Kwa muda mrefu sasa nimekuwa nikisikia na kuona jinsi wananchi wengi katika maeneo mbalimbali ya nchi hii, wanavyowalalamikia askari polisi wa kitengo cha usalama barabarani (trafiki). Siyo siri ndugu zetu hao wanachukiwa na wananchi wengi.

Binafsi nilikuwa sijapata kushuhudia kinachosababisha watu wengi kuwachukia trafiki. Wiki iliyopita ndiyo nimejionea. Sasa nimeamini msemo wa Waswahili kwamba lisemwalo lipo. Nimeamini kuwa askari hao ni kero katika jamii.

 

Naomba nisimulie angalau kwa muhtasari kitendo nilichoshuhudia Septemba 10, mwaka huu kama ifuatavyo:

 

Siku hiyo, wakati jua likielekea usawa wa utosi, nilikuwa ninasafiri kwa kutumia daladala inayofanya safari zake kati ya Masaki na Gongo la Mboto, jijini Dar es Salaam.

 

Abiria tuliokuwa tumesongamana, baadhi wakiwa wamekaa vitini na wengine wamesimama ndani ya daladala hiyo, tulishuhudia kitimbi cha aina yake tulipofika kituo cha Magomeni Mikumi.

 

Pale kituoni tulimkuta trafiki mmoja ‘akaipiga mkono’ daladala yetu kwa mbwembwe za aina yake. Iliposimama askari yule akatembea shoto-kulia hadi dirishani kwa dereva na kumuuliza leseni ya udereva.

 

Dereva alimwonesha leseni yake, trafiki akaiona na kujiridhisha kuwa ni halali. Mara akarudi nyuma kidogo kwa mwendo wa kijeshi na kukagua risiti za bima zilizobandikwa juu ya kioo cha mbele cha daladala ile, akajiridhisha kuwa ni hai.

 

Trafiki akarudi tena hatua mbili nyuma, safari hii akasimama mguu sawa mbele ya uso wa daladala ile. Akamwamuru dereva awashe taa ya kiashirio (indicator) ya upande wa kushoto, dereva akawasha. Kisha akamwamuru awashe ya upande wa kulia, dereva akawasha. Trafiki akatikisa kichwa kuashiria kuwa mambo ni sawasawa kabisa.

 

Trafiki yule hakuishia hapo, akamwamuru dereva wetu, “Washa full light (taa kubwa za mwanga mweupe).” Dereva akatekeleza amri hiyo haraka. Askari akaonesha dolegumba kuashiria kuwa hakuna tatizo.

 

Mara tena, akamwamuru awashe vifutio vya kioo cha gari (wipers). Dereva akawasha, lakini kilichoonekana kufanya kazi ni cha upande wa kulia (upande wa dereva) pekee.

 

Trafiki kuona hivyo, akamwamuru dereva ashuke chini na amfuate pembeni kidogo mwa barabara kituoni pale. Wakati huo dakika takriban 20 zilikuwa zimeshapita tangu daladala yetu izuiwe na askari yule. Abiria tumechemka joto, kila mmoja anavuja jasho. Watoto wachanga waliokuwa wamebebwa na mama zao wanalia ovyo kutokana na hali ya hewa iliyobadilika kuwa mbaya ndani ya daladala.

 

Adha hiyo iliwalazimu abiria wengi ndani ya daladala ile kunung’unikia kitendo cha kucheleweshwa na trafiki yule, baadhi wakitoa matamshi ya kumkejeli na wengine kulishutumu Jeshi la Polisi kwa jumla.

 

Hata hivyo, unajua kilichofuata baada ya mabishano, au niseme mvutano wa wawili wale? Dereva alirudi na kuelekea ulipo mlango wa abiria akamwomba kondakta wake atoe Sh 30,000 alipe faini aliyotozwa na trafiki yule kutokana na kosa la wiper ya upande wa kushoto kushindwa kufanya kazi.

 

Baada ya hapo dereva aliingia na kuwasha daladala tayari kwa kuendelea na safari. Hadi hapo tulikuwa tumepoteza dakika 40 hivi kituoni pale!

 

Lakini tena, katika tukio lisilo la kawaida, trafiki yule alimwamuru dereva asimamishe gari tena. Akaanza kuhoji kwamba mbona tairi moja la nyuma ni ‘kipara’?

 

Kitendo hicho kilichochea hasira za abiria, wakaanza ‘kutapika nyongo’. Wakamshambulia trafiki yule kwa matusi waziwazi hadi akaona aibu na kuamua kuruhusu daladala iendelee na safari.

 

Binafsi sitaki kuamini kwamba utaratibu uliotumiwa na trafiki yule kukagua daladala ile ndiyo mfumo rasmi wa Jeshi la Polisi Tanzania. Naamini jeshi hilo lina utaratibu mzuri wa kushughulikia makosa ya ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani bila kusababisha kero kwa abiria.

 

Kwa vyovyote vile, hakuna mtu anayeweza kufurahia ‘sinema’ iliyooneshwa na askari yule katika daladala ile. Alionesha ubabaishaji mkubwa, lakini zaidi yote aliwakera na kuwaudhi abiria kwa kiasi kisichovumilika. Kuwachelewesha abiria kwa muda wa dakika 40 kituoni ni kero kubwa.

 

Jeshi la Polisi linalopaswa kuwa kimbilio la kila mtu kutokana na jukumu lake la kulinda usalama wa raia na mali zao, leo ndilo linaelekea kuwa chukizo kwa raia wengi. Askari polisi wasiyo waadilifu na waaminifu wanaonea na kunyanyasa raia, wanawapiga na kuwabambikia raia kesi za makosa ya jinai!

 

Nirudi kwenye mada yangu. Ninaamini wapo trafiki wanaofanya kazi za kusimamia sheria za usalama barabarani kwa utaratibu mzuri usiokuwa na bughudha kwa abiria, dereva na kondakta.

 

Lakini kuendelea kuwa na trafiki wa aina ya yule aliyekagua daladala ile katika kituo cha Magomeni Mikumi ni kuendelelea kuchochea chuki ya wananchi dhidi ya Jeshi la Polisi, hasa askari wa usalama barabarani.

 

Umefika wakati Jeshi la Polisi lijitathmini upya kiutendaji na kuchukua hatua madhubuti za kujisafisha mbele ya umma kwa kuwapumzisha kazi askari walioporomoka kimaadili, wanaoendekeza tabia na vitendo vinavyosababisha wananchi kulichukia na kukosa imani nalo.

 

By Jamhuri