamia miradi ya maendeleo. Hawana longo longo. Hawana urafiki na watumishi wazembe.

Ni aina ya viongozi ambao lile wanaloliamini wangependa lishughulikiwe hapo hapo na kumalizwa.

Dk. Magufuli, na Lowassa si viongozi wa kuweka viporo. Wanaamini kila jambo linawezekana, na kuwa kinachotakiwa ni dhamira tu ya utekelezaji. Si viongozi wa kumung’unya maneno wala kuridhishwa na viji-sababu au visingizio.

Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu si mwepesi. Wapo wanaosema Dk. Magufuli anafaa sana kuwa Rais wa Awamu ya Tano, lakini chama alichomo ndicho kinachomponza. Wapo wanaosema laiti angekuwa Ukawa, ushindi wake ungetangazwa kabla ya kuhitimishwa kwa misa ya kwanza ya siku hiyo ya Jumapili!

Wapo wanaomuona Lowassa kama mtu anayefaa kuwa Rais wa Awamu ya Tano. Ukiacha pambo la ufisadi ambalo amevikwa, wanasema kitendo cha yeye kujiunga Ukawa kimewafanya wasiwe na shauku ya kumchagua. Wanatoa mfano wa marafiki zake kama kina Andrew Chenge, Hussein Bashe, Peter Selukamba, na wengine wengi ambao hawakukubaliana na uamuzi wake wa kuihama CCM. Haya yanasemwa.

Wenye uamuzi wa nani awe Rais wa Awamu ya Tano ni wapigakura wa Tanzania ambao kwa namna ya pekee, wamekuwa wakifurika kwenye mikutano ya kampeni kuwasikiliza. Sipendi kuwa mpiga ramli, lakini kama ni kufananisha, basi naweza kusema CCM na Ukawa wameteka siasa za Tanzania kwa staili kama ile ya Democrat na Republican –vyama vikuu vya siasa nchini Marekani! Hii inanifanya nisiwe na shaka kuwa rais wetu ajaye yu miongoni mwa miamba hiyo miwili, ingawa Dk. Magufuli ana nafasi kubwa zaidi inayopambwa na historia na uimara wa chama chake.

Kwa maudhui ya makala hii, naomba nijaribu kuangalia hoja za Mwalimu Mwangulumbi juu ya Dk. Magufuli. Ni ukweli kwamba Dk. Magufuli, amehusika kwenye bomoabomoa ya majengo yaliyo katika hifadhi ya barabara. Mfano wa dhamira yake hiyo aliuonyesha kwa kubomoa nyumba yake na ya familia yake. Akabomoa ofisi za wizara yake zilizokuwa Ubungo, Dare s Salaam. Akawa analitazama kwa jicho la pekee lile jengo la Makao Makuu ya Tanesco ambalo nalo limo kwenye hifadhi ya barabara. Anaamini thamani ya jengo lile hailingani wala haikaribii hasara kubwa wanayopata wananchi na Taifa kutokana na jengo hilo kuwa kikwazo cha upanuzi wa barabara ambayo ingeondoa msongamano.

Katika Bajeti yake ya mwaka 2012/2013, Dk. Magufuli aliwambia wabunge: “Kwenye masuala ya barabara tuache siasa. Sheria zimepitishwa hapa ikiwamo sheria namba 13 ya mwaka 2007 na sheria hii ya road reserve (hifadhi ya barabara) imeanza tangu mwaka 1932.

Sasa ni vizuri tufike mahali tusimamie sheria. Kwa sababu huwezi ukajenga barabara wakati watu wengine wako kwenye barabara. Ni lazima tufike mahali tuamue hata kama ni kwa machungu.

Nilisema siku moja jengo la TANESCO liko kwenye road reserve- si uongo, liko kwenye road reserve hata kama nilisibomoe mimi, siku moja litabomolewa tu unless (labda) tubadilishe sheria.

Hata kama ni jengo la serikali. Ukweli unabaki pale pale, “unless” tufike siku moja tubadilishe sheria zetu kwamba kwa barabara za Dar es Salaam upana wake sasa utakuwa ni upana wa kupita bajaji. Lakini kama hii sheria ipo iliyopitishwa na Bunge, itabaki ni vile vile.

