Toleo lililopita tuliishia aya isemayo: “Mwenyezi Mungu hakukuumba kwa bahati mbaya, kwa Mungu hakuna bahati mbaya, Mungu hana bahati na sibu.” Sasa endelea…

Mfalme Daudi alimtukuza Mungu kwa kusema: “Ninakusifu (Mungu) kwa kuwa nimeumbwa kwa namna ya ajabu, ya kutisha’’ (Zab 139:14).

Usimwaibishe Mungu kwa kuishi maisha ya kujikataa, kujikataa ni kumwaibisha Mungu aliyekuumba kwa sura na mfano wake (Mwanzo 1:26-27).

Kujikataa ni kumwambia Mungu hakukuumba vizuri, kujikataa ni kuzikataa baraka za Mungu katika maisha yako.

Anza kukataa kujikataa, kataa kuwa maskini, kataa kuwa ombaomba, kataa kuwa mlevi, kataa kuwa mzinzi. Kataa kuwa mchepuko, kataa kuwa  muongo, kataa kuwa mnafiki, kataa kuwa na kiburi, kataa kuwa na majivuno.

Kujikataa ni kukubali kushindwa kufanikiwa, unapojidharau unakuwa adui wa mafanikio yako. Iko hivi; kutokuwa na mipango mikubwa katika maisha yako ni kujikataa.

Kutokujistahi ni kujikataa, kutojipenda ni kujikataa, kutokujiamini ni kujikataa. Kutokujitakia mema ni kujikataa.

Kuishi na chuki moyoni mwako ni kujikataa, kutokusamehe ni kujikataa, kuwawazia watu wengine mabaya ni kujikataa.

Leo andika upya historia ya maisha yako, jiwekee agano la kufanikiwa. Jikubali kuanzia leo na  siku zote zijazo, jipende kuanzia leo na siku zote zijazo.

Jiamini kuanzia leo na siku zote zijazo, jisamehe, jiheshimu kuanzia leo na siku zote zijazo.

Mwanasaikolojia wa Uswisi, Carl Jung, anasema kujua giza lako mwenyewe ni mbinu bora ya kukabiliana na giza la watu wengine.

Kila mtu ni kiongozi wa maisha yake na maisha ya wengine, usipojiongoza wewe mwenyewe huwezi kuwaongoza wengine. Kesho inakuja.

Usipojiandaa vizuri leo, kesho yako itakuwa na lawama, fanya kazi kwa bidii ili kesho yako iwe njema.

Lawama ni mtaji wa walioshindwa kufanikiwa, acha kulalamika. Jiondoe kwenye kundi la watu wanaolalamikia kila jambo.

Waandishi wa kitabu cha ‘The Power of No’, James Altucher na Claudia Altucher wanasema: “Kulalamika ni kukimbiza fursa, unapoacha kulalamika unaanza kuona kila hali ya fursa, unafungua mlango wa kupata mawazo mapya. Hakuna aliyefanikiwa kwa kulalamika, usilalamike.”

Mwandishi T. L. Osbon anasema: “Ukiacha kujifunza unaanza kufa, tafuta wazo jipya kila siku. Kumbuka; usipotumia nguvu nyingi kuwaza mawazo  yatakayoibadili dunia ni lazima utaajiriwa na watu waliotumia nguvu nyingi kuwaza mawazo yaliyoibadili dunia.”

Mwandishi wa vitabu vya kiroho, Tony Evans, anasema watu wengi wanatumia muda wao mwingi kuishi maisha ya watu wengine. Simamia ndoto yako.

Huko Marekani msichana wa Kiprotestanti aligeuka na kuwa Mkatoliki, alijiunga na shirika la watawa kinyume cha  mategemeo ya familia yake. Baba yake mzazi alimwandikia barua ili auache utawa na kurudi nyumbani.

Sehemu ya barua yake ilisomeka: “Nitakuachia dola milioni kumi na mbili kwa sharti kwamba utauacha utawa na kutoka konventini.”

Msichana huyu aliyekuwa amekubali kumfuata Yesu Kristo kwa mtindo wa maisha ya wakfu alimjibu baba yake kupitia barua.

Sehemu ya barua ya msichana huyu kwa baba yake ilisomeka: “Baba nilijiandaa kuwa mtawa, utajiri ulionao naomba uwasaidie watu wasiojiweza. Baba yangu wa mbinguni ni tajiri zaidi ya baba yangu wa duniani.”

Msichana huyu alibaki konventini na kuwa mtawa, maisha ya msichana huyu yanatufundisha umuhimu wa kusimamia ndoto.

599 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!