Zimejitokeza hoja mbalimbali za kwa nini wananchi wa Bukoba Vijijini wanapendelea makao makuu ya halmashauri yao yawe katika eneo la Ibwera, katika Kata ya Ibwera iliyoko kwenye Tarafa ya Katerero. Kwa vile kuna hoja zinazokinzana, ngoja tukazitazame hoja hizo kusudi tukaone ni zipi zenye uzito zaidi.

Kabla ya hapa nilishaandika kwamba sehemu ya Bukoba Vijijini ambayo iko upande wa magharibi mwa wilaya hiyo ni bora ingetengwa na kuitwa wilaya ya Ikimba. Nilijaribu kujieleza nikionyesha mantiki ya kufanya hivyo, ila kuna baadhi ya wadau waliojaribu kuonyesha kuwa kuanzisha wilaya ndani ya nyingine ni kuzidi kuibebesha mzigo serikali. Hao wanaihurumia serikali bila kueleza fedha zinapaswa zifanye nini kama si kuhudumia wananchi kwa mtindo wa kuwasogezea huduma karibu yao.

Turudi kwenye hoja ya halmashauri. Kama nilivyokwisha kusema, eneo la Ibwera liko katikati ya Wilaya ya Bukoba Vijijini, wapo wanaopinga wazo hilo ila hao mimi sibishani nao, ukweli ni kwamba wanabishana na Mwenyezi Mungu aliyeumba wilaya yetu namna ilivyo.

Ni kwamba eneo la Ibwera lina sehemu maarufu inayoitwa Kati, asili ya jina hilo ni wakoloni. Wakati Wazungu wa madhehebu ya dini ya Kikatoliki na Waluteri wanakuja, ikabidi wakoloni waingilie kati kwa kuwatenganisha ili kuepusha msuguano wa kiimani. Wakatoliki wakaelekezwa kwenda sehemu moja inayoitwa Mwemage, iliyo kilimani, Waluteri nao wakaelekezwa Kagondo, Rwija, nako kilimani pia.

Kwa vile ni kawaida ya Wazungu kupendelea sehemu za miinuko, basi wote wakakaa raha mustarehe. Wakatoliki wakajenga kanisa, hospitali, shule za msingi za wasichana na wavulana pamoja na makazi ya watawa. Vivyo hivyo kwa upande wa Waluteri kule Kagondo nako kukajengwa, ikiwa ni pamoja na chuo cha Biblia na muziki.

Sehemu hizo mbili zilizidi kuboreshwa mwaka hadi mwaka na kuiongezea thamani sehemu ya Ibwera kiasi kwamba hakuna mtu anayeweza kusema kuwa makao ya halmashauri yamepelekwa porini.

Sehemu ya katikati ikaachwa wazi ikijionyesha kwamba hapo ni katikati, au kwa kifupi Kati. Na ikitazamwa si kati kwa Ibwera peke yake, ila kwa eneo lote la Bukoba Vijijini, au Ikimba kama nilivyokwisha kueleza katika makala iliyotangulia.

Sababu hata Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kipindi anakitangaza Chama cha TANU kuelekea Uhuru,  alipendelea sana kupatumia pale Kati kupata chakula cha mchana baada ya mizunguko mirefu upande wa Bukoba Vijijini akiongea na wananchi.

Kitu kingine ni kwamba hakuna eneo jingine katika Wilaya ya Bukoba Vijijini lililo rafiki kutembelewa kama Ibwera, sababu mtu akitokea Katoro baada ya mwendo wa muda mfupi anapandisha na kufika Ibwera, vivyo hivyo akitokea Kasharu, Izimbya, Rubale, Ruhunga, Katoro na kadhalika.

Pia akitokea Bugabo maeneo ya Rubafu, Maruku, Katoma atapandisha na kupumzika Ibwera. Umbali uliopo kutoka Rukoma, Kibirizi, Kamuli kufika Ibwera ni sawa na umbali uliopo kutoka Bugabo kuja Ibwera. Ndiyo maana Ibwera panaonekana ni katikati. Na hakuna sehemu nyingine iliyo kama Ibwera.

Ni kwamba kila upande unaotokea kufika Ibwera safari inakuwa bado inaendelea, tofauti na maeneo mengine ambayo ukifika safari inakuwa imegota kwa maana ya kufika mwisho wa eneo au wilaya, sehemu ya aina hiyo inakuwa upande ikiwa imejitenga na watu.

Aidha, ikisemwa halmashauri iwe maeneo ya Kemondo Bay, kama inavyosemwa na baadhi ya watu walioshindwa mpangilio, ni kwamba watu wengi wa wilaya husika watakuwa wamewekwa pembeni wakati watu wa wilaya nyingine wakiwa ndio wanaonufaika. Kemondo Bay inakuwa rahisi kuwahudumia watu wa Muleba na Muleba Kaskazini kuliko watu wa Bukoba Vijijini.

Sababu kutoka maeneo ya Kamachumu, Muleba Kaskazini mpaka Kemondo Bay ni kama kilometa saba na kumi na tano mtawalia. Na barabara ni ya lami tu kiasi cha kuwafanya watu hao wa wilaya nyingine wateleze tu kufika Kemondo Bay kupata mahitaji yao.

Wakati kuna sehemu za mbali za Bukoba Vijijini, ambazo mtu inambidi imtoke nauli ya Sh 4,500 kufika Kemondo Bay, maeneo ya Wilaya ya Muleba wanatumia nauli ya Sh 2,000 tu kufika Kemondo Bay! Tukajiulize, ni yupi ananufaika zaidi na halmashauri hiyo kuwa pale? Ni mtu wa Bukoba Vijijini au Muleba?

Hata Rais John Magufuli alisema kwamba ni bora halmashauri ikawa ndani ya watu kuliko watu kuifuata halmashauri uhamishoni.

Sababu Kemondo Bay bado inahesabika ni sehemu ya Bukoba Mjini. Mfano nauli ya kutoka Kibirizi mpaka Bukoba Mjini ni Sh 4,500 ambayo ndiyo nauli ya kutoka Kibirizi kufika Kemondo Bay. Kwa hiyo, mwananchi wa Kibirizi, Kamuli, Rukoma na kwingineko, atakuwa amesaidiwa nini kwa kuyatoa makao ya halmashauri yake sehemu moja ya mjini na kuyapeleka sehemu  ya pili ya mjini?

Lakini kwa nini itokee yote hiyo wakati eneo muafaka kwa shughuli hiyo lipo na linapatikana bila kikwazo chochote?

Baada ya maelezo yote hayo, ninashauri halmashauri ya Bukoba Vijijini ipelekwe Ibwera kama kuwatendea haki watu wa Bukoba Vijijini.

prudencekarugendo@yahoo.com

0654 031 701

353 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!