Dk. Magufili aliposimamia ubomoaji nyumba pale Ubungo, alifanya hivyo kisheria. Ndiyo maana hata waliolalamika, walishindwa mbele ya Jaji Frederick Werema. Walikuwa wavamizi.

Akinukuu vifungu kadhaa vya sheria, Dk. Magufuli alisema: “Wizara imeendelea kuzingatia sheria mbalimbali, hususani Sheria ya Barabara Na. 13 ya Mwaka 2007. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, Ibara ya 26 (Kifungu cha 1 na 2), inatutaka wananchi wote kufuata na kutii Katiba na sheria za nchi.

“Kwa mantiki hii, inashangaza sana pale wizara inapoombwa kulipa fidia wananchi ambao kwa mujibu wa sheria wamo ndani ya hifadhi ya barabara. Baadhi ya maombi hayo yanatoka kwetu sisi viongozi ikiwa ni pamoja na kwenu waheshimiwa wabunge mliopitisha Sheria Na. 13 ya Mwaka 2007.

“Kufanya hivyo ni kukiuka sheria ambazo ndizo zinatuongoza. Wizara itaendelea kuzingatia sheria na wananchi wote walio ndani ya eneo la hifadhi ya barabara na wale waliokwisha ondolewa hawatalipwa fidia. Kwa wananchi ambao bado wapo ndani ya hifadhi ya barabara wanatakiwa waondoke wenyewe bila fidia.”

Haya ni maneno ya kijasiri yanayotolewa na kiongozi jasiri. Dk. Magufuli si wa kutaka kumfurahisha mtu wala kumuudhi mtu. Mara zote amesema anasimamia sheria, na kama wapo wanaoona sheria anazosimamia hazifai, wazipeleke bungeni zibadilishwe. Tunamtaka kiongozi wa aina hiyo.

Kwa kuwa mambo aliyoyasema kakangu Mwangulumbi ni mengi, si vibaya nikagusia hili la malori. Nilipata kuandika makala kwenye ukurasa huu huu katika Toleo Na. 105 kuhusu suala hilo. Makala ilikuwa na kichwa cha habari: Pinda: Mwanasheria anayepindisha sheria”.

Nilisema, naomba nikukuu: “Dk. Magufuli, kama walivyo binadamu wengine, ana upungufu wake. Nilishampinga sana kwenye suala la uuzaji nyumba za Serikali. Na kwa kweli nitaendelea kumpinga kwa hilo. Lakini waswahili husema ‘mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni’. Katika hili la malori, nilitangaza tangu mapema kabisa kumuunga mkono. Namuunga mkono kwa sababu kama ni ubaya si Magufuli, bali ni wa sheria iliyopo. Kwanini tumhukumu kiongozi anayesimamia sheria hata kama ni mbaya? Wanaoona mbaya kwanini wasiende bungeni kuifuta au kuirekebisha? Aliapa kulinda au kuvunja sheria?

Dk. Magufuli alipozungumza na waandishi wa habari juu ya kuondolewa kwa nafuu ya kutolipa tozo kwa uzito wa magari unaozidi ndani ya asilimia tano ya uzito unaokubaliwa kisheria, aliwapa nakala za sheria na kanuni wana habari hao.

Baada ya mvutano kati yake na wamiliki wa malori, nimelazimika kuzisoma sheria hizo ambazo ni Sheria ya Usalama Barabarani Na. 30 ya mwaka 1973; Sheria ya Usalama Barabarani Sura Na. 168 ya mwaka 2002 pamoja na Kanuni za Usalama Barabarani za mwaka 2001. Wana habari wanazo sheria hizi (hapa naomba Mwangulumbi azisome sheria hizi).

Sheria hizo na kanuni zake ZILIFUTWA na aliyekuwa Waziri wa Ujenzi, Basil Mramba katika barua yake ya Julai 19, 2006. Yeye ndiye aliyeamuru wenye malori na wasafirishaji wengine wasilipe faini kwa kuzidisha uzito! Hapa ikumbukwe kuwa Tanzania imeruhusu mizigo yenye uzito wa tani 56 isafirishwe katika barabara zake. Nimeingia kwenye mtandao na kuona kuwa hata huko Ulaya, uzito wa juu kabisa unaoruhusiwa ni tani 44. Hapa sisi ni tani 56, lakini ukiongeza na hizo asilimia tano, maana yake ni karibu tani 60! Huu ni mzaha.

