Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani

Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amewakumbusha Waratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kuhakikisha wanafanya ufuatiliaji kwa wanufaika wa mpango huo ili kuwatoa walioimarika na kutoa nafasi kwa wenye hali mbaya.

Vilevile amewataka Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa mkoa huo kuendelea kutoa kipaumbele kwenye suala la kutokomeza umasikini kwenye maeneo yao kwa kuwa na mfumo wa ufuatiliaji kwa walengwa wa TASAF.

Ameyasema hayo katika kikao cha kujadili Utekelezaji wa shughuli za TASAF ambapo alipokea taarifa ya utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa na mfuko huo sambamba na ushuhuda kutoka kwa wanafunzi wa vyuo vikuu walionufaika.

Amesema kukiwa na ufuatiliaji wa miradi ya mfuko huo itasaidia ile inayokwama vikwazo kuondolewa kwa wakati na kuikamilisha ili iweze kuwanufaisha wananchi.

” Lengo la TASAF ni kuondoa umasikini uliokithiri , wale ambao tunaona wamevuka na kuanza kuimarika tuwatoe ili wengine waingizwe kwenye mpango na kuwasaidia kubadili maisha yao tutambue kuwa unapowasaidia masikini ni ibada pia” amesema.

” Nawasisitiza Wakuu wa Wilaya hili ni eneo ambalo tulisimamie vizuri TASAF ni kipaumbele cha Rais vipaumbele vyetu tunavipata kutokana na vipaumbele vya nchi namshukuru Rais kwa kuendelea kugusa maisha ya kaya masikini” amesisitiza.

Mratibu wa TASAF mkoa wa Pwani Roseline Kimaro,amesema mafanikio yanayopatikana Pwani katika utekelezaji wa miradi inatokana na ushirikiano uliopo baina ya Mkoa na waratibu wa Tasaf katika Halmashauri mbalimbali.

Amesema ,kwasasa wanafunzi 52 wa vyuo vikuu ambao wanasoma kupitia mpango huo walianza kunufaika kuanzia shule za msingi baada ya wazazi wao kuingizwa kwenye mradi.

Katika kikao hicho Kunenge amekabidhi tuzo kwa Halmashauri zilizofanya vizuri kwenye miradi ya TASAF sambamba na Afisa Kilimonkata ya Janga Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Mugisha Vicent ambaye amefanya vizuri kwenye mradi wa kilimo.

By Jamhuri