Waziri Mkuu Pinda ni mwanasheria. Napata shida kuamini kuwa kwa weledi wake kama mwanasheria, anashindwa kutambua kuwa Waziri (Mramba) hana mamlaka ya kufuta kwa ‘waraka au mwongozo’ sheria iliyotungwa na Bunge. Alichofanya Mramba ni kuvunja sheria iliyo wazi kabisa. Mramba hakuwa, na kamwe hatakuwa na mamlaka ya kufuta sheria kwa kutoa mwongozo!

Kosa hilo hilo la Mramba limerejewa tena na Waziri Mkuu Pinda. Mramba tunaweza kumsamehe kwa sababu, kwanza yeye si mwanasheria, na pili inawezekana alishauriwa na wanasheria wasiotaka kusoma sheria. Pinda ni mwanasheria, anashindwaje kuliona hili?

Serikali inaendeshwa kwa taratibu zinazotawaliwa na sheria. Bila shaka linapokuja jambo kama hili, Mwanasheria Mkuu wa Serikali anapaswa kusaidia kupatikana kwa suluhu. Je, ina maana hata Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameshindwa kumshauri Waziri Mkuu kwamba Mramba mwongozo wake ulikuwa batili? Je, Mwanasheria Mkuu wa Serikali alishindwa kumweleza Waziri Mkuu kwamba sheria haibadilishwi kwa barua ya waziri, bali kwa kuandaa ‘amendment’ na kuiwasilisha bungeni?

Waziri Mkuu amesema itaundwa tume kwa ajili ya kupata suluhu ya kudumu ya mgogoro huu. Kwanini ahangaike na Tume wakati mahali pekee pa kumaliza kadhia hii ni bungeni kwa kupeleka marekebisho ya sheria? Hizi tume ni matumizi mabaya ya fedha za umma.

Juzi amejitokeza Azim Dewji, na kudai kwamba Serikali imepata hasara ya Sh bilioni 20 kwa mgomo bandia walioufanya. Hizi ni porojo. Dewji amepata nguvu za kumsema Magufuli kwa sababu bado anaugulia maumivu ya kufuata sheria aliyoyapata baada ya Magufuli kuzuia maboti yake mabovu kusafirishwa kwa barabara hadi Mwanza. Maboti yenyewe yalikuwa mabovu na sasa yanafaa kuwa vyuma chakavu. Huhitaji akili za ziada kutambua kuwa huyu hata kuwa mbele kumsema Magufuli kunatokana na maumivu hayo ya kuzuiwa kwa maboti yake mabovu!

Pili, watu kama kina Hans Pope kushangilia malori yabebe uzito wa tani zaidi ya 56 si jambo la ajabu. Huyu anataka barabara zife. Wengine walidiriki kumuua Rais wa nchi, bila shaka wao kuziua barabara si kazi ya kuwatoa jasho. Hili nalo halihitaji kusumbua vichwa. Mfanyabiashara Pope anatamba kuwa mwaka jana alilipa serikalini Sh milioni 200 kutokana na biashara yake ya malori! Sawa, Sh milioni 200 ni kitu gani kwa malori yanayoua barabara? Kilometa moja ya barabara ya lami inajengwa kwa wastani wa Sh milioni 700 hadi Sh milioni 1,000. Kwa hiyo Pope anataka aharibu barabara kwa sababu analipa fedha ambazo hazitoshi kujenga hata robo kilometa!

Waziri Mkuu Pinda anatambua kuwa wenye malori hawa ni matajiri. Wana fedha nyingi, na kwa sababu hiyo wana ushawishi wa hali ya juu. Anatambua kuwa wanasiasa wengi wana malori, na kwa sababu hiyo wasingependa kuona reli zikifanya kazi.

Wala hili si la kustaajabisha kwa sababu unaona hata Waziri wa Uchukuzi, Dk. Mwakyembe badala ya kusaidia kuboresha reli na bandari ili zitumiwe kusafirisha mizigo mizito, amekuwa sehemu ya wanaolalamikia mgomo wa malori kwamba umesababisha mlundikano bandarini! Dk. Magufuli ambacho hakijui ni kwamba ameamua kupambana na wenye fedha, na kwa bahati mbaya umma nao umeshindwa kupewa elimu stahiki juu ya ulaghai huu wa kina Dewji na Pope.

Wakati wakubwa hawa wakiendeleza mapambano, zipo kampuni ambazo nimesoma kwenye vyombo vya habari kwamba kwa miaka mingi malori na mabasi yao hayazidishi uzito. Kampuni hizo ni kama Dar Express, Cargo Star, Hood, Coca Cola, BM Bus, Bakhresa, TBL, Golden Coach, Kanji Lalji, Tawaqal, Condolidated Logistic, Ramada Transport na BP ambayo kwa sasa ni Puma.

Kwanini hawa wafaulu, lakini kina Dewji washindwe? Hawa hawa watetezi wa uzito bila shaka ndiyo wanaosali usiku na mchana reli zisifanye kazi. Leo ni kwa Dk. Magufuli, lakini ikitokea Dk. Mwakyembe akaanza kujenga reli, na yeye watamshughulikia tu! Hawa wapo kimaslahi zaidi.

Hizi barabara si mali za wafanyabiashara wamiliki wa malori na mabasi. Barabara za Tanzania zinajengwa kwa kodi za wananchi wote. Mikopo ya barabara hizi italipwa hadi na vitukuu vyetu. Kama hivyo ndivyo, hatuna sababu ya kushabikia wanaozidisha uzito.

Lakini kubwa zaidi ni kwamba nchi inaongozwa kwa sheria. Bila kuheshimu sheria, nchi hii itakuwa kituko. Hali inakuwa mbaya zaidi pale Waziri Mkuu, kiongozi mkubwa kabisa, anapoamua kubariki barua ya waziri wa zamani ifute au ipindishe sheria zilizotungwa na Bunge. Kuna maana gani ya kuwa na Bunge? Kuna maana gani ya mawaziri, akiwamo Waziri Mkuu kula viapo vya utii wa sheria za nchi?

Kanuni ya 17(1) ya Sheria ya Usalama Barabarani, inasema hivi kwa kimombo: “Any Person aggrieved by the decision of the authorized officer or the Road Authority refusing to grant a weigh bridge report or any permit required to be granted under these Regulations may appeal against that decision to the Minister.

(2) Where a person is not satisfied by the decision of the Minister he may appeal to the High Court and the provisions of the Criminal procedure Act, shall apply.”

Hapa kinachoelezwa ni kwamba kama mtu hakuridhishwa na uamuzi wa Waziri, anachopaswa kufanya ni kwenda kufungua kesi katika Mahakama Kuu.

Wenye malori wanaijua kanuni hii, na Waziri Mkuu anaijua pia. Wanatambua kuwa wakienda mahakamani watashindwa. Njia ya mkato waliyoamua kuitumia ni ya kwenda kwa Waziri Mkuu ambaye hatajwi kwenye sheria hii. Kwa hiyo kilichofanywa na Pinda ni ubabe tu kwa sababu ni Waziri Mkuu. Amefanya hivyo akijua Magufuli hawezi kumpinga. Haya ni matumizi mabaya ya madaraka. Huu ndiyo ukweli ambao wana habari hawataki kuusema, na jamii imefungwa isiujue.

Sioni ni kwa namna gani Pinda ataumaliza mgogoro huu kwa staili aliyoamua kuitumia ya kuvunja sheria. Sioni ni kwanini Mwanasheria Mkuu wa Serikali asiwe sehemu ya lawama kwa kushindwa kumwongoza au kumshauri Waziri Mkuu kwenye jambo hili lisilohitaji mhitimu wa cheti cha sheria.

Moja ya matatizo makubwa katika nchi yetu ni viongozi kukosa misimamo. Viongozi kama Mheshimiwa Pinda wapo radhi kuvunja sheria alimradi tu waridhishe kundi la watu wachache.” Mwisho

Kwa kuwa ukurasa huu hautoshi kujibu hoja zote za Komredi Mwangulumbi, naomba niishie hapa kwa leo. Lengo kuu ni kujaribu kuweka sawa baadhi ya mambo ya wagombea urais ili wapigakura watekeleze wajibu wao kwa haki ifikapo Oktoba 25, 2015. Muhimu, nchi hii inamhitaji Rais mwenye msukumo wa utendaji kazi na usimamizi wa sheria na haki. Haki haipo tu kwa aliye na nyumba kwenye hifadhi ya barabara, bali ipo pia kwa wale wanaohitaji barabara kwa shughuli zao za kiuchumi.

By Jamhuri